18 Jun 2009


Hivi karibuni watunga sheria (wabunge) wetu watatu "waliungana" kuandika kitabu walichokipa jina "BUNGE LENYE MENO".Ukiangalia sehemu ndogo tu ya wasifu wa wabunge hao utamaizi kuwa "muungano huo wa uandishi" ulikuwa ni mithili ya "ndoa za makaratasi" (marriages of inconvenience).

Dkt Wilbroad Slaa,Spika Samuel Sitta na John Momose Cheyo!Nadhani kitu pekee kinachoweza kuwafanya wafanane ni "wote ni wabunge",and the similarity stops there.Wakati Dkt Slaa amejijengea jina kubwa kama kinara wa mapambano ya ufisadi,ni vigumu kum-define Spika Sitta linapokuja suala la mapambano dhidi ya ufisadi.Lakini si vigumu kukumbuka kuwa ni Sitta huyuhuyu aliyempa kadi nyekundu Zitto Kabwe alipombana ex-waziri Nazir Karamagi kuhusu sakata la Buzwagi.Na ni Sitta huyuhuyu aliyetishia kumshtaki Dkt Slaa alipoibua tuhuma ufisadi ndani ya Benki Kuu akidai kuwa ni ushahidi wa kufoji!Eti leo tunaambiwa Spika huyuhuyu nae ni kinara wa mapambano ya ufisadi!


Tukija kwa John Cheyo,nadhani amebaki kuwa UDP,kwa maana ya one-man party.Sera yake ya mapesa ilijaa utani ambao ungekuwa na maana zaidi kwenye sanaa za maigizo kuliko katika siasa makini.Amebaki kuwa jina tu.Sidhani kama kunamfano wowote hai unaoweza kutumika kumtambulisha Cheyo kama mwanaharakati wa mapambano dhidi ya ufisadi.


Sasa hao ndio waandishi wa kitabu BUNGE LENYE MENO.Lakini kwa vile nafahamu kwamba uchambuzi makini unahitaji kwenda mbali zaidi ya kuangalia personalities,naomba kugeukia hoja yangu ya kupingana na ya akina Sitta kuwa bunge la sasa lina meno.Binafsi nasema kama ni meno basi ni ya plastiki.Nadhani unafahamu mtoto mchanga anapoanza kuota meno huwa yanaota meno ambayo yanaitwa meno kwa vile tu yamekaa sehemu yalipo meno.Ukimnywesha uji wa moto basi kilio chake hapo ni balaa!Ni meno machanga yasiyomudu kutafuna vitu vigumu.


Na ndio bunge letu lilivyo.Utasikia kelele,vitisho,na vitu kama hivyo kila waheshimiwa wanapokutana hapo Dodoma ambapo mwisho wa siku akaunti zao zinaingiza kipato cha zaidi ya mwezi mzima kwa Mtanzania wa kawaida,huku kila mwisho wa mwezi wakiondoka na mamilioni lukuki.Basi angalau kipato chao kingeendana na hali halisi ya uchumi wa nchi yetu.


Wabunge wa CCM,ambao wanatengeneza zaidi ya robo tatu ya bunge letu,ndio vichekesho zaidi.Utamsikia huyu akisema hili kabla ya mwenzie kumkalia kooni akitaka mwongozo wa Spika kwa madai ya "kukiuka kanuni za bunge".Lakini ukifuatilia kwa makini,mara nyingi mwongozo huo huombwa pale anapojitokeza mbunge mmoja kuelezea yale yanayozungumzwa na Watanzania wengi mitaani,kwa mfano ishu ya ufisadi.Sasa kwa vile kuna wabunge wenye deni kubwa zaidi kwa CCM na vigogo wake,njia pekee ya kulipa deni hilo ni kuomba mwongozo wa Spika ili kuwaziba midomo wale wanaoongea yasiyopendeza masikioni mwa watawala.


Majuzi,Mbunge wa Nzega Lukas Selelii amemwomba Mungu awalaani mawaziri kwa madai kwamba wamekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya ufisadi nchini.Mbunge wa Pangani Mohammed Rished akaomba mwongozo....sijui kuonyesha anafahamu zaidi sheria za Bunge au kwa vile yaliyoongelewa na Selelii hayakumpendeza mbunge Rished.Kwani si kweli kwamba maamuzi mengi yaliyopelekea skandali za ufisadi yalipitishwa na Baraza la Mawaziri?Kabineti ingetimiza wajibu wake tungekuwa na Richmond?au Kiwira?Au TICTS?au Buzwagi?Au IPTL?Orodha ni ndefu.Sasa Rished alihitaji mwongozo kwa vile Selelii kumuomba Mungu awalaani watu waliofanya maamuzi yaliyopelekea ufisadi ni kosa la jinai au?Halafu tunaambiwa tuna "bunge lenye meno"!In this case,haya wala si meno ya plastiki bali ni mapengo kabisa.


Fuatilia kwa karibu mjadala wa Bajeti unavyoendelea huko Dodoma.Kuna kauli za uchungu kutoka kwa baadhi ya wabunge kama Selelii,Mwambalaswa,Mpendazoe na,kama kawaida,wabunge wa upinzani kama vile Dkt Slaa.Lakini kauli pekee hazimsaidii Mtanzania masikini asiyejua hatma ya maisha yake.Kelele hizi zimekuwepo tangu bunge hili linaanza.Ndio,zimesaidia kuundwa kwa kamati mbalimbali kama ile ya Mwakyembe.Lakini kuunda kamati kisha kutofanyia kazi mapendekezo yake ni sawa na ufisadi tu.Ikumbukwe kuwa kamati hizo hutumia mamilioni ya fedha za walipa kodi.Ukubwa wa gaharama za kuendesha kamati za aina hiyo ungeweza kupunguziwa maumivu laiti mapendekezo yanayotolewa yangekuwa yanafanyiwa kazi.Hadi leo wahusika wa Richmond (achana na yule decoy mwenye kesi mahakamani) wanaendelea "kupeta".


Laiti Bunge lingekuwa na meno,isingetosha kwa Lowassa,Msabaha na Karamagi kujiuzulu tu.Walipaswa wakabidhiwe kwa vyombo vya dola.Kadhalika,watendaji wa serikali waliotajwa kuhusika walipaswa kuwajibishwa mara moja.Badala yake,hadithi zimeendelea kila kinapojiri kikao kingine cha bunge,huko waandishi wetu mahiri wa kunukuu wakija na vichwa vya habari kama "Moto kuwaka Bungeni","Ishu ya EPA kuibuliwa tena Bungeni"...Huwezi kuwalaumu sana kwa vile vyombo vya habari vinaendeshwa kibiashara na kichwa cha habari chenye mvuto kinauza gazeti!


Bunge lenye meno lisingekuwa linapigwa danadana na Waziri Ngeleja kuhusu ishu ya Kiwira.Bunge lenye meno lisingekubali mkataba wa TICTS uendelee kuwa hoja ya moto kila kikao lakini inayoishia kuwa ya moto pasipo mabadiliko,only for it kuwa ya moto tena kwenye kikao kingine.Yayumkinika kusema kuwa kama ni moto wa hoja,basi ni wa njiti ya kiberiti kwenye upepo mkali;hudumu kwa sekunde tu.


Sintajadili zaidi kwa vile itakuwa sawa na kupre-empty muswada wa chapisho naloandaa kama mapitio (majibu?) ya kitabu hicho cha wabunge hao.Ila kwa kifupi,si rahisi kuwa na bunge lenye meno wakati wabunge wenyewe wanaishi maisha tofauti na hao wanaopaswa kuwawakilisha bungeni (nikimaanisha maslahi yao).Tusidanganyane,mtu anayelipwa milioni 6 na ushee kwa mwezi hawezi hata chembe kuwa mwakilishi mzuri wa mtu asiye na uhakika wa kukamata angalau shs 10,000 kwa mwezi.Haya ni matabaka mawili tofauti,na japo kinadharia wabunge wanapaswa kuwa sehemu ya tabaka tawaliwa kwa maana ya uwakilishi wa wananchi,maslahi yao makubwa yanawaingiza kwenye tabaka tawala na hivyo kuwaweka kwenye mgongano wa moja kwa moja direct confrontation) na tabaka tawaliwa la wananchi wa kawaida.Katika hali hiyo,serikali kwa maana ya the executive branch of the government,inapata free pass kwani wanaopaswa kuihoji nao wanajikuta wakihojiwa na wanaowawakilisha.Kiuhalisia,mpiga kura is hardly represented bungeni.


Lakini tukiweka kando suala la kipato na matabaka,tatizo la msingi zaidi kwenye bunge hili ni kutanguliza mbele maslahi ya chama badala ya maslahi ya nchi.Umoja na mshikamano ndani ya CCM unatafsiriwa kuwa ni muhimu zaidi kuliko umoja na mshikamano wa kitaifa.Wengi wa wabunge wa CCM wanahofia kuzungumzia baadhi ya masuala yanayolihusu taifa ambayo kwa namna moja au nyingine yanaifanya CCM inyooshewe kidole.Hakuna mbunge wa CCM anayeweza kuzuia bajeti ya wizara flani,hata kama ni mbovu namna gani,kwa vile akifanya hivyo atatafsiriwa kuwa anavunja mshikamano wa chama.Mbunge katika bunge lenye meno hawezi kuogopa tafsiri ya chama chake,bali wapigakura wake.

Kwa anayehitaji nakala ya bure ya kitabu hicho cha BUNGE LENYE MENO (as an ebook),tuwasiliane.

1 comment:

  1. Well job done, Evarist, unajitahidi sana kuelimisha watanzania kwa makala zako zenye akili.

    Jenipher

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.