17 Nov 2008

Picha (ni kielelezo tu,haihusiani na habari) kwa hisani ya MJENGWA

WALIMU wanaofundisha katika shule zilizopo wilayani Monduli mkoani Arusha ambao waliajiriwa toka Julai mwaka huu, wapo katika hali mbaya kimaisha kiasi cha kufikia hatua ya kufanya kazi za kugonga kokoto ili kujikimu kimaisha.

Hali hiyo imetokana na walimu hao kutolipwa mishahara yao ya miezi zaidi ya minne toka waajiriwe, licha ya kusaini mkataba wa miaka mitano.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima, umebaini kuwa walimu walioathirika kwa kiasi na hali hiyo ni waliopo katika maeneo ya Loolkisare, Moita, Meserani Juu, Mto wa Mbu, Losomingo na Lepulko ambapo inadaiwa walimu hawana hata nauli ya kuwafikisha katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.

Akizungumza na Tanzania Daima, mmoja wa walimu hao, Goodluck Namoyo, alisema hali zao ni mbaya kifedha na wanajiandaa kukutana leo ili kujadili hatma yao.

Katika maeneo mengine ya Loolkisare na shule zilizopo vijiji vya mbali walimu wanaingia darasani kwa muda mfupi na muda mwingi wanatumia kufanya kazi za vibarua kwa kugonga kokoto ili kuwawezesha kupata angalau fedha za kujikimu.

Kaimu Afisa Elimu wa wilaya ya Monduli Emanueli Maundi, alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kuongeza kuwa walimu 40 hawajalipwa mishahara yao mpaka sasa na wao kama idara ya elimu, wamefanya jitihada kunusuru hali hiyo.

''Ndugu yangu mwandishi hivi tunavyoongea licha ya mweka hazina kuwasilisha majina ya walimu hao wizarani kwa muda mrefu sasa, hali bado ni tete na imemlazimu afisa elimu hiyo kwenda jijini Dar- es- salaam kushughulikia mishahara ya walimu hao kwani wana hali mbaya sana hivi sasa,'' alisema Maundi.

Naye katibu wa chama cha walimu wilaya za Monduli na Longido Godwin Mushi, alisema hali ya walimu hao inadhihirisha ni jinsi gani walimu hawathaminiwi kwani toka waajiriwe, hawajalipwa.

''Sidhani kama mwalimu huyo anaweza kumshauri ndugu yake yoyote apende kuwa mwalimu kutokana na hali aliyokumbana nayo yeye hivi sasa na hali hiyo ni hatari zaidi kwa siku za baadaye juu ya mustakabali wa elimu nchini, ''alisema Mushi.

Akizungumzia hali hiyo Mkaguzi wa Elimu wa Wilaya ya Monduli, Ernest Mwende, alisema kazi ya walimu kwa sasa ni ngumu kutokana na kupungua kwa thamani ya mwalimu.
CHANZO: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.