7 Feb 2010


Naomba kujadili mada ambayo imekuwa ikijirudia mara kwa mara kuhusu “wanaume wa kibongo”.Nikiri kuwa sina hakika neno “wanaume wa kibongo” linamaanisha Watanzania pekee au Waafrika kwa ujumla au Weusi (Blacks) wote.Ila kwa madhumuni ya mjadala huu,nitayumkinisha kuwa walengwa ni wanaume wa Kitanzania.

Pengine mtazamo wangu unaweza kuathiriwa na ukweli kuwa nami ni “mwanaume wa Kibongo” (Mtanzania).Hata hivyo,nitajitahidi kuepuka kujipendelea (subjectivity).

Kama nilivyopata utata kwenye neno “wanaume wa kibongo” (na hivyo kutumia dhana ya Watanzania) najikuta kwenye utata mwingine kuhusu neno “wanaume wa Kizungu”.Je linamaanisha watu weupe (Whites)?Au watu wa “dunia ya kwanza”/nchi za Magharibi ikijumuisha na weusi/non-Whites waliozaliwa huku?Je “wazungu” hao wanajumuisha pia wale wanaotoka “Ulaya iliyochoka” kwa mfano Ulaya Mashariki-ambapo baadhi yao wanalazimika kuja kutafuta maisha bora Ulaya Magharibi na kwingineko?

Tukiweka kando utata huo wa maana inayokusudiwa, kuna suala jingine ambalo ni muhimu kuliweka wazi.Nilipokuja Ulaya mara ya kwanza, nilikuwa na picha ya “wamisionari” –watu walioacha “raha” za kwao kwenda kuishi maeneo magumu kabisa kwao.Na nilikuwa na picha ya watu wenye upendo,huruma na wanaoguswa mno na shida zetu za kimwili na kiroho.

Lakini haikunichukua hata mwezi kugundua kuwa Ulaya nilokuwa naifikiria awali ina viumbe wa aina tofauti kama ilivyo huko nyumbani.Kuna wenye upendo na wenye chuki,kuna wenye busara na majuha,kuna wenye akili na machizi,nk.La kwanza nililobaini ni UBAGUZI.Sio tu wa rangi bali hata wa kipato.Wakati kimsingi jamii nyingi za kiafrika zimejengwa katika misingi ya ushirikiano,usawa na utu, kwa hawa wenzetu “ubinafsi” ( individuality, katika hisia chanya na hasi) una nafasi muhimu katika mafanikio au kufeli kwa mtu.Jitihada za mtu binafsi zina umuhimu mkubwa zaidi kuliko za ushirika/ujamaa.Hilo linaweza kuwa na uzuri wake lakini pia kuna suala la madaraja (classes) ambayo mfumo wa kibepari umeyaimarisha vizuri.

Na hili la madaraja ni muhimu sana katika kuzielewa jamii hizi.Kuna wale walioelimika na kuielewa dunia, na wengi wao-japo si wote- wanafahamu kwanini Afrika au Waafrika tuko jinsi tulivyo.Lakini kwa wale “waliokwepa umande”- japo si wote-kwao Afrika na Waafrika ni vitu vilivyopo duniani kimakosa.Ni katika kundi hili la pili ndipo kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na “wapuuzi” wanaoamini kuwa Waafrika tunaishi maporini au kwenye miti huku tukizungukwa na nzi,tukijisaidia popote,na upuuzi mwingine kama huo.Kwa takriban mwongo mmoja niliokaa hapa Uingereza nimeshakutana na watu wa aina hiyo mara kadhaa na majibu yangu huwa “kama sie tunaishi kwenye miti je balozi wenu huko kwetu naye anamudu vipi kuishi kwenye mti?”.Ila mara nyingi huwa naishia kuwatukana tu.

Kuna suala la ubaguzi.Kwa hapa Uingereza,baadhi ya Waingereza wanakiri bayana kwamba “ubaguzi ni sehemu ya utamaduni wa baadhi yao...na ndio maana unaona Wakatoliki na Waprotestanti wanaendelea kupingana huko Ireland ya Kaskazini”.Wengine wanakwenda mbali zaidi na kueleza imani yao kuwa hisia hizo za kibaguzi zilichangia sana ukoloni wa dunia “ya watu wasiostaarabika”.Ni muhimu hapa kukumbushia angalizo kuwa wakoloni walikuwa haohao “wazungu walio bora kuliko Wabongo” japo hilo ni suala la kihistoria zaidi kuliko malavidavi.

Kwahiyo dada zangu wanaoamini kuwa “wanaume wa kizungu ni bora zaidi kuliko wa kibongo” wanapaswa kufahamu kwamba miongoni mwa “wazungu” hao kuna wanaompinga Obama, si kwa vile hajatimiza ahadi zake bali tatizo ni weusi wake,kuna wafuasi wa British National Party (BNP),kuna neo-Nazis (vijukuu vya Hitler) na wengineo wenye “chuki binafsi” wakiamini kuwa vyanzo vya matatizo ya nchi zao sio Weusi tu bali Waasia na wageni wengineo.Nasisitiza,NI BAADHI.Miongoni mwa "wazungu" hao ni MAKABURU,wanaharamu waliowabagua wasio-weupe hususan Weusi huko Afrika Kusini kwa vile tu waliamini kuwa asili yao ni bora zaidi.Miongoni mwao pia ni wenye mtazamo wa akina James Watson mwanataaluma mahiri kwa madai yake kuwa Waafrika wana akili pungufu kulinganisha wa "wazungu".

Kama ambavyo huko nyumbani kuna wacha Mungu na washirikina,ndivyo ilivyo kwa “wazungu” pia. Kuna wanaoangalia upendo,haiba,urembo na sifa nyinginezo za kibinadamu badala ya rangi ya binti,lakini pia kuna akina Nick Griffin,Jean-Marie Le Pen,nk ambao kwao rangi ya mtu ni kigezo muhimu cha utu/ “ushenzi” wake.

Labda swali naloweza kuwauliza dada zangu wanaohitimisha kuwa “wanaume wa kizungu ni bora kuliko wa kibongo” ni hili: je mama zetu waliolewa na wazungu kiasi cha kututengenezea familia bora zilizotufikisha tulipo sasa?Au je takwimu zinasemaje kuhusu idadi ya waume katika ndoa nyingi “zenye furaha” huko nyumbani?Japo nahofia kutoa takwimu pasipo utafiti lakini yayumkinika kusema takriban asilimia 90 ya waume kwenye ndoa “zilizotulia” huko nyumbani bado ni wanaume wa kibongo.Hapa simaanishi kuwa walioolewa na wasio “wabongo” hawana furaha na ndoa zao bali nasisitiza hoja kuwa kama mama zetu walikuwa kwenye furaha katika ndoa na baba zetu wabongo,sasa hoja ya “wanaume wa kibongo kutokuwa mwafaka kwenye ndoa” inatoka wapi?

Hivi wakati dada zetu wanaponyoosha vidole kuwashutumu wanaume wa kibongo wanajaribu japo kiduchu kujiangalia na wao wenyewe?Mbona hata huku kuna hadithi nyingi tu za watu kusaliti ndoa zao/mahusiano yao?Je Bill Clinton alipomsaliti Hillary kwa Monica Lewinsky alikuwa Mndengereko?Vipi kuhusu John Terry au seneta Edward Kennedy?

Katika sosholojia kuna theme inayohusu deviance (kwenye kinyume na taratibu zilizokubalika katika jamii husika).Hapo,baadhi ya wanasosholojia wanaamini kuwa umalaya ni uvumbuzi,yaani kwa mfano mwanamke mrembo anajua “anatakwa” na kuna walio tayari kutoa fedha kumpata kwa hiyo “anajipeleka sokoni,mwenye kiku kikali ale nyama”.Kuna wanaofanya hivyo kwa vile hali ya uchumi inawasukuma kufanya hivyo,na kuna wale wanaofanya hivyo kutokana na kufata mkumbo,huku wengine wakifanya hivyo kutumia uhuru wao wa kupenda chochote watakacho ikiwa ni pamoja na ngono.

Malezi,imani ya kidini na mchango wa wanaotuzunguka ni miongoni mwa mambo muhimu sana katika kutengeneza tabia ya mtu.Baadhi ya wansayansi ya jamii wanabashiri kuwa mtoto anayekulia familia ya mzazi mmoja (single parent) ana uwezekano wa kuwa single parent ukubwani kwa vile “kama baba/mama aliweza kunilea peke yake kwanini kie nishindwe?” (socialisation).Wapo pia wanaoamini kuwa mtoto anayekulia familia inayothamini umuhimu wa ndoa anaweza kuiga mfano wa wazazi wake na hivyo “kutulia” ukubwani.

Mwisho,naomba kuhitimisha kwa kusema kwamba ni mambo machache sana duniani ambayo yanatokea tu pasipo sababu. Kama kila mume/boyfriend wa kibongo “anakukimbia” pengine tatizo ni wewe na sio wao,hasa ikizingatiwa kuwa wao si mapacha.Lakini na muhimu zaidi ni la kiroho.Kwa sie tunaoamini Mungu,hakuna liwezekanalo kwa mwanadamu pasipo baraka za Mungu.Pengine kabla ya kukimbilia kulaumu “wanaume wa kibongo” ni muhimu kwa walalamikaji kutazama upya mahusiano yao na Muumba.Kuna ishu inayonong’onwa na baadhi ya wanaume (hususan walio nje ya Tanzania) kwamba dada zetu wa kibongo wanaondekeza tamaa za makaratasi na kubabaika lakini naomba nisiligusie kwa vile,again,tamaa kwa Wakatoliki ni mzizi wa dhambi.Kwa aliyemshika Mungu na kisha kupatiwa chaguo lake,chochote atachopewa kitakuwa ni mapenzi ya Mungu,hivyo masuala ya tamaa yatakuwa hayana nafasi.

Naweza kuwa siko sahihi lakini huo ndio mtazamo wangu.


1 comment:

  1. ninaungana na hitimisho lako mzee wa ughaibuni. hapo ndipo penye hekima na akili, yeyeote anaweza kubaini

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube