27 Feb 2010

Pinda(2)

na Mwandishi Wetu, Urambo

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amemmwagia sifa kemkem Spika wa Bunge, Samuel Sitta akisema amejenga Bunge lenye sifa na umakini.

Pinda ambaye majuzi alimmwagia sifa Mbunge wa Igunga, Rostam Azziz (CCM) akiwataka wananchi wake wampime kwa kazi yake ni si kwa maneno ya bungeni, alisema Sitta amekuwa anaongoza Bunge kwa nia nzuri, na kwamba wanaolalamikia kazi yake ni wapotoshaji.

Alikuwa akihutubia wananchi katika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa juzi, akasema Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo, amelifanya Bunge lisifiwe hata nje ya nchi.

Katika kusisitiza hili, Pinda alisema: “Hata watu wa nje wanalisifu Bunge letu…wanasema naam, hili ndilo Bunge…Bunge likicharuka kuhusu ufisadi wanasema hata si bure, nani asiyejua ufisadi? Ufisadi si rushwa? Bunge linachofanya ni watu wawe waadilifu.”

Aliwataka Watanzania waungane katika vita dhidi ya rushwa, kwani imesemwa tangu zamani kwamba rushwa ni adui wa haki.

Kwa takribani miaka miwili, Sitta amekuwa na uhusiano mbaya na baadhi ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wengi wakiwa wabunge wenzake, kuhusu anavyoliendesha Bunge.

Miongoni mwa walioathirika kwa “kazi nzuri ya Sitta” ni Rostam ambaye pamoja na rafiki yake Edward Lowassa (Monduli – CCM) walihusishwa kinamna na kashfa ya Richmond, ambayo ilisababisha Lowassa kujiuzulu wadhifa wake wa Waziri Mkuu.

Kutokana na msimamo wa Sitta na athari za Kamati ya Mwakyembe, CCM iligawanyika makundi mawili, moja upande wa Sitta jingine likiwa upande wa Lowassa na Rostam.

Uhasama wa makundi hayo uliongezeka na kujikita katika vikao vingine vikuu vya maamuzi vya CCM, kiasi kwamba mwaka jana, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) walimbana Sitta katika moja ya vikao vyao, wakapendekeza avuliwe uanachama na afukuzwe ubunge, kwa maelezo kuwa anatumia vibaya nafasi yake kwa kuiaibisha CCM.

Sitta aliponea chupuchupu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuunda Kamati ya Mwinyi, ambayo kwa muda sasa imekuwa ikihaha kuwapatanisha mahasimu hao; na sasa imefanikiwa kupunguza uhasama wa wazi miongoni mwao.

Katika kikao cha 18 cha Bunge kilichomalizika siku chache zilizopita, Sitta aliwashangaza wananchi alipofunga mjadala wa Richmond, huku akitarajiwa atumie fursa hiyo kuibana serikali itekeleze maagizo 23 ya Bunge kuhusu watu waliojihusisha na kashfa hiyo.

Sitta pamoja na wabunge waliokuwa wamejipambanua kuwa ni wapiganaji vita dhidi ya ufisadi wamelazimika kunywea, licha ya kutambua kuwa maazimio muhimu yaliyomtaka Rais Kikwete kuwajibisha waliokumbwa na kashfa hiyo hayakutekelezwa.

Katika kikao cha NEC kilichoisha hivi karibuni, Sitta aligoma kusuluhishwa na Lowassa na kundi lake, akidai kwamba hana ugomvi binafsi, bali anapambana na ufisadi. Kamati ya Mwinyi imeongezewa muda ili iwapatanishe mahasimu hao.

Mara baada ya kikao cha NEC, Pinda alianza ziara ya wiki sita mkoani Tabora; na alipofika Igunga, alitoa kauli ya kumtetea na kumsafisha Rostam kwa kauli ambayo baadhi ya wachambuzi walidai inalidhalilisha Bunge, kwani ilionekana kana kwamba “maneno ya bungeni” si maneno ya maana kwa wananchi kuyatumia kumpima mbunge wao.

Aliwataka wananchi wa Igunga wampime Rostam kwa kazi zake jimboni, si kwa “maneno ya bungeni;” Bunge lile lile linaloongozwa na Sitta.

Jana Waziri Mkuu alitembelea Wilaya ya Sikonge. Ziara yake mkoani Tabora inatarajiwa kuhitimishwa leo.

CHANZO: Tanzania Daima


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2020

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Nisapoti

Podcast

Chaneli Ya YouTube