20 Apr 2010

Hapa chini kuna habari ambayo kama ni ya kweli basi hatma ya nchi yetu iko mashakani.Lakini kabla hujaisoma,angalia picha ifuatayo na inaweza kukusaidia kukupa uelewa wa namna tulivyofika tulipo.


KUMBE Rais Jakaya Kikwete hakusoma sheria aliyosaini kwa mbwembe. Sasa baada ya kugundua kasoro zake anataka ikarabatiwe kwa njia ya kanuni, MwanaHALISI limeelezwa.

Hilo liligundulika katika mkutano wa wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wenyeviti na makatibu wa wilaya uliomalizika wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.

Taarifa za ndani zinasema, bila aibu na hasa kwa ujasiri wa kiongozi mkuu wa nchi, Rais Kikwete alimuuliza Philip Marmo, waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, maana ya baadhi ya vifungu katika sheria hiyo.

Lakini katika hali ambayo haikutegemewa, Marmo alijibu kana kwamba anamkejeli rais, jambo ambalo lilistua wajumbe wa kikao hicho cha juu cha utekelezaji wa sera za chama.

MwanaHALISI limeelezwa kwamba Rais Kikwete alistushwa na kifungu cha sheria kinachotaka mgombea kuwasilisha katika ofisi za msajili, taarifa ya fedha atakazotumia.

Kifungu hicho kinatoa siku saba kabla ya siku ya mwisho ya NEC kutangaza majina ya wagombea.

Kifungu kingine kinachodaiwa kumstua kinahusu idadi ya wajumbe wa kampeni. Kwa CCM, yenye hata vikundi vya ngoma na nyimbo kama ToT, kuweka timu ndogo kunaweza kupunguza shamrashamra na kuathiri kampeni.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, ilikuwa baada ya rais kupitia maeneo hayo, alimuuliza Waziri Marmo iwapo kile alichokuwa akifafanua kimetokana na sheria iliyopitishwa.

Naye Marmo, akiongea kwa sauti ya unyenyekevu alijibu, “…hiki ndicho ulichosaini.”

Kwa kauli ya Marmo, Rais Kikwete alionekana kustuka na kusema, kama hali ni hivyo, basi sheria itakuwa imeingilia hata mchakato wa wagombea ndani ya vyama, kimeeleza chanzo chetu.

Taarifa zinamnukuu rais akihoji kwa nini “sheria imekwenda mbali mno” na kuagiza papohapo kuwa wahusika waangalie ambapo sheria inaingiliana na watengeneze kanuni zitakazoleta nafuu.

Rais amenukuliwa akimwagiza Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutengeneza “kanuni vizuri” ili kuondoa mwingiliano unaoleta ugumu wa utekelezaji.

Hoja ya maelekezo ya sheria mpya ya gharama za uchaguzi ilikuwa moja ya ajenda za kikao cha NEC, wenyeviti na makatibu wa CCM wilaya kutoka kote nchini.

Tarehe 17 Machi mwaka huu, Rais Kikwete alisaini hadharani na kwa mbwembwe Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ikulu Dar es Salaam ambapo hafla hiyo ilihudhuriwa na majaji, wabunge, viongozi wa serikali na vyama vya siasa, mabalozi na waandishi wa habari.

Hata hivyo, sheria hii imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya siasa na wanaharakati, kabla na baada ya kusainiwa kuwa itakuwa ya udhibiti kwa wenye msimamo tofauti na watawala.

Aidha, siku tatu baada ya sheria hiyo kusainiwa, mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa alitupa kombora kwa kusema sheria aliyosaini rais ilikuwa na vipengele ambavyo havikujadiliwa bungeni na kwamba “viliingizwa kinyemela.”

Ubishi wa Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Frederick Werema kwamba hakukuwa na chochote kilichofanywa kinyemela ndio umekuza hoja ya Dk. Slaa na kufanya achimbue zaidi kshfa hiyo.

Katika kufukua, Dk. Slaa amekwenda hadi kwenye kumbukumbu za bunge (Hansard) na kuthibititisha kuwa Kifungu 7 (3) ambacho kimo katika sheria aliyosaini rais hakikujadiliwa bungeni na hivyo hakikurekodiwa katika hansard.

Mtunga sheria huyo kutoka Karatu amesema pia kuwa chochote kilichojadiliwa bila kuamuliwa na bunge kilikuwa kinatarajiwa tu katika kanuni au fafanuzi za au ainisho za maneno na taratibu lakini siyo katika vifungu vya sheria.

Katika majibu yake kwa kauli za Dk. Slaa, Jaji Werema alitetea serikali na kuthibitisha kuwa kifungu hicho kiliwekwa na waziri Marmo.

Dk. Slaa amesema katika andishi maalum, “Hakuna mwenye mamlaka, hata rais hana mamlaka hayo, sembuse waziri.

“Baada ya mjadala katika Kamti ya Bunge zima, maneno yakikubaliwa ndiyo hayo yanaingia kwenye sheria na serikali haina mamlaka ya kwenda kuyarekebisha inavyotaka. Ndiyo maana ya kusema ‘kifungu kimepitishwa,’ ” ameeleza Dk. Slaa.

Akiweka msisitizo, Dk. Slaa anasema, “Kitendo cha kuchomeka kinyemela ni kitendo kibaya sana na kinapaswa kulaaniwa, kwa sababu, kwa utaratibu huu wataalam wanaweza kuipeleka nchi pabaya kwa kupenyeza jambo lolote wanalotaka wao hata kama halijajadiliwa au limekataliwa na Bunge.”

Dk. Slaa anafafanua hatua ya serikali ya kuingiza mambo kinmyemela katika sheria kuwa ni kosa la jinai na kusema hata kifingu walichochomeka kinyemela kina madhara makubwa.

Kifungu kilichoongezwa na serikali kinataka timu ya kampeni kukaguliwa na watendaji wa serikali ya CCM.

“Kampeni ndiyo inayobeba mikakati na siri yote ya uchaguzi. Haiingii akilini kabisa kuwa serikali (pengine unayotaka kuiondoa kwenye uchaguzi ambayo ndio haki ya msingi ya kila mgombea) ndiyo inaweka mkono wake kwenye udhibiti wa mikakti hiyo,” anafafanua Dk. Slaa.

Anasema kuweka kifungu kama hicho ni “wenda wazimu, kwa mtu yeyote aliyefikiria jambo hilo, au anaandika tu kutoka mezani na au hajui maana halisi na majukumu yake.”

Kutokana na kuibuka kwa kashfa hii, serikali sasa imeamua sheria hiyo irejeshwe bungeni ili kufanyiwa marekebisho yanayostahili.

Naye Dk. Slaa tayari ametoa pendekezo: “Namna pekee ya kuepukana na athari hiyo ni kwa serikali kukiri imefanya makosa, na ndio ustaarabu bila kutafuta visingizio.”

Anasema serikali iwasilishe kwenye Mkutano wa 19 wa Bunge hili ulioanza jana, kitu kinachoitwa “Miscellaneous Amendment” – marekebisho ya sheria mbalimbali – na au ikichelewa sana katika Bunge la Bajeti.

Wachunguzi wa mambo wanasema Rais Kikwete atakuwa amesikitishwa sana na hatua ya wasaidizi wake ya “kumchomekea” vitu ambavyo baadaye vinamomonyoa hadhi yake kama mkuu wa nchi.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa wamempotosha au wameshindwa kumsaidia rais, ni pamoja na Jaji Werema ambaye ametetea uingizaji kinyemela kipengele ambacho hakikujadiliwa bungeni.

Mwingine anayetajwa ni waziri Marmo ambaye ambaye nduye hasa ametajwa kubuni na kuingiza maneno ya kifungu kinacholaaniwa.

CHANZO: Mwanahalisi.

4 comments:

  1. Hehehehe very funny the amount in words is different from the figures duh hiii kali

    ReplyDelete
  2. Thanks Tina for your comments.

    ReplyDelete
  3. dah!!, mimi sina la kusema nimemuonyesha rafiki yangu mkeya alichoniuliza Rais wenu kaenda shule

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube