Showing posts with label UWAJIBIKAJI SERIKALINI. Show all posts
Showing posts with label UWAJIBIKAJI SERIKALINI. Show all posts

30 Apr 2009

Wingu la moshi jijini Dar kufuatia mlipuko wa mabomu maeneo ya Mbagala.Picha kwa hisani ya MICHUZI
Na Mussa Juma, Arusha

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, imeunda Tume ya Wataalam wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kuchunguza chanzo cha kulipuka silaha za aina mbali mbali katika ghala la kambi ya jeshi iliyopo eneo la Mbagala, jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Emanuel Nchimbi alitangaza uamuzi huo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Ngurdoto, jijini Arusha.

Nchimbi alisema Baraza hilo, litafanya kazi ya kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na athari zote ambazo zimetokana na mlipuko huo.

Alisema vilivyokuwepo katika ghala hilo ni mabomu na risasi za aina mbali mbali na silaha nyingine ndogo.

Naibu Waziri huyo, alitoa wito kwa wakazi wote wanaoishi jirani na kambi hiyo kutookota kitu chochote cha chuma na wanapokiona watoe taarifa katika kambi ya JWTZ iliyokaribu nao.

"Endapo wataona au kutilia shaka aina yoyote ya chuma , watoe taarifa haraka katika kambi ya jeshi iliyo karibu nao au katika timu ya wataalam wa jeshi hilo ambayo imeanza uchunguzi," alisema Nchimbi.

Hata hivyo, kwa niaba ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, alitoa pole kwa wote walioathirika na tukio hilo.

"Amiri jeshi mkuu anawapa pole wananchi wote wa Dar es Salaam na Pwani kwa usumbufu ambao wameupata kutokana na tukio hilo," alisema Nchimbi.

Alifahamisha bado chanzo cha ajali hakijajulikana na pia kutokana na sababu za kiusalama haitakuwa rahisi kutangaza athari za kijeshi zilizopatikana kutokana na tukio hilo.
CHANZO: Mwananchi
HIZI TUME HADI LINI?ILE YA AJALI YA CHENGE HAIJATOA TAARIFA YAKE JAPO TUKIO LENYEWE LILIHUSISHA WATU WANNE TU!JE TUKIO KUBWA KAMA HILI TAARIFA SI ITAKUWA MWAKA 2050!?
HIYO WIZARA YA NCHIMBI INA REKODI ISIYOPENDEZA KUHUSIANA NA TUME.HIVI IMESHATUAMBIA MATOKEO YA TUME ILIYOUNDWA KUCHUNGUZA AJALI YA HELIKOPTA YA JWTZ?
LAITI TUNGEKUWA NA UTAMADUNI WA KUWAJIBIKA,BASI MUDA HUU NCHIMBI NA WAZIRI WAKE DR MWINYI WANGEKUWA WAMESHAJIUZULU.LAKINI KWA VILE UWAJIBIKAJI NI MSAMIATI UNAOELEKEA KUTOLETA MAAN KWETU,BASI TUTARAJIE TUME MOJA BAADA YA NYINGINE...NA KWA VILE WATANZANIA WANAONGOZA KWA REKODI YA USAHAULIFU,AT THE END OF THE DAY WAHUSIKA WATAISHIA "KUUCHUNA" TU.

21 Apr 2009


Baraza la Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) limepitisha uamuzi wa kuishirikisha Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) kuhakiki vyeti vya wote wanaoomba kuwania nafasi za kisiasa ili sifa zao kielimu zitambulike.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Mayunga Nkunya, aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam, TCU imewasiliana na NEC kwa barua, ili utaratibu huo uanze kutumika katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.

Nkunya alitoa taarifa hiyo wakati akizungumzia maonyesho ya vyuo vikuu yaliyoandaliwa na TCU yatakayoanza kesho hadi Aprili 24, mwaka huu. “Baraza letu limepitisha uamuzi ili watu wanaotaka kugombea nafasi za kisiasa, vyeti vyao vihakikiwe, ili akipita sifa ijulikane rasmi kama ni daktari basi awe daktari na si daktari feki,” alisema Profesa Nkunya.

Hatua hiyo ya tume inatokana na kilichoelezwa na Nkunya kuwa ni kukithiri kwa vyuo na vyeti bandia nchini, jambo ambalo alisema wamejipanga kulivalia njuga kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha Tanzania haiangamii kitaalamu na kitaaluma.

Alisema orodha ya vyuo visivyotambulika vya nje ambavyo Watanzania wengi wakiwamo mawaziri na wabunge wamesoma, ni ya kweli na kwamba kama kuna mtu anahisi kuonewa ruhusa kwenda mahakamani...ENDELEA

CHANZO: Habarileo.

TAMKO ZURI LAKINI LINALOSTAHILI UMAKINI KATIKA KULIAMINI.HAWA TCU WAKATI WANAZUNGUMZIA UCHAGUZI WA 2010,WANATAKA KUTUMBIA HAWAKUWEPO 2005?AU WATAPATA NGUVU HIYO 2010?JE KAMA SASA WANASHINDWA KUWASHUGHULIKIA HAO "MADAKTARI WA FALSAFA" WALIOKWAA SHAHADA ZAO MTANDAONI TUTAAMINI VIPI KUWA WATAWEZA HIYO 2010?
TATIZO LA NCHI YETU SIO SHERIA,KWANI ZIMEKUWEPO TANGU TUNAKABIDHIWA UHURU NA MKOLONI.TATIZO NI UTEKELEZAJI WA SHERIA HIZO.KUNA MBUNGE ALIKUWA NA TUHUMA ZA KUFOJI ELIMU (SIO YA CHUO KIKUU) BALI YA SEKONDARI.CHA AJABU HADI LEO "ANAPETA".JE HII HAILETI USHAWISHI KWA VIHIYO WENGINE KUJARIBU BAHATI ZAO?

TATIZO LA PILI LA NCHI YETU SIO SHERIA BALI UTEKELEZAJI WAKE UNAOELEMEA ZAIDI AINA YA MKOSAJI.YALEYALE YA ANAEIBA KUKU KWA NJAA KUITWA MWIZI LAKINI ANAYEFUJA MABILIONI ANAOTWA M-BADHIRIFU (NA SANASANA BADALA YA KWENDA JELA ATAHAMISHWA KITUO CHA KAZI).KUNA SHERIA KWA AJILI YA VIGOGO (KAMA AKINA CHEYO WANAOUA KWENYE AJALI LAKINI WANAUNDIWA TUME BADALA YA SHERIA KUCHUKUA MKONDO WAKE) NA SHERIA NYINGINE NI KWA AJILI YA MAKABWELA.

18 Apr 2009

Na Leon Bahati

SAKATA la Halmashauri ya Karatu, kugomea kulipia malazi ya Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein na ujumbe wake limechukuwa sura mpya, baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Celina Kombani kuunga mkono uamuzi wa halmashauri ni sahihi.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Kombani alisema halmashauri za wilaya haziwajibiki kuchangia ziara za mawaziri, rais au makamu wake, wanapotembelea katika maeneo yao.

Kombani alibainisha kuwa kama ingekuwa utaratibu huo upo, halmashauri nyingi zingefilisika hasa ambazo mawaziri wanatoka, kwa sababu wana utaratibu maalumu wa kutembelea zaidi ya mara tano kwenye maeneo yao, kwa mwaka.

"Kwa mfano kwa mwaka mimi hufanya ziara mara sita katika wilaya yangu ya Ulanga (Morogoro). Tukisema wanigharamie basi ingefilisika pamoja na halmashauri nyingine ambazo zina mawaziri," alisema Kombani ambaye ni Mbunge wa Ulanga Mashariki.

Akielezea kuhusu taratibu za matumizi ya fedha kwenye halmashauri, alisema kwa kawaida matumizi yote hupitishwa kwenye vikao vya madiwani.

Alibainisha kuwa gharama za msafara wa rais, makamu wa rais na mawaziri hugharamiwa na serikali kuu, kulingana na taratibu zilizowekwa.

"Ndiyo maana rais anapokuwa kwenye ziara huenda na vyakula vyake," alisema Kombani lakini akafahamisha kuwa halmashauri zinaweza kutenga fungu kwa ajili ya kuuandalia ugeni kwenye maeneo yao chakula cha jioni.

Iwapo halmashauri itaamua kufanya hivyo, alisema kuwa ni lazima fungu hilo liwe limepitishwa na halmashauri kupitia vikao vyake halali na si mkurugenzi na watendaji wake.

Alipoulizwa juu ya adhabu ya kiongozi wa halmashauri atakayetoa fedha pasipokufuata taratibu; alisema kila halmashauri ina taratibu zake za kuwajadili viongozi au maofisa waliokiuka taratibu na kuwachukulia hatua.

Suala la Halmashauri ya Karatu, kugomea kulipia malazi ya Makamu wa Rais pamoja na ujumbe wake liliripotiwa na gazeti la Mwananchi Jumatano iliyopita likionyesha kuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Mathew Sedoyeka alimjia juu na kumtaka aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Majid Myao, aandike barua ya kujieleza kwanini alikataa kutoa fedha za kulipia ziara ya makamu wa rais wilayani humo.

Sedoyeka hakufurahishwa na kitendo cha halmashauri hiyo kugoma kulipa kiasi cha Sh2 milioni ambazo ni malipo ya kulala siku moja pamoja na chakula kwa ujumbe huo wa makamu wa rais, katika hoteli ya Bougain Villea ya mjini Karatu.

Kwenye barua ya kujieleza iliyoandikwa Machi 3, 2009 yenye kumbukumbu namba kdc/ded/cv.3/1/121, Myao amejitetea kuwa uamuzi wa kutolipiwa ziara hiyo, umetokana na kamati ya fedha ya madiwani kukataa kuidhinisha fedha hizo.

Alisema kutokana na kutoidhinishwa malipo hayo, aliona angekiuka Sheria namba tisa ya mwaka 1982 ambayo inahusu masuala ya matumizi ya fedha za halmashauri na maamuzi ya kamati ya fedha.

“Kama mimi ningetoa malipo hayo ni wazi ningekiuka sheria za serikali za mitaa hasa ikizingatiwa madiwani katika kikao chao halali ndio waligomea,” alieleza Myao.

Akizungumzia sakata hilo, Mbunge wa Jimbo la Karatu, Dk Willibrod Slaa alisema alichofanya ofisa huyo wa serikali ilikuwa halali kwa sababu walikuwa hawana bajeti ya malipo hayo.

Dk Slaa alitoa wito kwa serikali kutomuadhibu mtendaji yoyote wa halmashauri hiyo kutokana na uamuzi uliochukuliwa, ambao ulizingatia maadili ya kazi na utekelezaji wa utawala bora.
CHANZO: Mwananchi

15 Apr 2009


SAKATA la halmashauri ya Karatu, kugomea kulipia malazi ya Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein na ujumbe wake limechukuwa sura mpya baada ya aliyekuwa kaimu mkurugenzi wakati wa ziara hiyo, Majid Myao kutakiwa kutoa maelezo.

Myao aliitwa na mkuu wa wilaya ya Karatu, Mathew Sedoyeka hivi karibuni ili akatoe maelezo juu ya suala hilo hasa kutokana na halmashauri hiyo kugoma kulipa kiasi cha Sh2milioni ambazo ni malipo ya kulala siku moja na chakula kwa ujumbe huo, katika hoteli ya Bougain Villea ya mjini Karatu.

Kwa mujibu wa maelezo ya maandishi ya Myao, yaliyopo katika barua yake ya Machi 3, 2009 yenye kumbukumbu namba kdc/ded/cv.3/1/121, Myao amejitetea kuwa uamuzi wa kutolipiwa ziara hiyo, umetokana kamati ya fedha ya madiwani kukataa kuidhinisha fedha hizo.

Alisema kutokana na kutoidhinishwa malipo hayo, aliona angekiuka sheria namba tisa ya mwaka 1982 ambayo inahusu masuala ya matumizi ya fedha za halmashauri na maamuzi ya kamati ya fedha.

“Kama mimi ningetoa malipo hayo ni wazi ningekiuka sheria za serikali za mitaa hasa ikizingatiwa madiwani katika kikao chao halali ndio waligomea,”alieleza Myao.

Akizungumzia sakata hilo, mbunge wa jimbo la Karatu,
Dk Wilbroad Slaa alisema ni halali kwani walikuwa hawana bajeti ya malipo hayo na aliomba mtendaji yoyote wa halmashauri hiyo asiwajibishwe kwa suala hilo.

CHANZO: Mwananchi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.