4 Dec 2008


MAUAJI ya albino yanaendelea kutikisa, na safari hii kwa kutumia silaha kali, licha ya serikali kuanza operesheni maalum ya kupambana na uovu huo baada ya mlemavu wa ngozi anayefahamika kama Ezekiel John, 47, kuuawa kwa risasi na watu wasiojulikana ambao walitoweka na mkono wake wa kulia.

Mlemavu huyo wa ngozi aliuawa wakati akiwa nyumbani kwake.

Kamanda wa polisi mkoani Kigoma, Abdihaki Rashid alisema katika taarifa yake jana kuwa watu hao walivamia nyumbani kwa marehemu na kumpiga risasi mgongoni, na baadaye kumkata mkono ambao walitoweka nao.

“Tukio hilo lilitokea juzi, katika Kijiji cha Muyama wilayani Kasulu na askari waliokwenda kufanya uchunguzi wa awali katika eneo la tukio hawajarudi, hivyo watakaporejea tutatoa taarifa za kina zaidi,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Mauaji ya albino yametapakaa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa yakihusishwa na imani za kishirikina na tayari watu wengi wenye ulemavu wa ngozi wameshauawa kikatili na watu wasiojulikana ambao hukata viungo vya albino na kutoweka navyo.

Serikali imepeleka askari wa kikosi maalum cha kupambana na ukatili huo, lakini taarifa za kuuawa kwa albino zinaendelea kumiminika, huku polisi wanne wakiripotiwa kuwekwa ndani kwa tuhuma za kuwaachia wauaji wa albino baada ya kuhongwa fedha.

Mwanzoni mwa wiki hii watu waliokuwa wamejifunika sura zao walimvamia mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye ulemavu huo, Mateso Dunia, 13 na kumuua kikatili.

Mtoto huyo wa darasa la tatu alikuwa mkazi wa Kijiji cha Gunihuna kilicho katika Kata ya Iponya wilayani Bukombe. Hilo lilikuwa tukio la pili wilayani humo kwa mtoto albino kuuawa tangu mauaji hayo ya kikatili yanayohusishwa na imani za uchawi yaanze Kanda ya Ziwa.

Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya jeshi hilo kuwakamata polisi wanne ambao wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa wauaji wa albino na kuwaachia huru.

Mwanafunzi huyo albino aliuawa juzi majira ya saa 6:00 wakati akiwa anarudi nyumbani na wenzake. Walikuwa wakitoka kuangalia video.

Hata hivyo baadaye miguu miwili ya albino ilikamatwa kwa mganga wa jadi ambaye alikimbia kabla polisi hawajamfikia.

Katika hatua nyingine taarifa hiyo ilisema kwamba, katika Kijiji cha Munyange, Polisi wakiwa katika doria ya kawaida, waliwakurupusha watu waliodhaniwa kuwa ni majambazi na kukimbia.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba watu hao wakiwa katika harakati za kukimbia, walidondosha mabomu mawili ya kutupa kwa mkono.

CHANZO: Mwananchi

HIVI JAMII ITAENDELEA KUWA WATAZAMAJI WA UKATILI HUU HADI LINI?HII NI AIBU KUBWA KWA TAIFA LETU KWANI LICHA YA KUONEKANA KITOVU CHA UKATILI DHIDI YA WALEMAVU (WA NGOZI) TUNAONEKANA KAMA KITUO CHA USHIRIKINA USIOTHAMINI UHAI WA BINADAMU WENZETU.INGEKUWA NCHI ZA WENZETU,KUNA MTU ANGEWAJIBIKA LAKINI KWETU NI BUSINESS AS USUAL AS IF NOTHING IS HAPPENING,WAZIRI WA MAMBO YA NDANI ANAPASWA KUWAJIBIKA KWA HILI.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.