Showing posts with label JOHN CHEYO. Show all posts
Showing posts with label JOHN CHEYO. Show all posts

25 Jun 2011

Kabla ya kuwaletea habari na picha kuhusu ziara ya wabunge kadhaa waliokuja hapa Uingereza kufuatilia malipo ya fedha za rada,ninaomba kuweka bayana mtizamo wangu katika suala hili.Kwanza,naona kilichofanywa na wabunge hao ni mithili ya kuuza ng'ombe kwa ajili ya kesi ya kuku.Nilitamani walioongea na wabunge hao kuwauliza umuhimu wa wao kuwepo Uingereza muda huu ambapo kikao cha Bunge la Bajeti kinaendelea huko Dodoma.Kuna dharura gani kwa wao kuja hapa muda huu badala ya kusubiri kikao hicho cha Bunge kimalizike?Je wanawatendea haki wapiga kura wao?Na nani anawawakilisha wapiga kura wao wakati huu?

Nimesema hii ni sawa na kuuza ng'ombe kwa ajili ya kumudu kesi ya kuku kwa vile kila mbunge aliyekuja analipwa mamilioni ya fedha kama posho za kujikimu.Waheshimiwa hawa wanadai fedha za rada zitatumika kuendeleza elimu ya watoto huko nyumbani.Swali la kwanza,kwanini wasingeokoa fedha zinazotumika kama posho zao kwa muda wote watakapokuwa hapa Uingereza,kisha fedha hizo zikaelekezwa kwenye elimu ya watoto wetu huko nyumbani?Binafsi,nadhani suala hilo lingeweza kabisa kushughulikiwa na ubalozi wetu hapa Uingereza unless watuambie kuwa hawana imani na utendaji kazi na Balozi wetu Peter Kallaghe (ambaye ninamfahamu vizuri kuwa ni mchapa kazi mahiri tangu alipokuwa huko Foreign Affairs na Ikulu--nimefanya nae kazi pasipo kufahamiana,just in case you doubt my assessment of him).

Lakini la muhimu zaidi ni ukweli kwamba historia inatufundisha kwamba fedha za aina hii husihia mifukoni mwa wajanja wachache.Sana sana zitawezesha kumalizika kwa ujenzi wa mahekalu ya vigogo,kama sio kuongeza idadi ya nyumba ndogo zao na misururu ya magari yao ya kifahari.Hivi waheshimiwa hawa wanaweza kutuambia kwanini wanatolea macho hayo mamilioni ya rada ilhali wameshindwa kuhoji kuhusu marejesho ya fedha za EPA?Vipi kuhusu zile fedha za mfuko wa pembejeo?Vipi kuhusu "stimulus package" yetu ya kizushi?

Let's be honest,na nilitegemea sana wanahabari waliotuwakilisha kwenye press conference ya wabunge hao wangeibua hoja hizi,waheshimiwa hawa wamekuja Uingereza kutalii tu.Period!So far,katika habari husika hawatuelezi namna gani ujio wao utawezesha fedha hizo kupatikana,na kutuhakikishia kuwa kweli zitaelekezwa kwenye elimu ya watoto wetu.Remember,kamwe tatizo la viongozi wetu halijawahi kuwa kwenye upungufu wa maneno matamu bali utekelezaji wa ahaid wanazojiwekea wao wenyewe.

Anyway,naomba kuwasilisha habari husika kama nilivyotumiwa na Miss Jestina

Wabunge wanne waliokuja Uingereza kuzungumzia mgogoro wa pesa za kampuni inayouza vifaa vya ulinzi –BAE Systems wamefafanua namna zitakavyotumiwa. Wakiongea katika Ubalozi wetu Uingereza mjini London, Ijumaa mchana, viongozi hao walihimiza wanachofanya ni kufuatilia matokeo ya mahakama ya sheria inayochunguza rushwa (Serious Fraud Office-SFO) maana kadri muda unavyokwenda ndivyo riba inaongezeka.
Wabunge walikutana na House of Lords ambao ni maofisa na viongozi wa ngazi za juu sana wenye usemi mzito katika masuala ya kisisiasa Uingereza.

Mwezi Desemba mwaka jana SFO iliiamuru kampuni ya BAE kulipa faini paundi laki tano na kuipa serikali ya Tanzania paundi 29.5 milioni sawa na shilingi 75.3 bilioni za kitanzania kama pesa za kujisafisha uso. Toka tamko hilo litokee miezi sita iliyopita imezuka migogoro kadhaa.
Upande mmoja BAE system wanataka fedha zisipewe serikali ya Tanzania bali kwa mashirika ya fadhila toka nchi za nje upande mwingine uongozi wa Tanzania unasisitiza serikali inao mfumo imara utakaohakikisha fedha zitawafikia wahusika.

Mgogoro ulianza mwaka 1999 wakati Tanzania ilipotaka kununua vifaa vya kusaidia ulinzi wa viwanja vya ndege toka kampuni ya BAE. Ilidaiwa kuwa mfanya biashara Shailesh Vithlani wa kampuni ya Merlin aliyefanya dili kati ya BAE na Tanzania alipewa asilimia 30 ya pesa ya mauzo kama hongo. Pesa hizo ziliwekwa katika akaunti yake ya benki Uswisi. Wahusika wengine ni aliyekuwa Wakili wa Serikali, Andrew Chenge na Gavana wa benki kuu, Idriss Rashid. Wote hawajashtakiwa na Vithlani anadaiwa kujificha Uswisi, ilhali SFO imetoa tamko afikishwe mahakamani.

Akijibu swali kuhusu kutokuelewana huku, mwenyekiti wa msafara Mbunge Job Ndugai ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Taifa, alisema si vizuri BAE kutuingilia au kutueleza nini cha kufanya na pesa hizo ambazo ni maslahi yetu .
“Sisi tunafahamu mfumo gani utakaohakikisha pesa hizo zinatumika sawasawa, zikienda kwa mashirika ya ufadhili ni kama zimetolewa kwa watu wa nje.”

Mbunge mwingine, John Momose Cheyo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayohusika na Hesabu za Umma, aliwahakikishia wanahabari kwamba katika miaka kumi toka tukio hilo la 1999 vyombo vya serikali dhidi ya rushwa vimebadilika na kuimarika. “Matumizi halali ya fedha yatakahakikisha pesa zitatumika kujenga elimu,” alisema Mbuge huyo wa Bariadi Mashariki.

Toka SFO ilipoamuru BAE Systems ilipe faini kwa mahakama na fidia kwa Tanzania yametokea pia madai kwamba wapo walioandikia BAE barua pepe kuwa wasiilipe serikali ya Tanzania pesa hizo.
Wabunge wanasisitiza pesa zitaendeleza elimu.

Mbunge Maalum, Angellah Kairuki ambaye ni pia Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Utawala, alielezea kwamba ingawa pesa hizo zinaonekana nyingi lakini hazitasuluhisha matatizo yote ya elimu nchini, mathalan, kuongeza mishahara ya waalimu.
Alitoa mifano ya ukosefu wa madaftari, vyoo na vitabu vya kusaidia waalimu kufundisha. Mifano hiyo inayolenga shule za msingi na sekondari inatokana na matizo makubwa ya wanafunzi kujisaidia porini na kukosa vifaa muhimu vya elimu.

Mbunge Mussa Zungu wa Ilala, na vile vile Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, alikumbusha kwamba tatizo halikuanzwa na Watanzania. “Ni suala lililoamuliwa na mahakama ya Uingereza; sisi tuchohitaji ni kuendeleza elimu.”

Habari imeandikiwa na Freddy Macha akishirikiana Jestina George pamoja na
URBAN PULSE CREATIVE

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA

Na kwa kumalizia,tuache kumchosha Mungu kwa kutaka aibariki nchi yetu ilhali sie wenyewe hatujibidiishi kuifanya Tanzania kuwa lulu ya Afrika na pengine dunia kwa ujumla.Au tunamtaka Mungu aibariki nchi yetu ili mambo yakizidi kwenda mrama tumlaumu yeye badala ya kujilaumu kwa uzembe wetu?

Pia naomba kutoa wito kwa wanahabari wenzangu (hoping hamto-mind kukosolewa),let's go beyond the "photo-op" cancer inayowasumbua wengi wa wanahabari wenzetu huko nyumbani.Picha ni muhimu lakini la muhimu zaidi ni kuwabana viongozi wababaishaji kila wanapojipendekeza kuleta porojo zao.Mtakumbukwa kwa kuuwakilisha umma vyema na sio picha.Sorry guys,I think you could have done better than just reporting what they said.You just gave them a free pass na pengine bado hawaamini kama wamesalimika kuulizwa maswali magumu na Watanzania waliopo "dunia ya kwanza".

15 Jul 2009


na Charles Mullinda

IMEBAINIKA kuwa, Ofisi ya Bunge imetumia vibaya mamilioni ya shilingi yaliyotolewa na serikali kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2007/2008.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wabunge wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika mahojiano yao na Tanzania Daima Jumatano yaliyofanyika wiki iliyopita mjini Dodoma kwa wakati tofauti.

Wakizungumza kwa sharti la majina yao kutoandikwa gazetini, kwa kile walichoeleza kuwa ni kuogopa kuandamwa na baadhi ya wabunge wenzao, walisema ushahidi wa maelezo yao umo katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CGA) ya mwaka wa fedha wa 2007/2008.

Mmoja wa wabunge hao alieleza kuwa licha ya ripoti ya CGA kubainisha matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha katika Ofisi ya Bunge, Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, alizuia kujadiliwa kwa ripoti hiyo baada ya kushauriana na baadhi ya vigogo wa Ofisi ya Bunge, jambo ambalo linazuia kuchukuliwa hatua zozote za kisheria au kurekebisha hali hiyo hadi sasa.

Alisema Ofisi ya Bunge imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kuhakikisha ripoti hiyo haijadiliwi na PAC, kwa hofu kwamba inaweza kusababisha baadhi ya watendaji kuwajibishwa na baadhi ya wanasiasa kuchafuka majina yao.

Cheyo, Mwenyekiti wa PAC na Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), alipoulizwa na gazeti hili kuhusu madai hayo, alisema ni kweli ripoti ya CAG kuhusu matumizi ya fedha za serikali katika Ofisi ya Bunge si nzuri, kwa sababu inaonyesha upungufu mkubwa wa urejeshaji masufuru pamoja na matumuzi mengine mabaya ya fedha za ofisi hiyo.

Hata hivyo, alikana kuikalia ripoti hiyo kwa namna yoyote na kueleza kuwa, aliamua kuiweka pembeni baada ya kushauriana na kukubaliana na wajumbe wote wa kamati hiyo kuwa hawawezi kuijadili, kwa sababu walishindwa kumhoji Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ambaye wakati kamati hiyo akikutana kujadili ripoti mbalimbali za CGA kuhusu hesabu za taasisi za serikali, alikuwa hajaapishwa na rais kushika wadhifa huo.

“Ni kweli ripoti ya CAG kuhusu matumuzi ya fedha katika Ofisi ya Bunge si nzuri, inaonyesha upungufu mkubwa katika urejeshaji wa masurufu, na ripoti zote ambazo zinaonyesha hivyo kihasibu huwa ni mbaya. Sasa kwa Spika hii si nzuri, inamtia doa, anaweza asiaminike tena iwapo itawekwa wazi, kwa sababu ataonekana hafanani na kauli zake.

“Siyasemi haya kwa sababu nina kisasi na Spika, bali ni kwa sababu umeniuliza. Unajua Spika amenijeruhi hivi karibuni, sasa sitaki nionekana kama ninalipa kisasi. Lakini ukweli unabaki pale pale kwa sababu umeandikwa vitabuni kuwa kuna kasoro katika Ofisi ya Bunge ambayo inasimamiwa na Spika,” alisema Cheyo.

Spika Sitta alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Cheyo, alisema hahusiki kwa namna yoyote na uchukuaji wa masurufu, hivyo hapaswi kunyooshewa kidole iwapo imebainika kuwapo kwa kasoro zozote za matumuzi mabaya ya fedha za serikali katika ofisi yake.

Spika alisema taratibu ziko wazi kuwa wanaochukua masufuru kwa ajili yake ni wasaidizi wake wanaohusika kumuandalia safari zake zote, ndani na nje ya nchi.

“Mimi sihusiki kuchukua masurufu, wanaohusika ni wasaidizi wangu, sasa kama kuna kasoro, wao ndio wanajua. Nina ofisi yangu binafsi kama viongozi wengine wakuu wa kitaifa, sitembei na fedha mfukoni, wasaidizi wangu wa ofisi hiyo ndio wanaoniandalia safari na ziara zangu zote. Wao ndio wanaonilipia kila kitu, walinzi, maradhi, kila kitu, ndio wanaochukua fedha za masurufu kwa niaba yangu,” alisema Spika Sitta.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa alitumia fedha nyingi za Ofisi ya Bunge kugharamia vikao na tafrija zilizokuwa zikifanyikia nyumbani kwake wakati mkewe, Margaret Sitta, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, akiwania nafasi ya kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alisema madai hayo inabidi yafafanuliwe.

“Ninachokijua mimi kuhusu hili, ni kweli kulikuwa na vitu vya aina hiyo wakati huo, lakini ninachokumbuka ni kwamba gharama nyingi za mikusanyiko hiyo nilikuwa ninatumia fedha zangu za mfukoni, nilikuwa nalipa mwenyewe. Lakini hili ili nilielewe vizuri, inabidi lifafanuliwe,” alisema.

Naye Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah alipoulizwa kuhusu hali hiyo, alisema hawezi kuzungumza jambo hilo, kwa sababu alipoingia katika wadhifa huo alikuta hali hiyo imeshatokea.

Alibainisha kuwa ni kweli hakuhojiwa na Kamati ya PAC kwa sababu alikuwa hajaapishwa na rais, lakini kwa sasa kamati hiyo inaweza kuendelea na kazi zake kama kawaida, bila kupata kipingamizi kutoka kwa mtu yeyote.

“Mimi nilipoingia katika ofisi hii, hali hiyo niliikuta, hivyo siwezi kusema kitu, kwa sababu sikuwapo, siwezi kuizungumzia. Ninachoweza kukitolea maelezo ni kile ambacho kimefanyika wakati wa kipindi changu.

“Lakini suala la ripoti hiyo kukaliwa halipo, PAC ikitaka kukaa kuijadili hata kesho ni sawa tu, hakuna tatizo, waje wakae, wao wana ratiba zao za vikao, kuna ripoti nyingi tu hazijajadiliwa, hizi hazijakaliwa, naomba kwa sababu linahusu Ofisi ya Spika, isichukuliwe kuwa linazimwa,” alisema Dk. Kashililah.

Ripoti ya CAG, ambayo Tanzania Daima Jumatano imeiona, katika ukurasa wake wa 43, fungu la 42, inaitaja Ofisi ya Bunge katika orodha ya taasisi za serikali zilizopewa hati zenye shaka, kwa kukiuka taratibu za kihasibu.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa Ofisi ya Bunge ilifanya malipo ya matibabu nje ya nchi ya zaidi ya sh milioni 101 bila kuidhinishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, uhamisho wa fedha wa zaidi ya sh milioni 63 kutoka kifungu kimoja kwenda kingine bila kibali na malipo yenye thamani ya sh milioni 7.8 yalifanyika bila kibali.

Upungufu mwingine uliotajwa katika ripoti hiyo ni malipo yenye nyaraka pungufu ya sh milioni 526, malipo yasiyo halali ya sh milioni 102.5, malipo yenye shaka ya sh milioni 63.9, mishahara isiyolipwa na ambayo haikurejeshwa Hazina sh milioni 17.1, sh milioni 3.4 za mishahara ya watumishi walioachishwa kazi inayoendelea kulipwa kwenye akaunti zao benki na usuluhisho wa tofauti ya sh milioni 1.1 kati ya bakaa ya benki na bakaa inayoonyeshwa katika daftari la mapato na matumizi haukufanyika.

Marekebisho yasiyostahili yaliyojumuishwa kwenye hundi ambazo hazijawasilishwa benki ni sh milioni tano, masurufu maalumu ya sh milioni 50.2


KINACHOKWAMISHA VITA DHIDI YA UFISADI NI HUU MTINDO WA KUENDESHA MAMBO KISHKAJI.UKITAFAKARI KAULI YA CHEYO KUHOFIA KUHUSISHA HABARI ZA UFISADI HUO NA HATUA YA SPIKA KUMTOA NJE YA BUNGE HIVI KARIBUNI UTAGUNDUA KUWA BADALA YA MBUNGE HUYO KUSHUGHULIKIA SUALA HILO KAMA MWENYEKITI WA KAMATI HUSIKA,YEYE ANAJIONA KAMA JOHN MOMOSE CHEYO ALIYETOLEWA NJE NA SAMUEL SITTA,BADALA YA OFISI YA BUNGE ILIYO CHINI YA SPIKA NA WATENDAJI KADHAA.

NA UNAFIKI MWINGINE NI WA HAO WABUNGE WALIONUKULIWA KATIKA HABARI HII AMBAYO HAWATAKI KUTAJWA MAJINA KISA WANAOGOPA KUANDAMWA NA WABUNGE WENZAO.KWANI WALIINGIZWA BUNGENI NA HAO WABUNGE WENZAO WANAOWAOGOPA AU WANANCHI HUKO MAJIMBONI?

WIZI MTUPU!


29 Jun 2009

Bwana Mapesa,John Momose Cheyo,Mbunge wa Bariadi kwa tiketi ya UDP akitoka nje ya jengo la bunge baada ya kukumbana na makali ya viwango na spidi vya Mheshimiwa Spika Samuel Sitta.Ironically,Cheyo ni mwandishi-mwenza (co-author) wa kitabu BUNGE LENYE MENO.

CHANZO: Jamii Forums

18 Jun 2009


Hivi karibuni watunga sheria (wabunge) wetu watatu "waliungana" kuandika kitabu walichokipa jina "BUNGE LENYE MENO".Ukiangalia sehemu ndogo tu ya wasifu wa wabunge hao utamaizi kuwa "muungano huo wa uandishi" ulikuwa ni mithili ya "ndoa za makaratasi" (marriages of inconvenience).

Dkt Wilbroad Slaa,Spika Samuel Sitta na John Momose Cheyo!Nadhani kitu pekee kinachoweza kuwafanya wafanane ni "wote ni wabunge",and the similarity stops there.Wakati Dkt Slaa amejijengea jina kubwa kama kinara wa mapambano ya ufisadi,ni vigumu kum-define Spika Sitta linapokuja suala la mapambano dhidi ya ufisadi.Lakini si vigumu kukumbuka kuwa ni Sitta huyuhuyu aliyempa kadi nyekundu Zitto Kabwe alipombana ex-waziri Nazir Karamagi kuhusu sakata la Buzwagi.Na ni Sitta huyuhuyu aliyetishia kumshtaki Dkt Slaa alipoibua tuhuma ufisadi ndani ya Benki Kuu akidai kuwa ni ushahidi wa kufoji!Eti leo tunaambiwa Spika huyuhuyu nae ni kinara wa mapambano ya ufisadi!


Tukija kwa John Cheyo,nadhani amebaki kuwa UDP,kwa maana ya one-man party.Sera yake ya mapesa ilijaa utani ambao ungekuwa na maana zaidi kwenye sanaa za maigizo kuliko katika siasa makini.Amebaki kuwa jina tu.Sidhani kama kunamfano wowote hai unaoweza kutumika kumtambulisha Cheyo kama mwanaharakati wa mapambano dhidi ya ufisadi.


Sasa hao ndio waandishi wa kitabu BUNGE LENYE MENO.Lakini kwa vile nafahamu kwamba uchambuzi makini unahitaji kwenda mbali zaidi ya kuangalia personalities,naomba kugeukia hoja yangu ya kupingana na ya akina Sitta kuwa bunge la sasa lina meno.Binafsi nasema kama ni meno basi ni ya plastiki.Nadhani unafahamu mtoto mchanga anapoanza kuota meno huwa yanaota meno ambayo yanaitwa meno kwa vile tu yamekaa sehemu yalipo meno.Ukimnywesha uji wa moto basi kilio chake hapo ni balaa!Ni meno machanga yasiyomudu kutafuna vitu vigumu.


Na ndio bunge letu lilivyo.Utasikia kelele,vitisho,na vitu kama hivyo kila waheshimiwa wanapokutana hapo Dodoma ambapo mwisho wa siku akaunti zao zinaingiza kipato cha zaidi ya mwezi mzima kwa Mtanzania wa kawaida,huku kila mwisho wa mwezi wakiondoka na mamilioni lukuki.Basi angalau kipato chao kingeendana na hali halisi ya uchumi wa nchi yetu.


Wabunge wa CCM,ambao wanatengeneza zaidi ya robo tatu ya bunge letu,ndio vichekesho zaidi.Utamsikia huyu akisema hili kabla ya mwenzie kumkalia kooni akitaka mwongozo wa Spika kwa madai ya "kukiuka kanuni za bunge".Lakini ukifuatilia kwa makini,mara nyingi mwongozo huo huombwa pale anapojitokeza mbunge mmoja kuelezea yale yanayozungumzwa na Watanzania wengi mitaani,kwa mfano ishu ya ufisadi.Sasa kwa vile kuna wabunge wenye deni kubwa zaidi kwa CCM na vigogo wake,njia pekee ya kulipa deni hilo ni kuomba mwongozo wa Spika ili kuwaziba midomo wale wanaoongea yasiyopendeza masikioni mwa watawala.


Majuzi,Mbunge wa Nzega Lukas Selelii amemwomba Mungu awalaani mawaziri kwa madai kwamba wamekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya ufisadi nchini.Mbunge wa Pangani Mohammed Rished akaomba mwongozo....sijui kuonyesha anafahamu zaidi sheria za Bunge au kwa vile yaliyoongelewa na Selelii hayakumpendeza mbunge Rished.Kwani si kweli kwamba maamuzi mengi yaliyopelekea skandali za ufisadi yalipitishwa na Baraza la Mawaziri?Kabineti ingetimiza wajibu wake tungekuwa na Richmond?au Kiwira?Au TICTS?au Buzwagi?Au IPTL?Orodha ni ndefu.Sasa Rished alihitaji mwongozo kwa vile Selelii kumuomba Mungu awalaani watu waliofanya maamuzi yaliyopelekea ufisadi ni kosa la jinai au?Halafu tunaambiwa tuna "bunge lenye meno"!In this case,haya wala si meno ya plastiki bali ni mapengo kabisa.


Fuatilia kwa karibu mjadala wa Bajeti unavyoendelea huko Dodoma.Kuna kauli za uchungu kutoka kwa baadhi ya wabunge kama Selelii,Mwambalaswa,Mpendazoe na,kama kawaida,wabunge wa upinzani kama vile Dkt Slaa.Lakini kauli pekee hazimsaidii Mtanzania masikini asiyejua hatma ya maisha yake.Kelele hizi zimekuwepo tangu bunge hili linaanza.Ndio,zimesaidia kuundwa kwa kamati mbalimbali kama ile ya Mwakyembe.Lakini kuunda kamati kisha kutofanyia kazi mapendekezo yake ni sawa na ufisadi tu.Ikumbukwe kuwa kamati hizo hutumia mamilioni ya fedha za walipa kodi.Ukubwa wa gaharama za kuendesha kamati za aina hiyo ungeweza kupunguziwa maumivu laiti mapendekezo yanayotolewa yangekuwa yanafanyiwa kazi.Hadi leo wahusika wa Richmond (achana na yule decoy mwenye kesi mahakamani) wanaendelea "kupeta".


Laiti Bunge lingekuwa na meno,isingetosha kwa Lowassa,Msabaha na Karamagi kujiuzulu tu.Walipaswa wakabidhiwe kwa vyombo vya dola.Kadhalika,watendaji wa serikali waliotajwa kuhusika walipaswa kuwajibishwa mara moja.Badala yake,hadithi zimeendelea kila kinapojiri kikao kingine cha bunge,huko waandishi wetu mahiri wa kunukuu wakija na vichwa vya habari kama "Moto kuwaka Bungeni","Ishu ya EPA kuibuliwa tena Bungeni"...Huwezi kuwalaumu sana kwa vile vyombo vya habari vinaendeshwa kibiashara na kichwa cha habari chenye mvuto kinauza gazeti!


Bunge lenye meno lisingekuwa linapigwa danadana na Waziri Ngeleja kuhusu ishu ya Kiwira.Bunge lenye meno lisingekubali mkataba wa TICTS uendelee kuwa hoja ya moto kila kikao lakini inayoishia kuwa ya moto pasipo mabadiliko,only for it kuwa ya moto tena kwenye kikao kingine.Yayumkinika kusema kuwa kama ni moto wa hoja,basi ni wa njiti ya kiberiti kwenye upepo mkali;hudumu kwa sekunde tu.


Sintajadili zaidi kwa vile itakuwa sawa na kupre-empty muswada wa chapisho naloandaa kama mapitio (majibu?) ya kitabu hicho cha wabunge hao.Ila kwa kifupi,si rahisi kuwa na bunge lenye meno wakati wabunge wenyewe wanaishi maisha tofauti na hao wanaopaswa kuwawakilisha bungeni (nikimaanisha maslahi yao).Tusidanganyane,mtu anayelipwa milioni 6 na ushee kwa mwezi hawezi hata chembe kuwa mwakilishi mzuri wa mtu asiye na uhakika wa kukamata angalau shs 10,000 kwa mwezi.Haya ni matabaka mawili tofauti,na japo kinadharia wabunge wanapaswa kuwa sehemu ya tabaka tawaliwa kwa maana ya uwakilishi wa wananchi,maslahi yao makubwa yanawaingiza kwenye tabaka tawala na hivyo kuwaweka kwenye mgongano wa moja kwa moja direct confrontation) na tabaka tawaliwa la wananchi wa kawaida.Katika hali hiyo,serikali kwa maana ya the executive branch of the government,inapata free pass kwani wanaopaswa kuihoji nao wanajikuta wakihojiwa na wanaowawakilisha.Kiuhalisia,mpiga kura is hardly represented bungeni.


Lakini tukiweka kando suala la kipato na matabaka,tatizo la msingi zaidi kwenye bunge hili ni kutanguliza mbele maslahi ya chama badala ya maslahi ya nchi.Umoja na mshikamano ndani ya CCM unatafsiriwa kuwa ni muhimu zaidi kuliko umoja na mshikamano wa kitaifa.Wengi wa wabunge wa CCM wanahofia kuzungumzia baadhi ya masuala yanayolihusu taifa ambayo kwa namna moja au nyingine yanaifanya CCM inyooshewe kidole.Hakuna mbunge wa CCM anayeweza kuzuia bajeti ya wizara flani,hata kama ni mbovu namna gani,kwa vile akifanya hivyo atatafsiriwa kuwa anavunja mshikamano wa chama.Mbunge katika bunge lenye meno hawezi kuogopa tafsiri ya chama chake,bali wapigakura wake.

Kwa anayehitaji nakala ya bure ya kitabu hicho cha BUNGE LENYE MENO (as an ebook),tuwasiliane.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube