14 Feb 2009


WAKATI serikali ikiendelea na mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya uraia ya Sh222 bilioni, imebainika kwamba kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno na kama wangemtumia Mpigachapa wa Serikali kazi hiyo ingetumia Sh95 bilioni tu. Habari zilizopatikana zinaeleza kwamba, ingawa mpigachapa wa serikali alishaomba zabuni hiyo kufanya kazi hiyo, lakini hajachaguliwa bila ya sababu maalumu.

Siri hiyo ilifichuka juzi wakati Kamati ya Bunge ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali (Miscellaneous Amendments) ilipotembelea ofisi ya Mpigachapa Mkuu kujionea utendaji kazi ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Benson Mpesya ambaye ni Mbunge wa Mbeya mjini kupitia CCM na kugundua kuwa ofisi hiyo ya serikali ina uwezo wa kufanya hiyo kazi kwa bei nafuu zaidi.

Mbunge wa Moshi mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Philimon Ndesamburo ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa serikali, itoe sababu za kuikatalia Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wake, kuandaa vitambulisho vya uraia kwa gharama ya Sh95 bilioni badala yake kung'ang'ania zabuni itakayogharimu Sh222 bilioni.

Akifafanua hoja yake mbunge huyo, alisema akiwa kwenye ziara hiyo, alimuuliza Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, kama Ofisi yake inao uwezo wa kuchapa vitambulisho vya taifa na aliwajibu wajumbe wa Kamati ya Bunge kwamba, ofisi yake inaweza kutengeneza vitambulisho hivyo kama itapatiwa fedha.

Mbunge huyo alimkariri Chibogoyo akisema kwamba, ofisi yake ilishaomba kazi ya kuchapa vitambulisho hivyo kwa gharama ya Sh95 bilioni miaka miwili iliyopita, lakini hadi sasa hajui kinachoendelea. Ndesamburo alisema kauli ya Mpiga Chapa iliwashitua wajumbe wote wa kamati hiyo iliyoambatana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

"Mimi ninachotaka kujua kutoka serikalini ni kwa nini isiimarishe zaidi ofisi yake ambayo mpaka sasa inachapa siri nyingi za serikali kwa kuipatia kazi hiyo hata kama ni Sh150 bilioni kwa sasa, ili kuondokana na utata unaoendelea?" alihoji.

Mbunge huyo alisema mpigachapa mkuu alieleza kwamba, kabla ya kuomba kazi hiyo alifanya utafiti katika nchi kadhaa ikiwamo Ujerumani na kuona wazi kwamba, kazi hiyo ingefanyika kwa kiwango cha kimataifa kwa gharama ya Sh95 bilioni.

"Serikali ingepunguza gharama na kuondoa malumbano yanayoendelea kama ingetoa kazi kwa Ofisi yake (mpiga chapa), ambayo inaongozwa na mtu ambaye alikuwa Rais wa Shirikisho la Wapigachapa wakuu duniani," alisema na kuongeza:

"Mpigachapa Mkuu anasema sehemu ya fedha hizo zitatumika kununua mtambo wa kisasa ambao baada ya kuchapa vitambulisho utabaki hapa hapa nchini."

Chibogoyo alipopigiwa simu jana ili kufafanua taarifa hizo, alikataa katakata kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba, mambo ya wabunge yanatolewa na wabunge wenyewe. Naye Mpesya licha ya kukiri kwamba kamati yake ilitembelea ofisi hiyo ili kupata maelezo mbalimbali hususan jinsi ya kuchapa sheria, hakutaka kufafanua zaidi juu ya yaliyojitokeza.

Akizungumzia hali hiyo jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, alisema kwa sasa bado mchakato huo unaendelea, hivyo hawezi kuzungumza lolote juu ya suala hilo kwa kuwa kila mmoja ameomba tenda na serikali bado inaendelea kuzichambua.

“Kwa kuwa mchakato wenyewe bado haujaanza, siwezi kusema lolote juu ya hilo, hivyo basi nakuomba usubiri mpaka zoezi hilo litakapokamilika ndipo ujue ni nani ameshinda tenda hiyo na kuniuliza swali lako,” alisema Masha. Aliongeza kuwa kuchelewa kwa mchakato wa kutengeneza vitambulisho vya uraia, kunatokana na kumtafuta mzabuni mwenye sifa anayeweza kusimamia kazi hiyo kwa umakini.

Kazi ya kuchapisha vitambulisho vya uraia imekuwa chanzo cha mvutano mkubwa miongoni mwa wanasiasa na baadhi ya watendaji wa serikali. Katika mkutano wa bunge uliomalizika wiki hii mjini Dodoma, Mbunge wa Karatu, Dk Wilibrod Slaa alitaka kuwasilisha hoja binafsi akidai kuwa waziri Masha ameingilia kati mchakato wa kuchapisha vitambulisho hivyo kinyume cha taratibu. Hata hivyo, hoja hiyo ilishindwa kujadiliwa na wabunge baada ya Spika kuizuia kwa maelezo kwamba, kufanya hivyo ni kuingilia kati mchakato mzima wa zabuni hiyo unaoendelea.

Suala la kuchapisha vitambulisho vya uraia nchini, limekuwa likiingia utata mara kwa mara kutokana na baadhi ya wakubwa kudaiwa kutaka kujinufaisha na zabuni hiyo. Mchakato wake wa zabuni ya kuchapa vitambulisho hivyo ulianza mwaka 2004 na kwamba, umekuwa ukisuasua kutokana na kuzingirwa na mizengwe.

Mradi huo ulioanza kuzungumzwa miaka ya katikati ya 1970 na ambao utagharimu kiasi cha Sh222 bilioni, unaelezwa kwamba umo katika hatua za mwisho za kutaka kutekelezwa japo taarifa zinaonyesha kwamba, ni mpango mwingine mkubwa wa ulaji fedha za umma.

CHANZO: Mwananchi

NENO MCHAKATO LIMETOKEA KUWA OFFICIAL SUBSTITUTE YA "UJANJAUJANJA WA KIFISADI".ETI MCHAKATO UNAENDELEA KUMPATA MZABUNI MWENYE SIFA ANAYEWEZA KUSIMAMIA KAZI KWA UMAKINI!HIVI KAMA OFISI YA MPIGACHAPA MKUU WA SERIKALI HAINA SIFA HIZO,KWANINI BASI INAENDELEA KUWEPO?TUACHE HILO,HIVI KATIKA UCHAPISHAJI WA NYARAKA NYETI KAMA VITAMBULISHO VYA URAIA,KUNA MZABUNI MWENYE SIFA ZA MASLAHI YA TAIFA KIUSALAMA ZAIDI YA GOVERNMENT PRINTER?WELL,KWENYE KUSAKA UPENYO WA KUFISADI,KILA EXCUSE ITATOLEWA.

PENGINE WAKATI UMEFIKA WA KUACHANA KABISA NA WAZO HILI LA VITAMBULISHO VYA TAIFA MAANA DANADANA ZINAZOCHOCHEWA NA UFISADI ZIMEKUWA ZIKIENDELEA MIAKA NENDA MIAKA RUDI.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube