24 Mar 2010


Kwa muda mrefu sasa Kanisa Katoliki limejikuta likigubikwa na kashfa za ngono.Hivi karibuni pepo mbaya amezidi kulizungukia Kanisa hio baada ya taarifa kwamba kaka wa Baba Mtakatifu,Georg Ratziger, aliwatangwa makofi wanakwaya wake katika miaka ya 1960.Kwa kitambo sasa,inaonekana Kanisa limekumbwa na jukumu kubwa la kuomba msamaha kutokana na tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia (na ulawiti) sambamba na jitihada za kusafisha sura yake.Hata hivyo,pamoja na kuendelea kuibuka kwa tuhuma hizo zisizopendeza,Kanisa Katoliki limeendelea kubaki 'safi' barani Afrika.Je hali hiyo inasababishwa na nini?Na je itaendelea kwa muda gani?Binafsi siamini kwamba tuhuma zinazolikabili Kanisa hilo haziligusi Bara la Afrika,na hususan Tanzania.Tofauti iliyopo ni kwamba imani za kiroho katika nchi zilizoendelea zina tofauti ya namna flani na ilivyo katika nchi zinazoendelea.Yayumkinika kusema watumishi wa Bwana katika nchi kama Tanzania wameendelea kunufaika na unyenyekevu uliokubuhu kutoka kwa waumini wao ilhali katika nchi za Magaharibi imani haimaanishikufumbia macho mauvu ya wasimamizi wa imani hiyo (i.e. watumishi wa Bwana).

Nadhani si mie peke yangu ninayefahamu kwamba baadhi ya watumishi wa Bwana wana watoto,kinyume kabisa na kanuni na taratibu za Kanisa Katoliki.Katika jimbo nililozaliwa,suala hilolinaonekana la kawaida sana kiasi kwamba baadhi ya watumishi wa Bwana wanamudu kuhudumia 'familia' zao (wanawake waliowapa ujauzito na kupata watoto wa wachunga kondoo wa Bwana) pasipo kificho.

Utumishi wa Bwana katika nchi yetu hauna tofauti sana na kinachoendelea kwenye siasa zetu.Tunafahamu wanasiasa wabovu lakini kwa vile wanamwaga vijizawadi hivi na vile tunaendelea kuwalea na hatimaye wanaoendelea kuipeleka mrama nchi yetu.Waumini wengi wa Kanisa Katoliki huko nyumbani wanafahamu fika maovu yanayotendwa na BAADHI ya watumishi wa Bwana lakini wanaendelea kufumbia macho.Natambua kuwa Maandiko Matakatifu yanasisitiza kuzingatia zaidi maneno/mafundisho ya viongozi wetu wa dini na sio kutilia mkazo mateno yao,lakini ni dhahiri padre mzinzi hawezi kuwa na mamlaka ya kiroho (moral authority) kukemea uvunjaji wa amri ya sita.

Na kuna imani kwamba kusuasua kwa baadhi ya viongozi wa dini huko nyumbani kukemea ufisadi na maovu mengine ya wanasiasa kunasababishwa na ukweli kwamba baadhi ya viongozi hao wa dini wanatambua kuwa 'hawako safi kihivyo'.Kama ilivyokuwa wakati wa sakata kati ya serikali na madhehebu ya dini kuhusu ushuru katika bidhaa zinazoingizwa nchi na madhehebu hayo,ambapo baadhi ya wanasiasa walidiriki kusema 'wanafahamu mengi kuhusu baadhi ya viongozi hao wa dini' ni dhahiri wachunga kondoo wa Bwana wanafahamu fika kuwa matendo yanayokiuka maadili yao yanafahamika na wanasiasa wangeweza 'kuwaumbua' kwa kuyaweka hadharani.

Hakuna anayefahamu hatma ya pepo huyu mchafu anayelitesa Kanisa letu lakini kilicho bayana ni athari zake kwa kondoo wa Bwana.Tayari kuna taarifa kwamba kuna mtikisiko wa kiimani katika nchi zinazofahamika kama vinara wa Ukatoliki kwa mfano Ujerumani,Austria na Ufaransa.Hali pia si shwari huko Vatican kiasi kwamba 'mpunga mapepo mkuu' (chief exorcist) katika makao makuu ya Kanisa hilo,Father Gabriel Amorth alinukuliwa akisema kuwa shetani ameweka makazi yake sehemu hiyo.

Wakati Kanisa Katoliki barani Afrika,Tanzania included,likiwa shwari katika kipindi hiki cha upepo mbaya wa shetani,ni muhimu kwa wachunga kondoo wa Bwana wanaokiuka mafundisho ya Kanisa hilo kujirudi wakitambua kuwa siri zao haitadumu milele.Pia ni muhimu kwao kufahamu kuwa japo wanasitiriwa kutokana na unyenyekevu uliopitiliza wa waumini wao,Mungu wanayemtumikia anaowaona na anakasirishwa sana.Japo wanaweza kuendelea kusalimika kutokana na waumini kuendelea 'kuwafumbia macho',ni dhahiri kuwa wasipobadilika wataishia kuwa kuni za kuchochea moto unaowachoma wadhambi huko 'motoni'.

Juma Kuu linapaswa kuwa kipindi kizuri kwa Kanisa Katoliki kila mahali kungalia wapi limejikwaa (na sio lilipoangukia) na kisha kufanya marekebisho yanayostahili.Na kwa Nguvu za Bwana,yote yanawezekana.

Tmsifu Yesu Kristo,Milele Amen.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube