25 Nov 2008

Picha kwa Hisani ya MICHUZI.

Fuatilia latest kuhusu ishu hiyo kwa kuBONYEZA HAPA

UPDATED:
Mramba, Yona waenda rumande kwa ufisadi
*Wakosa dhamana ya Sh7.8bn, waenda rumande na kandambili
James Magai na Paulina Richard

MAWAZIRI wawili waliowahi kuongoza wizara mbalimbali ikiwamo nyeti ya fedha katika serikali ya awamu tatu, Basil Mramba na Daniel Yona wamefikishwa kortini kwa matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.

Kufikishwa kizimbani kwa mawaziri hao kunaashiria mwanzo wa utekelezaji wa ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali na watendaji wake kuwa itashughulikia vigogo wote wanaotuhumiwa na ufisadi baada ya wananchi wengi kutoridhishwa na ukubwa wa majina ya watu walioshtakiwa katika kashfa ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Ni wiki iliyopita tu wakati Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah alipotangaza kuwa muda mfupi ujao vigogo wanaohusika kwenye kashfa mbalimbali za ufisadi watafikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Na hali ilikuwa hivyo jana wakati habari zilipozagaa asubuhi kuwa Mramba na Yonah wangepandishwa kizimbani na hivyo kufanya watu waliopata fununu hizo kujazana mahakama ya Kisutu.

Wawili hao walikuwa wameshafika mahakamanio hapo majira ya saa 2:45 asubuhi, wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser VX, lenye rangi ya kijani na mistari ya rangi nyekundu na nyeupe ubavuni lenye namba za usajili T319 ATD.

Lakini namba za gari zilizokuwa katika kisahani cha namba (Plate number) zilikuwa tofauti na zilizokuwa katika vioo vya gari hilo ambazo ni T 562 AJK.

Lakini hawakushuka kwenye gari hilo lililokuwa na vioo vya giza, hadi walipotakiwa kwenda kizimbani.

Mramba na Yona walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana mbele ya Hakimu Hezron Mwankenja saa 5.40 na wakasomewa mashtaka na baadaye kupelekwa rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Vigogo hao walifikishwa mahakamani baada ya uvumi wa tukio hilo kudumu kwa takribani majuma mawili.

Wakati wakiingia mahakamani jana Mramba, ambaye ni mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 1200 ya mwaka huu, alisikika akiwahoji waandishi iwapo wamefurahi kufikishwa kwao mahakanai hapo, huku akidai kuwa watapiga picha nyingi sana kwa kuwa huo ni mwanzo tu.

Watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka matano ya pamoja, baadaye Mramba akasomewa manane zaidi peke yake, na kufanya akabiliwe na jumla ya makosa 13.

Mwendesha mashtaka ambaye ni wakili wa serikali, Stanslaus Boniface aliyataja makosa yanayowakabili wote kwa pamoja kuwa ni matumizi mabaya ya ofisi kwa kuiruhusu kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers ya Uingereza kuingia mkataba wa kudhibiti madini ya dhahabu kinyume cha sheria.

Boniface alifafanua kuwa kati ya Agosti 2002 na Juni 14, 2004 watuhumiwa wakiwa katika nafasi za uwaziri wa fedha na uwaziri wa Nishanti na Madini waliruhusu kampuni hiyo na mshirika wake, M/S Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation kusaini mkataba wa kudhibiti madini ya dhahabu kinyume cha sheria ya Manunuzi ya Umma na ya Madini.

Katika kosa la pili, Boniface alidai kuwa Mei 28, 2005 watuhumiwa hao walitumia vibaya madaraka yao kuingia mkataba wa nyongeza wa miaka miwili kwa kampuni hiyo kuanzia Juni 14, 2005 hadi 23 Juni 2007 kinyume cha sheria ya Manunuzi ya Umma na ya Madini.

Katika kosa la tatu Boniface alidai kuwa kati ya Machi 28 ,2005 na Mei 28,2005 watuhumiwa wakiwa watumishi wa umma walitumia vibaya madaraka yao kwa kumwalika Dk Enrique Segura wa kampuni hiyo kurasimisha mkataba huo wa nyongeza ya muda kabla ya mazungumzo na timu ya serikali kushughulikia suala hilo.

Boniface aliendelea kuieleza mahakama kuwa katika kosa la nne kati ya Machi 2005 na Mei 28, 2005 watuhumiwa waliachia suala la udhibiti wa madini lifanywe kienyeji bila kumshirikisha mwanasheria wa serikali kama ilivyopendekezwa na timu ya mazungumzo ya serikali, jambo lililosababisha ongezeko la muda wa mkataba huo wa miaka miwili.

Na katika kosa la tano ambalo lilimhusu mshitakiwa wa kwanza, Mramba, Boniface alidai kuwa Oktoba 10 Mramba alitumia vibaya mamlaka yake kwa kudharau ushauri wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wa kutotoa msahama wa kodi kwa kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Busines Corpotion.

Katika kosa la sita ambalo pia linamhusu Mramba peke yake Boniface alidai kuwa kati ya Desemba 18 na 19, 2003 Mramba akiwa Waziri wa Fedha alitumia vibaya mamlaka yake kwa kutoa Tangazo la Serikali (GN) la mwaka 2003 lilitoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo katika shughuli zake za usambazaji wa bidhaa na utoaji huduma kinyume cha mapekezo yaliyotolewa na TRA.

Boniface alidai kuwa kuanzia kosa la saba hadi la 11 ambayo karibu yote yanafanana ambapo Mramba akiwa waziri wa fedha anadaiwa kutoa msahama wa kodi ya mapato kwa kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kutumia madaraka yake kutoa GN namba 424 /2003 na 497/2004 kati ya Desemba 19, 2003 na Oktoba 15, 2004 kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Katika kosa la 12 ambalo linawahusu watuhumiwa wote wawili, Boniface aliendelea kudai kuwa watuhumiwa hao wakiwa mawaziri kwa makusudi na kwa kutokuwa makini waliruhusu makataba ambao uliipa upendeleo kampuni hiyo na kuisababishia serikali hasara ya Sh 11,752,350,148.00.

Na katika kosa la 13 ambalo pia linamhusu Mramba peke yake Boniface alidai kuwa Mramba akiwa waziri wa fedha kati ya 2003 na 2007, alishindwa kuchukua tahadhari katika, kutoa matangazo ya serikali namba GN 23/2003, 424/2003, 497/2004, 498/2004 , 377/2005 na 378/2005 yaliyolenga kusaidi kampuni hiyo kutolipa kodi na hivyo kuisababishia serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.

Watuhumiwa wote walikana makosa hayo na mawakili wao kuomba dhamana huku upande wa mashtaka ukisema kuwa hauna pingamizi.

Pamoja na maombi hayo ya dhamana, mmoja wa mawakili wa utetezi Tadayo alimuomba Hakimu Mwankenja atoe masharti nafuu kwa wateja wao akidai kuwa suala hilo limekuwa likipelelezwa kwa zaidi ya miaka mitatu na walitoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kufika mahakamani hapo bila kukamatwa.

“Hivyo hakuna hofu kuwa wanaweza kukimbia,” alisisitiza Tadayo na kumuomba hakimu azingatie sehemu ya pili ya sheria ya dhamana ya watuhumiwa kutoa nusu ya fedha wanazodaiwa kuiba au hati ya mali yenye tahamani sawa na nusu ya fedha hiyo.

Hata hivyo, akitoa masharti ya dhamana Hakimu Mwankenja alitupilia mbali ombi la mawakili hao la kuwataka washtakiwa kuwasilisha hati ya mali na badala yake watoe pesa taslimu Sh3.9 bilioni kila mmoja.

Pia aliwataka wawasilishe hati zao za kusafiria na kutokutoka nje ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kuwa wadhamini wawili waliothibitishwa na mahakama.

Mwankenja aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2 itakapotajwa tena na kuwataka washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi hapo watakapotimiza masharti hayo.

Mara baada ya kesi hiyo kuahirishwa mamia ya watu waliofurika mahakamani hapo kiasi cha kujaa ndani na nje ya ukumbi wa mahakama waliwafuata mlango wa nyuma wa mahakama hiyo lilikokuwa gari walilokwenda nalo mahakamani hapo na kuwasubiria.

Wakati washtakiwa hao wakiingia ndani ya gari hilo na kuondoka mahakamani kupelekwa mahabusu, wananchi waliwazomea kwa kuimba wimbo wa “wezi, wezi hao huku wengine wakitaka hata kuwamwagia mchanga ndani ya gari hilo.

Wakati hayo yakiendele baadhi ya ndugu wa watuhumiwa hao walikuwa wakilia kimyakimya na kujifuta machozi huku wakiwa wameshikilia viatu vya washtakiwa hao mikononi na kuwaangalia wakiondoka na kanda mbili ambazo waliwanunulia mahakamani hapo.

Mapema saa 2: 45 waandishi wa Mwananchi walipofika mahakamani hapo waliwakuta watuhumiwa wakiwa wamekwishafika mahakamani hapo huku wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Landcruiser VX, lenye rangi ya kijani na mistari nyekundu na nyeupe ubavuni lenye namba za usajili T319 ATD.

Lakini namba za gari zilizokuwa katika kisahani cha namba (Plate number) zilikuwa tofauti na zilizokuwa katika vioo vya gari hilo ambazo ni T 562 AJK.

Watuhumiwa hao waliendelea kukaa ndani ya gari hilo na walipoteremka moja kwa moja walipandishwa kizimbani.

Kitendo cha watuhumiwa hao na kuendelea kubaki ndani ya gari hata baada ya kufika mahakamani hapo kiliwashangaza wengi na kufanya wajiulize maswali kuwa iweje wao wasishuke ndani ya gari na kuingizwa katika chumba maalumu cha mahabusu wakati wakisubiri kupandishwa kizimbani kama ilivyo kawaida kwa watuhumiwa wengine.

Mramba alikuwa amevalia kaunda suti yenye rangi ya kijivu na viatu vyeusi, mshirika wake, Yona akiwa amevalia kaunda suti yenye rangi ya khaki na viatu kahawia
CHANZO: Mwananchi

HII INATIA MOYO SANA.LAKINI KIU YA WENGI ITAKIDHIWA KWA MAFISADI WA KAGODA NAO KUWEKWA HADHARANI NA HATIMAYE KUPANDISHWA KIZIMBANI.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.