8 Nov 2008

Na Daniel Mjema, Dodoma
SERIKALI imekiri kuwa gazeti lake la Habari Leo liliandika habari ya uchochezi na kuliahidi Bunge kuwa italichukulia hatua zinazostahili gazeti hilo.

Hatua hiyo ya serikali inafuatia agizo la Bunge kwamba ilichukulie hatua kali gazeti hilo kwa kuchapisha habari za uchochezi dhidi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikali na Rais Jakaya Kikwete.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo baada Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, kulalamika kuhusina na kitendo cha gazeti hilo la serikali kuchapisha habari hiyo.

Awali mbunge huyo aliomba mwongozo wa Spika jana kuhusiana na habari hiyo akisema kuwa ni nzito na ya uchochezi kuliko iliyoandikwa na gazeti la MwanaHALISI lililofungiwa miezi mitatu hivi karibuni na waziri huyo.

Habari hiyo iliyochapwa Jumatano wiki hii katika toleo namba 636 ilikuwa na kichwa cha habari likichosema ‘Kundi la wabunge wa CCM lasuka zengwe la EPA” na kuelezea njama za wabunge hao wa CCM kumpinga Rais kuhusu hatua zake dhiti ya watuhumiwa wa EPA.

Ole Sendeka alisema habari hiyo ni ya uchochezi mkubwa, hasa inapodai kuwa zipo njama za wabunge wa CCM za kumpinga Rais Jakaya Kikwete kuhusu uamuzi wake katika sakata la kashfa ya fedha za EPA.

Mbunge huyo alisema gazeti hilo limejenga hoja kuonyesha kwamba wabunge hao wa CCM wamekuwa wakitumiwa na watu waliopo nje ya Bunge kupinga maamuzi ya Rais baada ya kuagiza kuwa watuhumiwa wafikishwe kortini.

Ole Sendeka alisema habari hiyo ni nzito na ya uchochezi kuliko ile ya gazeti la MwanaHALISI, kwa sababu inawagombanisha wabunge hao na Serikali pamoja na Rais na kutaka mwongozo wa Spika ni hatua gani zitachukuliwa.

Baada ya maelezo hayo, Spika Samwel Sitta aliungana na Mbunge huyo na kusema kuwa hata yeye alishtuka sana aliposoma habari hizo na kuongeza kuwa huo ni mchezo mchafu ambao serikali inapaswa kuuchukulia hatua kali.

“Hata mimi nilishtuka sana niliposoma habari hiyo, kwa kweli ni mchezo mchafu sana, ingekuwa imeandikwa na gazeti hovyo hovyo hivi tusingeshangaa sana, lakini hili ni gazeti la Serikali,” alisema Sitta.

Sitta ambaye alionekana kukerwa na habari hiyo aliongeza kusema kuwa: “Linapokuwa limechapisha gazeti la Serikali, hili ni jambo zito sana, hivyo naagiza wahusika waliotajwa na gazeti hilo waandike malalamiko rasmi kwa waziri husika”.

Spika alisema pamoja na wahusika ambao ni wabunge wa CCM, kuwasilisha malalamiko hayo na kupeleka kwa waziri nakala za gazeti hilo, Bunge litafuatilia kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya chimbo hicho cha habari cha serikali.

Mara baada ya maelezo hayo , Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, ambaye ndiye aliyelifungia gazeti la MwanaHALSI alisimama na kukiri kuwa gazeti hilo la serikali kuandika habari hizo za uchochezi.

Hata hivyo, alisema kuwa wizara yake imekwishachukua hatua kwa kuwaandikia wahusika kuwataka wajieleze kuhusu ukweli wa habari hiyo na baada ya kupokea maelezo hayo serikali itachukua hatua zinazostahili.

Pamoja na maelezo hayo, Spika alimweleza waziri huyo kuwa ni vyema taarifa ya jinsi serikali ilivyolishughulikia suala hilo iwasilishwe katika ofisi ya Spika ili naye aishirikishe Kamati ya Bunge ya Maadili.

Mwezi mmoja uliopita serikali ililiufnugia kwa miezi mitatu gazeti la MwanaHALISI kwa maelezo kwamba limeandika habari ya uchochezi iliyokuwa na kichwa kisemacho: ‘Njama za kungoa Kitwete zafichuka’, ambayo ilieleza kwamba ndani ya CCM kuna watu wanataka kumzuia Rais Kikwete asigombee urais tena kipindi cha pili.

Waziri husika alisema serikali imechukua hatua kwa sababu gazeti hili imeandika habari yenye lengo la kumchonganisha Rais na mtoto wake aliyedaiwa kutumiwa na kundi la baadhi ya vigogo wa CCM wanaotaka kumwengua ili asigombee kipindi cha pili.

Hatua ya waziri huyo kulifungia gazeti hilo kilipingwa na wadau mbali mbali wa habari na kufuatiwa na maandamano ya amani ya wahiri wa vyombo vya habari nchini hadi katika ofizi za wizara hiyo wakiwa wameziba midomo na gundi ya karatasi au plasta.

CHANZO: Mwananchi


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.