15 Oct 2008


WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wasomi wengine, wameulaumu uongozi wa chuo hicho kwa kushindwa kuandaa mdahalo maalumu kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka tisa ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Wakizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi wa mikutano wa Nkurumah, chuoni hapo Dar es Salaam jana, baadhi ya wanafunzi walisema walifika asubuhi kushiriki mdahalo huo, lakini wakakuta ukumbi umefungwa na hakukuwa na maelekezo yoyote. 

Mbunge wa Serikali ya Wanafunzi UDSM (DARUSO), Bw. Owawa Stephen, alisema kitendo hicho kimedhihirisha jinsi viongozi wa chuo hicho walivyoanza kumsahau Mwalimu Nyerere. 
"Hii imedhihirisha kuwa chuo kinaelekea upande wa mabepari ndiyo maana wanaona hakuna umuhimu wa kumuenzi Nyerere," alisema Bw. Stephen na kuongeza kuwa inawezekana uongozi wa chuo hicho umeogopa kuandaa mdahalo huo kwa kuhofia hoja ambazo zingetolewa kutokana na vitendo vinavyoendelea nchini ambavyo Mwalimu alivikemea. 

Mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Bw. Cosmas Makune, alisema ni aibu kwa wasomi kushindwa kumuenzi Mwalimu Nyerere katika kipindi hiki ambacho vitendo vya kifisadi vimekithiri. 
"Leo wanatuzuia sisi wasomi, tunaosoma kwa kodi za wananchi tusipaze sauti zetu na kuongelea yanayoendelea nchini," alilalamika Bw. Makune na kuongeza kuwa mdahalo huo kama ungefanyika ungekuwa na maslahi makubwa kwa Taifa. 
"Ni jambo la kushangaza kuona maprofesa wanaogopa hata kutoa nafasi kwa wanafunzi kutoa mawazo yao...hawa ni maprofesa gani wasioonesha vitendo?," alihoji Bw. Makune. 

Naye Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kitivo cha Siasa za Sayansi (DUPSA), Bi Elizabeth Maginga, alisema viongozi wa chuo hicho wameanza kuzuia fikra za wasomi na imedhihirisha kuwa hawatambuliwi. 

"Ni jambo la kushangaza, siku ambayo ni muhimu kuongelea masuala ya msingi, ukumbi unafungwa, wanachokifanya ni kutulazimisha tuanze kumsahau Mwalimu Nyerere," alisema. 
Aliongeza kuwa yanayotokea sasa ndiyo ambayo Mwalimu Nyerere aliyapinga. 

"Wamekimbia, wamejua mjadala utatoa changamoto nzito," alisema Bi Elizabeth na kuongeza kuwa DUPSA ilikuwa na mpango wa kuandaa mdahalo huo, lakini uongozi uliahidi kufanya hivyo, ahadi ambayo haikutekelezwa. 
Katika mbao hakukuwa na matangazo yoyote yaliyoeleza chochote kuhusiana na jinsi wasomi watakavyomuenzi Mwalimu Nyerere. 

Majira ilifika kwenye ofisi za baadhi ya viongozi wa chuo hicho kupata ufafanuzi, lakini wote hawakuwa chuoni hapo. 
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rweikaza Mukandala naye alipotafutwa kwa njia ya simu, haikuwa hewani.

CHANZO: Majira

1 comment:

  1. awali sikuamini hali hiyo. nikajua labda itakuwa ghafla tutaitwa au kuwepo taarifa ya kujulishwa kumbukumbu lakini wapi bwana yaani jamaa wanaishi shwari hawaoni noma inashangaza lakini salama. labda ghadhabu kwamba mapenzi ya serikali yamehamia chuo kikuu cha Dodoma. siku hiz hawaishi kulalamika eti serikali imeitupa mlimani ipo dodoma. sijui maana yake nini hawa jamaa

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube