16 Mar 2010


RAIS Jakaya Kikwete ameweka hadharani mambo yanayomchefua katika utendaji wake kuwa ni viongozi wa mashirika ya umma na taasisi zilizo katika hali mbaya kifedha, kumghilibu ili awaongezee mitaji wakati historia inaonyesha kuwa kufilisika kwa mashirika hayo kumetokana na utendaji mbovu.

Rais Kikwete alisema anajisikia vizuri na hata moyo wa kuongeza msukumo katika kuitaka serikali itoe fedha kwa taasisi zinazojiendesha kwa faida ili ziendelee kufanya vizuri kuliko taasisi hizo zinazofilisika.

Rais Kikwete alisema hayo jana alipokuwa akibadilishana mawazo na watendaji wakuu wa tume mpya ya mipango mara baada ya kuwaapisha Ikulu jana.

. Utakuta shirika lilikuwa na ndege tisa. Sasa lina ndege mbili. Anakuja mtu anasema, Mheshimiwa tungeweza kufanya vizuri iwapo tungeongezewa ndege saba,? alisema Rais Kikwete wakati akipata kinywaji na watendaji hao watano, akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

?Ebu fikiria, walikuwa na ndege tisa sasa zimepungua hadi mbili, lakini wao wanaona sasa waongezewe nyingine. Hii inaingia akilini!

?Ingekuwa sasa wanazo 13 halafu wakaja na maelezo kwamba wangefanya vizuri zaidi iwapo wangeongezewa, hapo inaweza kuingia akilini.?

Rais Kikwete aliwaonya watendaji hao wakuu wa chombo hicho ambacho kitategemewa kufanya mapinduzi ya kiuchumi nchini kwamba viongozi wa mashirika na taasisi wa namna hiyo watafika kwao, hivyo wawe makini katika kuamua kulingana na matakwa yao.

Ingawa Rais Kikwete alionekana kueleza hilo kama mfano tu, mazingira yalionyesha kuwa ni moja ya mambo makuu aliyotaka kuwausia katika utendaji wao, kwenye majukumu waliyopewa watekeleze.

Hali hiyo alidhihirisha kutokana na kurudia mara tatu, kusisitiza juu ya ghiliba za viongozi hao wabovu aliosema kuwa licha ya kufanya vibaya kiutendaji, huishawishi serikali izidi kutoa fedha.

Ingawa Rais Kikwete hakutaja shirika lenye tabia hiyo, kauli yake inaweza kuhusishwa na kuyumba kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambalo hivi sasa limebakiwa na ndege mbili tu baada ya kuyumba kiutendaji.

ATCL, ambayo ilikuwa ikitamba katika miaka ya themanini kutokana na kuwa na ukiritimba katika usafiri wa anga, iliingia mkataba na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) kwa ajili ya kuboresha huduma zake, lakini likajikuta likiporomoka zaidi hadi mkataba ulipovunjwa mwaka 2006.

Mwaka jana, shirika hilo lilizuiwa kufanya safari za anga baada ya kunyang'anywa leseni ya kupaa angani, hatua ambayo ililidhoofisha zaidi shirika hilo. Baada ya kurejeshewa leseni hiyo, bado ATCL imeshindwa kurudi katika hali yake ya kawaida licha ya serikali kutumbukiza fedha nyingi kujaribu kulinasua.

Takribani wiki mbili zilizopita, ndege ya ATCL ilipata hitilafu wakati ikitua mkoani Mwanza na kusababisha shirika hilo kusimamisha tena huduma zake kutokana na kukwama kwa ndege hiyo.

Awali kabla ya mazungumzo hayo ya chai, Rais Kikwete alimwapisha Dk Philipo Mpango kuwa katibu mtendaji wa Tume ya Mipango, akisaidiwa na manaibu katibu wanne; Maduka Kessy, Happiness Mgalula, Florence Mwandri na Cliphod Tandale.

Tume hiyo ya Mipango imeundwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete baada ya kuivunja iliyokuwa Wizara ya Mipango na Uchumi, alipokuwa anaunda baraza jipya la mawaziri mwaka 2007.

Mara baada ya kuvunja wizara hiyo, idara ya uchumi iliunganishwa na iliyokuwa Wizara ya Fedha na kuifanya iwe na jina jipya la Wizara ya Fedha na Uchumi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mpango alisema tume hiyo itakuwa chombo muhimu cha serikali katika kuweka mipango yenye tija kiuchumi kwa taifa.

Lakini alisema kwamba anakabiliwa na changamoto kubwa ya kupanga mipango mizuri ya nchi ambayo itasababisha mapinduzi ya kiuchumi, hasa ikizingatiwa kwamba kwa kipindi kirefu mikakati imekuwa ikiwekwa lakini bado Tanzania inaendelea kuorodheshwa kwenye nchi maskini.

?Kinachoniumiza ni kuona taifa linaendelea kuwa maskini hata baada ya miaka 40 ya uhuru,? alieleza Dk Mpango.

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakikwamisha nchi kuendelea, alisema, ni taifa kuwa na vipaumbele vingi kuliko rasilimali yake ya kiuchumi.

Katika mazingira hayo, alisema mikakati mingi imekuwa haikamiliki kutokana na kile kidogo kinachopatikana.

Dk Mpango akasema pamoja na kwamba mawazo ya tume yake yatatokana na ushauri wa wataalamu wake, binafsi anaona watatilia mkazo vipaumbele vichache ili suala la maendeleo liwe la hatua kwa hatua.

Alitoa mfano wa Bandari ya Dar es Salaam kwamba inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo nchini iwapo itaimarishwa pamoja na miundombinu ya reli ili nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), zitegemee kupitisha bidhaa zake Tanzania.

CHANZO:Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube