Showing posts with label THE ROAD TO 2010. Show all posts
Showing posts with label THE ROAD TO 2010. Show all posts

9 Apr 2010

JK alisaini sheria hiyo kwa mbwembe kama alivyoahidi.Siku chache baadaye,Dkt Wilboard Slaa akaibua hoja kuhusu 'usanii' uliofanyika kuongeza vipengere katika Sheria hiyo.Spika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakatetea 'usanii' huo.Licha ya mlolongo wa matukio hayo kuashiria kuwa sheria hii yenye nia njema itabaki kuwa maandishi tu,walengwa wakuu wa sheria hiyo wameamua kuipuuza na 'misaada' inatolewa kama kawaida katika kujitengenezea mazingira ya ushindi kwenye uchaguzi. Dk. Nkya kujitosa ubunge Morogoro Kusini Mashariki

na Joseph Malembeka, Morogoro

NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Lucy Nkya, ametangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo la Morogoro Kusini Mashariki.
Dk. Nkya alitangaza nia hiyo akiwa katika ziara ya kukagua maenndeleo na utekelezaji wa ahadi alizotoa baada ya kuchanguliwa kuwa mbunge wa Viti Maalum.

“Nawatakeni wanachama wenzangu ndani ya CCM muelewe kuwa na mimi nakuja huku mbali na kuwa kuna wenzangu waliotangaza nia hii,” alisema Dk.Nkya.

Dk. Nkya ambaye kwa nyakati tofauti alikabidhi vitu mbalimbali yakiwemo mabati, vipaza sauti, saruji, vyerehani, misumari, baiskeli na fedha taslimu sh 1,500,000 kwa wananchi na wana CCM katika kata mbalimbali aliwataka wana CCM kukiimarisha chama na wao kiuchumi.

“Sasa hivi tunakwenda kwenye hekaheka za uchaguzi ila nawatakeni mbali na siasa jiimarisheni kiuchumi kwa kulima mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame tuepukane na janga la njaa,” alitahadharisha Dk. Nkya.

Dk. Lucy Nkya anakuwa miongoni mwa watu saba walioonyesha nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo. Wengine ni mbunge wa sasa wa jimbo hilo (Samir Lotto), Jamira Mohamed, Amani Mwenigoha, Gabriel Mkwawe, Semindu Pawa na Salumu Salum Mkangala.

CHANZO: Tanzania Daima.

2 Feb 2010


Hivi karibuni Tume ya Uchaguzi ilieleza kwamba inaangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya majimbo ya uchaguzi.Niende moja kwa moja kwenye hoja yangu: ni rahisi kwa Tume hiyo kuwa na wazo kama hilo kwa vile halina athari zozote kwenye mishahara au posho zao.Kinyume chake,tunaambiwa zoezi la tathmini linatarajiwa kugharimu mabilioni ya shilingi.Unadhani zinakwenda wapi hizo kama si kwa haohao wanaokuja na wazo la kuongeza majimbo?

Mzazi mwenye busara hawezi katu kufikiri kuongeza idadi ya watoto wakati hao alionao sasa "wanampelekesha" linapokuja suala la kumudu gharama za matundo/malezi.Ni katika mantiki hiyohiyo,Tume ya Uchaguzi,ilipaswa kutambua kuwa uwezo wetu kiuchumi hauwezi kumudu majimbo zaidi ya hayo tuliyonayo sasa.

Lakini jingine lililo muhimu zaidi ni kuangalia ufanisi wa wawakilishi tulionao sasa.Naamini wengi tutaafikiana kwamba idadi kubwa ya wabunge hadi sasa haijasaidia kumkomboa Mtanzania kutka kwenye lindi la umasikini wa kutupwa.Tunashuhudia jinsi Bunge na Serikali wanavyotunishiana misuli kuhusu mazingaombwe ya Richmond,Kiwira,nk.Je kuongeza idadi ya wabunge kutaongeza "misuli zaidi" kwa Bunge.Jibu la haraka ni HAPANA.

Wengi wa wabunge wetu ni wabinafsi wanaoangalia maslahi yao binafsi.Umuhimu wa wapiga kura wao na majimbo wanayowakilisha unakuja pale tu kunapojiri uchaguzi.Wabunge,hususan wa CCM,wameweka mbele maslahi ya Chama kuliko wananchi wanaowawakilisha.Hilo lisingekuwa tatizo kama CCM ingekuwa chama kinachowajali wananchi badala ya mafisadi.

Na kwanini wazo la majimbo mapya lije mwaka huu tunapotarajia uchaguzi mkuu?Kwanini sio mwaka jana,juzi au 2007?Jibu jepesi ni kwamba wazo la majimbo mapya halina uhusiano na kukuza demokrasia au kuongeza uwakilishi bali ni kuwatafutia ulaji vigogo wanaonyemelea ubunge au wale ambao ubunge wao uko hatarini kutokana na upinzani kwa wanaotaka nafasi hiyo.

Nihitimishe kwa kueleza kuwa kuongeza idadi ya majimbo si moja ya vipaumbele vyetu kwa sasa.Pengine badala ya wazo hilo la kuwatengenezea watu ulaji,Tume ingetafakari ni namna gani wapiga kura watawezeshwa kuwabana wawakilishi wasiotekeleza wajibu wao majimboni.Tume pia inapaswa kuelewa kwamba wabunge watakaoongezwa pindi wazo la majimbo mapya likikamilika watapaswa kuongoza watu "hai",na ili "uhai" wa watu hao uwe na uhakika wa kuwepo ni muhimu kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa kurekebisha hali ya uchumi wetu,sambamba na kuwabana mchwa (mafisadi) wanaotafuna kila kidogo tulichonacho.

4 Jan 2010


Je mama Kikwete ameanza kampeni kwa ajili ya mumewe?

na Nkwazi Mhango

Siku hizi mke wa rais, Salma Kikwete, anaonekana kwenye kurasa za mbele za magazeti karibu kila siku akiwa mikoani akihamasisha hili na lile. Wengi wanahoji. Kwanini sasa na si tangu mwanzo mume wake alipoingia ikulu? Na kwanini asiseme wazi kuwa anampigia kampeni mumewe? Maana, inajulikana alivyo mwana CCM damu damu tena mjumbe wa vikao vyake?

Watetezi wake wanaweza kusema anafanya kazi ya shirika lake lisilo la kiserikali la WAMA. Haiwezekani mumewe akawa mkuu wa serikali naye akawa na shirika lisilo la kiserikali kusiwe na mgongano wa kimaslahi kisheria. Uzoefu tulioupata toka kwa Anna Mkapa ungetosha kumsaidia rais Jakaya Kikwete kuondokana na aina hii ya ufisadi sugu na unyemelezi kwa kutumia mgongo wa ikulu kama angekuwa ni mtu wa kujifunza na kudhamiria kutenda haki kwa taifa.

Ngo yake ni ya mashaka-kwanini ianzishwe baada ya mumewe kuwa rais? Kuanzisha NGO baada ya mume kuwa rais ni ishara tosha ya ufisadi na usasi wa ngawira. Mbona hatuoni wake wa viongozi wa vyama vingine wakiwa na NGOs? Hata wakiwa nazo nani atazichangia iwapo wanaochangia NGOs za wake wa marais wanatafuta kuwa karibu na ikulu ili waihujumu nchi kwa kupata upendeleo kama ilivyokuwa kwa EOTF ambayo ilitumiwa na watu wengi kuliibia taifa? Mke wa Kaisari hapaswi kutenda tendo lenye kuweza kutia shaka au doa utawala wa mumewe.

Tuliishi na kumuona baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere. Mkewe-mama Maria-hakuwahi kujihusisha na upuuzi mdogo mdogo wa kutafuta pesa kwa mgongo wa mumewe.

Niliwahi kuwaandikia barua EOTF na WAMA kuwaonya juu ya hatari ya kuitumia ikulu. Hawakuwahi kunijibu zaidi ya kufumba macho na kuendelea kutengeneza pesa kwa mgogo wa ikulu. Ila nafurahi. WAMA wamefanya jambo moja (la maana la kuondoa aibu)-kuondoa maneno yasemayo WAMA Foundation the office of the First Lady of the United Republic of Tanzania kwenye wavuti wao. Niliandika baruapepe ifuatayo kwa WAMA tarehe 3 Septemba 09:

Kama mzalendo, nimejaribu kukusanya baadhi ya maoni kuhusiana jinsi ufisadi unavyoingia ikulu kiasi cha kututatiza. Kwa sasa Anna Mkapa mke wa rais wa zamani na mumwe wako msambweni. Ukiangalia kinachofanywa na WAMA hakina tofauti na Fursa sawa kwa Wote (Wake za wakubwa).
Kuondoa aibu, nimejitolea kuwasiliana nanyi ili angalau mjue tunavyojihisi kwenye wimbi hili la ufisadi wa kutumia madaraka ya waume zenu. Mama Salma NGO yako ni ulaji mtupu kusema ukweli. Acha kuna kesho. Ni uamuzi wako kuamua. Kuna kesho wakati madaraka yatakuwa mikononi mwa wengine. Hasa nikizingatia kilichompata Regina Chiluba ambacho kinapaswa kumpata hata Anna Mkapa, nimeona bora niseme hata kama nitapuuziwa. Ila najua ujumbe utafika. Someni alama za nyakati na mjue kuwa madaraka yana mwisho na yanalevya. Kuna siku mtakumbuka mchango huu.
Kila la heri,

Bahati mbaya sana , hata wavuti wa Kurungenzi ya habari Ikulu unaonekana kutangaza biashara ya WAMA badala ya wizara za serikali! Ajabu hakuna anayestuka wala kupiga kelele!

Kama umma ukishupaa NGO hii inaweza kufutwa hata na mahakama kutokana na mgongano wa maslahi ukiachia mbali kuwa kichaka cha ufisadi kutokana na uwezekano wa kuchangiwa pesa chafu kutokana na kutokuwapo sheria makini ya kuchuja na kutangaza wafadhili wa WAMA.

Hata hivyo nimefarijika kuwa sauti yangu imesikika na fedheha imeondoka. Maana neno Jamhuri ya Muungano, kisheria, halipaswi kutumiwa na mtu au taasisi yoyote isipokuwa mihimili mitatu ya dola yaani Bunge, Mahakama na Utawala. Cheo cha Ofisi ya First lady hakimo katika katiba yetu.

Kwanini mapenzi kwa wanawake na watoto yaanze baada ya kuupata urais kama siyo gea ya kuitumia vibaya ikulu? Ina maana rais na washauri wake hawalioni hili au wameridhia kwa sababu NGO ya mke wa rais inaweza kutumika kama kivuli cha kuanza kampeni hata kabla ya tume kutanganza hivyo? Inabidi tustuke. Ajabu hata wapinzani hawajaliona hili!

Tanzania inaweza kuwa nchi pekee ambapo rais na mkewe wote ni marais. Kikwete ni rais wa jamhuri huku mkewe akiwa rais wa WAMA. Ukitaka kujua hili jikumbushe mapokezi anayopewa na coverage anayopata Salma kwenye vyombo vya habari. Ajabu ukitafuta uhalali wake kikatiba haupo!

Hata kama anajulikana kwa ubabe na upayukaji wake, bado mke wa rais wa Kenya Lucy Kibaki hana mamlaka kama aliyo nayo Salma ambaye anaweza kuingia mkoa wowote kwa kisingizio cha NGO yake na kufanya shughuli za kisiasa kama kulakiwa na viongozi wa mikoa na kukagua miradi ya maendeleo ukiachia mbali kutoa kauli mbiu zinazoonyesha wazi kumpigia debe mumewe.

Salma anchomzidi Lucy ni ile hali ya kufanya kitu waitacho waingereza one woman show. Kwani kila lilipo jina WAMA yupo yeye. Hii maana yake ni kwamba yeye ni dikteta na mpenda madaraka anayetaka kufanya kila kitu peke yake. Kwanini hatuoni makamu wake au hata wasaidizi wengine wakifanya shughuli za WAMA kama kweli ni ya umma kama anavyodai? Kuthitibitisha hili, tembelea tovuti ya WAMA uone ukweli huu. Hii haiwezi ikawa taasisi ya wanawake na watoto wa Tanzania .

Kuonyesha kuna namna ya kampeni na kutumia mamlaka ya mume wake, hivi karibuni, Mama Kikwete amewahi kutoa namba yake ya simu ya mkononi ambayo ni 0754-294450 kwa wanawake mkoani Singida ili waweze kumpigia au kumtumia ujumbe mfupi wa maneno pindi waume zao watakapowanyanyasa kutokana na kitendo cha wao kwenda kupima kwaajili ya kujua afya zao. Japo kwa juu hili linaweza kuonekana ni jambo bora, kwa mtu anayejua mipaka ya mamlaka yake na utaratibu wa utawala kisheria, angeshauri wahusika waelekeze madai yao kunakohusika-polisi, vituo vya kutetea haki za binadamu hata wizarani.
Licha ya kuwa ubabe, hii ni kampeni ya wazi kuonyesha wahusika wanawajali wananchi jambo ambalo si kweli. Kwanini hasira zake zisielekezwe kwenye kumshauri mumewe kupambana na ufisadi kama ana uchungu na nchi hii? Yaani hajui kuwa ujinga na umaskini ndivyo vyanzo vya haya yote? Sijui hata kwenye kupokea misaada anauliza usafi wa mtoaji.

Kwa nijuavyo upenzi wa sifa wa watawala wetu na watu wao, kama utafanyika uchunguzi huru juu ya matumizi ya MAWA, ushingae pesa inayotumiwa kwenye ziara ikawa kubwa kuliko hiyo inayowafikia walengwa. Bahati mbaya sijwahi kusoma popote taarifa ya mahesabu ya mwaka ya si WAMA wala EOTF.

Wengi wanaweza kuona kama tunamuandama mke wa rais au kutotambua umuhimu wa kupigania haki za akina mama. Kwanini mke wa rais wakati tuna wizara yenye watendaji wanaolipwa pesa ya kodi yetu? Kwanini misaada hiyo anayopokea isipelekwe wizarani au kwenye mashirika huru kama kweli ana uchungu na walengwa na si kujipatia umaarufu, pesa na kubwa zaidi kutumia ikulu kwa manufaa binafsi yawe yake au mumewe na marafiki zake?

Je Salma Kikwete ameanza kampeni kwa ajili ya mumewe hata kabla ya kipenga kupulizwa? Je akina mama wa Tanzania wataingia mkenge wake huku waume na kaka zao wakizidi kuteswa na sera za Kikwete za kuvumilia mafisadi? Je atawalainisha wasahau kuwa Kikwete hajatimiza ahadi hata moja? Je watahoji uhalali wa NGO yake na kumwambia ukweli kuwa ni ya mashaka na ulaji?

19 Dec 2009


Ahadi za urais 2005 zamtesa Kikwete uchaguzi wa mwakani

Rais Jakaya Kikwet, mzigo mzito wa ahadi zake za mwaka 2005 unamkabili uchaguzi ujao 2010.
Na Mwandishi Wetu
MIEZI michache ikiwa imebaki kabla ya kuanza kwenda kwa wananchi kuomba ridhaa ya kuongoza nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano, Rais Jakaya Kikwete anaonekana kukabiliwa na mzigo mzito wa kutekeleza ahadi nyingi alizozitoa wakati wa kampeni za mwaka 2005.

Kikwete alipata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 baada ya kunyakua takriban asilimia 80 ya kura, akiwa pia ameshinda kwa kishindo dhidi ya wapinzani wake kwenye uteuzi wa mgombea wa CCM.

Lakini kadri muda unavyokwenda ndivyo umaarufu wake unaonekana kupungua huku tafiti mbalimbali zikionyesha kuwa umaarufu aliokuwa nao wakati akiingia madarakani unaendelea kuporomoka, ikiwa ni miezi tisa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Wakati akizunguka sehemu mbalimbali nchini kuomba kura za wananchi, Kikwete alikuwa akitoa ahadi kem kem ambazo alizielezea kwa kifupi kwenye kauli mbiu yake ya â€Å“Naisha Bora kwa Kila Mtanzania” ambayo mkakati wake wa kuitekeleza ulikuwa ni â€Å“ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya”.

Mbali na ahadi ambazo alikuwa akizitoa kwa wananchi kila sehemu alipoelezwa tatizo, ikiwa ni pamoja na matatizo sugu ya maji, miundombinu, huduma za afya na pembejeo, Rais Kikwete pia alitoa ahadi za ujumla kabla na baada ya kushinda uchaguzi kumrithi Benjamin Mkapa.

Baadhi ya ahadi hizo za Rais Kikwete kabla na baada ya kuingia madarakani ni pamoja na kuweka kipaumbele katika kilimo, akitumia kaulimbiu ya Kilimo Kwanza, kupitia upya mikataba ya madini ili inufaishe nchi na wawekezaji, na kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi wa elimu ya juu anayekosa masomo kwa kukosa karo.

Ahadi nyingine ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za umma, kuumaliza mgogoro wa Zanzibar, kuimarisha uhusiano wa kimataifa, kukomesha tatizo la ufisadi, kupambana na tatizo la uhalifu, ikiwa ni pamoja na biashara ya dawa za kulevya na ujambazi, kuandaa mdahalo wa kitaifa wa michezo kwa lengo la kuinua michezo na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma....INAENDELEA HAPA

13 Sept 2009


Lowassa Tishio Ndani ya CCM

Nguvu ya kundi lake yatawala ndani ya NEC

KUNA kila dalili kwa aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa, kupitishwa na vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2010.

Taarifa za kuaminika kutoka kwa vigogo kadhaa ndani ya CCM na kwa baadhi ya wabunge wa chama hicho kikongwe nchini, zimethibitisha nia ya Lowassa kuwania kiti hicho, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa kupitishwa na vikao vya juu kuwa mgombea pekee badala ya Rais Jakaya Kikwete, anayetarajiwa kuomba tena nafasi hiyo ili kumalizia kipindi kingine cha miaka mitano cha kuliongoza taifa.

Taarifa hizo zimefafanua kuwa nafasi ya Kikwete kupitishwa na CCM kuwa mgombea urais haitabiriki iwapo Lowassa ataamua kuwania nafasi hiyo ambayo pia humpa nafasi kiongozi kuwa mwenyekiti wa chama.

Ikiwa imesalia miezi 13 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, tayari Lowassa anaonekana kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama, huku akiungwa mkono na wajumbe wengi wa vikao vya juu, hususan wale wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC).

Siku moja tu baada ya Rais Kikwete, kuzungumza na wananchi kwa staili mpya ya kujibu maswali ya papo kwa papo, Tanzania Daima Jumapili, ilizungumza na mbunge mmoja maarufu wa CCM, juu ya mustakabali wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010, kwa sharti la kutotajwa jina lake.

“Kwa NEC hii niliyoiona kwenye kikao kilichopita, Lowassa anaweza kabisa kupitishwa kuwa mgombea urais wa CCM 2010 badala ya Bwana Mkubwa (Kikwete). Maana kwanza urais anautaka na jinsi nilivyoiona hii NEC, wajumbe wengi tayari wamesha declare interests kwa Lowassa …wengi wanamuunga mkono na ndiyo maana tumekuwa na vita kali ya makundi ndani ya chama.

“Kwa kweli Bwana Mkubwa sijui hali itakuwaje, nafasi ya kupitishwa kwake eti kwa sababu ni rais anayemaliza muda wake itakuwa ngumu sana, niseme tu kwamba haitabiriki,” alisema mbunge huyo aliyejizolea umaarufu kwa kupambana na ufisadi.

Nguvu ya Lowassa ndani ya NEC ndiyo inayodaiwa nusura imwangushe Spika wa Bunge, Samuel Sitta, baada ya wajumbe wengi kudai kwamba anaihujumu serikali bungeni, hivyo kupendekeza avuliwe uanachama, hali inayotafsiriwa kuwa walikusudia kulipiza kisasi dhidi ya hatua ya spika huyo kuunda Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la Richmond na ripoti yake kusababisha Lowassa kujiuzulu.

Kwa upande mwingine, baadhi ya vigogo kadhaa wa CCM wamekanusha kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa wiki hii kwamba kuna uadui miongoni mwa wabunge na baina ya wabunge na mawaziri, na kufafanua kuwa uadui uliopo ni baina ya baadhi ya wabunge na chama chao.

“Alichosema rais kwamba wabunge wana uadui hata wanafikia hatua ya kuogopana, kwamba wanaweza kuwekeana sumu, kwa kweli si sahihi, uadui uliopo si kati ya wabunge na wabunge, bali ni kati ya baadhi ya wabunge na chama chenyewe. Kwani waliotaka kumsulubu Sitta kwenye NEC ni wabunge wenzake? Si wabunge wenzake, walikuwa ni wajumbe tu wa kikao kile cha chama, ambao wengi wako upande wa Lowassa. Wao bado wana kisasi na lile suala la Richmond na wako wengi kweli,” alisema kigogo huyo wa CCM.

Lowassa ambaye inaaminika kuwa ni rafiki wa siku nyingi wa Rais Kikwete, alijiuzulu uwaziri mkuu Februari 2007, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kutoa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni ‘hewa’ ya Richmod Development Company LLC.

Baadhi ya watu walio karibu na watu hao wanadai tangu kujiuzulu kwake, amekuwa katika kundi tofauti na Kikwete, huku akiwa na nguvu kubwa ya kichama inayodaiwa kuzidisha uhasama wa kimakundi ndani ya chama hicho.

Mbali ya nguvu hiyo ya kichama, wadadisi wa mambo waliozungumza na gazeti hili, walisema uwezekano wa Lowassa kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa serikalini unatokana na ukweli kuwa mwenendo wa hivi karibuni wa utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu sakata la Richmond umeonekana kumsafisha mwanasiasa huyo kuwa hakuhusika kabisa katika sakata hilo, kwani tayari serikali yenyewe imeshatangaza kutowachukulia hatua baadhi ya watendaji waliokuwa chini yake kwa sababu ya kile kilichoelezewa kuwa hawakuhusika katika sakata hilo.

Katika mkutano wa 16 wa Bunge, serikali ilitangaza kuwa haijawachukulia hatua baadhi ya watumishi wake kadhaa ilioagizwa na Bunge, kwa sababu ya kutobainika kuhusika na mazingira ya rushwa na kuwafanya waipe ushindi wa zabuni ya kuzalisha umeme Kampuni ya Richmond.

Miongoni mwa watumishi ambao kamati teule ya Bunge iliyokuwa chini ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ilipendekeza wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria lakini hawakuchukuliwa hatua kama ilivyopendekezwa na Bunge ni Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika, huku Mkurugenzi wa Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, akichukuliwa hatua ndogo ya kuonywa.

“Lowassa anaweza kabisa kugombea urais, kwa sababu tayari jina lake limeshatakata, maana serikali yenyewe imeshasema kwamba kina Mwanyika hawakuwa na makosa yoyote katika suala la Richmond. Sasa kama Mwanyika hakuwa na kosa basi ni dhahiri kuwa kwa mtazamo wa watu Lowassa alionewa tu, kwa hiyo anaweza kabisa kufufuka kisiasa na kugombea urais,” alisema.

Wakati hali ikiendelea hivyo, hatima ya vita hiyo ya makundi sasa inaonekana kumtegemea Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati maalumu iliyoundwa na Kikwete ili kufanya kile kinachoelezewa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa kama utafiti wa kutafuta suluhu ya kuinusuru CCM kutoka kwenye vita hiyo.

Wakati kamati hiyo ina wajumbe wengine kama Abdulhaman Kinana na Pius Msekwa, ni Mwinyi pekee anayeonekana kuungwa mkono na wana CCM wa makundi yote, hivyo kuwa tegemeo pekee katika kutafuta suluhu, kwani wajumbe wenzake bado wanaonekana kuwa ni sehemu ya watu wanaochochea vita hiyo ya makundi.


3 Jul 2009


Mufti Simba aagiza Waislamu waikatae CCM

Mufti Issa bin Shaaban Simba, amekasilishwa na uamuzi wa serikali kuhusu Mahakama ya Kadhi.

Na Ummy Muya

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema kutokana na serikali kutupilia mbali ombi la kunzisha Mahakama ya Kadhi, Waislamu hawataipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Katika taarifa yake, Bakwata ilifikia hatua ya kusema Waislamu wasimchague Rais Jakaya Kikwete iwapo atasimamishwa na CCM kugombea urais, ikiwa ni pamoja na wabunge na madiwani watakaosimamishwa na chama hicho tawala kutokana na kitendo cha serikali kutupilia mbali hoja ya Mahakama ya Kadhi.

Kauli hiyo imetolewa jana wakati Mufti Issa bin Shaaban Simba alipokuwa akitoa tamko kupinga uamuzi wa serikali kutaka kutumia sheria za dini ya Kiislamu katika mahakama za kawaida badala ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi, kitu ambacho alisema anaamini kitawanyima haki Waislamu.

Alisema serikali imedhihirisha kuwa inaendeshwa na Wakristo na si kweli kama serikali haina dini na akamtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kubatilisha kauli hiyo kwa kuwa inamchafua Rais Jakaya Kikwete mbele ya umma wa Waislamu.

Waziri ametuthibitishia kama Rais Kikwete alikuwa akitulaghai ili tumpigie kura kwa kigezo kuwa suala hilo litashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi na sio kuchanganywa kama ilivyokuwa mwaka 1970 katika Sheria ya Ndoa na kuwanyima haki Waislamu,alisema.

Alisema kwa muda mrefu sana Waislamu wamekuwa kimya wakitumia hekima na busara kudai haki zao, lakini katika hatua hii ambayo serikali imefikia hawapo tayari kuendelea kudhalilishwa na kuwa kitendo hicho ni dhalimu.

Mufti alisema wamekuwa wakiiomba Mahakama ya Kadhi kwa zaidi ya miaka 20 na hivyo hawezi kuendelea kuwa kimya na kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa kwa kuwa mahakama hiyo ni haki yao.

Alisema kauli ya Waziri Chikawe imedhihirisha kuwa serikali ina wenyewe na Waislamu wamewekwa katika tabaka la pili pamoja na Rais Jakaya Kikwete kuwatuliza kwa ahadi kuwa watalipatia ufumbuzi suala hilo.

Natoa wito kwa Masheikh wote nchini na Waislamu wa madhehebu yote kupinga vikali kauli iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na kwamba Waislamu waige mfano wa Waislamu wa Afrika Kusini,alisema Mufti na kuhoji:

Kwa nini iwe Afrika ya Kusini na isiwe Zanzibar, Uganda na Kenya ambazo zipo ndani ya Afrika Mashariki? Kwa niaba ya Waislamu nasema serikali haikututendea haki na imetuchukiza sana,alisema.

Alisema lengo la kuomba mahakama hiyo ni kuhakikisha Waislamu wanashughulikia masuala yao ya ndoa na mirathi na si vinginevyo, hivyo waziri asipotoshe jamii kwa kutumia mifano ambayo haiko sahihi.

Mahakama hii haitawakata wezi mikono kwa kuwa nchi hii ina katiba na sheria na sisi tutazirudisha kesi zote za jinai mikononi mwa serikali. Sifahamu hiyo kamati ambayo waziri alisema alikuwa amekaa na kutoa tamko hilo ilikuwa na watu gani,alihoji.

Aliongeza kuwa kutokana na mapungufu hayo waziri arudi tena na kukutana na masheikh ili apate muongozo wa nini Waislamu wanahitaji na sio kuzungumza bila kuwa na usahihi wa kile anachosema.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya tamko la Bakwata, masheikh walikuwa na mitazamo tofauti. Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum Mussa alisema wapo baadhi ya Waislamu ambao watakubali kutokana na ufinyu wao wa elimu ya dini.

Mussa alisema haoni sababu ya serikali kufanya njia ya mkato katika suala hilo kwani Waislamu wanahitaji Mahakama ya Kadhi kama ilivyo kwa wafanyabiashara ambao wana mahakama yao.

Hukumu inayotolewa katika Mahakama ya Kadhi ni ibada kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W) hivyo ni lazima kwa atakayetoa hukumu hiyo awe Muislamu na si vinginevyo,alisema.

Namshanga waziri anapotaka sheria hizi zitumiwe katika mahakama za kawaida. Aliona wapi John akawa imamu,alihoji sheikh huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.

Naye katibu wa Bakwata wilayani Ilala, Sheikh Issa Ausi alisema historia iko wazi. Waasisi na wanaharakati ambao waliitoa Tanganyika mikononi mwa wakoloni walikuwa Waislamu, na akahoji sababu za serikali kuwa mstari wa mbele kuwafunga midomo leo.

Bakwata imezinduka sasa Waislamu wote tumeungana katika kupigania haki zetu na kutetea maslahi yetu na serikali itambue kuwa Bakwata iko hai hao Wakristo walikuwa wapi wakati sisi tukipigania uhuru,alihoji.

Wakati huohuo, Sheikh Salum Rwambo alisema anawashangaa wabunge Waislamu ambao baadhi ni mahajat na malhaj wanakaa kimya na kushindwa kutetea hoja za msingi na kudai kuwa huo sasa ndio mwisho wao wa kuwaita masheikh na kutaka waombewe dua ili wasipate wepesi katika kampeni zao.

Sheikh Rwambo pia alimsifia mbunge wa Nzega Lucas Selelii kwamba ni miongoni mwa wabunge katika Bunge hilo wanaozungumza ukweli na kwa kujiamini tofauti na wengine ambao wanaenda kukaa bila kufanya kazi zilizowapeleka .


CHANZO: Mwananchi


KWA MWENENDO HUU SI AJABU KUSIKIA HATA WATANZANIA WALIOAHIDIWA MAISHA BORA NAO WAKAJITOKEZA KUDAI HAWAITAKI CCM....HOJA IKIWA MAISHA BORA YALIYOAHIDIWA YAMEISHIA KWA KUNDI DOGO LA MAFISADI PEKEE!

20 Jun 2009


Ahadi tupu za kiwete zaelekea kutengeneza kitanzi cha CCM 2010

Na Mwandishi Wetu

IKIWA imesalia takriban miezi 18 kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwakani, sasa ni dhahiri kuwa Rais Jakaya Kikwete ana kibarua kigumu cha kukamilisha ahadi lukuki alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Mazingira hayo pia yanawaweka njiapanda wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kutetea tena nafasi zao.

Baadhi ya wabunge tayari wameliona hilo na miongoni wamelisema bungeni wakiwashutumu mawaziri ambao wamekuwa wakilimbikiza miradi ya maendeleo kwa upendeleo kwenye maeneo yao bila kuzingatia vipaumbele vya taifa, hata baadhi yao walifikia hatua ya kutishia kukwamisha bajeti iliyopitishwa Alhamisi iliyopita.

Kauli kali zaidi ilitoka kwa Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii aliyeomba dua kwa Mungu awalaami mawaziri hao.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, ahadi kadhaa alizozitoa Rais Kikwete bado hazijatekelezwa na kwa kipindi kilichosalia ni vigumu kufanya hivyo.

Miongoni mwa ahadi alizotoa Rais Kikwete na hazijaonekana matunda yake dhahiri ni zile zilizoandamana na kaulimbiu yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya na mpango wa ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’.

Kigogo mmoja ndani ya CCM amelieleza gazeti hili kwamba ahadi hiyo ya maisha bora ndiyo ilimpatia Kikwete kura za kishindo na isipotengenezewa mkakati maalumu inaweza kuwa ndio kitanzi chake na wabunge wengi wa CCM.

Alisema ahadi hiyo imesababisha baadhi ya vigogo wa chama na serikali kubadili kauli, na kusema kwamba maisha bora hayatawafuata wananchi kama hawafanyi kazi kwa bidii.

Kwa mujibu wa watu mbalimbali waliozungumza na Mwananchi Jumapili, na hata kauli za wabunge wanapochangia bungeni, Watanzania walio wengi bado wana hali duni ya kimaisha, jambo ambalo litakuwa gumu kulieleza kwa wapigakura hapo mwakani.

Kutokana na ahadi hiyo serikali ilitoa Sh30 bilioni ambazo zilipewa jina la mabilioni ya Kikwete, lakini hazikufika kwa maskini walio wengi kutokana na masharti yake kuwa magumu, na kuangukia kwenye mikono ya wasio wajasiriamali wadogo, hivyo kukwamisha mpango huo wa rais.

Ahadi nyingine zinazoelekea kushindikana ni ya mwafaka wa kisiasa wa Zanzibar ambao Rais Kikwete aliuweka kwenye kipaumbele, lakini hadi sasa hakuna mafanikio yoyote na tayari Chama cha Wananchi (CUF), kimetangaza kujitoa katika mazungumzo.

Ahadi nyingine ni ujenzi wa madaraja ya Kilombero mkoani Morogoro na Kigamboni, jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa ahadi kubwa alizotoa Kikwete na hadi sasa hakuna dalili zinazoweza kuashiria kuwa ipo nia ya utekelezaji.

Hata hivyo, Waziri wa Miundombinu, Dk Shukuru Kawambwa alipoulizwa alisema kwamba daraja la Kilombero limetengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2009/10.

Kuhusu daraja la Kigamboni, alirudia kauli za muda mrefu kuwa hilo limo kwenye mkakati wa kuanza kujengwa wakati wowote chini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali.

Ahadi nyingine ambazo hazijatekelezwa, zimeelezwa kuwa ni kilio cha mahakama nchini juu ya suala la masilahi ya watumishi na vifaa vya kazi.

Hivi karibuni, Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan alisikika akilalamika kuwa kiwango cha mafungu yanayoahidiwa kutengwa kwa mahakama hufika kwao kikiwa pungufu.

Suala jingine limeelezwa kuwa ni uboreshaji wa mashirika ya umma ambayo bado yako mikononi mwa serikali, lakini kila kukicha yamekuwa na matatizo na kuzua malalamiko mengi.

Kwa upande wa barabara ambazo ziliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na ambazo bado ni Tabora-Nzega, Bunda-Ukerewe na Marangu-Mkuu Rombo-Tarakea-Kamwanga.

Aliahidi pia kulifanya jimbo la Rorya mkoani Mara kuwa wilaya, lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua.

Mambo mengine ilikuwa ni kupambana na rushwa, lakini pamoja na hali hiyo kuonekana kuzaa matunda kwa mambo mengi yaliyokuwa yamejificha kuchimbuliwa na kuwekwa hadharani, malalamiko yanayoibuka ni baadhi ya watuhumiwa kutofikishwa mahakamani.

Rais Kikwete pia aliahidi kuondoa kero nyingi za Muungano lakini licha ya kuunda kamati ya kuzijadili na kuzishughulikia chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, zipo dalili za baadhi ya wananchi kutoridhika.

Tatizo kubwa linalojitokeza ni baadhi ya Wazanzibari, wakiwamo viongozi wa SMZ kutoa kauli zinazoonyesha dalili za waziwazi kwamba wanadhulumiwa ndani ya Muungano.

Pamoja na hali hiyo, Rais Kikwete atajivunia kwa kutekeleza ahadi yake ya kulifanya Bunge kuwa huru kwani limeonyesha dhahiri kuwa na meno kwa kufichua udhaifu wa baadhi ya vigogo serikali bila kuwa na woga.

Ameonyesha mafanikio pia katika ahadi yake ya kuendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu.

Hata hivyo, katika kipengele hicho kuna manung’uniko kadhaa kama vile baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kuendelea na nyadhifa zao wakati taratibu za utumishi wa umma ziko wazi kwamba wangepaswa kusimamishwa au kupewa likizo ama kuhamishiwa sehemu nyingine, ili uchunguzi huru ufanyike.

Mafanikio mengine ni kutekeleza ahadi ya kuongeza nafasi za elimu ya juu baada ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Ahadi nyingine ambayo Rais Kikwete ameonekana wazi kuivalia njuga ni kuboresha kilimo; na tayari mikakati kadhaa ikiwepo ya pembejeo za kilimo imewekwa, ingawa kuna malalamiko ya pembejeo kutofika kwa wakulima na wakulima wa karafuu na kahawa kutokuwa huru kutafuta masoko yao nje ya nchi.

Nguvu kubwa ya serikali yake kuielekeza kwenye kilimo imechagizwa na mtikisiko wa uchumi duniani ambao umetishia uchumi wa nchi nyingi hasa maskini ambazo zinategemea chakula kutoka nje.

Licha ya mafanikio hayo, serikali ya Kikwete inakabiliwa na changamoto kadhaa hasa za wananchi kutoridhika na mambo mbalimbali yanayotendwa na serikali yake.

Lingine ni wananchi kuona kuwa bado serikali ina matumizi makubwa ya fedha na wakati huo huo inawabidi kufunga mkanda ili kuihudumia huku wakikabiliwa na mazingira magumu ya kipato.

Malalamiko mengine ni baadhi ya watendaji serikalini kuendelea kutumia magari ya kifahari na kutenga Sh19 bilioni kwa ajili ya chai maofisini.

CHANZO: Mwananchi

2 Jun 2009


Na Lilian Lugakingira, Bukoba

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeanza safari ndefu ya kumnadi Rais Jakaya Kikwete ili awe mgombea pekee katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, na tayari wilaya ya Bukoba Mjini imetoa hundi ya Sh1milioni za kulipia fomu yake ya kuwania nafasi hiyo.

Hundi hiyo ilitolewa jana na Umoja wa Vijana wa CCM wilaya ya Bukoba Mjini kwa maelezo kuwa umeridhishwa na uongozi wa Kikwete katika kutekeleza na kutimiza ilani ya CCM, na hivyo kuungana na jumuiya nyingine, vikundi na watu mbalimbali waliojitokeza kuanza kumkapenia Kikwete.

Hata hivyo, katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aliiambia Mwananchi jana kuwa hajui kwa nini jumuiya hiyo ya vijana wa chama chake imefanya hivyo na kwamba atawatafuta ili kupata ukweli na sababu za kitendo hicho.

"Niano msimamo wa chama, lakini siwezi kusema kwa sababu sijajua wamefanya nini. Bila shaka wanayo sababu," alisema Makamba baada ya kuuliza maswali mengi kuhusu kitendo hicho cha UVCCM Bukoba.

Katika halfa iliyofanyika mjini hapa, mwenyekiti wa UVCCM wa Bukoba Mjini, Chifu Kalumuna alimkabidhi mwenyekiti wa CCM wilayani Bukoba Mjini, luteni mstaafu Ally Shamte hundi ya fedha za kuchukulia fomu hizo.

Katika hafla hiyo, Kalumuna pia alimkabidhi mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki hundi ya Sh 100,000 kwa ajili ya kuchukulia fomu za kuwania ubunge katika uchaguzi huo.

Akizungumzia sababu za kutoa fedha kwa Kikwete na Kagasheki kwa ajili ya kuchukulia fomu, katibu wa vijana wa Bukoba Mjini, Yusuph Kaliat alisema wamefanya hivyo kutokana na kuridhika na ufanisi katika utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Sisi kama vijana na nguzo ya taifa, tumeamua kutoa zawadi hiyo ili viongozi hao waendelee kuongoza, kila mmoja kwa nafasi aliyokuwa nayo,” alisema Kaliat katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi kadhaa wa CCM na UVCCM, akiwemo Kagasheki.

Chifu Kalumuna alikabidhi hundi zote mbili kwa Balozi Kagasheki ambaye naye alimkabidhi Shamte.Hakuna maelezo yaliyotolewa kwa nini UVCCM wilaya ya Bukoba imeamua kutoa fedha hizo sasa, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya mchakato wa uteuzi za majina ya wagombea na kuanza kampeni.

Kwa kawaida, CCM ina kipindi chake cha kuanza kampeni za ndani kwa wagombea wa nafasi zote za kuanzia serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais, lakini muda rasmi unaoruhusiwa na Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kuanza kampeni ni miezi minne kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Uchaguzi mkuu utafanyika mwezi Agosti mwaka 2010.

Kitendo cha wilaya hiyo kutoa fedha kwa ajili ya kuchukulia fomu kinaelekea kuwa ni mkakati mpya wa kumnadi Kikwete pamoja na Kagasheki, ambaye hivi karibuni alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema hatawania kiti hicho tena.

Fedha hizo za jumuiya ya vijana ya Bukoba Mjini ni sehemu ya kampeni kadhaa ambazo zimekuwa zikionekana katika miezi ya karibuni kumpigia debe Kikwete, ambaye alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Hivi karibuni Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Manyara ulimpendekeza Kikwete kuwa mgombea pekee wa nafasi ya urais katika chama chao cha CCM.Umoja huo ulitoa msimamo huo Mei 30 katika mkutano mkuu wa mkoa uliofanyika kata ya Magugu wilayani Babati ambako mgeni rasmi alikuwa katibu mkuu wa UWT, Hasna Sudi Mwilima.Risala ya akina mama hao iliyosomwa na katibu wa mkoa, Venosa Mjema ilisema wamenufaika zaidi na uongozi wa Rais Kikwete tangu alipoingia madarakani mwaka 2005.

Pia mkoa wa Rukwa ulionyesha kuridhishwa na uongozi wa Kikwete katika hafla ya kuchangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa shule za mkoa huo.Katika hafla hiyo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam na ambayo mgeni rasmi alikuwa Kikwete, kiasi cha Sh 1.4bilioni kilichangwa kwa fedha taslimu au ahadi.

Wanachama wengine wa CCM waliowahi kutoa kauli za kutaka Kikwete awe mgombea pekee wa chama hicho ni pamoja na makamu mstaafu wa rais, Samuel Malecela, mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Dodoma, Pancras Ndejembi na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Dar es Salaam, Mzee Hemed Mkali.

Baada ya wazee hao kutoa kauli hiyo mapema mwaka huu, Mbunge wa Sumve, John Shibuda alidai kwamba atachukua fomu kuwania urais mwaka 2010. Shibuda pia alikuwa miongoni mwa wana-CCM 11 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 2005.

Wengine ni makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, Malecela, waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof Mark Mwandosya, Balozi Patrick Chokara, Balozi Ali Karume, Dk Abdallah Kigoda, Dk William Shija, Dk Salim Ahmed Salim na Idd Simba.

Akionekana kunogesha kampeni za chini kwa chini hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Shinyanga, Rais Kikwete mwenyewe alisema haoni sababu kwa nini akina mama waliofaidika na mradi huo wamnyime kura mwakani.

Nasema, kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kupata usingizimimi sioni kwa nini akina mama walionufaika na mradi huu waninyime kura,” alisema Kikwete huku akishangiliwa na akina mama waliofika kwenye uzinduzi
huo.

CHANZO: Mwananchi
HABARI INAYOSHABIHIANA NA HII: UWT Wamteua Kikwete Kuwa Mgombea Pekee

PENGINE NI MUHIMU KUJIULIZA HAO UVCCM WILAYA YA BUKOBA MJINI WANA MRADI GANI WA KUWAWEZESHA KUWAKIRIMU "WAGOMBEA" HAO WATARAJIWA!PENGINE UTAULIZA KWANINI NI MUHIMU.WELL,NI RAHISI SANA KWA MAFISADI KUTUMIA COVER KAMA HIYO KUJIPENYEZA KWENYE ANGA ZA KITAIFA KWA MINAJILI YA KUFISADI NCHI BAADA YA UCHAGUZI HUO.

LAKINI CHA SEHEMU MUHIMU ZAIDI KATIKA HABARI HIYO HAPO JUU NI HIYO NUKUU NILIYOI-HIGHLIGHT KWA RANGI NYEKUNDU.IT SAYS IT ALL

16 Apr 2009

Raiamwema Merged
Raiamwema Merged JIMMY PHILEMON Habari katika toleo la wiki hii la jarida la Raia Mwema

Picha kwa hisani ya KENNEDY

Mwanahalisi Merged
Mwanahalisi Merged JIMMY PHILEMON Article ya Mwanahalisi kuhusu ufisadi na 2010.

Picha kwa hisani ya Kennedy

13 Apr 2009


Ally Sonda, Moshi

MBUNGE wa Jimbo la Vunjo(CCM) Aloyce Kimaro,amewataka mafisadi wanaojiandaa kumng'oa madarakani Rais Jakaya Kikwete na kundi la wabunge waliojitoa kafara kupinga ufisadi kuvunja mtandao wao mara moja kwa kuwa hautafanikiwa.

Akizungumza kwa kujiamini na huku akishangiliwa na umati wa watu,Kimaro alisema mwaka ujao wa uchaguzi, Rais Kikwete atashinda kwa kura nyingi sanjari na wabunge mahiri wanaomsaidia kupambana na ufisadi wakiwa ndani na nje ya Bunge.

Kimaro ambaye alikuwa akiwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kata ya Kahe Mashariki,alisema mafisadi wote wasiotaka Kikwete aendelee kuiongoza nchi kutokana na chuki za kuumbuliwa wataaibika zaidi mwaka ujao.

"Hivi sasa tunajua kuwa wapo mafisadi wanajipanga kuhakikisha kuwa Rais na wabunge waliojitoa mhanga kufa kwa kupinga ufisadi nikiwemo mimi tunang'oka mwaka 2010. Nasema hivi, hang'oki mtu hapa,Kikwete ni Rais hadi 2015 na sisi wabunge tutashinda vilevile, Mungu yupo mbele yetu,"alisema Kimaro.

Alisema bomu alilolilipua bungeni kuhusu uuzwaji wa nyumba za serikali ambalo limeanza kuleta mafanikio baada ya nyumba hizo kuanza kurejeshwa ni sehemu ndogo sana ya mikakati yake ya kupambana na mafisadi 'wanaoitafuna' nchi bila kunawa.Kimaro alisema ufisadi ndani ya Tanzania ni mkubwa na ndiyo sababu nchi inaendelea kuwa maskini na hivyo kujiendesha kwa kuombaomba misaada kutokana na watu wachache kuiba raslimali za taifa na kuzitorosha nje ya nchi.

Akizungumzia watu wanaolimezea mate jimbo lake na hivyo kujipanga kuwania ubunge mwakani, Kimaro alisema hana tatizo na vyama vya upinzani ambavyo vimeanza kutangaza kusimamisha wagombea, bali ugomvi wake ni kwa wanaCCM walioanza kujitangazia ubunge wa jimbo hilo hivi sasa. Aliiomba CCM wilaya ya Moshi Vijijini, kuwaonya wanachama hao kwa madai kuwa wanaleta mgawanyiko ndani ya CCM, kitendo ambacho kinaweza kutumika vibaya na kambi ya upinzani kuwasambaratisha wanaCCM.

"Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM, nakiomba Chama kiwaonye wanaCCM hawa wanaojitangazia ubunge wa Vunjo wakati wanajua kuwa mimi ndiye Mbunge halali wa Vunjo,nakuomba sana waonye la sivyo wataona cha mtema kuni,"alisema Kimaro bila kufafanua.

Katika mkutano huo, uliohudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Moshi,ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya wilaya hiyo,Alhaji Musa Samizi,Mwenyekiti wa CCM,Gabriel Masenga aliwataka wanaCCM wote wanaotaka ubunge wa Moshi Vijijini na Vunjo wasubiri muda muafaka ufike.

"Napenda kuwaomba wanaCCM wote wanaotaka Ubunge kwenye majimbo yetu mawili (Moshi Vijijini na Vunjo) wawe watulivu muda muafaka ufike,tutawapa fomu,tutawachuja kwa kura kama wanafaa,kujipitishapitisha hivi sasa ni kuleta vurugu ndani ya Chama na Jumuiya zake"alisema Masenga.

Masenga alitumia mkutano huo kuwataka baadhi ya wanachama wanaokikashifu Chama na viongozi wake baada ya kuadhibiwa kwa mujibu wa Katiba na hivyo kutishia kukihama CCM , waondoke mara moja na kujiunga upinzani kwa madai kuwa kuendelea kwao kuwa CCM ni sawa na kukumbatia Bomu.

"Wapo baadhi ya wanaCCM wameadhibiwa kwa kukiuka katiba ya Chama,sasa wana hasira wamekuwa wakikashifu Chama na baadhi ya viongozi,sasa kwa niaba ya Chama nawaomba waondoke CCM,huenda wakijiunga na vyama vya upinzani watafanya kazi yao vizuri ya kupambana na CCM,"alisema Masenga kwa kujiamini.
CHANZO: Mwananchi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.