19 Mar 2010


Katika gazeti la Tanzania Daima toleo la jana (mtandaoni) kulikuwa na habari kuhusu Taasisi ya Kimataifa ya Malaria No More kumfungulia mashtaka msanii nguli wa bongofleva,Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu.Kwa mujibu wa habari hizo,Malaria No More imefungua kesi hiyo ya madai kfuatia kauli za Sugu kuwa wazo la kufanya tamasha (lililofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na Rais JK) la kuhamasisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria lilikuwa lake.Kwa vile suala hili liko mahakamani,na kwa vile mie si mjuzi wa sheria,sintazungumzia kesi hiyo bali nitaangalia kipenre katika habari husika kuwa tangu mwaka 2006 Malaria No More ikishirikiana na Wizara ya Afya imetoa vyandarua 267Binafsi nimeshtushwa sana na takwimu hiyo.Yaani kwa wastani,taasisi hiyo imekuwa ikitoa vyandarua 66 kwa mwaka.Kama takwimu hizo ni sahihi basi huu utakuwa ni mzaha wa hali ya juu.Pamoja na nia njema ya Malaria No More lakini vyandarua 66 kwa mwaka ni idadi ndogo mno.Kwa mujibu wa PBS Newshour malaria husababisha vifo vya watoto wa Kitanzania kati ya 60,000 na 80,000 kwa mwaka.Sasa huhitaji kuwa mtaalam wa hisabati kutambua kuwa wastani wa vyandarua 66 kwa mwaka ni mithili ya tone kwenye bahari.

Hata hilo tamasha lenyewe la kuhamasisha mapambano dhidi ya malaria lilikuwa na mzaha wa aina flani.Kwa mfano,ilielezwa kuwa "wageni maalum" walipewa zawadi za vyandarua huku "walalahoi" ambao kimsingi ndio waathiriwa wakubwa wa malaria walisahaulika.Sasa kama tunaamua kufanya hamasa ya kitaifa dhidi ya janga halafu tunaleta "ubaguzi" kati ya waheshimiwa na walalahoi,hiyo malaria itatokomezwa kweli?

Kama ambavyo blogu hii imekuwa ikiandika mara kadhaa,tatizo letu kama nchi haliko kwenye mipango bali usimamizi na utekelezaji wa mipango hiyo.Matamasha yanaweza kuwepo kila wikiendi lakini pasipo usimamizi mzuri na utekelezaji wenye lengo la kuzaa matunda itakuwa ni kazi bure.

Na kwa waungwana wa Malaria No More,pamoja na nia njema mliyonayo ya kutusaidia kutokomeza ugonjwa huu hatari,ni dhahiri kuwa kasi yenu ni ya kutia shaka.Nimerejea kusoma habari husika mara mbili mbili nikidhani labda ni makosa ya kiuchapishaji lakini inaelekea takwimu zenu ni sahihi.Kwa mwenendo mlionao (wa kutoa vyandarua 267 tu tangu mwaka 2006) mtaendelea kubaki "wadau muhimu" katika mapambano dhidi ya malaria lakini ni wazi kuwa mafanikio ya harakati zenu yatabaki kuwa kiduchu.

Mwisho,nadhani kuna umuhimu wa pande zote husika katika sakata hili la nani mmiliki wa wazo la tamasha la kuhamasisha vita dhidi ya malaria kukaa pamoja na kutafuta mwafaka.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube