18 Nov 2008

Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara mkoani Kilimanjaro (MUCCoBS) kimewatimua wanafunzi 595 wa mwaka wa kwanza kutokana na kuanzisha mgomo chuoni hapo. 

Aidha wanafunzi hao pamoja na mgomo huo,wametuhumiwa pia kuhatarisha maisha ya baadhi ya wanafunzi wenzao wa mwaka wa pili na wa tatu sambamba na wahadhiri chuoni hapo baada ya kuwamwagia mchanga na kuwarushia mawe wakiwa darasani. 

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Suleiman Chambo alisema jana kuwa kutokana na mgomo huo, menejimenti iliamua kuwasimamisha masomo wanafunzi hao kwa muda usiojulikana na umewataka wawe wameondoka chuoni hapo hadi kufikia jana saa 10 jioni. 

"Wanafunzi wa mwaka wa kwanza walipoona wenzao wa mwaka wa pili na tatu hawawaungi mkono waliamua kuwafuata madarasani na kuwamwagia mchanga na kuwarushia mawe huku mhadhiri mmoja akiwa darasani, Profesa Temba, ambaye alinusurika kipigo na ilimbidi kuingia chini ya meza ili kujinusuru," alisema. 

Aliongeza kudai kuwa wanafunzi hao hawana madai ya msingi na kwamba moja ya madai yao ni kuishinikiza Serikali kuwalipia mikopo kwa asilimia 100 huku madai mengine ni kuwaunga mkono wanafunzi wenzao katika vyuo vikuu vilivyofungwa. 

"Tumeamua kuwarudisha nyumbani kwa muda usiojulikana, na wakirudi waandike barua wathibitishe kulipa ada kwa asilimia 100, waombe kurudi chuoni na kufuata taratibu za chuo na walete vyeti vya kuonesha kwamba wana sifa za kurudia shahada wanayosomea," alisema. 

Alidai kuwa wanafunzi hao pia walitishia maisha ya Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Zamu Mlimila ambaye alilazimika kuokolewa na polisi baada ya wanafunzi kumzonga kwa lengo la kumshinikiza atangaze mgomo chuoni hapo.

CHANZO: Majira

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.