18 Apr 2009

Na Leon Bahati

SAKATA la Halmashauri ya Karatu, kugomea kulipia malazi ya Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein na ujumbe wake limechukuwa sura mpya, baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Celina Kombani kuunga mkono uamuzi wa halmashauri ni sahihi.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Kombani alisema halmashauri za wilaya haziwajibiki kuchangia ziara za mawaziri, rais au makamu wake, wanapotembelea katika maeneo yao.

Kombani alibainisha kuwa kama ingekuwa utaratibu huo upo, halmashauri nyingi zingefilisika hasa ambazo mawaziri wanatoka, kwa sababu wana utaratibu maalumu wa kutembelea zaidi ya mara tano kwenye maeneo yao, kwa mwaka.

"Kwa mfano kwa mwaka mimi hufanya ziara mara sita katika wilaya yangu ya Ulanga (Morogoro). Tukisema wanigharamie basi ingefilisika pamoja na halmashauri nyingine ambazo zina mawaziri," alisema Kombani ambaye ni Mbunge wa Ulanga Mashariki.

Akielezea kuhusu taratibu za matumizi ya fedha kwenye halmashauri, alisema kwa kawaida matumizi yote hupitishwa kwenye vikao vya madiwani.

Alibainisha kuwa gharama za msafara wa rais, makamu wa rais na mawaziri hugharamiwa na serikali kuu, kulingana na taratibu zilizowekwa.

"Ndiyo maana rais anapokuwa kwenye ziara huenda na vyakula vyake," alisema Kombani lakini akafahamisha kuwa halmashauri zinaweza kutenga fungu kwa ajili ya kuuandalia ugeni kwenye maeneo yao chakula cha jioni.

Iwapo halmashauri itaamua kufanya hivyo, alisema kuwa ni lazima fungu hilo liwe limepitishwa na halmashauri kupitia vikao vyake halali na si mkurugenzi na watendaji wake.

Alipoulizwa juu ya adhabu ya kiongozi wa halmashauri atakayetoa fedha pasipokufuata taratibu; alisema kila halmashauri ina taratibu zake za kuwajadili viongozi au maofisa waliokiuka taratibu na kuwachukulia hatua.

Suala la Halmashauri ya Karatu, kugomea kulipia malazi ya Makamu wa Rais pamoja na ujumbe wake liliripotiwa na gazeti la Mwananchi Jumatano iliyopita likionyesha kuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Mathew Sedoyeka alimjia juu na kumtaka aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Majid Myao, aandike barua ya kujieleza kwanini alikataa kutoa fedha za kulipia ziara ya makamu wa rais wilayani humo.

Sedoyeka hakufurahishwa na kitendo cha halmashauri hiyo kugoma kulipa kiasi cha Sh2 milioni ambazo ni malipo ya kulala siku moja pamoja na chakula kwa ujumbe huo wa makamu wa rais, katika hoteli ya Bougain Villea ya mjini Karatu.

Kwenye barua ya kujieleza iliyoandikwa Machi 3, 2009 yenye kumbukumbu namba kdc/ded/cv.3/1/121, Myao amejitetea kuwa uamuzi wa kutolipiwa ziara hiyo, umetokana na kamati ya fedha ya madiwani kukataa kuidhinisha fedha hizo.

Alisema kutokana na kutoidhinishwa malipo hayo, aliona angekiuka Sheria namba tisa ya mwaka 1982 ambayo inahusu masuala ya matumizi ya fedha za halmashauri na maamuzi ya kamati ya fedha.

“Kama mimi ningetoa malipo hayo ni wazi ningekiuka sheria za serikali za mitaa hasa ikizingatiwa madiwani katika kikao chao halali ndio waligomea,” alieleza Myao.

Akizungumzia sakata hilo, Mbunge wa Jimbo la Karatu, Dk Willibrod Slaa alisema alichofanya ofisa huyo wa serikali ilikuwa halali kwa sababu walikuwa hawana bajeti ya malipo hayo.

Dk Slaa alitoa wito kwa serikali kutomuadhibu mtendaji yoyote wa halmashauri hiyo kutokana na uamuzi uliochukuliwa, ambao ulizingatia maadili ya kazi na utekelezaji wa utawala bora.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube