Showing posts with label MAUAJI YA ALBINO. Show all posts
Showing posts with label MAUAJI YA ALBINO. Show all posts

2 Mar 2009

UAMUZI WA SERIKALI KUHUSU KURA YA MAONI DHIDI YA WAUAJI WA ALBINO-ULIOTANGAZWA NA RAIS JK KWENYE HOTUBA YAKE YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI- UMEPOKELEWA KWA HISIA TOFAUTI NA BAADHI YA WANANCHI KAMA INAVYOELEZWA KATIKA HABARI NAMBARI 2 HAPO CHINI.KWA MTAZAMO WANGU,NADHANI WANANCHI WANA KILA SABABU YA KUHOJI UAMUZI HUO WA SERIKALI HASA KWA VILE IMEKUWA NI KAMA DESTURI KWA NCHI YETU KUTANGAZA HATUA KALI ZA KISIASA AMBAZO HUISHIA KUBAKI HISTORIA TU PASIPO MAFANIKIO.WENGI TUNAKUMBUKA KUHUSU DEADLINE WALIYOPEWA WALA RUSHWA MWANZONI MWA MWAKA 2006 NA ORODHA YA MAJINA YA WANAOJIHUSISHWA NA BIASHARA YA MADAWA YA KULEVYA ILIYOKABIDHIWA KWA (ALIYEKUWA )WAZIRI BAKARI MWAPACHU....LAKINI HADI LEO HAKUNA HATUA YOYOTE ILIYOCHUKULIWA.KWANZA SOMA HABARI HUSIKA KISHA TUJADILI ZAIDI:

Kikwete:Wanaoua albinokuanza kutajwa kwa kura
mwezi huu

Claud Mshana

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa, maandalizi ya zoezi la upigaji kura za maoni za kung'amua wauaji wa albino na vikongwe, limekamilika na litazinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Akizungumza jana kwenye hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Februari, Rais Kikwete alisema kuwa maandalizi ya kutekeleza zoezi hilo yamekamilika na kwamba, waziri mkuu atafanya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi huu.

Alisema kuwa alitoa maagizo ya kufanyika kwa zoezi hilo mwezi Desemba mwaka jana kwamba wananchi wapige kura kutaja majina ya waovu hao, akiwa na dhamira ya kuwapa nafasi wananchi kushiriki kikamilifu.

"Maandalizi ya kutekeleza uamuzi wangu huo yanaelekea kukamilika, mheshimiwa waziri mkuu atafanya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2009 na zoezi lenyewe la kupiga kura kufanyika kuanzia wiki ya pili ya Machi, 2009."

Alifafanua kuwa katika zoezi hilo pia wauaji wa vikongwe, majambazi wa kutumia silaha na wauzaji wa dawa za kulevya nao watahusishwa. Alitaja utaratibu wa kuendesha zoezi hilo utakuwa ni kufuata kanda na kwamba mikoa imegawanywa katika kanda saba ambazo ni Kanda ya Ziwa inayojumuisha mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza na Shinyanga.

Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma; Kanda ya Kati (Dodoma na Singida), Kanda ya Kusini (Lindi na Mtwara), Kanda ya Magharibi (Kigoma na Tabora), Kanda ya Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara), na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro).
Wakuu wa mikoa yote nchini wameshapewa mwongozo wa jinsi ya kutekeleza zoezi hilo na kutaja miongoni mwa mambo watakayotakiwa kuzingatia ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hilo, upigaji kura ufanyike mwezi Machi kwa tarehe zitakazopangwa kwa kuzingatia kanda hizo.

"Kamati za ulinzi na usalama za mikoa zikiongozwa na wakuu wa mikoa zisimamie zoezi hili kwa makini. Kadhalika, kamati za ulinzi na usalama za wilaya zikiongozwa na wakuu wa wilaya zitaongoza utekelezaji katika wilaya zao na kushirikisha serikali za vijiji na mitaa," alisema Rais Kikwete.

"Napenda kuitumia fursa hii kuwasihi Watanzania; wake kwa waume; vijana na wazee tujitokeze kwa wingi kuwataja watu wanaojihusisha na maovu hayo katika jamii. Kura ni siri, hakuna atakayejua umemtaja nani. Hata msimamizi wa kituo hawezi kujua," alisema......
CHANZO: Mwananchi

NA IFUATAYO NI HABARI KUHUSU REACTION YA BAADHI YA WANANCHI JIJINI DAR ES AALAAM KUHUSIANA NA UAMUZI HUO WA KURA YA MAONI KUWATAMBUA WAUAJI WA MAALBINO.


Dar wataka serikali iweke wazi chanzo cha mauaji ya
albino


Na Boniface Meena

WANANCHI wa Mkoa wa Dar es Salaam wameiomba serikali itafute na kuewaleza chanzo cha mauaji ya albino, badala ya kuendelea kutoa kauli za kisiasa wakati hali inaendelea kuwa mbaya.

Pia wamesema hawadhani kama upigaji kura kuhusu mauaji hayo kama utasaidia kwa kuwa hata kesi za waliokamatwa kwa kuhusishwa na mauaji hayo hazijasikika. Mbali na hilo wameitaka serikali kuanzisha mahakama maalum kwaajili ya kusikiliza kesi za mauaji hayo ili waweze kujua maamuzi yanayotolewa na mahakama. Wakizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Temeke ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Kihato wananchi hao walidai serikali inaoneka kutokuwa makini na suala hilo kwa kuwa hakuna hata kesi moja ya mauaji ya albino iliyotolewa hukumu hadi hivi sasa.

Mbunge wa kuteuliwa, Al-Shaimar Kweiger alidai kuwa kuna mtandao mkubwa wa matajiri unaohusika na mauaji hayo ambao alisema hadhani kama unaweza kuishinda serikali katika kupambana nao. "Hili suala limeshazungumziwa sana, tumezunguka na Waziri Mkuu sehemu nyingi, lakini hawakomi nadhani kuna mtandao mkubwa wa watu wenye fedha uko nyuma ya jambo hili," alisema Kweiger.

Josephat Torner ambaye ni mwanaharkati wa kupinga mauaji ya albino alisema suala hilo linaonekana kuwa la kisiasa kwa kuwa hakuna hatua za haraka zilizochukuliwa kuwasaisdia wahanga wa mauaji hayo. "Tunataka kujua serikali imefikia wapi tangu suala hili lilipotangazwa kuwa ni la kitaifa," alihoji Torner. Torner ambaye ni albino alisema hawadhani kama upigaji kura utasaidia, kwani wanaona kama ni mchezo wa kisiasa hivyop wangependa kujua wako katika hali gani hivi sasa kuhusu mauaji hayo.

Christopher Andendekisye ambaye ni Mkurugenzi wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shivyawata) alisema, kama serikali haitakuwa makini na mauaji hayo yanaweza kuendelea kwa muda mrefu kwa kuwa chanzo chake bado hakijajulikana. "Itabidi tuwe na wiki maalum au mahakama maalumu kwaajili ya kusikiliza kesi za mauaji haya na kama haiwezekani tuambiwe chanzo ni nini," alisema Andendekisye. Maria Chale ambaye ni albino alidai kuwa inaonekana serikali mpaka sasa haijui chanzo kitu ambacho kinatia wasiwasi kama zoezi hilo litafanikiwa.

Steven pascal ambaye ni katibu wa Albino muungano Investiment Trust(Amit), alisema ni bora jeshi (JWTZ) watumike kuwaska wanaohusika na mauaji hayo. "Ni bora Jeshi lihusishwe kwani hawa jamaa (wanajeshi) akipigwa mwenzao mmoja kijiji kizima kinazingira mpaka wapatikane wahusuka," alisema Pascal. Wananchi hao walisemas hayo jana wakitoa maoni yao mbele ya DC Kihato ambaye alikutana nao kuwaeleza juu ya uzinduzi wa upigaji kura za maoni dhidi ya mauaji ya albino utakaofanyika jijini Dar es Salaam Machi 5, mwaka huu.

Akijibu baadhi ya maoni yaliyotolewa na wananchi hao, Kihato ni kweli serikali haijatatua tatizo hilo kama wananchi wanavyotaka lakini inajitahidi kuhakikisha mauaji hayo yanatokomezwa, ndiyo maana wameitisha kura ya maoni.


CHANZO: Mwananchi

KATIKA HABARI YA KWANZA,KUNA MANENO NIMEYAONYESHA KWA RANGI NYEKUNDU KWA SABABU MAALUMU.PAMOJA NA NIA NZURI YA SERIKALI KUTAFUTA UFUMBUZI WA KUDUMU WA MAUAJI YA MAALBINO,WAZO LA KURA YA MAONI LINAWEZA LISIWE NA MAFANIKO YANAYOKUSUDIWA.KWANZA,KAMA MANENO YENYE RANGI NYEKUNDU YANAVYOONYESHA "...Alifafanua kuwa katika zoezi hilo pia wauaji wa vikongwe, majambazi wa kutumia silaha na wauzaji wa dawa za kulevya nao watahusishwa..." KUTANUA WIGO WA WALENGWA KUNALIFANYA ZOEZI HILO KUWA PANA ZAIDI ILHALI MAANDALIZI YAKIWA DUNI.ZAIDI,IWAPO KWELI DHAMIRA NI KUWASAKA WAUAJI WA MAALBINO,KUNA HAJA GANI KUINGIZA HABARI ZA WAUZA MADAYA YA KULEVYA,KWA MFANO,AMBAO HUKO NYUMA TULISHAAMBIWA KUWA ORODHA YAO ILIKABIDHIWA KWA WAZIRI MWAPACHU NAE AKADAI KUWA AMEIKABIDHI KWA RAIS?

JINGINE AMBALO LINAHITAJI TAFAKURI NI UTATA KATIKA KAULI ZA VIONGOZI WETU.RAIS ANASEMA ALITOA AGIZO MWEZI DESEMBA,LAKINI TUNAKUMBUKA KAULI ZA WAZIRI MKUU HAPO KATIKATI KWAMBA WAUAJI WA MAALBINO NAO WAUAWE (JAPO BAADAYE ALIOMBA MSAMAHA KWA MACHOZI HUKO BUNGENI)....INA MAANA AGIZO LA DESEMBA LILIPUUZWA NA KUBADILISHWA KUWA "JINO KWA JINO" KABLA HALIJAFUTWA KUFUATIA KELELE ZA WADAU KUHUSU HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA WA SHERIA?

NA KAMA AGIZO LILITOLEWA DISEMBA,KWANINI BASI ICHUKUE MIEZI MITATU MIZIMA KUTOA UAMUZI HUU AMBAO KWA HAKIKA UNAHITAJI MAANDALIZI MAZURI NA YA KUTOSHA (HUSUSAN UHAMASISHAJI)?JE WIKI MBILI ZINATOSHA ?RAIS ANASEMA "...maandalizi ya kutekeleza zoezi hilo yamekamilika na kwamba, waziri mkuu atafanya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi huu...zoezi lenyewe la kupiga kura kufanyika kuanzia wiki ya pili ya Machi, 2009."ARE WE ARE WE REALLY SERIOUS?KURA YA MAONI WIKI MOJA BAADA YA UZINDUZI!?JE MAANDALIZI YANAYODAIWA KUKAMILIKA HAYAKUPASWA KUJUMUISHA UHAMASISHAJI WA WANANCHI?PASIPO UMAKINI,ZOEZI HILI LITAISHIA KUTUNISHA POSHO ZA WAHUSIKA NA WAUAJI WA MAALBINO,WAUZA UNGA NA MAJAMBAZI WAKAENDELEA "KUPETA."

SWALI JINGINE LA MSINGI NI KUHUSU MATOKEO YA KURA HIYO YA MAONI.HIVI KWA MFANO BLOGU HII IKIPIGIWA KURA NYINGI KUWA NDIO SPONSOR WA WAUAJI WA MAALBINO (GOD FORBID),NINI KINAFUATA?MHUSIKA ATAKAMATWA NA KUHOJIWA KWA VILE KURA NYINGI ZIMESEMA HIVYO?MHUSIKA ATATAKIWA AJIELEZE KWANINI WANANCHI WENGI WAMEMPIGIA KURA "ZA CHUKI"?AU WAPELELEZI WATAINGIA UWANJANI KUANZA UCHUNGUZI?VIPI ILE TASK FORCE ILIYOUNDWA HUKO NYUMA?

KWA NCHI INAYOHESHIMU UTAWALA WA SHERIA INATARAJIWA KUWA MATOKEO YA KURA HIYO HAYATACHUKULIWA KUWA NDIO HUKUMU DHIDI YA WATAJWA.HIYO ITAMAANISHA KUFANYIA UCHUNGUZI MAJINA YA WALIOPATA KURA NYINGI.KISHA UCHUNGUZI UTAPOKAMILIKA NA USHAHIDI WA KUTOSHA KUPATIKANA NDIPO ZIANZE HATUA ZA KISHERIA KWA VILE,KWA MUJIBU WA SHERIA, NI MAHAKAMA PEKEE (NA SIO MATOKEO YA KURA YA MAONI) INAYOWEZA KUMTIA MTUHUMIWA HATIANI AU KUMWACHIA HURU.

MWISHO,NI MUHIMU PIA KUKUMBUKA NAMNA UTAMADUNI WA RUSHWA UNAVYOATHIRI MWENENDO WA MAISHA YA MTANZANIA KILA SIKU.HIVI KAMA BAADHI YA WAHESHIMIWA WANAWEZA KUNUNUA KURA ILI WATUWAKILISHE HUKO BUNGENI,KWA MFANO,ITASHINDIKANA VIPI KWA MATAJIRI WANAOFADHILI MAUAJI YA MAALBINO KUNUNUA KURA "ZA KUPENDWA" NA WAPIGA KURA?VIPI IWAPO MATOKEO YA KURA YATAONYESHA MAJINA YA BAADHI YA WAHUSIKA WA KAMPUNI YA KAGODA?HAKUTAKUWA NA KIGUGUGMIZI KAMA KILICHOPO KWENYE UFISADI WA KAMPUNI HIYO KWENYE FEDHA ZA EPA?

NA VIPI IWAPO WANYONGE WATAPIGIWA KURA ZA CHUKI?

MASWALI NI MENGI KULIKO MAJIBU.KWA HAKIKA DHAMIRA KUHUSU KURA YA MAONI NI NZURI LAKINI WASIWASI WANGU MKUBWA NI KATIKA UTEKELEZAJI WAKE.NA KAMA WALIVYOSEMA BAADHI YA WAKAZI WA DAR KATIKA STORI NAMBA 2,MAFANIKIO KATIKA HARAKATI ZA KUKOMESHA MAUAJI YA ALBINO YANAHITAJI JITIHADA ZA ZAIDI YA KAULI ZA KISIASA.

25 Jan 2009


Hatimaye katika kukabiliana na wimbi la mauaji ya albino,Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameagiza leseni za waganga wa jadi wote zifutwe.Majuzi,Pinda alikaririwa akiagiza wananchi kuchukua sheria mkononi kwa kuwaua "wauaji wa maalbino".Hatua zote mbili zinaweza kutofanikiwa kwa vile inaelekea kana kwamba zimechukuliwa pasipo kufanyiwa utafiti wa kina.


Kuruhusu wananchi wafanye "jino kwa jino" dhidi ya wanaoua maalbino kunaweza kulipeleka Taifa mahala pabaya.Taasisi pekee yenye mamlaka ya kuhukumu ni mahakama zetu,na hizo ndio zinazoweza kuhakiki makosa halasi tofauti na majungu,chuki,visasi,nk na haki inatarajiwa kuwa imetendeka pindi hukumu itapokuwa ya kifo au mshtakiwa kuachiwa huru kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani.Hilo haliwezekani katika "mahakama za jino kwa jino mitaani".Si ajabu watu waliokosana kwa sababu zao binafsi wakishia kupigana mapanga kwa kisingizio cha "kudhibiti mauaji ya maalbino".Ikumbukwe kuwa ni rahisi kuruhusu uvunjifu wa sheria lakini ni zaidi ya vigumu kurejesha heshima na utiifu kwa sheria.


Tuje kwa hili la kufuta leseni za waganga wa jadi.Je amri hii inamaanisha ni marufuku kwa mtu yeyote kujihusisha na uganga wa jadi au...?Sijaelewa vizuri hapo lakini nahisi inamaanisha hivyo kwani katika hali ya kawaida,kufanya shughuli inayohitaji leseni pasipo kuwa na leseni husika ni uvunjifu wa sheria.Swali la kwanza,hivi ni waganga wa jadi wangapi wenye leseni (tukiachana na hao Maprofesa wanaojitangaza kwenye magazeti kuwa wanatibu ukimwi,wanawezesha kufaulu pasipo kusoma,na miujiza mingine)?Nauliza hivyo kwani haitaleta mnaana yoyote kumfutia mtu leseni ambayo hajawahi kuwa nayo hata siku moja.Swali la pili,je utekelezaji wa amri hiyo utasimamiwa vipi?Polisi watazungukia mganga mmoja hadi mwingine nchi nzima kuhakikisha kuwa hafanyi uganga?
Swali la tatu,je tumefikia hatua ya kufanya maamuzi kwa kigezo cha "samaki mmoja akioza basi wote wameoza"?Nauliza hivyo kwani tafsiri ya moja kwa moja ya kuwafutia leseni masangoma ni kwamba wao ndio wahusika muhimu katika suala la mauaji ya maalbino.Hii "overgeneralization" inatoka wapi?Mbona wale wazembe wa Muhimbili walipompasua kichwa mgonjwa wa goti na wa goti akapasuliwa kichwa walioadhibiwa ni madaktari husika tu na sio kada nzima ya madaktari hapo Muhimbili au nchi nzima?Au mbona ilipobainika kwamba kuna uhuni umefanyika pale BoT kwenye ishu ya EPA,aliyefukuzwa kazi ni Ballali pekee na wengine wameendelea kuwa madarakani hadi leo?Au mbona aliyekuwa balozi wetu huko Italy alipokumbwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma haikupelekea kutimua mabalozi wote?Sasa iweje "uhuni" wa baadhi ya waganga wa jadi upelekee hukumu kwa wote wanaohusika kwenye taaluma hiyo (na yayumkinika kusema kuwa wengi wao-hususan vijijini-ni waadilifu katika kazi yao)?


Naomba nisisitize kwamba hapa simaanishi two wrongs make a right.Hapana,najaribu kuangalia approaches za nyuma katika kukabiliana na matatizo mbalimbali na namna zinavyokinzanna na hii ya ku-revoke leseni za waganga wa jadi.


Kwa wanaofahamu umuhimu wa tiba asili katika jamii husasan katika kipindi hiki cha uchangiaji wa gharama kwenye public health facilities,ni dhahiri hatua ya kuwafutia leseni waganga wote wa jadi itaathiri Watanzania wengi wanaotegemea huduma hizo (aidha kutokana na imani,nature ya maradhi yao au uwezo duni katika kumudu gharama za huduma za afya hospitalini).


Japo ni muhimu sana kutafuta ufumbuzi wa haraka kukomesha mauaji dhidi ya maalbino,ni muhimu zaidi kutumia common sense and viable approaches kuliko hatua ambazo pamoja na nia zake nzuri zinaweza kutuletea matatizo zaidi.Tukirihusu sheria zivunjwe kwa kuruhusu kuua wanaoua maalbino (badala ya kuwafikisha kwenye vyombo vya dola) basi tusishangae pindi baadhi ya wananchi watakapoamua kuchukua sheria mkononi dhidi ya mafisadi,kwa mfano,badala ya kusubiri kesi zilizoko mahakamani,ripoti za tume,nk

4 Dec 2008


MAUAJI ya albino yanaendelea kutikisa, na safari hii kwa kutumia silaha kali, licha ya serikali kuanza operesheni maalum ya kupambana na uovu huo baada ya mlemavu wa ngozi anayefahamika kama Ezekiel John, 47, kuuawa kwa risasi na watu wasiojulikana ambao walitoweka na mkono wake wa kulia.

Mlemavu huyo wa ngozi aliuawa wakati akiwa nyumbani kwake.

Kamanda wa polisi mkoani Kigoma, Abdihaki Rashid alisema katika taarifa yake jana kuwa watu hao walivamia nyumbani kwa marehemu na kumpiga risasi mgongoni, na baadaye kumkata mkono ambao walitoweka nao.

“Tukio hilo lilitokea juzi, katika Kijiji cha Muyama wilayani Kasulu na askari waliokwenda kufanya uchunguzi wa awali katika eneo la tukio hawajarudi, hivyo watakaporejea tutatoa taarifa za kina zaidi,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Mauaji ya albino yametapakaa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa yakihusishwa na imani za kishirikina na tayari watu wengi wenye ulemavu wa ngozi wameshauawa kikatili na watu wasiojulikana ambao hukata viungo vya albino na kutoweka navyo.

Serikali imepeleka askari wa kikosi maalum cha kupambana na ukatili huo, lakini taarifa za kuuawa kwa albino zinaendelea kumiminika, huku polisi wanne wakiripotiwa kuwekwa ndani kwa tuhuma za kuwaachia wauaji wa albino baada ya kuhongwa fedha.

Mwanzoni mwa wiki hii watu waliokuwa wamejifunika sura zao walimvamia mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye ulemavu huo, Mateso Dunia, 13 na kumuua kikatili.

Mtoto huyo wa darasa la tatu alikuwa mkazi wa Kijiji cha Gunihuna kilicho katika Kata ya Iponya wilayani Bukombe. Hilo lilikuwa tukio la pili wilayani humo kwa mtoto albino kuuawa tangu mauaji hayo ya kikatili yanayohusishwa na imani za uchawi yaanze Kanda ya Ziwa.

Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya jeshi hilo kuwakamata polisi wanne ambao wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa wauaji wa albino na kuwaachia huru.

Mwanafunzi huyo albino aliuawa juzi majira ya saa 6:00 wakati akiwa anarudi nyumbani na wenzake. Walikuwa wakitoka kuangalia video.

Hata hivyo baadaye miguu miwili ya albino ilikamatwa kwa mganga wa jadi ambaye alikimbia kabla polisi hawajamfikia.

Katika hatua nyingine taarifa hiyo ilisema kwamba, katika Kijiji cha Munyange, Polisi wakiwa katika doria ya kawaida, waliwakurupusha watu waliodhaniwa kuwa ni majambazi na kukimbia.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba watu hao wakiwa katika harakati za kukimbia, walidondosha mabomu mawili ya kutupa kwa mkono.

CHANZO: Mwananchi

HIVI JAMII ITAENDELEA KUWA WATAZAMAJI WA UKATILI HUU HADI LINI?HII NI AIBU KUBWA KWA TAIFA LETU KWANI LICHA YA KUONEKANA KITOVU CHA UKATILI DHIDI YA WALEMAVU (WA NGOZI) TUNAONEKANA KAMA KITUO CHA USHIRIKINA USIOTHAMINI UHAI WA BINADAMU WENZETU.INGEKUWA NCHI ZA WENZETU,KUNA MTU ANGEWAJIBIKA LAKINI KWETU NI BUSINESS AS USUAL AS IF NOTHING IS HAPPENING,WAZIRI WA MAMBO YA NDANI ANAPASWA KUWAJIBIKA KWA HILI.

19 Nov 2008

Picha kwa hisani ya LUKWANGULE

Albino anusurika kunyofolewa mkono (Majira Novemba 16,2008)

*Mnyofoaji alimrubuni kuwa anataka kumwoa 

Na Benedict Kaguo, Tanga 

WIMBI la mauaji ya albino limechukua sura mpya mkoani Tanga baada ya Bibi Aisha Yusuph mwenye ulemavu huo kunusurika kuuawa kikatili. 

Imedaiwa Bibi Aisha alinusurika kuuawa na Bw. Mohamed Athuman baada ya kutaka kumkata mkono ili kwenda kuuza. 

Polisi mkoani hapa tayari imemkamata Bw. Athuman ambaye ni mkazi wa kijiji cha Dindira, Korogwe kwa tuhuma za kutaka kumuua Bi Aisha. 

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Bw. Anthony Rutta, alisema mtuhumiwa huyo alitaka kutenda kosa hilo kwa kujifanya anataka kumchumbia Aisha. 

Tukio hilo lilitokea Novemba 13 mwaka huu saa 12 jioni katika kijiji cha 
Dindira. 

Bw. Athuman amelazwa katika Hospitali ya wilaya Korogwe Magunga kutokana na kipigo cha wananchi wenye hasira baada ya kubainika kutaka kumuua albino huyo. 

Polisi Tanga inawashikilia watu wawili kuhusu tukio hilo ambao ni Bw. Eliaza Seif na Bw. Shaaban Ramadhan wote wakazi wa Dindira. 

Watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya upelelezi kukamilika.

Waua albino na kutoweka na miguu yake (Majira Julai 1,2008)

Na Mary Ng'oboko, Mwanza 

JESHI la Polisi mkoa wa Mwanza, linawatafuta watu wanne kwa tuhuma za kumkatakata na mapanga hadi kumuua albino na kutoweka na miguu yake. 

Akizungumza jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Khamis Bhai, alisema watu hao walifika nyumbani kwa albino huyo wakiwa na mapanga na wamevaa makoti meusi. 

Kamanda Bhai alimtaja marehemu kuwa ni Bw. Nyerere Ludaila (50) ambaye ni mkazi wa eneo la Usagara wilayani Misungwi mkoani hapa. 

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 2.30 usiku katika kijiji cha Nyaligwe, Usagara. 

Kamanda Bhai alisema inasemekana albino huyo alikuwa ni mganga wa kienyeji na kwamba wiki mbili kabla ya tukio, alikuwa na ugomvi na mtoto wake mkubwa uliosababishwa na mtoto huyo kudai urithi wa mali kutoka kwa baba yake, huku angali hai, lakini baba yake hakuwa tayari kutoa urithi huo. 

"Baada ya tukio la mauaji, mtoto huyo wa albino ambaye hatujaweza kupata jina lake, alikimbia na hajaonekana nyumbani hadi sasa, nasi tunaendelea kumtafuta tukishirikiana na wananchi," alisema Kaimu Kamanda Bhai. 

Alisema hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo na kwamba polisi wanaendeleza juhudi za kuwatafuta wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Wafukua kaburi wakidhani la albino, watoweka na mifupa (Majira Agosti 6,2008)

Na Theonestina Juma, Bukoba 

WATU wasiojulikana wamefukua kaburi la mtu waliyedhani ni albino aliyefariki dunia miaka 18 iliyopita na kutokomea na mifupa yake yote. 

Habari kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Bw. Henry Salewi, zilisema tukio hilo lilitokea Julai 30 mwaka huu usiku, katika kitongoji cha Igabilo kijiji cha Ihangiro kata ya Nshamba wilayani Muleba. 

Ilielezwa kuwa watu hao wasiojulikana walifukua kaburi la albino aliyejulikana kwa jina la Bibi Hilda Angelo (60) aliyefariki dunia Februari 6, 2001 kwa lengo la kuchukua mifupa yake inayoaminika kutumika kwa masuala ya kishirikina. 

Hata hivyo, inadaiwa kuwa watu hao hawakulenga kaburi la albino huyo kutokana na la mumewe Bw. Mkalimo Rufurani aliyefariki dunia mwaka 1990 kuwa karibu nalo. 

Ilielezwa kuwa makaburi ya wanandoa hao yalipangwa sehemu moja na hivyo watu hao walipofika walifukua kaburi la mume badala ya mke aliyekuwa albino na kuondoka na mifupa. 

Habari zaidi zilieleza kuwa watu wa familia hiyo walipoamka walikuta kaburi likiwa wazi huku mifupa yote ikiwa imechukuliwa na watu wasiojuliakana. 

Novemba 26 mwaka jana, katika kitongoji cha Nyakashenye kijiji na kata ya Rushwa, Muleba, watu wasiojulikana walifukua kaburi la Zeuria Yustance aliyefariki dunia Oktoba 29, 2006 wakati akijifungua na kuchukua masalia ya mifupa yake yote na kutokomea nayo. 

Hili ni tukio la pili kutokea wilayani humo ya watu wasiojulikana kufukua makaburi ya maalbino kwa lengo la kuchukua mifupa. 

Katika tukio lingine katika kijiji cha Nyambogo kata ya Ilememleza wilayani Chato, umeokotwa mwili wa mwanaume ukiwa umecharangwa mapanga na kisha kuteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana. 

Hata hivyo haijajulikana mtu huyo alikuwa akituhumiwa kwa kosa gani hadi kufikia hatua ya watu hao wasiojulikana kumteketeza kwa moto. 

Uchunguzi zaidi unafanywa na Jeshi la Polisi Wilayani humo ikiwa ni pamoja na kuwasaka watu waliojulikana katika mauaji hayo ya kikatili.

'Biashara ya viungo vya albino vigogo wanahusika' (Majira Oktoba 16,2008)

*Yahofiwa kuongezeka katika uchaguzi 2010 

Na Gladness Mboma 

SIRI nzito juu ya mauaji ya albino yanayoendelea kutokea sehemu mbalimbali nchini imefichuliwa kufuatia utafiti wa kina uliofanywa na albino wenyewe na sasa wameamua kukifikisha kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete. 

Kwa mujibu wa utafiti huo, imebainika kuwa watu wanaotumwa kukata viungo hivyo na kuua albino wanapewa fedha nyingi na vigogo ambao huvitumia kishirikina. 

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania, Bw. Ernest Kumaya, wakati akizungumzia maandamano ya amani ya kupinga na kulaani mauaji yanayoendelea dhidi yao nchini. 

"Tunaamini kabisa watu wanaonunua viungo hivi vya albino ni watu matajiri na wenye madaraka makubwa katika maeneo malimbali ikiwamo serikalini. 

"Mtu maskini hana uwezo na hawezi kununua kiungo kimoja kinachouzwa sh. milioni 13 hadi 14 ni matajiri ndio wenye uwezo wa kununua," alisisitiza Bw. Kumaya akibainisha waliyoyagundua. 

Alisema kutokana na hali hiyo wana hofu kubwa katika uchaguzi mkuu wa 2010 viungo vyao vitazidi kuongezeka kwani kipindi hicho cha kuelekea uchaguzi mbalimbali nchini vitendo vya kishirikina pia huongezeka. 

"Wakati huo kila kiongozi atataka kuhakikisha anashinda, hivyo kwa kuwa viungo vyetu ni biashara, vitendo vya kishirikina vya mauaji ya albino kwa ajili ya kuchukua viungo vyetu vitaendelea kutawala," alisema. 

Alisema katika uchunguzi wao wa Septemba mwaka huu albino waligundua pia kuwapo kwa kikundi cha watu wasiozidi 10 wakiwamo wanawake ambao wamekuwa wakifanya mauaji hayo. 

Bw. Kumaya alisema kikundi hicho ambacho kilikuwa kipo Kanda ya Ziwa hasa Mwanza kimehamia Bukoba na baadaye wanahofia kwamba kitahamia Dar es Salaam. 

Akigusia maandamano waliyopanga kuyafanya Oktoba 19 mwaka huu na Rais Kikwete kutarajiwa kuwa mgeni rasmi, Bw. Kumaya alisema msukumo uliowafanya waandae maandamano ni kutoona juhudi hasa za kumaliza tatizo la mauaji dhidi ya albino, ambapo yanazidi kuongezeka huku viongozi wakuu na watoa uamuzi wakiendelea kukaa kimya. 

Maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia kwenye viwanja vya Shule ya Walemavu ya Uhuru Mchanganyiko na kuishia viwanja vya Karimjee. 

"Kutolipa kipaumbele suala la mauaji ya albino kitaifa, mfano vifo vinavyotokea katika migodi ya madini ya Mererani viliundiwa Tume na kushughulikiwa maafa hayo ni mambo yaliyotufanya tuandamane. 

"Vifo vya watoto vilivyotokea wakati wa Sikukuu ya Idd mkoani Tabora, Serikali imetia mkono wake kwa kutoa pole kwa wafiwa yakiwamo mashirika kutoa rambirambi zao kuonesha kuguswa na janga hilo, lakini suala la mauaji ya albino nchini viongozi hawajaweza kuchukua hatua madhubuti zenye kuonesha mwelekeo," alidai.
NILIWAHI KUANDIKA MAKALA KATIKA GAZETI LA RAIA MWEMA KUHUSIANA NA SUALA HILI.UNAWEZA KUJIKUMBUSHA NILIYOJADILI HUMO KWA KUBONYEZA HAPA



21 Oct 2008

Albino Girl Killed For Witchcraft
Tuesday, October 21 02:52 pm
Sky News
A gang murdered and mutilated a 10-year-old albino girl in Tanzania - because they wanted to sell her body parts to witch doctors. Skip related content

Esther Charles was killed in Shilela in the western region of the African country on Sunday.

She died just hours after President Jakaya Kikwete called for a crackdown on gangs, saying the killing of albinos has "stained the country's good image".

At least 26 other albinos, mostly women and children, have been killed in different parts of the east African country over the past year.

Albinos lack melanin pigment in the skin, eyes and hair, which protects from the sun's ultraviolet rays.

But witch doctors believe they have magical powers to bring fortune, and discrimination against albinos is rife across sub-Saharan Africa.

In 2007, police in Tanzania reported several cases of people digging up the bodies of children to remove organs, in many cases the genitals and eyes, to make potions used in rituals.

Shilela councillor Joseph Manyara told a rally organised by the Tanzania Albino Society (TAS): "It is utterly stupid for some people to believe that albinos have magic powers and their parts can make them rich.

"People should be provided with education to understand that it is only through hard working that they can prosper in life and not through selling albinos' body parts."

Police said they have arrested 47 people suspected to be involved in the killings this year.

But TAS chairman Ernest Kimaya blasted authorities over the speed at which the murders were solved.

He said: "We are yet to witness any convictions and incidents of the murder of albinos are on the rise."

There are about 150,000 albinos in the country, and more than 8,000 of them are registered with the TAS.

Some families kill albino babies upon birth, Tanzanian authorities say.

And authorities in Kenya and Burundi, where albino killings have also been reported in recent months, have started to give added protection.

Some reports say albino skin is prized in the Democratic Republic of Congo, another troubled African nation where superstition is high.

SOURCE: Sky News

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.