2 Apr 2010

Jana ilikuwa Siku ya Wajinga Duniani.Binafsi niliiadhimisha kwa matendo mawili.Kwanza niliweka 'breaking news ya kizushi' kuwa Baba Mtakatifu Benedikti wa 16 ametangaza kujiuzulu kufuatia skandali ya ngono na ulawiti inayolikabili Kanisa Katoliki.Pili,kwenye ukurasa wangu wa Facebook niweka tahadhari kuwa 'pranks' kama kuwapigia simu polisi na kudai wewe ni gaidi wa kujilipua bomu la kujitoa mhanga (suicide bomber)zinaweza kumwingiza mtu matatani hata kama zilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wajinga.Vitendo au kauli za utani katika Siku ya Wajinga zina mipaka yake. Nimekutana na habari katika gazeti la Mwananchi kuwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu imetoa ushauri wa kununuliwa ndege nyingine ya rais kwa madai kuwa zilizopo zimechoka.Naamini kuwa kauli hiyo ilikuwa sio serious bali ni sehemu tu ya maadhimisho ya Siku ya Wajinga Duniani.Kama kauli ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Mohammed Missanga ilikuwa ya dhati basi yayumkinika kusema kwamba baadhi ya wanasiasa wetu wana upeo finyu kupindukia linapokuja suala la vipaumbele vyetu kama taifa.

Of course,rais kama mheshimiwa hawezi kusafiri kwa miguu au kwa punda,japo wengi wa anaowatawala ni masikini wa kutupwa ambao hawawezi kumudu hata gharama ya mlo wa siku.Lakini pamoja na uheshimiwa huo wa rais,na umuhimu wa yeye kusafiri kwa ndege yake maalum,wazo la kumnunulia ndege mpya ni mufilisi na linalopaswa kukemewa kwa nguvu zote.Kama hoja ni uzamani wa ndege zilizopo basi kuna haja gani ya kupuuzia malalamiko ya wafanyakazi wa serikali wanaotoshia kugoma kwa madai ya mishahara kiduchu?Maana nao pia mishahara yao ni ya zamani kama zilivyo ndege za rais.

Missanga na Kamati yake wanapendekeza pia kununuliwa helikopta zitakazowezesha viongozi kufika maeneo yanayokumbwa na majanga.Hivi la muhimu ni kufika kwa viongozi katika maeneo hayo au first responders (eg zimamoto)?Kwanini kipaumbele kisiwe katika kuboresha vitendea kazi vya first responders badala ya nyenzo za usafiri wa viongozi?Kwahiyo kiongozi akishafika eneo la janga atasaidia kuokoa maisha ya wahanga wa janga husika?Au Missanga na wenzake anajaribu kutueleza kuwa mara nyingi hakuna jambo linalofanyika hadi kiongozi afike mahala husika?Kama ni hivyo,la muhimu si ndege au helikopta mpya bali uongozi na usimamizi mzuri wa nguvu kazi,sambamba na kukomesha tabia ya kusubiri maagizo ya rais au viongozi wengine wakuu katika kuutumikia umma.

Na kichekesho cha mwaka,na kilichonifanya niamini kuwa kauli ya Missanga na wenzie ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wajinga,ni ukweli kuwa ndege za rais zimetumika kwa asilimia 37 tu hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu.Kwa lugha sahihi,ndege hizo zimetumika chini ya nusu ya mahitaji yake.Je hiyo si sababu tosha kuonyesha kuwa ndege hazina umuhimu na ndio maana zinatumika 'kwa bahati mbaya'?

Leo ni Ijumaa Kuu.Kwa Wakristo,hii ni siku ambapo mkombozi wetu Yesu Kristo alitoa maisha yake msalabani kuwakomboa wanadamu.Japo natambua kuwa uongozi wa kisiasa ni tofauti na wa kidini lakini mfano wa Bwana Yesu kutoa maisha yake kwa ajili ya wanadamu unapaswa kuigwa na viongozi wetu kwa maana ya kujitoa mhanga kwa ajili ya wanaowaongoza.Na mhanga ninaozungumzia hapa sio wa kujitoa maisha kama alivyofanya Bwana Yesu bali kuangalia kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na ufanisi.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.