15 Nov 2008

Na Francis Godwin, Iringa 

SIKU moja baada ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoa wa Iringa kulazimika kutumia mabomu ya machozi kutuliza vurugu za wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), uongozi wa chuo hicho umetangaza kukifunga kwa muda usiojulikana. 

Uamuzi huo umeifanya idadi ya vyuo vishiriki vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vilivyofungwa hadi sasa kufikia vitatu. Awali Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kampasi kuu na juzi Chuo Kishiriki cha Elimu Chang'ombe vilifungwa kutokana na wanafunzi kugoma na kuandamana ndani ya vyuo hivyo wakipinga sera ya kuchangia elimu ya juu. 

Juzi majira ya saa 9 alasiri wanafunzi hao walianza kuwashinikiza wenzao kuanza mgomo usio na kikomo kwa lengo la kutaka kutimiziwa mikopo yote na serikali kwa asilimia 100. 

Kutokana na taarifa ya mgomo huo kuwa ya ghafla kwa wanafunzi hao baadhi yao waliamua kuendelea kujisomea katika vyumba vya madarasa hali iliyopelekea kundi hilo la wanafunzi wanaotaka wenzao wagome kuanza kuwashambulia kwa virungu na fimbo huku wakidai kuwa ni wasaliti wa mgomo huo. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja kati ya viongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji wa juu wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo alisema kuwa katika vurugu hizo za wanafunzi zaidi ya wanafunzi watatu wamejeruhiwa vibaya na kulazwa katika zahanati ya chuo kwa matibabu zaidi. 

Wanafunzi waliojeruhiwa ni Bw. Leslea Mkuchika, Bi Naima Kalaghe na Bi. Gloria Nyagawa ambapo Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo ya chuo, Bi. Iluminata Mbilinyi alisema kuwa wanafunzi hao wametibiwa na kuondoka katika eneo la chuo hicho kuelekea majumbani kwao. 

Barua ya kukifunga chuo hicho iliyosainiwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Prof. Rwekaza Mukandala na kubandikwa katika mbao za matangazo za chuo hicho iliwataka wanafunzi hao kuondoka mara moja chuoni hapo kwani wamekaidi amri ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Jumanne Maghembe ya kuwataka kusitisha mgomo huo. 

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia kundi la wanafunzi takribani 2000 waliokuwepo katika chuo hicho wakiondoka chuoni hapo kwa makundi. 

Pamoja na wanafunzi hao kukubali kuondoka chuoni hapo bado baadhi yao waliapa kuendelea na mgomo mpaka kieleweke iwapo Serikali haitakubali maombi yao ya kutaka kuondolewa kwa sera ya uchangiaji elimu. 

Naye Mwandishi Wetu Peter Masangwa anaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDASA) imeunda kamati ya watu watano kuchunguza kiini cha tatizo linalopelekea migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini mara kwa mara. 

Akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake Katibu wa UDASA Dkt. Deoscorous Ndoloi alisema tangu Bodi ya Mikopo ianzishwe imekuwa na migogoro na wanafunzi na kusababisha migomo isiyo ya lazima. 

Alionesha wasiwasi wake kuhusu uhalali wa sifa za kutolewa mikopo hiyo akisema wapo baadhi ya wanafunzi wamekasirika kuona mtu ambaye wanajua ana uwezo ndiye amefadhiliwa kwa asilimia 100 huku wale wasio na uwezo wakipewa asilimia 80 au 60 tu ya mkopo na kulazimika kutafuta vyanzo vingine kuweza kuendelea na masomo. 

Naye Mwandishi Wetu, Eckland Mwaffisi anaripoti kuwa siku moja baada ya kufungwa kwa muda usiojulikana, viongozi wa Serikali ya Wanafunzi kwenye Chuo Cha Ualimu Chang'ombe wameapa kuendeleza mgomo huo hata watakaporejeshwa iwapo madai yao hayatasikilizwa. 

Rais wa wanafunzi chuoni hapo, Bw. Ambege Uswege, alisema Dar es Salaam jana alisema, uamuzi wa kuwasimamisha masomo kwa muda usiojulikana, sio kigezo cha kumaliza tatizo na kwamba ufumbuzi wa tatizo hilo ni kutekeleza madai ya wanafunzi hao. 

"Pamoja na kukubali kuondoka katika mazingira ya chuo, tunasubili tamko la Serikali na kama watatoa tamko tofauti na lile tunalolitazamia, nitalazimika kukaa na Serikali yangu ili tuweze kutoa tamko la pamoja," alisema BW. Uswege. 

Alisema katika jitihada za kumaliza mgogoro huo, ni wajibu wa Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza kero za wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kuwapa ahadi za kutekeleza madai yao. 

"Serikali ya wanafunzi DUCE, ipo tayari kukaa meza moja na Serikali ili kuangalia uwezekano wa kumaliza mgogoro huu ambao unaangaliwa kwa mtazamo tofauti na wananchi mbalimbali," alisema.

CHANZO:Majira

TAFAKURI: MIGOGORO MINGI INAEPUKIKA IWAPO PANDE MOJA AU ZOTE ZITAJIBIDIISHA KUTAFUTA KINGA BADALA YA TIBA.WANAVYUO HUFIKIA HATUA YA KUGOMA KAMA SILAHA YAO PEKEE YA MWISHO.KWA AKINA SIE TULIO WANAFUNZI TUNAFAHAMU KUWA MWATHIRIKA MKUU WA MGOMO WA MASOMO NI MWANAFUNZI MWENYEWE,NA NDIO MAANA UAMUZI HUO HUWA MGUMU SANA.LAKINI WAFANYEJE?WAZAZI HAWANA UWEZO WA KUMUDU GHARAMA KUBWA ZA ELIMU YA JUU,NA IWAPO TUNATHAMINI ELIMU KWA DHATI BASI KUNA UMUHIMU WA KUPUNGUZA MASHANGINGI,SAMANI ZA OFISINI KUTOKA NJE NA ANASA NYINGINE KATIKA MATUMIZI ILI TUWEKEZE KATIKA SEKTA MUHIMU KAMA HII YA ELIMU.KUFUNGA CHUO NI KUAHIRISHA TU UTATUZI WA TATIZO.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.