9 Oct 2009Na Ramadhan Semtawa

RAIS Jakaya Kikwete aliweka hadharani matokeo ya uchunguzi wa vipimo vya afya yake, yanayoonyesha kuwa kiongozi huyo wa nchi ana afya njema baada ya tatizo la kuishiwa nguvu akiwa jukwaani mjini Mwanza Oktoba 4, kuibua mjadala.

Lakini vipimo hivyo vinaonyesha kuwa tatizo pekee linalomsumbua Rais Kikwete ni maumivu ya shingo ambayo yanatokana na kuumia nyakati za ujana au utoto.

Afya ya Rais Kikwete ilizuia mjadala baada ya kuishiwa nguvu akihutubia kwenye Uwanja wa Kirumba mjini Mwanza na kulazimika kubebwa na wasaidizi wake hadi chumba kidogo cha uwanjani hapo na ilielezwa baada ya rais kuzinduka kuwa tatizo hilo lilitokana na uchovu baada ya safari ndefu kati ya New York, Marekani na Dar es salaam na baadaye Arusha na Mwanza.

Pamoja na uchovu huo kuhusishwa na safari ndefu ya Rais Kikwete taarifa iliyopokelewa kutoka Radio Jamaica jana jioni zinasema kuwa rais atakwenda nchini Jamaica kwa ziara ya kikazi itakayoanza Novemba 24 na kumalizika Novemba 26.

Na jana daktari wa rais, Peter Mfisi alirejea tena kauli hiyo akisema uchovu, hasa wa safari, ndio uliosababisha kiongozi huyo wa nchi kuishiwa nguvu jukwaani, huku kukiwa na habari kuwa ataenda Jamaica mwezi ujao kwa safari ya kikazi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ikulu kuweka hadharani vipimo vya uchunguzi wa afya ya Rais Kikwete, ambaye pia aliwahi kuishiwa nguvu siku ya mwisho ya kampeni zilizomuingiza Ikulu, na kuanguka akiwa jukwaani.

Daktari wa rais, Peter Mfisi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa vipimo hivyo ni pamoja na cha damu kwa ajili ya kuangalia virusi vya Ukimwi ambacho huchukuliwa kila baada ya miezi sita.

"Nimekuja kufafanua afya ya mheshimiwa rais kutokana na tukio la Oktoba 4, 2009 (la kuishiwa nguvu jukwaani) pale Mwanza. Tukio hilo limesababisha mshtuko kwa watu wengi na kuendelea kuwa jambo linalozua mjadala kuhusu hali ya afya ya mheshimiwa," alisema daktari huyo.

"Naelewa sababu ya wananchi kuwa na hofu na kuwepo kwa mjadala miongoni mwao. Tatizo pekee ambalo limekuwa likimsumbua rais mara kwa mara ni maumivu ya shingo yanayotokana na kuumia utotoni na wakati wa ujana.

"Baadhi ya pingili za uti wa mgongo sehemu ya shingoni ziliathirika kutokana na kuumia huko na humsababishia maumivu. Mara nyingi matatizo hayo huwapata wanamichezo na wanajeshi."

Dk Mfisi aliongeza kusema: "Tumekuwa tunamfanyia mheshimiwa rais uchunguzi wa damu yake kwa vipimo mbalimbali vinavyotumika kutambua maradhi mbalimbali yanayohusu damu yenyewe na mwili mzima wa mwanadamu. Tumekuwa tunafanya hivyo hapa nchini na hata nje kwa nia ya kulinganisha matokeo yetu na kwa vipimo ambavyo sisi tunavyo.

"Matokeo ya uchunguzi wetu yameonyesha mheshimiwa rais yuko salama, hana maradhi ya damu au kisukari, wala Ukimwi au wingi wa mafuta (Cholestrol), kiwango cha madini, tezi la kibofu wala shingo, au ya ini, au ya homoni mbalimbali zilizoko mwilini na mengine."

Dk Mfisi alifafanua kwamba, uamuzi huo wa kutoa vipimo hivyo umetokana na ridhaa ya rais mwenyewe.

"Ni ridhaa ya mheshimiwa rais mwenyewe... kutokana na kiapo changu cha udaktari na maadili yangu ya kazi, siruhusiwi kutoa hadharani undani wa habari yoyote inayohusu mgonjwa ninayemtibu bila ridhaa yake," alisema Dk Mfisi.

Kwa mujibu wa daktari huyo, baada ya Rais Kikwete kuishiwa nguvu jukwaani, alichukua vipimo muhimu wakati akiwa kwenye chumba maalumu uwanjani hapo kama ilivyo kawaida na kwamba vipimo hivyo vimeshafanyiwa uchunguzi.

Alifafanua kwamba matokeo ya vipimo vilivyochukuliwa siku ya tukio la Mwanza yalionyesha shinikizo la damu (BP) lilikuwa kati ya 130 kwa 85 (vipimo vya kitaalamu), kitu ambacho ni cha kawaida kwa mtu mwenye umri kama wa Rais Kikwete.

"Mapigo ya moyo wake yalikuwa ni 76 kwa dakika ambayo pia ni ya kawaida; sukari kwenye damu ilikuwa 5.5 ambayo nayo ilikuwa ya kiwango cha kawaida; joto la mwili lilikuwa nyuzi 37.5 ambalo ni la kawaida," alifafanua Dk Mfisi.

"Mheshimiwa Rais pia hakuwa na kiungo chochote kilichoonekana kutetereka, jambo ambalo lilithibitisha kuwa hakupata kiharusi. Mheshimiwa Rais hakuwa na matatizo yoyote ya kiafya ambayo yangeweza kuhusishwa kuwa chanzo cha tukio lile (la Mwanza)."

Hata hivyo, Dk Mfisi alisema baada ya kurejea Dar es Salaam alijaribu kuwasiliana na madaktari wenzake wa ndani na nje ya nchi ambao wamekuwa wakishirikiana nao katika kuchunguza na kufuatilia afya ya Rais Kikwete.

"Wote hao baada ya kuwasimulia kilichotokea na matokeo ya vipimo nilivyomfanyia mheshimiwa rais, kwa tafakuri zao hawakuwa na wasiwasi wowote kuwa tukio hilo lilisababishwa na jambo jingine lolote isipokuwa uchovu," alisisitiza daktari huyo wa rais.

Aliongeza kwamba mmoja wao alimuona rais siku moja kabla ya kuondoka New York ambako alipata nafasi ya kumchunguza afya ya mkuu huyo wa nchi.

Dk Mfisi, akitoa mtiririko huo wa vipimo mbalimbali na matokeo alisema: " Blood Pressure (shinikizo la damu), tunafuatilia kwa karibu sana msukumo wa damu, mwenyewe tunampa mashine ya kujipima kila siku na anafanya hivyo, kwa jumla presha yake iko kwenye viwango vya kawaida.

"Aidha, uzito wake wa mwili unaendana ipasavyo na urefu wake, mheshimiwa Rais ni mtu mwenye mazoea ya kufanya mazoezi na yuko makini katika chakula anachokula."

Daktari huyo wa rais aliweka bayana kwamba, wanahusika kwa ukamilifu na kuelekeza kuhusu chakula anachokula na kuongeza kwamba "ana nidhamu ya kujipima pamoja na mazoezi na chakula."

Kuhusu moyo, Dk Mfisi alisema tayari walishamfanyia rais vipimo vya kitaalamu vinavyofahamika kama ECHO na ECG na vingine, na kwamba matokeo yameonyesha hakuna tatizo lolote.

Akizungumzia ubongo, alisema mwaka jana Rais Kikwete alifanyiwa uchunguzi wa afya ya ubongo wake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kutumia kipimo cha CT-Scan na matokeo yake yalionyesha kwamba, hakuwa na tatizo pia.

Dk Mfisi alisema Rais Kikwete aliwahi kufanyiwa uchunguzi wa ini, figo, bandama na kongosho kwa kutumia kipimo cha mionzi (ultra sound), uchunguzi ambao ulibaini viungo vyote hivyo viko salama.

"Kila mwaka tunapomfanyia uchunguzi wa afya ya mheshimiwa rais, tumekuwa tunafanyia uchunguzi wa viungo vyake muhimu vya tumboni kama vile ini, figo, bandama na kongosho na kwa kupima damu yake kwa vipimo vyote muhimu," aliongeza Dk Mfisi.

Kuhusu mfumo wa njia ya chakula, ambayo huhusisha koromeo la chakula, tumbo, utumbo mdogo, Dk Mfisi aliweka bayana kwamba matokeo ya uchunguzi yameonyesha hakuna tatizo lolote.

Alisema mwaka 2007 walimfanyia kipimo cha kitaalamu cha colonoscopy mjini Paris, Ufaransa, kuchunguza hali ya afya ya utumbo mkubwa na kwamba matokeo ya uchunguzi yalionyesha kuwa hana matatizo yoyote.

Alisema daktari aliyemfanyia rais kipimo hicho aliwaambia kuwa mkuu huyo wa nchi hahitaji kufanyiwa kipimo kama hicho tena mpaka baada ya miaka saba na kwamba daktari huyo alimtania rais kwa kusema kuwa "angefurahi kuazima utumbo" wake.

Kuhusu tezi la shingo, Dk Mfisi alisema kuwa akiwa mjini New York katika safari yake ya juzi, Rais Kikwete alifanyiwa uchunguzi wa afya ya tezi la shingo pamoja na kiwango chake cha utoaji wa homoni, matokeo yaliyoonyesha hakuna tatizo, hali kadhalika uchunguzi wa tezi la kibofu ulionyesha hana tatizo.

Dk Mfisi alisema rais hana tatizo la macho, masikio na pua na kwamba uvaaji miwani wa Kikwete haumaanishi kuwa ni maradhi.

"Tunapofanya uchunguzi wa macho ukiacha ile ya kuchunguza uwezo wa kuona, tunaangalia presha ya macho na hali ya viungo vya nje na ndani, mheshimiwa Rais hana matatizo yoyote," alisema.

CHANZO: Mwananchi

WAKATI DR MFISI AKITOA MAELEZO HAYO,MHADHIRI MWANDAMIZI KATIKA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM DR HAJI SEMBOJA AMENUKULIWA NA JARIDA LA RAIA MWEMA AKIELEZA KUWA URAIS NI ASASI NA SI MTU BINAFSI.

Urais si Kikwete binafsi, ni mfumo wa kitaasisi. Ni wazi kuwa Rais amesema yeye ndiye hakuzingatia ushauri wa wataalamu wake kutokana na kuwaondolea lawama. Ameamua kuwalinda kwa kubeba lawama, lakini ukitazama jambo hili kwa upana wake wasaidizi wake walipaswa kutambua tangu awali kuwa urais ni system nzima Ikulu hata mlinzi wa getini. Kwa hiyo, wasaidizi ndiyo wenye kuamua na si kila kitu kifanywe na Rais kama ambavyo wanasema sasa watajaribu kumpunguzia ratiba,” ALISEMA DR SEMBOJA NA KUSISITIZA KWAMBA“Sidhani kama ni sahihi kukubali kuwa Rais ndiye alikataa ushauri, kwa taratibu za kimfumo Rais anapangiwa kila kitu ni kama anaamriwa hivi. Kwa tukio hili ameamua tu kuwa na nidhamu ya kuwalinda wasaidizi wake, namwombea afya njema lakini ni muhimu tuzingatie kuwa wengi walioamua kufanya kila kitu wenyewe walipata matatizo, Ikulu sasa ifanye kazi kama Ikulu.”

BINAFSI NAAMINI TATIZO NI LA KIMFUMO ZAIDI.KUNA TAASISI ZENYE MAMLAKA NA WAJIBU WA KUPANGA RATIBA ZA RAIS SAMBAMBA KWA KUZINGATIA UHALISIA,USALAMA NA MAMBO MENGINE KAMA HAYO.KWA WENZETU WANAOZINGATIA KANUNI NA TARATIBU ZA KITAASISI,SI RAHISI KWA RAIS KUJIAMULIA MAMBO YAKE MWENYEWE PASIPO KUZINGATIA USHAURI WA KITAALAM.SI RAHISI,KWA MFANO,BARACK OBAMA KUJIAMULIA KWENDA MAHALA FLANI KINYUME NA USHAURI WA U.S. SECRET SERVICE.UBISHI WA RAIS KAMA BINADAMU HAUNA NAFASI KATIKA UFANISI WA TAASISI INAYOZINGATIA TAALUMA NA MAADILI.IKUMBUKWE KWAMBA LAITI RAIS AKING'ANG'ANIA KUFANYA ZIARA MAHALA FLANI KINYUME NA USHAURI WA WASAIDIZI WAKE KISHA AKAPATWA NA JANGA,WATAKAOBEBA LAWAMA NI WASAIDIZI HAO NA SI RAIS.LAKINI PIA KUNA SUALA LA FEDHA ZA WALIPA KODI ZINAZOTUMIWA NA TAASISI HUSIKA KUILINDA ASASI YA URAIS NA BINADAMU ALIYEKABIDHIWA DHAMANA YA URAIS.NI DHAHIRI KWAMBA RAIS AKIPUUZA USHAURI WA WA TAASISI HUSIKA INAMAANISHA PIA UPOTEVU WA FEDHA ZA WALIPA KODI.UTENDAJI WA AINA YA ZIMAMOTO,AU VIBAYA ZAIDI,KULENGA SHABAHA BAADA YA RISASI KUFYATUKA,UTATUGHARIMU HUKO MBELENI.LEO HII TUSINGEHITAJI DAKTARI WA RAIA KUWEKA HADHARANI TAARIFA NYETI ZA AFYA YA JK LAITI TAASISI HUSIKA ZINGEMLAZIMISHA JK KUFUATA USHAURI WA KITAALAMU KUHUSIANA NA RATIBA AU ZIARA ZAKE.TUSISUBIRI JAMBO LITOKEE NDIPO TUANZE KUTOA MAELEZO YA KITAALAMU. BY THE WAY,TAARIFA HIYO YA DAKTARI WA RAIS INAWEZA KUZUA MJADALA USIO NA TIJA KUHUSU MANTIKI YAKE.JAPO NI VEMA KUTOA UFAFANUZI KATIKA MASUALA YANAYOZUA UTATA (I WISH NA KWELI ISHU YA KAGODA INGEKUWA HIVYO) LAKINI KUNA UWEZEKANO WA "WABISHI" KUHOJI KAMA DAKTARI WA RAIS WA AFRIKA ANAWEZA KUTOA TAARIFA "MBAYA" DHIDI YA BOSI WAKE!

KWA SASA,MAMLAKA HUSIKA ZINAWEZA KUFARIJIKA BAADA YA KUPATA UTETEZI KUTOKA KWA JK.LAKINI NI VEMA ZIKATAMBUA KUWA JUKUMU LAO SI KUMWOGOPA MHESHIMIWA BALI KUFANYA KAZI ZAO KWA KUZINGATIA MAADILI NA TAALUMA.JK KAMA MTU ANAWEZA KUTOZINGATIA USHAURI WA MAMLAKA HIZO,LAKINI JK KAMA RAIS HARUHUSIWI KUJIAMULIA MAMBO YANAYOWEZA KUATHIRI ASASI YA URAIS.UOGA NA KUJIKOMBA NI MAMBO YASIYO NA NAFASI KATIKA PROFESSIONALISM.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube