Showing posts with label OIC. Show all posts
Showing posts with label OIC. Show all posts

13 Mar 2009


BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limeibua upya hoja za kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu Duniani (OIC), kwa kuitaka serikali kutafakari kwa kina na hekima juu ya kuridhia kuanzishwa kwa vyombo hivyo.

Kuibuka tena kwa hoja hizo kumekuja miezi michache baada ya Rais Jakaya Kikwete kufunga mijadala hiyo iliyokuwa ikielekea kuwagawa wananchi kwa misingi ya kidini.

Hoja hizo zimeibuliwa juzi kwenye Baraza la Maulid na Naibu Katibu Mkuu wa Utawala wa Bakwata, Suleiman Lolila, ambaye aliitaka serikali iangalie upya na kwa hekima na kama inawezekana iharakishe masuala hayo mawili.

“Tunaipongeza serikali kwa hekima kubwa na jitihada inayoitumia katika kushughulikia masuala ya Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC, Waislamu wanangoja kwa hamu na shauku kubwa ridhaa ya serikali, Inshallah, tunaiombea serikali ipate wepesi katika masuala haya maridhawa.

“Tunawaomba Waislamu wadhamirie kwa dhati katika suala hili la OIC na mahakama ya kadhi kwa kutokuruhusu mwanya wowote wa mifarakano miongoni mwetu, kwani mifarakano itakaribisha mgawanyiko na utengano miongoni mwa jamii,” alisema Lolila.

Naibu Katibu Mkuu huyo, akisoma risala ya Bakwata mbele ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alisema ili kuridhiwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na OIC kuna hitaji utulivu wa hali ya juu miongoni mwa waumini wa dini zote mbili (Waislamu na Wakristo) ili kuipa serikali nafasi ya kufanya maamuzi ya busara kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa miongoni mwa jamii.

Suala la uanzishwaji wa mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC, mwishoni mwa mwaka jana lilizua mjadala mpya nchini, baada ya kufika bungeni na kutishia kuwagawa wabunge kwa itikadi za kidini.

Oktoba mwaka jana katika hotuba yake, Rais Kikwete, hakutaka kuweka wazi ni lini Tanzania itaridhia kujiunga na OIC pamoja na uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, na badala yake aliwatuliza wananchi kwa kuwaambia wavute subira wakati serikali ikilifanyia kazi suala hilo kwa masilahi ya umma.

Rais Kikwete aliweka bayana kuwa ni mapema mno kuanza kutoa uamuzi wa masuala hayo, kwa kuwa bado utafiti haujakamilika pamoja na serikali kutotoa uamuzi wa mwisho, hivyo hakuna sababu kwa wananchi kulumbana.

31 Oct 2008

Picha kwa hisani ya BONGOPICHA

WAKATI serikali ikishutumiwa na viongozi wa madhehebu ya Kikristo, juu ya Tanzania kutaka kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu (OIC) na kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amekutana kwa siri na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kujadili masuala hayo.

Kikao hicho cha faragha cha viongozi hao wawili, kilichukua zaidi ya saa moja katika mazungmzo yao yaliyofanyika jana katika ofisi za Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kuanzia saa 10:30 jioni hadi saa 11:30.

Membe alikutana na Pengo jana ikiwa ni siku moja baada ya kardinali huyo kurejea nchi akitokea Vatican ambako alikwenda kwa shughuli za kanisa.

Akizungumza na Tanzania Daima, baada ya kumalizika kwa kikao hicho nyeti, Waziri Membe alikiri kuwa na kikao cha faragha na kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki nchini, lakini hakuwa tayari kusema nini walichojadiliana, kwa madai kuwa, hayapaswi kuwekwa hadharani kwa sasa.

“Unajua Kardinali Pengo ni kiongozi wa kiroho wa ngazi ya juu sana, kila tunapokuwa na masuala mazito ya kitaifa, tunapenda kupata ushauri wake pamoja na viongozi wengine wa kiroho ili kuona wanasemaje,” alisema Waziri Membe.

“Mbali na suala la OIC na Mahakama ya Kadhi, tumezungumza mambo mengi ya kitaifa ambayo mimi sipaswi kueleza zaidi kwa undani, kwani unaweza kumuuliza Baba Kardinali mwenyewe kama atataka kukueleza, lakini ni mambo ambayo yanahusiana na maisha ya Watanzania wote,” alisema Waziri Membe.

Kuhusu mjadala unaoendelea juu ya Tanzania kujiunga na OIC na jinsi hali ilivyo kwa sasa nchini, Waziri Membe alisema ni mambo ya kupita na utulivu utarejea hivi karibuni.

“Hali ya amani na utulivu itarudi hivi karibuni, hakuna shida, serikali ina amini na inawahakikishia wananchi kuwa hakuna vurugu kuhusiana na hilo wala suala lingine lolote.

“Watu watulie, wafanye kazi, serikali itakutana na wadau wote na nasema tena, hakuna tatizo kubwa hapa, tutahakikisha suala hili linaisha kwa amani bila kusababisha vurugu zozote,” aliongeza Membe.

Akizungumzia madai yaliyotolewa na Jumuiya ya Maaskofu wa CCT, kumtaka ajiuzulu hivi karibuni, alisema kuwa hilo hataki kuliongelea kwani amechoka, aachwe apumzike kwanza.

Jitihada za kumtafuta Kardinali Pengo, kuzungumzia juu ya kikao hicho cha siri ziligonga mwamba baada ya kuambiwa kuwa, ameingia kwenye kikao kingine na uongozi wa Kanisa la Mt. Joseph na haijulikani kingeisha saa ngapi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita maaskofu wanaounda Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), walielezea kusikitishwa, kushtushwa na kupinga ushawishi unaojengwa na serikali wa kutaka Tanzania iridhie kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Askofu Peter Kitula ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, alisema hawatakuwa tayari kukubalia kwa vyovyote vile kuona chama fulani cha siasa kikijaribu kutafuta ridhaa ya wapiga kura kwa gharama ya kutishia umoja wa kitaifa na amani ya nchi.

“Hapa ieleweke kuwa ni hatari na kamwe isiruhusiwe njia hii kutumika ili mradi chama fulani kishike dola hata kama ni kwa gharama ya kuvunjika kwa umoja wa kitaifa na amani ya nchi hii! Jambo hili hatutalikubali kwa vyovyote vile kwa chama chochote kitakachokubali mambo haya mawili aidha wakati wa kampeni za uchaguzi au wakati wowote ule,” lilisema tamko hilo la CCT lililoambatanishwa na majina ya maaskofu 64 wa nchi nzima.

Pasipo kufafafanua huku wakisema kwamba CCT, haifungamani na chama chochote cha siasa, maaskofu hao katika tamko lao walisema, iwapo itafikia hatua ya Tanzania kujiunga na OIC na Mahakama ya Kadhi kuridhiwa, basi wao watalazimika kufikiria upya jinsi ya kukishauri chama hicho tawala kwa kuzingatia kile walichokieleza kuwa ni manufaa ya Watanzania.

“Kipekee wakati huu, kutokana na yanayoendelea kujadiliwa bungeni, tunatoa tahadhari kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kutoruhusu kabisa kuendelea kwa mjadala huu kama ambavyo tumekuwa tukiomba mara kwa mara kwa nyakati tofauti zilizopita,” linasema tamko hilo.

Pamoja na hilo, maaskofu hao walimtaka Waziri Membe, kujiuzulu wadhifa wake kutokana na hatua yake ya kujenga ushawishi wenye mwelekeo wa kidini wa kuiingiza nchi katika OIC.

Mbali ya hayo, tamko lilisema kuwa hatua ya Tanzania kujiunga OIC inakwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 19 (2) na Sheria ya Vyama vya Siasa nchini.

Askofu Kitula alisema, wanapinga Tanzania kujiunga na OIC kwa maelezo kuwa, katiba ya jumuiya hiyo imejipambanua wazi kuwa na malengo ya kuendelea na kuulinda Uislamu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa, lenye watu wa imani nyingine za dini.

Akifafanua askofu huyo alisema, katika Ibara ya 1 (11) ya Katiba ya OIC, kuna kipengele kinachosomeka ‘kusambaza, kuendeleza na kuhifadhi mafundisho ya dini ya Kiislamu….kuendeleza utamaduni wa Kiislamu na kuulinda urithi wake’, maelezo ambayo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ambayo inahimiza uhiari na uhuru wa mtu binafsi katika masuala yanayohusu kueneza dini au masuala ya imani.

Askofu Kitula ambaye alisoma tamko hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCT, Akofu Donald Mtetemela, aliyesaini tamko hilo, alisema uamuzi wa kujiingiza katika masuala ya namna hiyo ni wa hatari, kwani yanaweza kuleta migogoro kutokana na kuwapo kwa dhana ya udini.

Maaskofu hao walimtaka Waziri Membe kuachana na kauli zake juu ya umuhimu wa kuingia kwenye jumuiya hiyo ya Kiislamu na kuhoji aliyemtuma kufanya hivyo.

CHANZO:Tanzania Daima

29 Oct 2008

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Dar es Salaam limewaonya maaskofu wa Jumuiya za Kikristo Tanzania (CCT) kutoitisha Serikali katika suala la kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu (OIC) na kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini wakitishia kuwa kitendo hicho ni uhafidhina na ugaidi. 

Tamko hilo limetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Mussa Salum kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mara baada ya kikao cha masheikh na maimamu wa mkoa huo kujadili pamoja na mambo mengine, kauli ya maaskofu hao. 

"Waislamu tunasema suala la Tanzania kujiunga ama kutojiunga ni suala la Serikali ya Tanzania kwa maslahi ya wananchi wote," alisema Sheikh Salum. 

Sheikh Salum aliongeza kuwa suala la Mahakama ya Kadhi ni haki ya Waislamu wa nchini na wala halina mjadala kwa kuwa haliwahusu watu wa dini nyingine na kwamba mifano mingi ipo katika nchi mbalimbali juu ya kuwepo kwa mahakama hizo. 

"Mahakama hizi zilikuwepo tangu ukoloni, hivyo hili siyo suala la kuomba kuanzishwa kwake bali tunaiomba Serikali izirejeshe," alisema. 

Pia masheikh na maimamu hao walihoji uhalali wa kuwepo kwa Balozi wa Vatican hapa nchini kuwa anawakilisha nchi gani na kuliita kuwa suala hilo limegubikwa na udini lakini Waislamu hawakuwa wakihoji. 

"Tunawaonya maaskofu kuacha kuishinikiza Serikali mara kwa mara kuhusu masuala yanayohusu Waislamu na waache kupandikiza chuki kwa waumini wao juu ya suala la OIC na Mahakama ya Kadhi na waumini wa dini ya kiislamu kwa ujumla," alisema. 

Mwishoni mwa wiki iliyopita maaskofu 64 wa makanisa mbalimbali nchini walisaini waraka wa kumpinga Waziri Membe aliyekaririwa awali akiwataka Watanzania kutoogopa kujiunga na OIC kwani ni jumuiya yenye maslahi mazuri ya kiuchumi kwa taifa, akikariri utafiti uliofanywa na Serikali. 

Tayari BAKWATA makao makuu imeshatangaza kuitisha mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu kesho kueleza msimamo wake kuhusu suala hilo.

CHANZO: Majira

27 Oct 2008


CCM haihusiki na OIC-Msekwa

27 Oct 2008
By Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeukana mpango wa Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) na kusema kwa hilo vyombo vya habari na maaskofu wanakionea. 

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, alisema suala la kujiunga na OIC limo mikononi mwa Serikali na CCM haihusiki. 

``Mbona mnanionea jamani, kwa kweli kuniuliza juu ya jambo hili mnatuonea. Suala la kujiunga na OIC sio la CCM na wala aliyesema maneno hayo sio mimi wala kiongozi wa Chama,`` alisema. 

Pamoja na Msekwa kuukana mpango huo, lakini maamuzi makubwa yanayohusu nchi hayawezi kuamuliwa na serikali bila chama tawala kutoa baraka zake. 

Hata hivyo, Msekwa alisema hawezi kuingia kwa undani kujibu kauli iliyotolewa na maaskofu 58 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwamba watauangalia upya uhusiano wao na Serikali pamoja na Chama tawala, iwapo mipango wa kuiingiza nchi katika jumuiya hiyo pamoja na kuruhusu kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi itaendelea. 

Alisema hawezi kuamini kwamba ni kweli maaskofu walitoa kauli hiyo, kwa vile katika mkutano huo yeye hakualikwa na wala hakuhudhuria. 

Alipoulizwa kwamba Serikali inaweza kuchukua uamuzi mkubwa kama huo (wa kujiunga na OIC) bila kupata baraka ya Chama tawala, Msekwa alizungumza kwa hasira huku akilalamika kwamba maswali hayo yana lengo la kumuonea. 

Hivi aliyetoa kauli ya OIC ni mtendaji wa Serikali au mtendaji wa CCM? alihoji na kuongeza: Unataka ufafanuzi juu ya uhalali au ubaya wa hicho unachouliza, tafadhali muoneni huyo huyo aliyesema, Chama hakihusiki, mbona mnaendelea kunisakama kwa jambo nisilolijua. 

Msekwa alisema anaamini Serikali ina majibu mazuri na yenye uhakika kwa vile haiwezi kufanya jambo ambalo halina maslahi. 

Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Kamillius Membe, aliwaambia waandishi wa habari kuwa suala la kujiunga na OIC halina madhara kwa taifa. 

Kauli hiyo iliamsha wasikwasi wa maaskofu ambao licha ya kukemea kauli ya Membe na kumtaka ajiuzulu, pia walisema kitendo hicho ni uvunjaji wa Katiba ya nchi na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa. 

Hata hivyo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lilipinga kauli ya maaskofu kwa kupitia kwa Kaimu Mufti, Sheikh Suleiman Gorogosi, kuwa inalengo la kupotosha. 

Wakati huo huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeunga mkono mpango wa Serikali ya Muungano wa Tanzania wa kutaka kujiunga na OIC kwa kuwa itasaidia juhudi za kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wake. 

Tamko hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alipokuwa akizungumza mjini Zanzibar baada ya kujitokeza kwa tofauti kati ya taasisi za kidini dhidi ya uamuzi wa Serikali ya Muungano. 

``Zanzibar tunaunga mkono uamuzi wa Serikali ya Muungano wa kufikiria Tanzania kujiunga na OIC kwa vile suala hilo halihusiani na mambo ya dini na litanufaisha jamii katika ustawi wa maendeleo, alisema Hamza. 

Alisema ndio maana Zanzibar imekuwa ikitetea kila mara Tanzania ijiunge na Jumuiya hiyo kwa vile misaada na mikopo inayotolewa na OIC ikiwemo miradi ya elimu na huduma za kijamii itanufaisha Watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za imani ya dini. 

Alisema kuna mataifa mengi yaliyojiunga na Jumuiya hiyo licha ya nchi hizo kuwa na waumini wachache wa dini ya kiislamu na kuzitolea mfano nchi hizo kuwa ni Uganda na Msumbiji ambazo tayari zimeshanufaika na mfuko wa maendeleo wa OIC katika sekta za elimu, afya na viwanda. 

Akizungumiza suala laMahakama ya kadhi,, Waziri Hamza alisema wananchi waondoe hofu kwa vile mahakama hiyo si jambo geni kutokana na mfumo huo kuwepo visiwani Zanzibar bila ya kuathiri madhehebu mengine ya dini. 

Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengodo Mvungi, amesema kunahitajika meza ya mazungumzo itakayokutanisha makundi yote ya Watanzania kujadili masuala mazito yanayowakabili kama kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na la kujiunga na OIC. 

Akizunguza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mvungi alisema malumbano yaliyozuka hivi karibuni, na ambayo bado yanaendelea yanaonyesha dalili mbaya kwa mustakabali wa kitaifa. 

Alisema matatizo yaliyopo nchini, yanasababishwa na mambo mengine, lakini lililokubwa zaidi ni ile tabia ambayo imejengeka nchini kwamba hakuna anayetaka kumsikiliza mwenzake. 

``Hoja kama OIC au Mahakama ya Kadhi zinatakiwa zijadiliwe kwa lugha ya utaifa, pande zote zinazohusika zikutane, zikae pamoja na zijadiliane kwa maslahi ya kitaifa, tuache pembeni dini zetu, kabila zetu na koo zetu,`` alisema na kuongeza ``Katika mambo mazito kama yanayoendelea nchini lazima utaifa utangulizwe mbele, vinginevyo tutaishia kulumbana na kugombana lakini hatutapata jawabu la matatizo yetu, alisema. 

SOURCE:Nipashe

26 Oct 2008


Moja ya matokeo (findings) katika utafiti wangu wa shahada ya uzamifu (ambao unahusu harakati za Waislamu nchini Tanzania) ni mtizamo wa asilimia kubwa ya Waislamu kwamba hawatendewi haki.Wapo wanaoona kuwa chanzo cha tatizo hilo ni sera za mkoloni (hawa si wengi),wengine wanaliona Kanisa Katoliki kama chanzo,huko wengine wakiilaumu serikali.Makundi hayo yako more complicated than nilivyoeleza.Kuna wanaohusisha ukoloni na ukristo,hivyo upinzani dhidi ya uislamu.Kuna wanaouona ukoloni kama mfumo wa kibaguzi (hapo ni siasa zaidi kuliko dini).Na kwa wanaolilaumu kanisa katoliki (au tuseme Wakristo),baadhi wanamwona Mwalimu Nyerere kama kibaraka wa Kanisa,wengine wanawatuhumu viongozi watengeneza sera hasa waliosomeshwa na kanisa (seminari) kuwa wanalitumikia kanisa indirectly.As to lawama kwa serikali,wengi wanaoiona kama inatumiwa na kanisa (hao ni wengi),na wanatuhumu baadhi ya viongozi wa serikali ambao ni waislamu kuwa wanatumika aidha kwa tamaa zao za kidunia au kwa vile hawana jinsi (mtumikie kafiri upate mtaji wako).Kwa kifupi,manung'uniko ya waislamu yalikuwepo wakati wa ukoloni (hasa kutokana na sera za kikoloni),yalikuwepo mara baada ya uhuru (japo hayakuonekana kutokana na siasa zilizozuia uhuru wa kujieleza) na yamejidhihirisha zaidi baada ya mageuzi ya miaka ya 80.Moja ya matatizo ya msingi ni ukimya wa policy makers katika at least ku-acknowledge existence ya manung'uniko hayo na dhamira thabiti ya kuyafanyia kazi.Kutambua kuwapo kwa tatizo ni hatua muhimu katika kulitafutia ufumbuzi.

Si nia yangu kutoa summary ya matokeo hayo hapa (nataraji kuchapisha kitabu baada ya kumaliza ngwe iliyobaki) bali lengo langu ni kuonyesha wasiwasi katika masuala mawili,kuanzishwa kwa mahakama za kadhi na Tanzania kujiunga na OIC,kwamba pasipo umakini nchi yetu itaelekea kubaya (I hope hapa sintaitwa mchochezi).Tayari viongozi wa kidini upande wa Wakristo wameeleza bayana upinzani juu ya masuala hayo.Viongozi wa Waislam nao wameeleza bayana kuchukizwa kwao na upinzani wa wenzao viongozi hao wa Wakristo,huku wakitarajia kuwa kinachosubiriwa ni utekelezaji tu.

Naomba kuweka wazi kuwa uchambuzi huu mfupi unafanyika kitaaluma,na hauhusiani na imani yangu kama Mkristo.Ni wazi kwamba hoja za kadhi na OIC zimekuwa zikitumiwa vibaya na wanasiasa,na wao ndio waliotufikisha hapa.Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 katika Sura ya Nane,Kipengere 108 (b) inaeleza dhamira ya chama hicho kulipatia ufumbuzi suala la kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi Tanzania Bara.Kwa kutotoa ufumbuzi huo hadi zaidi ya nusu ya muhula wake madarakani,yayumkinika kuhitimisha kuwa suala hilo liliingizwa kwenye Ilani aidha pasipo kufanyika utafiti wa kutosha au kwa madhumuni ya kupata kura za Waislamu.Kama ambavyo baadhi ya findings za utafiti wangu zinavyoonyesha,ukimya katika masuala yanahohitaji ufafanuzi au maamuzi unachangia sana kuelta mkorogani kwa wadau wa mambo hayo.Wanaodhani kwamba kwa suala hili litapotea kwa kukaa kimya,sio tu wanajidanganya bali pia wanaiweka nchi yetu mahala pabaya.

Kuhusu suala la OIC,again, kauli za wanasiasa ambazo hazilengi kutoa ufumbuzi wa matatizo bali kuyaahirisha kwa kuahidi "mchakato" (Man,I really hate this word) ndio zimetufikisha hapa tulipo.Kama hoja ilikuwa ni mchakato,then why not kufanya huo mchakato kabla ya kukurupuka kuongea as if maamuzi yameshafanyika?Kuna mfano unaotolewa mara kwa mara kuhusu uanachama wa Uganda kwenye OIC.Does it mean kila wanachofanya Waganda lazima nasi tufanye?Binafsi nisingependa kusema hapa kwamba naunga mkono au napinga Tanzania kujiunga na OIC (nina sababu zangu za msingi kitaaluma) lakini busara nyepesi tu ingeweza kutumika katika the so-called mchakato:kuwa honest kwa Watanzania pasipo kujali imani zao.Honesty nayozungumzia hapa ni pointi kama je Watanzania wanahitaji uanachama wa OIC?Nasema Watanzania na sio Waislamu au Wakristo kwa vile katiba inasema nchi yetu haina dini,ila wananchi wana dini.Tatizo la OIC ni la kikatiba zaidi kuliko kisiasa,na ilipaswa wanaolizungumzia walioanishe na vifungu husika vya katiba.Unfortunately,katiba yetu nayo ni sehemu ya matatizo yanayotukabili.

Kwa kuhitimisha,naomba akili na busara itumike katika kuyashughulikia masuala haya mawili.Let's put common sense infront of emotions.Kwa bahati mbaya,masuala ya imani yana tabia ya kuwafanya wahusika kuwa emotional.Ni muhimu pia kwa wanasiasa wetu kuweka mbele maslahi ya taifa na sio ya kufurahisha nafsi zao au kuwafurahisha watu wachache.It can be done,tukiweka mbele maslahi ya umoja,mshikamano,upendo na utaifa wetu. 

24 Oct 2008


Na Peter Edson
JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT) imemuonya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwa kauli zake kuhusu kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) zinaweza kusababisha mgawanyiko wa kitaifa na kumtaka aachane nazo au ajiuzulu wadhifa wake.

Tamko hilo la maaskofu wa makanisa ya Kikristo imekuja baada ya Waziri Membe kukaririwa akisema kuwa hakuna athari zozote kwa Tanzania kujiunga na taasisi hiyo, ambayo madhumuni yake ni kutetea binadamu na hasa Waislamu na sehemu takatifu.

Membe alisema hakuna haja ya kuwa na woga wa kujiunga na taasisi hiyo wakati katika mchakato wake wakristo na waislamu watanufaika na miradi itakayokuwa ikisimamiwa na OIC, na akashangaa ujasiri wa Watanzania wa kupambana na matatizo umekwenda wapi kiasi cha kuogopa nchi kujiunga na jumuiya hiyo.

Suala hilo liliwahi kuibuka mwishoni mwa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi wakati vyombo vya habari vilipofichua kuwa serikali ilijiunga kinyemela na jumuiya hiyo. Baadaye viongozi wa serikali walikiri kufanya hivyo kabla ya kujiondoa, lakini safari hii upinzani umekuwa mkubwa zaidi.

Wakitoa tamko lao kwa waandishi wa habari jana, maaskofu hao kutokana makanisa ya kiprotestanti walisema kauli ya Waziri Membe ina lengo la kutetea maslahi ya watu wachache.

Maaskofu hao walisema kwa kuwa katiba ya OIC hiyo inaeleza bayana kuwa italinda mila, desturi na tamaduni za kiislamu, kujiunga na jumuiya hiyo itakuwa ni kukiuka katiba ya nchi inayoeleza kuwa dini ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na kwamba shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchini.

"Kama serikali ikikubali, kutakuwa ni mwanzo wa kuruhusu kubomoka na kuvunjika kwa amani ya nchi kwa sababu yanagusa hisia na itikadi za wananchi," alisema Askofu Peter Kitula, ambaye ni makamu mwenyekiti wa kwanza wa CCT.

Askofu Kitula, ambaye alisoma tamko hilo la maaskofu, alisema baada ya kutafakari kwa roho ya kiutume na kinabii wameamua kupinga kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi pamoja na mchakato wa kujiunga na OIC.

Alisema katiba ya Tanzania ibara ya 19 kifungu cha 2 inaeleza wazi kuwa kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchini.

"Ibara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha kwamba mambo ya dini yanatenganishwa kabisa na shughuli za uendeshaji wa nchi," alisema.

Alisema sehemu hiyo ya katiba inapingana na ibara ya 1 kifungu cha 11 ya katiba ya OIC kinachosema kuwa jumuiya hiyo inatetea mila, tamaduni na desturi za kiislamu, kuwalinda na kuwaelimisha wananchi kuhusu uislamu nchini, jambo ambalo askofi huyo alisema linaonyesha wazi kuwa kujiunga na IOC itakuwa ni ukiukwaji wa katiba.

Alisema siku za hivi karibuni Bunge la Jamuhuri ya Muungano limekuwa likijadili miswada ya sheria ya kuanzisha au kujihusisha na vyombo hivyo viwili, lakini akasema kuwa kushinikiza kukubalika kwake ndani ya bunge ni kwenda kinyume na katiba.

Naye Owdernburg Mdegela, askofu wa dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutherani Tanzania (KKKT), alisema kitendo cha Waziri Membe kulizungumza jambo hilo bila kulionea haya ni kutetea maslahi ya watu wachache na kuvunja katiba.

Alisema Tanzania ina rasilimali za kutosha hivyo kujiunga na umoja huo kwa lengo la kutafuta misaada ama kutafuta kula na baadaye kupoteza mwelekao wa taifa, ni kujiingiza katika mtego ambao kujinasua kwake kunahitaji gharama ambayo ni kumwaga damu.

"Sisi tunasimama kama viongozi wa kanisa tukimwambia Membe kuwa hafai wadhifa huo, hivyo ni vema akaacha mara moja kutoa kauli zake zisizo na mantiki. Lakini kama hawezi, basi inampasa ajiuzulu," alisema Askofu Mdegela.

Naye askofu wa kanisa pentekoste, Sylivester Gamanywa alisema Waziri Membe anatoa kauli ambazo zina lengo la kuweka hisia binafsi na mgawanyiko wa kitaifa pamoja na kuvunjika kwa amani.

Alisema kitendo cha waziri huyo kusema kuwa serikali inaruhusu fedha chafu na kwamba kama mtu akikuta fedha za shetani inampasa kuzichukuwa, ni kuwadhalilisha Watanzania na taifa lao kwa ujumla.

Naye askofu wa Anglikana, Dk. Stephen Munga alisema kuwa waziri Membe hafai katika kushughulikia masuala ya kitaifa kwani hakuna mamalaka yoyote iliyomuagiza aende kuzungumzia suala la kuaanzishwa kwa OIC.

"Inampasa Waziri Membe afahamu kuwa sisi ni Tanzania na tutafuata mambo yetu na si kuiga masuala ya nje. Anavyosema tuwaige Waganda si jambo sahihi," alisema Dk. Munga.

Alisema kama kanisa msimamo wao ni kuyakataa mambo hayo mawili na kuitaka Serikali na mamlaka zake zote kuacha kuendelea kukaribisha mijadala ya mambo hayo kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda wa wenye dhamana ya mamlaka ya nchi hii na rasilimali zake.

"Tunauhakika kuwa yaliyomo ndani ya OIC ni hatari kabisa, kwani endapo yakikubalika katiba ya nchi itakuwa imevunjwa na Watanzania watakuwa wameingia katika migogoro itakayoua maridhiano, mshikamano, utengemano na umoja wa kitaifa," alisema Askofu Kitula.

"Kwa kuzingatia wajibu wetu wa kinabii na kiutume, tunatoa wito kwa bunge kutoruhusu kamwe uanzishwaji wa mahakama ya kadhi kwa kupitia mchakato wa utendaji wa mamlaka ya nchi, pia kutoridhia uanachama wa Tanzania katika OIC."

Akizungumzia tamko la maaskofu, mwenyekiti wa kamati ya msikiti wa Idrissa, Sheikh Ally Basaleh alisema kuwa awali kabla ya kuanza kwa mchakato wa masuala hayo serikali ilishafanya uchambuzi wa kina na kugundua umuhimu wa kuanzishwa kwa vyombo hivyo.

"Kauli za maaskofu hawa na viongozi wa kanisa zinadhihirisha kuwa wanakataa maamuzi yao ya awali kwamba Rais Jakaya Kikwete ni mteule wa Mungu, kwani ndiye anayesimamia masuala haya yote," alisema Basaleh.

Alisema waislamu ni sehemu ya jamii hivyo wao kama viongozi wa dini wanaandaa mchakato wa kutoa tamko litakalokuwa likitoa mchanganuo kuhusu uhalali wa kuanzishwa kwa vyombo vyote hivyo viwili nchini.
CHANZO: Mwananchi


Soma kwa makini stori hizi kisha make your own conclusion

STORI YA KWANZA:
Waziri Membe akana kuubeba msalaba OIC
Na Ramadhan Semtawa
WAZIRI wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernad Membe, amekuja juu akisema baadhi ya watu wamekuwa wakimtwisha mzigo kwamba, ameingiza Tanzania katika Jumuiya ya nchi za Kiislam Duniani (OIC), kitu ambacho si kweli.

Kauli hiyo ya Membe ni ya kwanza kuitoa hadharani tangu kuibuka kwa kasi kwa mjadala huo, ambao unaonekana kuigawa nchi katika misingi ya kiitikadi.

Akizungumzia hilo jijini Dar es Salaam jana, Membe alisema si kweli kwamba Tanzania imekwishajiunga na OIC na wala yeye hajasema lazima ijiunge.

Membe akifafanua huku akionekana kuguswa na tuhuma hizo dhidi yake kutokana na kutamka hilo bunge katika hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema uamuzi wa kujiunga au la, uko kwa wananchi.

"Nimekuwa kimya, kuachia na kusikiliza watu waseme, jamani, Tanzania haijajiunga na OIC wala sijasema lazima ijiunge," alisema na kuongeza:

"Uamuzi wa kujiunga au kutojiunga utakuwa chini ya wananchi, wasomi, NGOs na ninyi waandishi wa habari, ndiyo mtakaoamua."

Membe alikuwa akifafanua kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Iran, ambao unaonekana na baadhi ya watu kama wenye nia ya kuingiza nchi OIC.

Akifafanua zaidi, alisema watu wasiingize vitu visivyokuwa na msingi kwa ajili ya kutunga na kuzungumzia hisia, na kushauri wasome historia kufahamu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Membe huku akionekana kuchukizwa na fikra mbovu za kupandikiza udini katika nchi, alisema Watanzania ni watu wanaoheshimika duniani kwa umakini wao, ni aibu na haipendezi kujadili udini.

Alisema kama ni kujiunga na OIC ni jambo la kuamua, kwani Uganda ambako kuna Waislam asilimia 10 imeweza kujiunga huku Wakristo wakiwa ni asilimia 66 na wengine wapagani.

"Sasa jamani, msitake kunichinganisha na watu wangu, nawaambieni tena na tena, Tanzania haijajiunga na OIC na haitaweza kujiunga uamuzi huo ni ridhaa ya wananchi," alisisitiza.
CHANZO: Mwananchi

STORI YA PILI KUHUSU SUALA HILOHILO:
Waziri: Tanzania kujiunga OIC ni dhahiri
23 Oct 2008
By Muhibu Said

Tanzania inatarajia kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) wakati wowote katika siku zijazo baada ya serikali kuweka bayana azma hiyo jana.

Azma hiyo ya serikali iliwekwa bayana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi, alipozungumza na Nipashe jana, ikiwa ni wiki chache tangu Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe, aliambie Bunge kwamba, hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na jumuiya hiyo.


Balozi Iddi alisema mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC, unatarajiwa kuanza wakati wowote na kwamba, hatua ya mwanzo ya mchakato huo, viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano watakutana na wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa ajili ya kupata msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo.

Naibu Waziri huyo alisema hayo alipoulizwa na Nipashe kama mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC umeshaanza au la tangu Waziri Membe atoe kauli hiyo bungeni, mjini Dodoma, Agosti 22, mwaka huu.

``Bado hatujaanza mchakato. Kuna kikao tunachotaka kwanza kufanya kwa ajili ya kushauriana na wenzetu wa Zanzibar ili tuwe na msimamo mmoja kuhusu hilo. Ilikuwa tuanze sasa, lakini Mheshimiwa Waziri (Membe) hayupo na Bunge linatarajiwa kuanza,`` alisema Balozi Iddi.

Alisema mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC ni mrefu, ambao unatarajiwa pia kulishirikisha Baraza la Mawaziri kufikia maamuzi.

Balozi Iddi alisema hatua nyingine ya mchakato, ambayo serikali inatarajia kuichukua, ni kutoa elimu kwa umma ili kuwaondoa uoga wote walioonyesha hofu iwapo Tanzania itajiunga na jumuiya hiyo.

``Hao wanaopinga, ni waoga tu, hawajaeleweshwa kwani haina maana Tanzania itakuwa nchi ya Kiislamu. Zipo nchi kama vile Uganda zimejiunga na OIC, lakini hazijabadilika kuwa nchi za Kiislamu. Tutawaelewesha wakati ukifika, tunavyo vyombo vya kuelimisha hilo,`` alisema Balozi Iddi.

Agosti 22, mwaka huu Waziri Membe wakati akifunga mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na IOC.

Waziri Membe alisema serikali mwaka huu, ilifanya kikao na Baraza la Wawakilishi kuhusu suala hilo na kugundua kuwa nchi 21 zimejiunga na jumuiya hiyo.

Alisema kati ya nchi hizo, zimo pia nchi za Wakristo ambazo zimejiunga na hazijapata madhara yoyote.
``Tumeshakusanya takwimu za nje na kuona hakuna madhara yoyote ya kujiunga na IOC, bora tu kufuata taratibu,`` alisisitiza Waziri Membe.

Alisema suala hilo lilileta utata awali kwa sababu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, marehemu Ahmed Hassan Diria, alipeleka ombi la Zanzibar kujiunga kwenye jumuiya hiyo bila kuishirikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, alisema suala hilo limefanyiwa kazi na serikali na kuona kuwa hakuna madhara kujiunga na IOC.

Siku chache baada ya Waziri Membe kutoa kauli hiyo bungeni, viongozi wa makanisa na baadhi ya wasomi, akiwamo Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Dk. Methodius Kilaini, walipinga vikali kauli hiyo ya serikali.

Wengine waliopinga suala hilo, ni Askofu Stefano Msangi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT Tanzania, Dk. Alex Malasusa, Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengodo Mvungi.

Hata hivyo, Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mnyamani, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Sheikh Mohammed Iddi, amekuwa akijitokeza kuwapinga maaskofu kuhusu kauli zao za kupinga suala hilo.
CHANZO:Nipashe

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.