23 Dec 2008


WAKATI Ripoti ya kitaalam ikionyesha namna bora ya kupunguzwa matumizi ya magari ikiwamo ya kifahari maarufu kama mashangingi, serikali imeanza utekelezaji wa mpango mwingine mkubwa wa kuingiza magari mapya 792 kutoka Japan.

Mpango huo mkubwa wa serikali umekuja wakati ripoti ya kitaalamu inayotaka ijipunguzie matumizi yasiyo ya lazima katika ununuzi wa magari ikiwemo ya kifahari ikiwa imewasilishwa mezani kwa Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo tangu Aprili mwaka huu.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye wiki moja iliyopita alitoa angalizo kwa makatibu na manibu makatibu wakuu wa wizara kuhusu kupunguza matumizi ya magari ya kifahari, alinukuliwa na gazeti dada la The Citizen, akisema serikali haiwezi kupiga marufuku ununuzi wa magari hayo wakati imeshaagiza lakini alisisitiza kuwa hiyo itakuwa mzigo wa mwisho kuagizwa na mashangingi kiasi hicho.

Ingawa Pinda hakufafanua, lakini duru huru zaidi za habari kutoka serikalini zilidokeza gazeti hili jijini Dares Salaam jana kwamba, tayari magari 300 yalishaingizwa chini ya mpango huo. "Sehemu kubwa ya magari hayo ni Toyota Pickup, tayari 300 yameingizwa nchini chini ya mpango huo maalumu wa serikali," zilisema duru hizo za habari.

Kwa ufafanuzi zaidi, duru hizo zilisema katika orodha hiyo pia yapo mashangingi Vx na GX ambayo jumla yao ni kati ya 100.

Chini ya mpango huo, duru za habari zilisema gari nyingine ambazo ni nyingi ni pamoja na Toyota Land Cruiser Hard Top ambazo kwa takwimu za kiserikali moja hugharimu kati ya sh 72 hadi 75 milioni.

"Ukiacha Vx na Gx 100, magari mengine mengi katika orodha hiyo ni Toyota Land Cruiser Hard Top na Pickup ndiyo mengi katika orodha hiyo ya magari 792," kilifafanua zaidi chanzo hicho.

Waziri Mkuu Pinda alikaririwa jana na gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, katika mahojiano maalum akisema uamuzi wa kuzuia ununuzi wa magari hayo hauwezi kuchukuliwa kwa sasa, kwa kuwa tayari yameshaagizwa na yataanza kuingia nchini hivi karibuni.

“Uamuzi wa kuzuia ununuzi wa magari hayo hauwezi kufanyika sasa kwa kuwa magari 800 tayari yameshaagizwa kutoka kampuni inayoyatengeneza nchini Japan na yanatarajiwa kuanza kuingia nchini hivi karibuni,” alisema Pinda katika mahojiano hayo.

Hata hivyo, Pinda alieleza kuwa katika mwaka wa fedha ujao mambo yatakuwa tofauti kutokana na kuwataka makatibu wakuu kutoagiza magari hayo na fedha zitazopatikana katika zoezi la kuacha kununua magari hayo zinunue matrekta ambayo yatakuwa na matokeo yanayoonekana katika kilimo.

Hakuna mtu anaweza kufa kwa kutopanda gari la kifahari (Toyota Land Cruiser VX, GX) lakini kwa kukosa chakula itakuwa ni tatizo,” alisema Pinda katika mahojiano hayo.

Alisema uamuzi wake huo umekuwa ukiungwa mkono na Rais Jakaya Kikwete, ukiwa umelenga kumkomboa mkulima ambaye amekuwa anatumia jembe la mkono kwa miaka 47 ya uhuru wa nchi hii.

“Magari haya ya kifahari yamekuwa yananunuliwa kutokana na baadhi ya watumishi (wakurugenzi) kutaka kuendana na wakati wa magari ya kifahari yaliyopo sokoni,” alisema Pinda huku akisema serikali sasa inataka kuondokana na dhana hiyo.

Alipoulizwa mbona serikali imeamua kuendelea kununua magari hayo japokuwa yamekuwa yanasemwa kuwa ni mzigo kwa serikali, Pinda alisema wakati anaingia tayari magari yalikuwa yameshaagizwa na hivyo mpango huo utaanzia kwenye bajeti ijayo ya serikali.

Aliongeza kuwa “Nimeongea na makatibu wakuu wiki iliyopita nimewaambia kuhusu suala hili la uagizaji magari ya kifahari, sasa tuachane nalo na badala yake tujikite kwenye kilimo cha kisasa,”

Duru hizo zikieleza kwa kina mpango huo, Ripoti ambayo iko kwa Luhanjo na gazeti hili kufanikiwa kuona nakala yake, inaonyesha namna bora ya serikali kupunguza ununuzi wa magari hasa ya kifahari.

Katika mpango huo, moja ya jambo lililopendekezwa na watalaamu ni kuhakikisha gari la moja aina ya VX au Gx hubadilishwa na kukunuliwa jingine kila baada ya miaka saba tofauti na sasa, ambapo waziri, naibu au makatibu wakuu hubadili magari hayo kila baada ya miaka miwili.

Ripoti hiyo pia inaonyesha orodha ya viongozi wanaopaswa kutumia magari hayo kwa kupunguza viongozi wanaopaswa kutumia Vx na Gx, ambao wanapaswa kutumia ni mawaziri, manaibu, makatibu wakuu na manaibu wao, huku kuanzia wakurugenzi wakipasawa kutumia magari mengine ikiwemo Land Cruiser za kawaida.

Pia kumekuwa na pendekezo la kufuata utaratibu ambao hutumiwa na serikali kama ya Afrika Kusini, Namibia na Botswana ambazo hutumia Kampuni ya Emperial kwa ajili ya usimamizi wa kiteknolojia kwa ajili ya magari yote ya serikali ili kuyaangalia na kudhibiti yasitumike katika shughuli binafsi.

Emperial kwa kutumia teknolojia hiyo huweza kuonyesha hatua ya kila gari kwa kutumia mfumo maalumu wa usalama na pia kuzuia wizi hata wa mafuta katika magari ya serikali ambayo sasa hivi hakuna mfumo wa kuyadhibiti.

CHANZO:Mwananchi

NANI KASEMA MATREKTA KWA WAKULIMA NI MUHIMU KULIKO NYONGEZA YA MASHANGINGI KWA WAHESHIMIWA?EBO?NYIE MNATAKA WAHESHIMIWA WAKAGUE MAENDELEO WAKIWA KWENYE MATREKTA?UHESHIMIWA NI PAMOJA NA KUWA KWENYE GARI LA KIFAHARI.HIZI NDIZO PRIORITIES ZETU ZITAKAZOMWEZESHA KILA MTANZANIA KUWA NA MAISHA BORA HIVI PUNDE TU!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.