5 Oct 2009


KWANGU,MISINGI MIKUU YA NYERERE ILIKUWA UJENZI WA JAMII YENYE USAWA NA INAYOTHAMINI UTU WA BINADAMU.UHURU BILA USAWA NI POROJO.UMOJA KATIKA LINDI LA UMASIKINI NI SAWA NA USINGIZI WA PONO KWENYE UTANDO WA BUIBUI.NA MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA HAYAWEZI KUPATIKANA KATIKA SIASA ZA KUKUMBATIA MAFISADI SAMBAMBA KUKEMEA WAPAMBANAO NA UFISADI,KUTOJUA VIPAUMBELE VYA NCHI,NA KUENDELEZA AHADI ZA MAENDELEO ILHALI ZILE ZA AWALI HAZIJATEKELEZWA.

JK AMEKUMBUKA MISINGI YA MWALIMU.MSOME KATIKA HABARI IFUATAYO:

Mwandishi Maalum, Mwanza

RAIS Jakaya Kikwete ametaja misingi mikuu mitatu iliyowekwa na Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere katika kulijenga taifa la Tanzania, misingi ambayo rais alisema ni kumbukumbu yao kuu kwa kiongozi huyo wa harakati za Uhuru wa Tanganyika.

Rais Kikwete aliwashangaa Watanzania ambao wanabeza Uhuru wa Tanzania na kufurahia wakati jina la Tanzania linaposhambuliwa na wageni.

Aliitaja misingi hiyo mikuu kuwa ni uhuru, umoja wa taifa la Tanzania, na safari ya kujenga maisha bora kwa kila Mtanzania iliyoanza hata kabla ya Tanganyika kupata uhuru wake rasmi Desemba 9, 1961.

Rais Kikwete alisema hayo mjini Mwanza juzi alipozungumza na vijana wa CCM ambao wanaanza safari ya kuelekea kijijini Butiama mkoani Mara, ikiwa ni matembezi ya kumuezi Mwalimu Nyerere ambaye alifariki miaka 10 iliyopita baada ya kuugua saratani ya damu.

Mwalimu Nyerere alifariki Oktoba 14, 1999 akiwa amelazwa hospitali ya St Thomas jijini London, Uingereza.

Vijana 166 kutoka mikoa yote ya Tanzania wanashiriki katika matembezi hayo ya siku 10 ambayo yatapitia njia ambayo Mwalimu Nyerere alitembea mwaka 1967 katika kuunga mkono na kuhamasisha Azimio la Arusha.

Kauli mbiu ya matembezi hayo ni “Uhuru na Kazi” na miongoni mwa mambo ambayo vijana hao watafanya njiani ni kukarabati Shule ya Msingi ya Mwisenge ambako Mwalimu Nyerere alipata elimu yake ya msingi.

Rais Kikwete alisema kuwa urithi mkuu ambao Mwalimu aliwaachia Watanzania ni misingi hiyo mikuu ambayo imeendelea kulifanya Taifa la Tanzania kuwapo na kuwa imara.

Rais Kikwete alisema kuwa kila taifa duniani lina waasisi wake ambao wanastahili kuendelea kukumbukwa siyo tu kwa uasisi pekee, bali pia kwa mambo ambayo waliyasimamia, waliyaamini na waliyajenga.

"Wamarekani wanaye George Washington… sisi tunaye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere… na kila nchi ina muasisi wake ambaye anakumbukwa kwa aliyoyasimamia," alisema JK.

"La kwanza la kumkumbuka Mwalimu ni uhuru wa nchi yetu. Huyu alikuwa ni kiongozi aliyeambiwa achague kati ya siasa ama kazi ya ualimu… huyu mzee wetu akachagua siasa na utumishi wa umma bila hata kujua atakula nini.

"Akachagua kupigania uhuru wa nchi yetu. Kama mnavyojua nyote hii kazi ya siasa ni kamari... unakwenda kugombea ukijua kuna kupata ama kukosa... lakini yeye alifanya uamuzi sahihi wa kupigania uhuru,"

Rais Kikwete alisema kuwa uhuru siyo mipaka bali ni heshima ya nchi na ndiyo maana Tanzania haitasita kumkabili yoyote ambaye atajaribu kuchezea uhuru huo.

Alisisitiza: "Mwaka 1978 yule msanii na profesa wa historia na jiografia, Idi Amin alivamia nchi yetu… na sisi tukamfurumusha ili kulinda uhuru wetu na wako wenzetu ambao walipoteza maisha yao kwa ajili ya kulinda uhuru wetu. Wamelala Kaboya (mkoani Kagera) na tutaendelea kuwaenzi kwa sababu walijitolea kulinda uhuru wetu."

Rais Kikwete pia aliwashangaa watu wote ambao wanafurahia wakati heshima ya Tanzania inapobezwa na wageni.

"Uhuru siyo mipaka kama nilivyosema. Uhuru ni heshima ya taifa letu. Wako wale wenzetu wanaofurahi wakati wageni wanaposhambulia nchi yetu. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa uhuru wetu hauchezewi na mtu yoyote,"alisema.

Kuhusu umoja wa taifa, Rais Kikwete alisema Mwalimu alihakikisha kuwa uhuru wa nchi unazaa umoja ili nchi iwe moja na isigawanyike vipande vipande kwa sababu yoyote ile.

"Aliondoa viashiria vyote vya kuvunja umoja wa taifa tokea mwanzo kabisa. Aliondoa uchifu ili kuondoa nguvu za ukabila. Alitambua hatari ya dini na akataifisha shule zote za dini ili vijana wetu waelimishwe na kulelewa kama vijana wa taifa moja na siyo vijana wa dini tofauti,"alisema Kikwete.

Rais Kikwete alisema kuwa hata kabla ya uhuru, Mwalimu alitambua kuwa ili uhuru na umoja viweze kudumishwa ni lazima wananchi wake wapate maisha bora na ndiyo maana akawatambua maadui wakuu watatu – ujinga, maradhi na umasikini- na njia za kukabiliana na maadui hao.

CHANZO:
Mwananchi

BAADHI WANAHOJI KUHUSU MANTIKI YA UHURU ALIOPIGANIA BABA WA TAIFA NA WENZAKE.TULIMKIMBIZA MKOLONI ILI TUJITAWALE NA KUFAIDI RASLIMALI ZETU KWA HAKI NA USAWA.JAPO SIO EXCUSE,LAKINI MKOLONI HAKUTUJALI KWA VILE HAKUWA MTANZANIA.LEO HII WANAOTUTENDA VIBAYA ZAIDI YA WAKOLONI NI WATANZANIA WENZETU,WENGI WAO WAKIWA WALIOSOMOSHWA KWA SHIDA NA FEDHA ZA WATANZANIA WENZAO.KUNDI JINGINE NI LA MABWANYENYE WALIOPTA URAIA KWA VIJISENTI VYAO NA WAKOLONI -MAMBOLEO WALIOREJEA KWA JINA LA WAWEKEZAJI.NYERERE HAKUPIGANIA UHURU ILI WAGENI WAJE NA DOLA MOJA NA KUONDOKA NA MAMILIONI YA DOLA,AU AKINA LOWASSA KUTUINGIZA MKENGE KWENYE RICHMOND,NA USANII MWINGINE WA KISIASA.

UHURU PASIPO UONGOZI BORA NI SAWA NA KUWA NA VOGUE LENYE DEREVA MLEVI AU KIPOFU;LITATUMBUKIA MTARONI KAMA SI KUPORWA NA MAJAMBAZI.UHURU ILHALI TUMEBANWA NA NIRA ZA MAFISADI NI UTANI MBAYA KWA WALIOPIGANIA UHURU WA NCHI YETU.WEZI WA KAGODA WAMEHIFADHIWA HADI LEO,MASHIRIKA YA UMMA YAMEGEUKA KICHAKA CHA WATU KUHUJUMU KISHA WABADILISHIWE (REJEA MATTAKA NA ATCL),WAZEMBE WANAENDELEA KULINDWA KWA VILE TU KUWABADILISHA KTATHIBITISHA MAPUNGUFU YA ALIYEWATEUA IN THE FIRST PLACE,NA HADITHI NYINGINE ZA KUSIKITISHA.

HATUKUPIGANIA UHURU KUPATA HESHIMA FEKI MACHONI MWA JUMUIYA YA KIMATAIFA BALI AMANI NAFSINI NA MIILINI MWETU KAMA WATANZANIA.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.