TAARIFA KWA UMMA
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Peter Slaa amealikwa kuwa mmoja wa
wanajopo (panelists) wanne, kutoka Mabara ya Afrika, Asia, Amerika Kusini na
Ulaya, watakaojadili mada isemayo “Demokrasia Shinikizoni (democracy under
pressure)” nchini Ujerumani.
Katibu Mkuu Dkt. Slaa ambaye
amesafiri jana jioni kuelekea Ujerumani, atakuwa pamoja na wanajopo wenzake wengine
ambao ni Prof. Dr. Kyaw Yin Hlaing (Academic Director Myanmar Egress; kutoka
Rangum/Myanmar), Dkt. Aliaksandr Milinkiewitsch (Chairman, Movement for
Freedom; kutoka Minsk/ Belarus), Gavana Henrique Capriles Radonski (Leader of
the Opposition Movement Mesa de la Unidad Democratica; kutoka Carcas/
Venezuela).
Mjadala wa mada hiyo ya Demokrasia Shinikizoni,
itakuwa ni sehemu ya sherehe za miaka 50 za Siku ya Shirika la Konrad-Adenauer-Stiftung
(KAS Day) katika mahusiano yake ya kimataifa na wadau wake mbalimbali kutoka
nchi 80 duniani.
Mwenyekiti wa wanajopo katika
kuendesha mjadala huo ni Christoph Lanz (Director of Global Content; Deutsche
Welle, Berlin/ Germany)
Sherehe hizo pia zitahudhuriwa na
Kansela wa Ujerumani, Dr. Angela Merkel, Rais Mstaafu wa Chile, Seneta Eduardo
Frei Ruiz-Tangle na Rais Mstaafu wa Bunge la Ulaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa
KAS, Dr. Hans-Gert Pottering.
Shirika la KAS linatimiza miaka 50
tangu lilipoanza rasmi kujihusisha na ukuzaji wa demokrasia, uhuru, amani
maendeleo na haki. Kwa muda wote huo limekuwa likifanya kazi na wadau katika
nchi mbalimbali duniani kutimiza malengo hayo tajwa.
Mpaka sasa KAS ina ofisi 80 sehemu
mbalimbali duniani (pamoja na Tanzania), ikishirikiana na wadau wake katika
kuendesha miradi inayohusiana na malengo hayo katika nchi 120.
Katika kusherehekea Jubilee ya Miaka
50 ya Siku ya KAS itakayofanyika Juni 27, 2012, shirika hilo limeamua kukutana
na wadau na marafiki zake ambao pia wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika
utendaji kazi wa KAS katika shughuli za kupigania demokrasia na maendeleo kwa
ajili ya manufaa ya wananchi wa nchi husika.
Katika mada ya “Demokrasia
Shinikizoni”, wanajopo watajadili changamoto zinazowakabili watetezi wa
demokrasia katika tawala mbalimbali zinazotumia njia dhalimu zinazobana
upanukaji wa demokakrasia ambayo ni msingi muhimu wa maendeleo ya watu.
Imetolewa
leo Juni 25, 2012, Dar es Salaam na;
Tumaini
Makene
Afisa
Habari CHADEMA