30 Apr 2009


na Ratifa Baranyikwa, Dodoma

WAKATI Bunge zima likimwandama Mbunge wa Karatu, Dk. Wilibrod Slaa (CHADEMA), kutokana na msimamo wake kuwa posho za wabunge ni kubwa na kutaka zipunguzwe, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameungana na wabunge wengine kwa kusema kuwa posho hizo ni ndogo na kutaka ziongezwe.

Ingawa hakutaja jina, lakini kauli hiyo ya Waziri Mkuu imeonekana dhahiri kumjibu Dk. Slaa anayetaka mishahara na posho za wabunge zipunguzwe, kwamba ni kubwa mno ukilinganisha na watumishi wengine wa umma.

Pinda aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizindua mpango mkakati wa Bunge wa miaka mitano, wenye nia ya kulifikisha Bunge katika kiwango cha juu cha ufanisi.

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa, Pinda alitumia mwanya huo kuchomeka suala la posho za wabunge, ambalo limekuwa agenda kubwa katika mkutano wa 15 wa Bunge unaomalizika leo.

Akielezea hatua ambazo serikali imekuwa ikizifanya kwa upande wa Bunge, Pinda ambaye aliorodhesha hatua kadhaa za kuboresha maslahi ya Bunge, alisema lengo la serikali ni kuboresha maslahi na posho za wabunge ambazo kwa sasa bado ni ndogo.

“Lengo la serikali kwa Bunge ni kuboresha maslahi na posho za wabunge ambazo kwa kweli kwa sasa hazifikii stahiki, lengo ni kuhakikisha Bunge linaboreshewa maslahi ili liweze kufanya kazi yake stahiki na kwa kiwango cha kuridhisha,” alisema Pinda.

Awali, akizungumzia malengo makubwa saba ya mpango mkakati huo, alisema moja ya malengo hayo ni kuboresha maslahi na stahiki za wabunge ili kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ipasavyo.

Mbali na malengo hayo, mengine ya mkakati huo ni kuboresha muundo na utendaji wa ofisi za Bunge ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji, pia kuboresha mazingira ya utendaji kazi ya sekretarieti ya Bunge.

Limo pia suala la kukuza na kuimarisha ushiriki wa Bunge kuwafikia wadau mbalimbali kupitia mikutano, machapisho, vyombo vya habari na njia nyingine ya mawasiliano, pamoja na kukuza na kuinua vipaji vya wabunge.

Kwa upande wa serikali, mbali na malengo ya kuboresha maslahi na posho za wabunge kwa kuzingatia mazingira ya utendaji wao wa kazi, na hali ya uchumi, Pinda pia aliyataja malengo mengine kuwa ni kuwezesha Bunge kuwa na ukumbi mzuri wa kisasa unaotosheleza mahitaji, lengo ambalo kwa sasa tayari limekwishatekelezwa.

Kwa mujibu wa Pinda, lengo lingine ni kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa Bunge ambao ulianza kutumika mwaka 2007/08, kuwashirikisha katika ziara za nje za viongozi wa kitaifa, lakini pia kuharakisha ujenzi wa ofisi za wabunge katika majimbo yao.

Tangu alipotoa kauli hiyo akiwa kwenye moja ya mikutano ya chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, amekuwa akiandamwa na wabunge wenzake katika mkutano huu wa 15, wakipinga hoja hiyo kwa madai kuwa inawachonganisha wabunge na jamii.

Hali hiyo ilisababisha Dk. Slaa afikie hatua ya kuzomewa mara kadhaa kila jina lake linapotajwa kwenye vikao vya ndani na nje.

Mbunge huyo, hata hivyo, alisisitiza kwamba anasimama katika hoja zake, ikiwamo ya posho za wabunge kutaka kutazamwa upya.

Alisema ataendelea kuisimamia hoja hiyo kwa sababu anataka kuwapo kwa uwazi katika mishahara wanayolipwa viongozi mbalimbali wakiwamo wabunge.



0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.