10 Feb 2010


Baada ya danadana za muda mrefu ndani na nje ya bunge,hatimaye mjadala wa ujambazi wa Richmond umefungwa rasmi.Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka Dodoma,bunge limeridhia taarifa ya utekelezaji wa Azimio lake kuhusu suala la Richmond.Kwa lugha nyepesi,wawakilishi wetu wameridhia ujambazi uliofanywa na wahusika wa mradi huo wa kitapeli.

Kama ilivyo ada,CCM imeendelea kutumia wingi wa wabunge wake kuhakikisha kuwa matakwa yake yanatimia hata kama ni kinyume na matarajio ya Watanzania walio wengi.Wingi wa wabunge wa CCM umeendelea kuwa nyenzo muhimu kupunguza/kuondoa umuhimu wa wabunge kutoka vyama vya upinzani

Inasemekana kwamba msimamo wa pamoja wa wabunge wa CCM ulifikiwa katika kikao chake cha "kuwekana sawa",utaratibu uliiota miziz ndani ya chama hicho kila linapojiri jambo linaloashiria upinzani kwa ajili ya maslahi ya wananchi.

Wabunge wote walioamua kuzika mjadala wa Richmond ni sawa na wasaliti kwa vile nafsini na akilini mwao wanafahamu bayana kuwa namna pekee ya kumaliza suala hilo ilikuwa kwa wahusika kuwajibishwa.Madhara ya muda mrefu ya usaliti huo ni uwezekano wa kusambaa kwa virusi vya ufisadi ambavyo vinatambua bayana kuwa vina ulinzi wa kutosha kutoka chama tawala.

Kulikuwa na ugumu gani kuagiza suala hilo lipelekwe mahakamani ili kama wahusika walionewa basi iwe hivyo,na kama waliliingiza "mkenge" taifa basi wavune walichopanda?Hizi siasa za kulindana zitaendelea mpaka lini?CCM wanasahau kwamba hiki ni kipindi cha mpito tu,watafanya maamuzi ya kulindana mpaka wachoke,lakini siku ya siku watajilaumu kwa uzembe wao katika maamuzi.

Na kama kuna wa kusutwa basi na wale waliokuwa wakipata huku na kule wakijitambulisha kuwa ni "makamanda wa vita ya ufisadi".Nimeshaandika mara kadhaa kuhusu tunavyodanganyika kirahisi kila tunapowasikia akina Sitta wakidai "wanahujumiwa kwa vile wamesimama kidete kwenye mapambano dhidi ya ufisadi".Kwanini mapambano hayo yabaki ya kihisia/kufikirika zaidi kuliko vitendo?I just hope kwamba uamuzi wa kuzika hoja ya Richmond utajumuisha pia kuzikwa kwa kundi la wanafiki wajiitao "makamanda wa vita ya ufisadi".Kama ni makamanda basi ni wa mbao (wooden soldiers).

Lakini wenye uchungu wa dhati na nchi yetu bado wana fursa kubwa tu ya kutoa hukumu yao hapo Oktoba mwaka huu.Naendelea kuamini kuwa njia pekee ya kuikomboa Tanzania kutoka kwenye lindi na umasikini na bahari ya ufisadi ni kwa kuiondoa CCM madarakani.Tusitarajie lolote jipya kutoka kwa chama hicho kilichochoka kimawazo na kilichoishiwa na uwezo wa kutawala.Kuendelea kukiweka madarakani ni kukionea tu kwa vile kimeshatuthibitishia vipaumbele vyake.

Akina Muro wakituhumiwa rushwa basi hata kichanga kilichozaliwa jioni hii kitatambua namna dola "inavyowajibika".Yakija masuala ya akina Lowassa,Chenge,Kamragi,Msabaha na watuhumiwa wengine basi zinaanza ngonjera moja baada ya nyingine.Sasa kama walikuwa wanajua hatma ya mazingaombwe haya ni hii basi kulikuwa na haja gani ya kutuzingua kila kilipojiri kikao cha bunge?Na kama kawaida ya mengi ya magazeti yetu,danganya toto kuwa "bungeni hapatakalika kwa mjadala wa Richmond,Kiwira,TICTS,nk" ziliendelea kutawala vichwa vya habari.

Sababu nyingine ya ziada ya kuinyima CCM kura yako hapo Oktoba.

1 comment:

  1. Yaliyotokea yanasikitisha sana.

    Wanachotaka kutuambia hawa mabwana wanaoamini hakuna mwenye jeuri ya kuwafuatilia ni eti hakuna MKOSAJI. Si watumishi wa serikali, wala wanasiasa (wakiongozwa na Lowasa).

    Huu ni mchezo mchafu. Ndio maana tuna kila sababu za kupiga kampeni sisiemu ijifilie mbali.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube