11 Apr 2009

ASEMA WACHACHE WALIOTHUBUTU WAACHIWE WAPIGE VITA UFISADI

Salim Said


MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela amesema viongozi wa chama tawala (CCM) wanaogopa kupambana na ufisadi kwa kuwa wanaopambana nao ni viongozi au wabunge wenzao na hivyo kutaka wale wachache waliothubutu kuendeleza vita hiyo waachiwe.

Mama huyo, ambaye amekuwa mmoja wa watu wenye uwezo wa kujenga hoja bungeni wakati wa kuzungumzia ufisadi, alisema anashangaa jinsi viongozi wanavyoshindwa kupambana na ufisadi kama unavyoelezwa kwenye sura ya nane ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayozungumzia vita dhidi ya uovu huo.

Bila ya kutoa mifano bayana, mama huyo amesema ni wabunge wachache wanaoweza kusimama kidete kutetea kipengele hicho, akiwemo yeye; na kwamba kama vita ya ufisadi itafanyiwa kazi ipasavyo, nchi yote itakuwa na utulivu na amani, vitu ambavyo alisema vinahitajiwa na kila Mtanzania.

Akizungumza katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Star Tv, Kilango alisema ugumu wa kipengele hicho ni kwamba, wanapambana na wabunge, viongozi na wanachama wenzao wa CCM.

"Ugumu wa sura ya nane ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ni kwamba unapambana na mwanachama mwenzako, mbunge na hata kiongozi mwenzako. Na hii ndio inawafanya watu wengi kushindwa, isipokuwa wachache kama mimi ambao tumethubutu," alisema Kilango.

"Unaposimama imara kutaka kufanya mabadiliko, kutetea haki na kupinga ubatili, unapaswa kutegemea mengi na mimi niliyategemea na ndio maana sipati tabu katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi."

Kilango alisema viongozi na wananchi wa Tanzania wanapaswa kuwa wa kweli na wawazi katika kupinga rushwa kama wanavyofanya watu wa Marekani.

"Nchini Marekani mtu aliyetaka kurithi nafasi ya useneta wa Obama alitanguliza rushwa ili kuwashawishi wajumbe, jambo ambalo liliwafanya Wamarekani kusimama imara na kuzungumza ukweli kuhusu kashfa hiyo," alisema.

Kilango, ambaye alipata tuzo ya 'Mwanamke Jasiri' aliyopewa na serikali ya Marekani hivi karibuni, alisema jamii inapaswa kuwaunga mkono kwa nguvu zote wachache waliothubutu kuikemea rushwa nchini.

"Kuna watu wachache ambao walijiona wana haki ya kula mali za umma, lazima tuwanyoshee vidole na jamii ituunge mkono katika hili," alisema Kilango.

"Tunawaomba wengi wasiothubutu kusema, watuachie tulioweza... wasitubughudhi, wasitunyamazishe na wala wasiwe na nia ya kutaka kutumaliza kwa kuwa hawatafanikiwa kamwe. Sisi tutaendelea hadi awamu ijayo."

Katika kashfa nyingi za ufisadi, viongozi na wabunge wa CCM ndio wamekuwa wakituhumiwa kuhusika na miongoni mwa waliofikishwa mahakamani ni viongozi wa zamani katika serikali ya CCM, huku moto dhidi ya wabunge wa sasa ukizidi kuwaka katika kashfa za miradi mikubwa.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ununuzi wa rada, ambao umeelezwa kuwa ulifanywa kwa kuongeza bei ili iwe juu kwa lengo la kujipatia kamisheni nzuri, mradi wa uzalishaji umeme wa dharura uliosababisha mawaziri kujiuzulu baada ya kutajwa kwenye ripoti ya kamati teule ya bunge na mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia makaa ya mawe wa Kiwira.

Pia kashfa nyingine iliyohusisha wanachama na viongozi wa CCM ni wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), kashfa ambayo inahusisha majina vigogo wanaohusishwa na kampuni zilizochota fedha nyingi lakini imekuwa ni vigumu kuwataja.

Kashfa hizo zimekuwa zikisababisha malumbano baina ya wanachama wa CCM.

Lakini Kilango hakutaja majina ya watu wanaojaribu kuwazuia au kuwamaliza, bali aliapa kuendelea na vita hiyo kwa kuwa hayo ni maumbile yake.

"Mimi ndivyo nilivyozaliwa na ni maumbile yangu kuzungumza ukweli. Rangi nyekundu nitaisema kuwa ni nyekundu na bluu pia, wala hakuna mtu atakayeweza kuninyamazisha ili niseme kuwa ni nyeupe, kibaiolojia siku zote naweza," alisema na kuongeza:

"Wapo wapole, waoga ambao hata chumbani kulala peke yao wanaogopa, lakini pia wako majasiri wanaothubutu."

Alisema Watanzania walishachoshwa na rushwa na walifikia hatua ya kujenga imani kuwa wabunge wa CCM wapo kwa ajili ya kuilinda serikali yao na wanaoweza kuikosoa ni wabunge wa upinzani tu.

"Sasa wananchi wa Tanzania wanapaswa kuondoa imani hiyo na sisi tupo kwa ajili ya wananchi na msimamo wangu mimi chama hakiwezi kupendwa kama hakikosolewi. Tukikosoa ndio tunakipa afya na si kukidhoofisha kama wanavyodhani baadhi ya watu," alisema.

Alifafanua kuwa, vita dhidi ya rushwa ni kama mashindano ya riadha kwani kuna wanaoanza, wanaoshindwa katikati, wanaomaliza na pia kuna wasiothubutu kuanza.

Kilango alikataa kuwataja wale wanaompiga vita, lakini alisema anaposimama bungeni kuzungumza anafahamu kuwa anazungumza na dunia, hivyo hategemei kupigiwa makofi na wote au kapingwa na wote.

"Wanaopiga makofi nafurahi, pia kuna wale ninaogusa masilahi yao waache wachukie. Lakini mimi nimeamua kuwa kiongozi, hivyo sitishwi na sitatingishwa na watu wenye mitazamo tofauti na mimi. Dhamira yangu ya kuwatumikia Watanzania ipo palepale," alisisitiza
Kilango.

CHANZO: Mwananchi

BRAVO MHESHIMIWA KILANGO,IT'S HIGH TIME SOMEONE CALLS A SPADE A SPADE.WHEN YOU MAKE ENEMIES,THAT MEANS YOU'VE STOOD UP FOR SOMETHING YOU BELIEVE IN.IT IS IN PEOPLE LIKE YOU,MHESHIMIWA KILANGO,THAT MANY OF WAZALENDO AND WALALAHOI FIND A GLIME OF HOPE FOR TANZANIA.SILENCE IS NOT AN OPTION AS IT MIGHT BE TRANSLATED BY MAFISADI AS INSTITUTIONALISING THEIR SABOTAGE OF OUR ECONOMY AND PLUNDER OF WHATEVER IS LEFT OF OUR NATURAL RESOURCES.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube