29 Oct 2008

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Dar es Salaam limewaonya maaskofu wa Jumuiya za Kikristo Tanzania (CCT) kutoitisha Serikali katika suala la kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu (OIC) na kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini wakitishia kuwa kitendo hicho ni uhafidhina na ugaidi. 

Tamko hilo limetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Mussa Salum kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mara baada ya kikao cha masheikh na maimamu wa mkoa huo kujadili pamoja na mambo mengine, kauli ya maaskofu hao. 

"Waislamu tunasema suala la Tanzania kujiunga ama kutojiunga ni suala la Serikali ya Tanzania kwa maslahi ya wananchi wote," alisema Sheikh Salum. 

Sheikh Salum aliongeza kuwa suala la Mahakama ya Kadhi ni haki ya Waislamu wa nchini na wala halina mjadala kwa kuwa haliwahusu watu wa dini nyingine na kwamba mifano mingi ipo katika nchi mbalimbali juu ya kuwepo kwa mahakama hizo. 

"Mahakama hizi zilikuwepo tangu ukoloni, hivyo hili siyo suala la kuomba kuanzishwa kwake bali tunaiomba Serikali izirejeshe," alisema. 

Pia masheikh na maimamu hao walihoji uhalali wa kuwepo kwa Balozi wa Vatican hapa nchini kuwa anawakilisha nchi gani na kuliita kuwa suala hilo limegubikwa na udini lakini Waislamu hawakuwa wakihoji. 

"Tunawaonya maaskofu kuacha kuishinikiza Serikali mara kwa mara kuhusu masuala yanayohusu Waislamu na waache kupandikiza chuki kwa waumini wao juu ya suala la OIC na Mahakama ya Kadhi na waumini wa dini ya kiislamu kwa ujumla," alisema. 

Mwishoni mwa wiki iliyopita maaskofu 64 wa makanisa mbalimbali nchini walisaini waraka wa kumpinga Waziri Membe aliyekaririwa awali akiwataka Watanzania kutoogopa kujiunga na OIC kwani ni jumuiya yenye maslahi mazuri ya kiuchumi kwa taifa, akikariri utafiti uliofanywa na Serikali. 

Tayari BAKWATA makao makuu imeshatangaza kuitisha mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu kesho kueleza msimamo wake kuhusu suala hilo.

CHANZO: Majira

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.