26 Feb 2010



Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa TAKUKURU Dr. Edward Hosea akimkaribisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete kufungua mkutano mkuu wa Mwaka wa taasisi hiyo.Picha kwa hisani ya MJENGWA

Hivi karibuni,uongozi wa kampuni ya magari ya Toyota ya Japan ulifanya jambo moja la kiungwana kwa kuwaomba radhi wateja wake kutokana na hitilafu za kiufundi katika modeli moja ya magari yake.Japo sakata hilo bado ni bichi hasa kwa vile inaelekea hitilafu hiyo bado haijapatiwa ufumbuzi,na tayari kuna habari za kushuka kwa hisa za kampuni hiyo katika masoko mbalimbali ya mitaji duniani,ni dhahiri hatua ya kuomba radhi imeonyesha kwamba kwa namna flani kampuni hiyo inatambua wajibu wake na inawajali wateja wake.

Majuzi,Rais Jakaya Kikwete alimwaga sifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) huku akijigamba kwamba serikali ya awamu ya nne imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa.Binafsi sidhani kama kauli hiyo ya JK inaendana na hali halisi ya utendaji na ufanisi wa TAKUKURU.

Kimsingi,tatizo haliko kwenye taasisi hiyo pekee bali kwenye medani nzima ya utawala bora.Angalia,kwa mfano,kauli za Waziri mwenye dhamana ya Utawala Bora,Mheshimiwa Sophia Simba,wakati wa sakata lililowahusisha wafanyabiashara wawili mashuhuri Bwana Reginald Mengi na Bwana Rostam Aziz.Badala ya kuhamasisha wananchi wanaojitokeza kuwaumbua hadharani mafisadi,Waziri Simba aliamua kuelemea upande mmoja ambapo bila aibu alimkemea Bwana Mengi huku akimlinda Bwana Rostam.

TAKUKURU hiyohiyo inayopongezwa na JK haijafanikiwa kujisafisha na tuhuma za namna ilivyouhadaa umma kuhusu suala la utapeli wa kampuni ya Richmond.Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata hilo ilipendekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Dr Edward Hosea,uamuzi ambao uko mikononi wa aliyemteua Hosea,yaani JK mwenyewe.Kwa hali ilivyo,na ukitilia maanani pongezi alozotoa JK kuhusu ufanisi katika mapambano dhidi ya ufisadi,ni dhahiri kuwa Rais hana mpango wa kumwajibisha Dr Hosea.

Nimesema tatizo liko kwenye utawala bora kwa vile hata chama tulichokipa dhamana ya kutuongoza-CCM-kimeendelea kufanya dhihaka linapokuja suala la utawala bora.Hivi inaingia akilini kweli kusikia kuwa Mbunge wa Bariadi,Bwana Andrea Chenge,bado ni mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama hicho tawala licha ya kuhusishwa kwake na tuhuma za ufisadi wa ununuzi wa rada!?Tusisahau kuwa pamoja na mageuzi ya kisiasa ya miaka ya tisini,bado chama tawala kimeendelea kuwa na nguvu pengine zaidi ya serikali,hoja kubwa ikiwa serikali hiyo imeundwa kutokana na ushindi wa chama husika.Kinachopuuzwa ni ukweli kuwa chama hicho hakikuomba ridhaa ya wanachama wake pekee bali Watanzania kwa ujumla.

Ni dhahiri kwamba kunakosekana utashi na udhati wa kupambana na ufisadi.Na kikwazo kikubwa kimeendelea kuwa kuweka mbele maslahi binafsi na ya chama badala ya maslahi ya umma/taifa.Pengine,na kwa hakika,badala ya kutetea mapungufu,ni muhimu kwa CCM na serikali yake kuiga mfano wa kampuni ya Toyota.Imetuangusha sana sio tu kwa kulegea katika mapambano dhidi ya ufisadi bali pia kwa ushiriki wake kwa kuwalinda watuhumiwa wa ufisadi.Laiti chama hicho kingekuwa na dhamira na utashi wa kukabiliana na ufisadi basi ni dhahiri Kamati ya Mwinyi inayoshughulikia mpasuko ndani ya chama hicho (wengine wanadai hakuna mpasuko) ingekuwa na kazi nyepesi tu ya kupendekeza wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili wasafishwe au waadhibiwe huko.Ikumbukwe kuwa tuhuma zinazowakabili watuhumiwa hao hazijaiathiri CCM pekee bali Watanzania wote kwa ujumla.

Nimalizie kwa kukumbushia usemi wa Kiingereza kwamba To err is human but to rectify is greatness,yaani (kwa tafsiri isiyo rasmi) kukosea ni ubinadamu lakini kujirekebisha ni uungwana.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.