6 Dec 2008


MBUNGE wa Jimbo la Buchosa, Samwel Chitalilo ameingia katika mkasa mpya baada ya kudaiwa kumshambulia Mabula Matulanya, ambaye ni mlinzi wa ghati la ofisi ya kivuko cha Nyakaliro Kome, linalomilikiwa na serikali.

Mlinzi huyo anadai alishushiwa kipigo hicho na mbunge huyo kwa kushirikiana na washirika wake wawili mara baada ya kummulika tochi Chitalilo wakati akiwa kwenye haja ndogo karibu na mlango wa ofisi ya kivuko hicho, ambalo ni eneo la lindo lake.

Akizungumza na gazeti hili, mlinzi huyo alidai kuwa, shambulizi hilo lilimkumba Oktoba 10 mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku wakati alipoingia kazini kwake kumpokea lindo mlinzi mwenzake. Muda mfupi baada ya kukabidhiwa lindo hilo, alihisi kuwepo kwa mtu katika eneo la ofisi na hivyo kumulika eneo hilo kwa tochi.

Alisema kitendo cha kumulika tochi ndicho kilichomponza na kumsababishia kupata kipigo kutokana na mbunge huyo kukasirika, akidai kuwa alidhalilishwa kwa kumulikwa na tochi wakati akiwa kwenye haja ndogo na kwamba yeye kama mbunge hapaswi kufanyiwa hivyo.

“Nilimulika nikidhani pengine anaweza kuwa mwizi katika lindo lango... sikujua kama ni mbunge na wala sikuwa natambua kama alikuwa katika baa ya jirani akinywa pombe. Nilikuwa kazini, lakini licha ya kumueleza yote hayo nilishikwa na watu wake wawili na kuanza kushambuliwa na mbunge huyo kwa ngumi na mateke,” alidai.

Alidai kuwa baada ya kipigo hicho alikwenda katika kituo cha polisi cha Nyakalilo kutoa taarifa ambapo baadaye, Chitalilo, akiwa na wapambe hao wawili (majina tunayo), walimfuata na kuendelea kumshambulia akiwa kituoni hapo mbele ya mgambo wa kituo anayejulikana kwa jina moja la Shimo.

Alidai baada ya kuzuiwa na mgambo huyo, mbunge huyo na wapambe wake waliamua kupiga simu kituo kikubwa cha polisi ambako walitoa maelekezo kwa askari wa zamu aliyemweka ndani na kesho yake kuchukuliwa na polisi wa kituo kikuu cha wilaya ambao walimwandikisha maelezo.

"Lakini walininyima PF3 kwa ajili ya matibabu jambo ambalo limefanya nitibiwe kienyeji na kupona pasipo kumchukulia hatua yoyote mbunge huyo," alidai mlinzi huyo na kuomba vyombo vya usalama vimsaidie ili aweze kuchukua hatua dhidi ya mbunge huyo kwa vile ameshambuliwa akiwa kazini.

Naye Mbunge Chitalilo, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu mkasa huo, alikiri kuwepo kwa shambulio hilo na kusema kuwa mlinzi huyo alishambuliwa na wananchi waliokuwa jirani kutokana na yeye kulalamika kudhalilishwa kwa kumulikwa wakati akiwa anakojoa.

“Sikiliza suala hili, mimi nilishalisamehe, polisi kwa kuwaomba wamfutie mashtaka mlinzi huyo kwa vile watu wengi waliniomba samahani... alinidhalilisha kwa kunimulika makusudi licha ya kujua nilikuwa mimi... alishambuliwa na watu ambao nilifanya kazi ya kuwatuliza, sasa mimi kosa langu ni kumsamehe?” alihoji.

Hata hivyo, mbunge huyo alimsihi mwandishi kuachana na habari hizo kwa vile hazina maana katika jamii na kumtaka kufuatilia masuala ya maendeleo katika jimbo lake.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jamal Rwambow, hakuweza kupatikana kulitolea ufafanuzi jambo hilo kutokana na kuwa katika ukaguzi wa vituo vya polisi jijini Mwanza, ziara ambayo amekuwa akiifanya kwa lengo la kutambua na kubaini matatizo ya jeshi lake mkoani hapa.

CHANZO: Mwananchi

THIS GUY IS A FRAUD.LAKINI HAYA NDIO MATOKEO YA KUANGALIA HAIBA YA MGOMBEA (NA VIJISENTI VYAKE) WAKATI WA KAMPENI YA UBUNGE BADALA YA KUPIMA UWEZO WAKE.HUYU MTU ANA TUHUMA ZA KUFOJI CHETI CHA SHULE,ANADAIWA KUWALIZA WATU FLANI WALOMKOPESHA FEDHA KWA AJILI YA BIASHARA YAKE,NA SASA KITUKO HIKI!MBUNGE GANI MAKINI ATAKOJOA OVYO?KWANI ANGEKWENDA KUJISAIDIA MSALANI ANGEMULIKWA TOCHI NA HUYO MLINZI?HUU NI UHUNI WA KISIASA UNAOHITAJI ADHABU KALI COME 2010.

LAKINI MKASA HUU UNATUSAIDIA KUONYESHA NAMNA HAKI ILIVYO NA TAFSIRI TOFAUTI KATI YA WALALAHOI NA WAHESHIMIWA.MLINZI ALIYEKWENDA KUDAI HAKI YAKE AMEISHIA KUSWEKWA NDANI,MHESHIMIWA ALIYETUHUMIWA KWA SHAMBULIO YUKO HURU AKIJIGAMBA KWA "KUMSAMEHE" VICTIM WAKE!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.