18 Mar 2010


Vigogo watajwa kujipa fedha zilizotolewa BoT
Ni Zile za Kunusuru Uchumi (Stimulus Package)

MATUMIZI ya Sh trilioni 1.7 kuhami uchumi dhidi ya mtikisiko wa kiuchumi duniani ulioathiri kampuni za ununuzi pamba mikoa ya kanda ya ziwa na hatimaye kampuni hizo kumegewa sehemu ya fedha hizo sasa yamezua utata, na sasa baadhi ya wakubwa wanatajwa kuwa sehemu ya walionufaika na fedha hizo, Raia Mwema imeelezwa.

Fedha hizo kupitia mfuko maalumu, maarufu kwa jina la ‘Stimulus Package’ , zilipitishwa na Bunge wakati wa bajeti lakini Kambi ya Upinzani Bungeni, kupitia kwa kiongozi wake Hamad Rashid Mohamed ilionya fedha hizo kuibua kile kilichoitwa kashfa ya EPA namba mbili, na kupendekeza fungu hilo liundiwe sheria ili kuwabana wahusika lakini serikali ilipuuza, ikitumia wingi wa wabunge kutoka CCM.Takriban miezi sita sasa tangu fedha hizo kuanza kutolewa, uchunguzi wa Raia Mwema katika kipindi hicho umebaini kuwa baadhi ya fedha zimekwenda katika kampuni zisizofahamika ama ambazo wahusika halisi hawajulikani na badala yake wamewatanguliza watu wengine.

Imeelezwa kwamba sehemu ya kampuni zilizochotewa mamilioni kutoka kitita hicho cha Sh bilioni 1.7 zina uhusiano na vigogo serikalini na wanasiasa na kwamba fedha hizo hazikukidhi matarajio ya serikali kwa wakulima wa pamba.

Kampuni ambazo zinaonekana katika orodha ya zilizopendekezwa ama zilizopata fedha hizo ni pamoja na S & C Ginning Co.Ltd (yenye makao yake Bulamba), Simon Agency Ltd (Mwanza), Fresho Investment Co. Ltd (Shinyanga), Gaki Investment Co. Ltd (ya Shinyanga), Bedugu Ginning Co. Ltd (ya Musoma), Intergrated Cotton Fields Ltd ( ya Mwanza), Igunga Cotton Company (makao yake yako Dar es Salaam), Robasika-Agroproducts Ltd yenye makao yake Kaliua, Tabora na Chesano Cotton Ginnery yenye makao yake Bariadi, Shinyanga.

Kampuni nyingine kwenye orodha hiyo ni Copcot Cotton Trading (Geita), Allanoe Ginneries Ltd (Mwanza), Shinyanga Region Co-op Union (Shinganya), Vsarrian Tanzania Ltd (Bunda), Birchand Oil Mill (Mwanza), Jambo Oil Mill (Shinyanga), Afrisian Ginning Company (Dar es Salaam) na S.M Holdings Ltd (Mwanza).

Nyingine ni Nida Textile Mills Ltd, Hassanal R. Waiji (Maswa), Blore Tanzania Ltd (Mwanhuzi, Shinyanga), Al-Adawi Co.Ltd (Mwanza), Olam Tanzania Ltd (Mwanza), Kahama Oil Mill (Kahama), Kahama Cotton Co. Ltd (Kahama), NGS Investment Co. Ltd (Bariadi), Roko Investment Co Ltd, Cotton Agency & Ginners Ltd na Aham Investment Co. Ltd (Dar es Salaam).

Nyingine ni New Sam Trust Co Ltd (Bariadi), Busangwa Organic Farming Association (Shinyanga), BioSustain Tanzania Ltd (Dar es Salaam), MSK Solutions (Mwanza), Mass Trading (Tabora), Sibuka Co Ltd (Maswa), Nsagali Co. Ltd (Bariadi) na Vitrecs Oil Mill ya Mwanza.

Haikuweza kufahamika mara moja kama kampuni zinazoelezwa kuwa na uhusiano na wakubwa ndizo zilizoorodheshwa ama ni zile ambazo zinatajwa kupokea fedha bila majina ya kampuni hizo kuwa hadharani, lakini Raia Mwema, limethibitishiwa kuwapo wakubwa walionufaika na mamilioni kutoka kwenye “stimulus package.”

Katika hali inayothibitisha kuwa mambo si shwari kati ya wakulima wa pamba na wanunuzi ambao wengi wamepata mgawo wa stimulus package, Bodi ya Pamba Tanzania imejikuta katika lawama kali si tu kutoka kwa wananchi bali hata baadhi ya viongozi wa CCM, akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, kukiibuka shinikizo kwa Rais Jakaya Kikwete kuifuta bodi hiyo kwa madai kuwa, imeacha shughuli za ununuzi pamba kufanyika holela kupitia kwa mawakala ambao wanawaumiza wakulima.

Kwa upande mwingine, taarifa zaidi zinabainisha kuwa licha ya Bunge kupitisha Sh trilioni 1.7 kwa ajili ya stimulus package, ni sh bilioni 870.8 pekee hadi sasa, ndizo zimekwishatolewa na Benki Kuu (BoT), chombo ambacho kimepewa mamlaka ya kutoa fedha hizo.

Mpango huo wa stimulus package ilitiliwa shaka na Kambi ya Upinzani Bungeni kupitia kwa kiongozi wake, Hamad Rashid Mohamed na kupendekeza utungiwe sheria maalumu ya udhibiti kwa kurejea uzoefu wa baadhi ya nchi za Asia.

Mapendekezo hayo ya kambi hiyo yalilenga kuinusuru nchi na “EPA namba mbili.” Katika hotuba yake bungeni wakati wa kujadili stimulus package mwaka jana, , mjini Dodoma , Hamad Rashid Mohamed, kwa niaba ya wabunge wenzake kutoka vyama vya CUF, CHADEMA na UDP, alihoji masuala mbalimbali kuhusu matumizi ya fedha hizo Sh. trilioni 1.7, zilizotangazwa na Rais Kikwete.

“Tunataka sheria ya Appropriation Act iwe na Schedule maalumu ya Stimulus Package na iseme waziwazi nani atapata nini, kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge iwe inapata taarifa kila miezi 3 ya utekelezaji wa hiyo stimulus package.

“Ni ukweli uliowazi kuwa stimulus package inazinufaisha benki tu, kwa kuzipa mwanya wa kufanya biashara nzuri na Serikali kwa kutumia fedha za Serikali yenyewe, na ndio maana katika nchi nyingine serikali imelazimika kuwa na hisa ili kuhakikisha kuwa fedha iliyotolewa ambayo inatokana na kodi za wananchi inadhibitiwa na kurudi kwa walipa kodi na wapiga kura.”

Hamadi alisema katika bajeti ya mwaka 2007/08 na ile ya 2008/09 serikali ilijizuia kukopa kwenye mabenki, kwa kigezo kikubwa kuwa mabenki yaweze kufanya biashara ya kukopesha sekta binafsi na kuwa zuio hilo liliongeza ufanisi kwa mabenki kukopesha sekta binafsi kwani mikopo kwa sekta binafsi ilipanda hadi kufikia asilimia 40.

Stimulus Package itapunguza mikopo ya benki kwenda kwenye sekta binafsi, na yale mafanikio yaliyokwishafikiwa yatayeyuka, vinginevyo mabenki yawekewe viwango vya kufikia katika kutoa mikopo nje ya stimulus package.

“Kwa mujibu wa taarifa ya Sera ya Fedha ya BoT serikali itazikopesha benki Sh bilioni 270 kwa ajili ya kuzikopesha sekta binafsi. Itatoa Sh bilioni 205 ili kukopa kwenye benki hizo.

Je, benki hizo zikishindwa kutumia fedha zile ambazo serikali imeziweka ili kukopesha sekta binafsi kutumia fedha hizo kufanya biashara na serikali kwa fedha za serikali? Hili litadhibitiwa vipi? Waziri atueleze,”, alihoji Hamad na kuongeza kuwa;

“Mwaka huu wa bajeti ni ya kuongeza matumizi na madhara yake ni mpango huo wa kuhami uchumi kuongeza mfumuko wa bei.

“Serikali imeamua kufidia vyama vya ushirika na kampuni zinazonunua mazao ya wakulima na kuyauza kwa hasara. Katika soko huria kuna kupata faida na kupata hasara. Wafanyabiashara makini wa mazao hupanga bei zao za kununulia mazao kwa kuzingatia bei walioipata katika soko la baadaye.

“Hata hivyo wengine hawapendi kuchukua tahadhari kwa kutegemea kwamba bei itapanda na kwa hiyo watapata faida kubwa. Bei imeshuka kwa hiyo wamepata hasara.” Alihoji akisema; Je, hakuna wafanyabiashara wa mazao waliolipa mikopo waliokopa kwa kujibana. Serikali ina uhakika gani kuwa mikopo hii ilitumiwa vizuri?”

Pia alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua kampuni zitakazopewa fedha kutoka katika mpango wa kuhami uchuni.

Alitaka CAG kwanza kuthibitisha kuwa hasara waliopata haikutokana na matumizi mabaya ya mikopo na kwamba, gharama ya ukaguzi huu ilipwe na benki zilizokopesha. Alionya kuwa, la sivyo serikali inaweza kuliingiza taifa katika EPA namba mbili.

CHANZO:Raia Mwema.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.