5 Oct 2009


AONDOLEWA JUKWAANI, ASEMA NI UCHOVU WA SAFARI

Frederick Katulanda, Mwanza na Exuper Kachenje, Dar

RAIS Jakaya Kikwete jana alizidiwa ghafla wakati akihutubiwa waumini wa Kanisa la African Inland (AICT) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kulazimika kukatisha hotuba yake na baadaye kuondolewa uwanjani akiwa amebebwa na walinzi wake kabla ya kiongozi huyo kurejea jukwaani muda mfupi baadaye.

Rais Kikwete, ambaye alifika mkoani hapa akitokea Arusha ambako alifungua mkutano wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola, ikiwa ni siku chache tangu atoke Marekani kuhudhuria mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa, alikumbwa na mkasa huo majira ya saa 6:29 mchana.

Rais Kikwete alikatisha hotuba yake wakati akianza kuelezea suala la kudumisha amani upendo na mshikamano, akisema:"Wakati nilipokuwa nikipita kuomba ridhaa yenu kuongoza nchi hii, kote nilikopita niliomba kudumishwa kwa amani upendo na mshikamano…"

Ghafla alinyamaza na baadaye ikasikika sauti kutoka kwenye kipaza sauti chake ambayo inaonekana kuwa ya mlinzi wake, iliyosema "Kakae".

Baadaye Rais Kikwete aliuliza kwa sauti akisema "naweza kuhutubia nikiwa nimekaa"na kujibiwa na mwenyeji wake, Askoku Mkuu wa AICT, Daniel Nungwana kuwa "unaweza kukaa", jibu ambalo lilifanya aondoke kwenye eneo ambalo alikuwa akitumia kuhutubia jukwaani na kwenda kukaa meza kuu ambayo ilikuwa umbali wa takriban mita mbili.

Mara baada ya kukaa na vipaza sauti kurekebishwa ili aendelee na hotuba, Rais Kikwete alitamka kwa sauti ya juu iliyoonyesha kuwa afya yake si nzuri wakati alipoeleza kuwa “nimechoka sana kwa sababu ya safari” na kisha kuendelea na hotuba yake, lakini sauti yake ilizidi kubadilika na kuwa inayokwaruza na akakatisha hotuba yake, akiacha waumini wakinong’ona.

Baadaye Rais Kikwete, ambaye aliwahi kupoteza nguvu jukwaani wakati akihitimisha kampeni zake za uchaguzi kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam, alinyamaza na kutulia huku akiwa anaangalia upande wa mashariki, shingo yake ikilalia bega la kushoto na kichwa kuegemea kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro.

Dakika chache baadaye (saa 6: 35), mlinzi wake ambaye alisimama nyuma ya kiti chake, alimtikisa kwa muda, lakini rais hakuonekana kujibu kitu na ndipo walinzi wake na maofisa wengine wa usalama walipomzunguka kumkinga kuzuia watu wasimuone na baadaye kumbeba juu na kumpeleka kwenye chumba maalumu kilicho eneo la jukwaa kubwa la Uwanja wa CCM Kirumba.

Wakati akiingizwa chumbani humo, magari yote ya msafara wake yalielekea nje ya uwanja huo na kuegeshwa nje ambako kuna mlango, jambo lililoashiria kuwa iwapo afya yake isingetengemaa, angetolewa kupitia mlango huo na kukimbizwa hospitali.

Wakati harakati hizo zikiendelea, Kandoro alirejea jukwaani na kuelekea kwenye kipaza sauti. Kandoro aliwataka wananchi kutulia kwa maelezo kuwa hali ya rais ni nzuri na kwamba amepumzika kwa muda kutokana na uchovu.

"Nawaomba mtulie, Rais wetu amepumzika tu kwa muda kutokana na uchovu wa safari na yuko salama. Nawahakikishia kuwa yuko salama na huu ni uchovu tu kwani amesafiri sana kutoka nje ya nchi hadi Arusha na baadaye kuja hapa Mwanza. Hivi sasa amepumzika na atarudi hapa," alieleza Kandoro.

Kikwete alirejea jukwaani majira ya saa 6: 45 akitembea bila ya msaada wa walinzi ambao walikuwa nyuma yake na kwenda kukaa kwenye meza kuu ambako aliomba kipaza sauti na kusema maneno machache.

"Ndugu wachungaji na waumini, nguvu imerudi; nataka kutumia fursa hii kuzindua mfuko wenu maalumu; nami nachangia shilingi milioni moja,"alisema Kikwete na kuamsha kelele za shangwe na vigelegele.

Baadaye ratiba ya sherehe hizo iliendelea kwa harambee ya kuchangia mfuko maalumu wa watu wenye ulemavu wa ngozi ambao aliombwa na Askofu Nungwana kuchangia kwa kuuzindua kabla ya hotuba yake.

Askofu Musa Mwagwesela aliwatangazia wananchi kuwataka wajitokeze kuchangia mfuko huo kwa kipindi cha dakika tano, ili wamruhusu rais aondoke uwanjani hapo. Alisema ameombwa kufanya hivyo na watu wa usalama.

Zoezi hilo la wananchi na watu mbalimbali kuchangia mfuko huo liliendelea na majira ya saa 7:08 mchana Rais Kikwete aliombwa na mwenyeji wake Askofu Daniel Nungwana kuwashukuru wananchi kabla ya kuondoka.

Aliposimama Rais Kikwete alisema: "Kwanza nawaombeni radhi kwa mshtuko niliopata. Lakini umenitokea kwa ubishi wangu; ni kwa ajili ya uchovu wa safari."

Kikwete aliendelea kusema: "Nimerudi juzi saa 7:00 usiku. Nilikuwa Arusha kwenye mkutano wa bunge, walinishauri nipumzike nikasema ahaa hawa nao ngoja niende tu; waliniambia tunaona uchovu mwingi, nikasema hawa nao ahaa… nitaweza tu; nimekuja hapa… siku nyingine nitawasikiliza wanaonishauri."

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kukumbwa na mikasa hadharani. Aliishiwa nguvu ghafla wakati akihutubia mkutano wa mwisho wa kampeni kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2005. Alitolewa viwanja vya Jangwani na kwenda kupatiwa matibabu.

Lakini saa chache baadaye CCM ilitoa taarifa kuwa afya ya mgombea wake wa kiti cha urais ni nzuri na kwamba, mkasa huo ulitokana na rais kuwa alifunga na uchovu wa safari nyingi za kampeni hizo.

Alikumbana na mkasa mwingine mjini Mwanza Oktoba 15, 2005 wakati akiwa kwenye kampeni za kuwania kuingia Ikulu. Alikuwa akisimikwa kuwa mtemi wa kabila la Wasukuma kabla ya mtu mmoja, Lucas Omahe Garani, 34, ambaye ni mganga wa jadi, kujipenyeza hadi jukwaani na kujaribu kumvuta miguu, lakini akawahiwa na watu waliomzunguka Kikwete.

Alikuwa akisimikwa utemi na kikundi cha waganga kutoka Kituo cha Utamaduni wa Kisukuma cha Bujora ambacho kinamilikiwa na Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Mwanza.

Garani, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 13 jela kutokana na kosa hilo, alidai kuwa alifanya kitendo hicho kupinga uamuzi wa kikundi hicho cha waganga kumsimika chifu hadharani na mchana, kitu ambacho alidai kinakiuka mila za kisukuma.

Garani mkazi wa Mtaa wa Nyakabungo jijini Mwanza alikuwa anafanya kazi ya kutunza bustani ya ofisi za Dayosisi ya Victoria Nyanza ya Kanisa la Anglikana.

Kabla ya kuzidiwa na kukatisha hotuba yake jana, Rais Kikwete alilipongeza kanisa hilo kwa kutimiza miaka 100 na kwa kutoa huduma mbalimbali katika sekta ya afya na elimu.

Alisema serikali inatambua mchango wa mashirika ya dini na kusisitiza kuwa unapotaja maendeleo ya nchi hii, huwezi kukwepa mchango huu wa mashirika ya dini.

Hali haikuwa shwari kwa wananchi waliokuwa kwenye uwanja huo licha ya matangazo ya Kandoro kuwa afya ya rais ni nzuri. Kulikuwa na minong'ono mingi kutokana na kila mmoja kuuliza nini kimetokea kabla ya Askofu Mussa Magwesela kuwaambia waumini kuanza maombi maalumu kumuombea rais kutokana na hali iliyomkumba ghafla.

"Waumini wote naomba tumuombee mpendwa rais wetu; tumuombee Mungu amrejeshee afya yake,"alisema na mara moja waumini wakaanza maombi ya mmoja mmoja.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa baadaye na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilidai kuwa Rais Kikwete alilazimika kupumzika kwa dakika chache "baada ya kumaliza hotuba yake” katika sherehe hizo kutokana na kuzidiwa na uchovu.

"Nguvu imerudi…napenda sasa kuchukua nafasi hii kuzindua rasmi uchangiaji wa shughuli za kanisa lenu na mimi naanza na mchango wa Sh 1,000,000," taarifa hiyo ya Ikulu ilimkariri Rais Kikwete ikieleza kuwa baada ya mapumziko mafupi alirejea na kuendelea kushiriki shughuli hiyo.

Ilieleza kuwa Kikwete alianza kusikia uchovu wakati akisoma hotuba yake mbele ya maelfu ya waumini wa Kanisa hilo.

Taarifa hiyo inaeleza: "Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Oktoba 4, 2009, amelazimika kupumzika kwa dakika chache katika chumba cha mapumziko kwenye Uwanja wa Kirumba mjini Mwanza mara tu baada ya kumaliza hotuba yake wakati wa sherehe za miaka 100 tokea kuanzishwa kwa Kanisa la African Inland (AICT) nchini Tanzania.

"Mhe. Rais amelazimika kupumzika kutokana na kuzidiwa na uchovu kufuatia shughuli nyingi mfululizo katika siku za karibuni. Baada ya mapumziko hayo, Mhe. Rais aliendelea kushiriki katika shughuli hizo hadi mwisho wa shughuli hiyo ya AICT."

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Kikwete alikiri kupata matatizo hayo, akisema kuwa yalitokana na kutofuata ushauri wa wasaidizi wake waliomtaka apumzike baada ya kurejea kutoka Marekani. Taarifa hiyo imeeleza kuwa washauri walimtaka asiende Arusha kufungua mkutano huo wa mabunge na baadaye kumzuia asiende Mwanza.

Taarifa hiyo ya Ikulu inasema: "Kwa kweli mshtuko huu wa leo ni matokeo ya ubishi wangu. Nilishauriwa na wasaidizi wangu nipumzike baada ya kurejea nyumbani kutoka Marekani. Niliambiwa nisiende Arusha ama kuja hapa. Lakini nikakataa. Siku nyingine nitawasikiliza zaidi."

Taarifa hiyo ya Ikulu imeeleza kuwa rais amekuwa na shughuli nyingi katika miezi kadhaa iliyopita na kwamba hakuwahi kupumzika kutokana na ratiba ya shughuli hizo kufuatana.

Ilisema ndani ya siku 15 zilizopita Kikwete alikuwa New York, Marekani kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), juzi na jana alikuwa mjini Arusha na jana na leo mjini Mwanza alipokutwa na tukio hilo.

Taarifa hiyo ilikumbusha kuwa Septemba 20 Rais Kikwete aliondoka kwenda nchini Marekani kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na tangu hapo hajapumzika.

Kwa mujibu wa Ikulu Kikwete alirejea nchini kutoka Marekani saa 7:00 usiku wa kuamkia Ijumaa baada ya kusafiri kwa zaidi ya saa 19 na Ijumaa asubuhi alisafiri kwenda Arusha kufungua mkutano huo wa 55 wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola.

Wakati huohuo, Ofisi Binafsi ya Rais (OBR) imetangaza kuwa itaangalia upya ratiba ya rais kwa namna ya kumpunguzia mlundiko wa shughuli hata kama yeye binafsi ni “mpenzi mkubwa wa kuchapa kazi na kutumikia wananchi”.

OBR ndiyo husimamia upangaji ratiba za rais.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.