Nianze
makala hii kwa kutoa salamu zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki
wa marehemu Daniel John, ambaye hadi alipouawa kinyama alikuwa Katibu wa
Chadema kata ya Hananasifu, na pia kwa familia, ndugu,jamaa na marafiki wa
marehemu Acqulina Akwilin (samahani kama nimekosea jina).
Kwa
mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe,
mwili wa marehemu Daniel uliokotwa kwenye ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam
ukiwa na majeraha. Alieleza kuwa awali marehemu alichukuliwa na Land Rover
nyeupe na watu waliohifanya askari polisi, lakini tangu wakati huo Polisi
hawakuwa na taarifa zozote za kiuchunguzi, na hata jitihada za kupatikana mwili
huo zilifanywa na Chadema wenyewe.
DAR: Katibu wa Kata ya Hananasifu(CHADEMA) afariki dunia katika mazingira yenye utata. Mwili wake umekutwa ukiwa na jeraha la Panga kichwani— Jamii Forums (@JamiiForums) February 14, 2018
> Mwenyekiti wa CHADEMA, @freemanmbowetz amelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi | Soma https://t.co/KUeVlyNDlZ#JFLeo pic.twitter.com/KLJ2vstMBL
Kwa upande wa
marehemu Acquilina, kifo chake kilisababishwa na kasumba hatari inayozidi
kuzoeleka kwa watumishi wa vyombo vya dola kufanya mzaha katika matumizi ya
silaha za moto, ambapo katika tukio husika, polisi waliokuwa wakizuwia
maandamano ya wafuasi wa Chadema, walitumia risasi za moto,na moja kati ya
risasi hizo ilipelekea kifo cha binto huyo, ambaye hadi mauti yanamfika alikuwa
mwanafunzi katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) akisomea shahada ya
ununuzi na ugavi.
Mwanafunzi afariki baada ya kupigwa risasi Tanzania https://t.co/msRDdKeueE— bbcswahili (@bbcswahili) February 17, 2018
Ni muhimu
kutambua kuwa vifo vyote hivi viwili vingeweza kuepukika laiti utu na ubinadamu
wetu ungewekwa mbele ya chuki za kisiasa. Huhitaji kuwa mjuzi wa uchunguzi wa
mauaji kufahamu kuwa vifo hivyo ni matokeo ya chuki, hujuma, uonevu na kila
aina ya baya dhidi ya chama kikuu cha upinzani, Chadema, kuhusiana na kampeni
za uchaguzi mdogo katika jimbo la Kinondoni, ambalo kama ilivyo kwa jimbo la
Siha, ni "piga ua" kwa CCM ishinde. Yaani chama hicho tawala kilitarajiwa
kutumia kila mbinu kuhakikisha inashinda katika majimbo hayo mawili.
Lakini kabda
sijaingia kwa undani katika mada hii - ambayo lazima nikiri kwamba inanipa
wakati mgumu sana kuiandika kwa sababu nimebanwa na mchanganyiko wa majonzi na
hasira, sambamba na hofu ya kuona taifa langu likisukumwa kuelekea kwenye
upotevu wa amani na mshikamano wetu – naomba kuweka wazi masuala matatu ya
msingi kunihusu mie mwandishi wa mwakala hii.
Kwanza, mimi
licha ya kuwa na makazi nje ya Tanzania kwa takriban miaka 15 sasa bado no Mtanzania.
Utanzania wangu ni haki nilioirithi kutoka kwa wazazi wangu, na itabaki hivyo
milele. Naeleza hili kwa sababu kuwa wabaguzi wanaopenda kutuhukumu Watanzania
tunaoishi huku ughaibuni, na kutaka tuonekane kama Utanzania wetu sio kamili.
Kwa mantiki hiyo, kama Mtanzania, nina kila haki ya kutoa maoni yangu kuhusu
mustakabali wa taifa letu, hususan katika nyakati hizi ambapo kuna dalili za
wanaotaka kulipeleka kubaya taifa letu.
Pili, mwaka 2015
nilishiriki kikamilifu katika kampeni zilizomwingiza madarakani Rais John
Magufuli. Kwa upande mmoja nililazimika kumkampenia Magufuli kwa vile nilikuwa
nina "sababu binafsi" dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake mkuu, mgombea
urais wa tiketi ya UKAWA, Edward Lowassa. Wanasema "adui ya adui yako ni
rafiki yako."Kwa upande mwingine, nililipwa kutoa huduma ya ushauri wa
kitaalamu (usadi, yaani consultancy kwa kimombo) hususan kwenye mitandao ya
kijamii. Natanabaisha hili ili asije akakurupuka mtu na kusema "ah
ulishiriki kutupigia kampeni kwa vile tulikupa pesa."
Tatu, huko nyuma
nilikuwa mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Na kabla ya kuanza utumishi
katika taaluma hiyo muhimu na nyeti, nilikula kiapo kwa nchi yangu, kiapo
ambacho nitaishi nacho hadi ninaingia kaburini. Kiapo hicho sio cha kukitumikia
chama flani au viongozi wake bali Tanzania yetu. Nchi ni muhimu kuliko vyama vya siasa au wanasiasa.
Mtu aliyepikwa
na kuiva kwenye taaluma ya uafisa usalama wa taifa, katika nchi yoyote ile, anapaswa
kubaki kuwa mtiifu kwa nchi yake bila kujali yupo ndani au nje ya ajira ya
taasisi inayohusika na usalama wa taifa wa nchi husika.
Wanasema hata
nje ya ajira rasmi, kila mtu aliyewahi kuwa afisa usalama wa taifa anaendeshwa
na "sense of public duty born in
their previous lives" yaani wajibu kwa umma uliozaliwa katika maisha
yao huko nyuma. Jasusi mmoja mstaafu anaeleza “...I have obligations, professional obligations. If there’s a national
security emergency or possible national security issue, I should report it."
“ ‘You know, I have obligations, professional obligations. If there’s a national security emergency or possible national security issue, I should report it.’ ” ~ Steele— Evarist Chahali (@Chahali) February 8, 2018
Kwahiyo, hata
kama "maafisa wenzangu wa zamani" wataamua kukaa kimya kwa sababu
moja au nyingine – wengi wanahofia usalama wa maisha yao – sie wengine hatuwezi
kukaa kimya, hasa kwa vile baadhi yetu tumeshalipa gharama kubwa kwa kelele
zetu. Kukaa kimya ni sawa na kuafiki uhuni unaoendelea ambao ni tishio kwa
usalama wa taifa.
Lakini licha ya
wajibu huo unaotokana na utumishi wetu kwa nchi huko nyuma, Rais Magufuli
amefanikiwa kuvifunga mdomo vyombo vya habari kiasi kwamba haviwezi kusema
lolote kuhusu "mabaya" yake, na amefanikiwa kuvijengea nidhamu ya
uoga vyombo hivyo vya habari kiasi kwamba habari pekee zenye umuhimu kwao ni za
kumtukuza na kumpamba "mungu-mtu" huyo. Kwahiyo na sie tuliopikwa na kuiva kuhusu ujasiri, kujitoa mhanga na kutokuwa waoga tukiufyata na kukaa kimya - ilhali media zetu ndio zishapigwa kufuli - hali itazidi kuwa mbaya.
Rais wa Tanzania John Magufuli ayaonya baadhi ya magazeti nchini humo https://t.co/grUpqa52uq— DW (Kiswahili) (@dw_kiswahili) January 13, 2017
Baada ya kuweka
wazi nafasi yangu, sasa tuangalie kwa kina kinachoendelea huko nyumbani hasa
kuhusiana na uchaguzi mdogo kwenye jimbo la Kinondoni na Siha na kuuawa kwa Daudi
na Acquiline.
Ni muhimu
kutambua kwamba ukandamizaji dhidi ya vyama vya upinzani sio kitu kilichoanza
chini ya utawala wa Magufuli bali hali hiyo imedumu mfululzo tangu kuanzishwa
kwa mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992. Labda kilicho tofauti kwa zama
hizi ni "ujasiri" wa Magufuli kutoficha chuki yake dhidi ya vyama vya
upinzani. Yaani angalau akina Mwinyi,Mkapa na Kikwete walikuwa "wanauma na
kupuliza." Kwamba angalau walikuwa na "mshipa wa aibu" na
walijitahidi japo kutowaonea Wapinzani waziwazi.
Kwa wanaojua
"yanayojiri nyuma ya pazia" watakwambia kuwa hujuma dhidi ya vyama
vya upinzani ni miongoni mwa vipaumbele vikubwa kwa CCM na serikali zake, na
hiyo imepelekea kujengeka "symbiotic relationship" kati ya chama
hicho tawala na taasisi za dola, ambapo kila mmoja anategemea uhai wa mwenzie.
Lakini kama kuna
kitu kinachokera zaidi kuhusu hujuma dhidi ya demokrasia ni pale CCM na taasisi
zake hasa za dola wanapoweka mbele maslahi yao mbele ya utu na uhai wa
Watanzania. Na hili halijaanza jana au katika kampeni za chaguzi ndogo katika
majimbo ya Kinondoni na Siha.
Uchaguzi mkuu wa
kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 ulihusisha matukio mengi tu ambayo kwa
makusudi hayapo kwenye kumbukumbu za wazi (japo yamehifadhiwa mahala flani).
Lakini kama
wanavyosema "amekula asali sasa anachonga mzinga," baada ya hujuma za
kimyakimya za mwaka 1995 kuzaa matunda, CCM na taasisi zake ikanogewa, na
matokeo yake ni kwamba uchaguzi mkuu uliofuata, mwaka 2000 uliweka doa kubwa
kwa historia ya Tanzania yetu ambapo kwa mara ya kwanza nchi yetu ilizalisha
wakimbizi kufuatia unyama uliofanyika huko Zanzibar na kupelekea vifo kadhaa (idadi halisi ya vifo haijawahi kuwekwa hadharani japo "wenyewe"
walisema zaidi ya watu 19 ndio waliokufa kwenye machafuko hayo. Wasichosema pia
ni idadi ya watu waliobakwa, kuteswa na kuwekwa kizuizini.
Kwamba hujuma
hizo za CCM dhidi ya demokrasia zilipelekea vifo na majeruhi ni kitu kibaya
kabisa. Lakini kitu kingine kibaya ni ukweli kwamba hakuna mtu hata mmoja
aliyechukuliwa hata kutokana na unyAma waliofanyiwa Wazanzibari hao.
Kwa namna ya
kipekee, CCM ikawa kama imepewa ruhusa ya kutumia vyombo vyake vya dola kufanya
lolote itakalo ili ifanikishe hujuma zake dhidi ya Wapinzani na demokrasia kwa
ujumla, kisha iibuke na ushindi.
Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2005 ulikuwa na "uchafu kupindukia." Kundi lililofahamika kama "mtandao"
lilijipenyeza katika kila sekta, kuanzia kwenye vyombo vya habari, taasisi za
dola hadi kwenye taasisi za dini. Yayumkinika kabisa kuhitimisha kwamba
yaliyojiri wakati "mtandao unafanya jitihada za kumwingiza mtu wao
Ikulu" ni mabaya zaidi ya haya tunayoshuhudia sasa tangu Magufuli aingie
madarakani.
Kwanini basi
hayo yaliyojiri kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 hayajulikani? Jibu ni
kwamba, wakati mbinu iliyotumika mwaka 1995 na 2000 ilitegemea zaidi vyombo vya
dola, uchaguzi wa mwaka 2005 na 2010 ulitegemea zaidi nguvu ya fedha, nyingi
zikiwa fedha haramu. Na sehemu ya fedha hiyo ilitumika "kununua ukimya" wa wanahabari wengi tu.
Lakini si fedha tu bali pia kuna hujuma mbalimbali – nyingine chafu na za kuchefua – zilizotawala safari za ushindi wa chama tawala kwenye chaguzi hizo.
Lakini si fedha tu bali pia kuna hujuma mbalimbali – nyingine chafu na za kuchefua – zilizotawala safari za ushindi wa chama tawala kwenye chaguzi hizo.
Labda tofauti
nyingine kuhusu mwaka 2005 na 2010 ni ukweli kwamba wakati chaguzi hizo
zilihusisha "kikundi binafsi" yaani hicho cha wanamtandao ambacho
hakikuwa taasisi ya serikali au chama.
Lakini muda wote
huo, CCM ilikuwa kama imepwa ruhusa na Watanzania kuendeleza hujuma zake dhidi
ya Wapinzani na demokrasia kwa ujumla. Hakujawahi na utashi miongoni mwa
Watanzania kutaka kukabiliana kwa dhati za uhuni/uhalifu wa kisiasa. Na kwa
bahati mbaya, kwa vile vipaumbele vya Watanzania wengi ni kwenye
"ubuyu" na "kubeti/mkeka" basi habari mbaya ni uwezekano wa
CCM kuendelea kufanya itakavyo kwa muda mrefu sana.
Sio kama kwa
kubashiri kuwa unyanyasaji wa CCM utaendelea muda mrefu sana ninamaanisha kuwa
nimekata tamaa. Hapana. Ninakuwa mkweli tu. Tatizo ni zaidi ya CCM na uhuni
wake. Watanzania wenyewe ni sehemu ya mfumo unaowezesha CCM kufanya uhuni/uhalifu
huo.
Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015 ulihusisha pia matuki kadhaa yaliyojiri "nyuma ya pazia."
Na ukitaka kufahamu kuwa Tanzania yetu haijawahi kuhangaishwa na mauaji ya
kisiasa – kuanzia yale ya mwaka 2001 huko Zanzibar hadi haya ya Daudi wa Hananasifu
na dada Acquilina – ni kifo cha Mchungaji Christopher Mtikila.
Mchungaji Mtikila afariki kwa ajali ya gari Chalinze mkoani Pwani | Soma http://t.co/xRXAqextLi #RIPMtikila pic.twitter.com/HoNnzkjy3w— FikraPevu (@FikraPevu) October 4, 2015
Kwahiyo, na
ninaandika haya kwa uchungu mkubwa uliochanganyika na hasira, kuuawa kwa Daudi
na Acquilina kutaishia kuwa moja tu ya matuko yaliyowahi kutokea katika
Tanzania yetu. Tutawasikia wanasiasa wetu wa vyama vya upinzani wakiongea kwa
hisia kubwa. Tutashuhudia pia wanafiki wengi tu miongoni mwa wasanii wetu nao
wakijifanya kuguswa na vifo hivyo, lakini wakiwa makini kuepuka kumuudhi
"Bashite na baba yake" au kuitibua CCM. Tutashuhudia pia kundi la
wanafiki hatari ndani ya CCM wakijifanya kuumizwa na mauaji hayo, na kutaka
uchunguzi ufanyike, ilhali nao ni kondoo waliojivika ngozi ya mbwa mwitu.
Cheap politics + unafiki. Mbwa mwitu wanaojivika ngozi ya kondoo. Inapofika wakati wa kujitoa mhanga kwa minajili ya kuondoa mfumo kandamizi, hawa wanafiki huonyesha rangi yao halisi na kujivika ukada. https://t.co/39aZHTpFQt— Evarist Chahali (@Chahali) February 17, 2018
Bora tu JPM au Polepole ambao wapo honest kuhusu chuki zao kwa Upinzani/Wapinzani kuliko wanafiki "wanaouma na kupuliza." Bora maadui milioni kuliko "rafiki" mmoja mnafiki https://t.co/39aZHTpFQt— Evarist Chahali (@Chahali) February 17, 2018
Kama ambavyo
"mauaji mengine ya kisiasa" yalivyoruhusiwa kupita kimyakimya, ndivyo
unyama huu uliofanywa dhidi ya Daudi na Acquilina utakavyoruhusiwa uishe
kimyakimya.
Kwa upande mmoja
tusitarajie Rais Magufuli awajibike – sio kwa yeye binafsi kujiuzulu kwa sababu
hilo litakuwa kutarajia zaidi ya muujiza – kwa kumtimua Waziri husika na watendaji
katika jeshi la polisi. Kwa upande mwingine, hakuna wa kumshinikiza Rais
Magufuli achukue hatua stahili dhidi ya wahusika.
Na nisingependa
kuuma maneno hapa. Yeye Magufuli mwenyewe ni chanzo muhimu cha siasa hizi za
uhasama zinazoendelea kuitafuna Tanzania yetu. Huyu ni mtu ambaye wala hapati
shida kuonyesha chuki zake za waziwazi dhidi ya Wapinzani, Upinzani na
demokrasia kwa ujumla.
Tufike mahala tuambiane ukweli: @MagufuliJP anaipeleka Tanzania kusikostahili. And that is too bad. But what's even worse ni kwamba asilimia kubwa ya Watanzania wanasubiri miujiza, kwamba siku moja huyu bwana atabadilika. He won't. Worse is yet to come (God forbid)#MarkThisTweet pic.twitter.com/Uy3VnkOKOH— Evarist Chahali (@Chahali) February 17, 2018
Kama ilivyo kwa
madikteta wengine duniani, Magufuli amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutumia
ajenda yake ya ufisadi kama kisingizio cha kusigina haki za binadamu nchini
Tanzania, na kubinya kila fursa ya haki za kidemokrasia na uhuru wa habari. Kama
nilivyoeleza awali, amefanikiwa kuviziba midomo vyombo vya habari na ndio maana
hata habari za kusikitisha kuhusu mauaji ya Daudi na Acquiline hazijaripotiwa
vya kutosha.
Kwa kuviziba
midomo vyombo vya habari Magufuli amefanikiwa kuzuwia "habari asizozipenda"
na ndio maana hadi muda huu ni Watanzania wachache tu wanaofahamu kilichojiri
huko MKIRU katika kilichoitwa "operesheni dhidi ya ugaidi." Kuna siku
yaliyojiri huko – na ambayo yamechangia "kupotea" kwa mwandishi wa
gazeti la Mwananchi Azory Gwanda – yatajulikana hadharani. Haijalishi itachukua
miaka mingapi.
Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema mwandishi wa Mwananchi aliyetekwa, Azory Gwanda alikuwa anafuatilia taarifa za mauaji ya chini kwa chini yaliyokuwa yanaendelea Kibiti— Jamii Forums (@JamiiForums) December 9, 2017
> Wanadhani mazingira haya ndio yatakuwa yamepelekea usalama wake kuwa hatarini#JFLeo pic.twitter.com/HPsQzmc3XI
Lakini
"yaliyojiri MKIRU" ni uthibitisho mwingine wa hicho nilichoeleza hapo
juu kuwa Watanzania wenyewe ndio wanaopaswa kubeba lawama nyingi katika kasumba
ya CCM kutojali uhai katika harakati zake za kukandamiza demokrasia. Kwamba
kama yaliyojiri MKIRU yameachwa yaishe kienyeji, kwanini tutegemee hali tofauti
kwa vifo vya Daudi na Acquiline?
Kama ndugu zetu
wa Chadema (na kila mpenda haki) "wamekubali yaishe" kuhusu kifo cha
Kamanda Mashaka, "kupotea" kwa kada Ben Saanane (hata zile kampeni za
#BringBackBenAlive zimejifia kifo cha asili), na hawasumbuliwi na serikali ya
Magufuli kupuuzia jaribio la mauaji dhidi ya Tundu Lissu, kwanini tutarajie
jipya katika mauaji yaliyofanywa dhidi ya Daudi na Acquiline?
Yaani Mnadhimu
Mkuu wa upinzani anamwagiwa risasi hadharani wakati mkutano wa bunge unaendelea
huko Dodoma, na tunaambiwa kuwa tukio hilo lilitokea katika eneo lenye ulinzi
mkubwa na lenye CCTV, kwanini basi wanaosumbuliwa na tukio hilo wasitafute njia
stahili za japo kuifanya serikali ione aibu na kufanya japo "uchunguzi wa
kizushi"?
Kuhusu hujuma
"za kawaida" za uchaguzi, kama kila aina ya uhuni uliofanywa na CCM
kwenye chaguzi ndogo za madiwani katika kata 43 uliofanyika Novemba mwaka jana uliruhusiwa
upite "kimya kimya" – kwa maana kwamba hakuna hatua zozote zilizochukuliwa
dhidi ya uhuni huo – kwanini basi chaguzi hizi ndogo katika jimbo la Siha na
Kinondoni zilitarajiwa kuwa tofauti?
Na katika hili,
inapaswa wana-Chadema wajiulize kuhusu busara za viongozi wao kuamua kushiriki
katika chaguzi hizo ndogo Siha na Kinondoni ilhali mazingira yaliyokuwepo yalikuwa
yaleyale yaliyopelekea chama hicho kususia chaguzi nyingine ndogo tatu katika
majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini uliofanyika mwezi
uliopita.
Hadi wakati
ninaandika makala hii, tayari Tume ya Uachaguzi ilikuwa imeshamtangaza mgombea
wa CCM jimbo la Siha, Godwin Mollel kuwa mshindi kwa tofauti kubwa tu ya kura dhidi
ya mgombea wa Chadema. Hata kama CCM wameiba kura, ukubwa wa tofauti kati ya
kura za mgombea wao na huyo wa Chadema zinaashiria kuwa chama hicho kikuu cha
upinzani kilipitisha mgombea fyongo.
Mgombea wa CCM, Dk Godwin Mollel ametangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa mshindi wa Ubunge Jimbo la Siha baada ya kupata kura 25,611 dhidi ya mpinzani wake, Elvis Mosi wa CHADEMA aliyepata kura 5,905 - Mwananchi pic.twitter.com/hG6oT9GUpZ— Kwanza TV (@kwanza_tv) February 18, 2018
Na kama
ilivyotarajiwa mgombea wa CCM jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia, naye ametangazwa mshindi.
Mie mtumishi wako nilishabashiri mapema tu kuwa chama hicho tawala kingeshinda majimbo hayo, "iwe isiwe."
Breaking news: Aliyekuwa Mgombea Ubunge kwa ticket ya CCM, Maulid Mtulia ametangazwa kuibuka mshindi katika uchaguzi mdogo wa marudio wa Jimbo la Kinondoni.— millardayo (@millardayo_) February 18, 2018
Mtulia amepata kura 30,313 dhidi ya mpinzani wake Salum Mwalim (CHADEMA) aliyepata kura 12,353#MillardAyoUPDATES pic.twitter.com/rYsb0Jgbie
Mie mtumishi wako nilishabashiri mapema tu kuwa chama hicho tawala kingeshinda majimbo hayo, "iwe isiwe."
Ushindi kwa
wagombea hao wa CCM ulipaswa kupatikana kwa gharama yoyote kwa sababu laiti wangeshindwa,
kinachoelezwa kama "mkakati wa Magufuli kuua upinzani kwa kununua wabunge na
madiwani wa Upinzani" kingemfanya
achekwe hata huko kwenye chama chake.
Na kwa vile hadi
sasa wabunge na madiwani waliohama upinzani na kujiunga na CCM wamefanikiwa
kurudi madarakani baada ya chama hicho tawala kuwapa fursa ya kuwa wagombea
wake kwenye chaguzi ndogo, na kuwasaidia kwa hali na mali washinde, tutarajie
wabunge na madiwani wengin zaidi kuhama vyama vya upinzani na kujiunga na CCM.
Kisa? "Dili hilo linalipa," kwa CCM na kwa wanasiasa hao wanaohama.
Na unadhani
mbunge au diwani "mwenye moyo mwepesi" akiona jinsi chama chake "kilivyochukulia
poa" yaliyowasibu akina marehemu Mashaka na Daudi, na yaliyowasibu Ben
Saanane na Lissu, kwanini iwe ngumu kwake kushawishika kuhama?
Ningetamani sana
kuhitimisha makala hii kwa kushauri nini kifanyike lakini itakuwa kupoteza muda
wangu na muda wako msomaji. Ni vigumu mno kuwashauri watu waliokubali kwamba
mgao wa umeme ni stahili yao kwa zaidi ya miaka kumi sasa, na ambao kila mara
umeme unaporudi wanashangilia kana kwamba wamepewa upendeleo flani.
Kama Watanzania
wameshindwa kuilazimisha Tanesko iache mgao wa umeme, wataweza kweli
kuilazimisha CCM iache hujuma dhidi ya vyama vya upinzani na demokrasia kwa
ujumla? Ndio maana bila utu wala aibu, chama hicho tawala kinapata ujasiri wa kukifanyia mzaha kifo cha Acquiline ambapo kwa kudai polisi (haohao waliomuua binti huyo) wachukue hatua dhidi ya Mbowe. Utterly disgusting!
Na kama mauaji mbalimbali ya kisiasa huko nyuma yameachwa yapite na kusahaulika, kwanini tutarajie miujiza kwenye mauaji haya ya sasa dhidi ya wapendwa wetu Daudi na Acquline?
@ccm_tanzania This is too low. Kwanini msitumie akili badala ya makalio kutambua mnachofanyia mzaha huu ni uhai wa Mtanzania uliokatishwa kinyama na polisi haohao mnaowapa kinga kwa kumsingizia @freemanmbowetz? Hamna utu wala mshipa wa aibu? Mungu awalaani kwa hili— Evarist Chahali (@Chahali) February 18, 2018
cc @MagufuliJP pic.twitter.com/7lgzKh0ofe
Na kama mauaji mbalimbali ya kisiasa huko nyuma yameachwa yapite na kusahaulika, kwanini tutarajie miujiza kwenye mauaji haya ya sasa dhidi ya wapendwa wetu Daudi na Acquline?
Na ukweli
mchungu ni kwamba Magufuli ataendelea kuwapelekesha Watanzania atakavyo ka
sababu si watangulizi wake -Mwinyi, Mkapa na Kikwete – wenye jeuri ya kumwambia
"Ee bwana ee, huku unakoipeleka nchi siko." Hawawezi kwa sababu nao
ni kama "mateka." Madhambi waliyofanya kwenye tawala zao yanawafanya
wahofie hatma yao pindi wakimkosoa "mungu-mtu" aliyepo madarakani.
Na wakati
wastaafu au watumishi wa zamani wa Idara za Usalama wa Taifa kwenye nchi kama
Marekani wamekuwa mstari wa mbele kukemea kila tendo linalotishia usalama wa
nchi hiyo – kwa mfano 'ndoa' kati ya Rais Donald Trump na Russia – wastaafu wetu
sie hawana jeuri ya kufungua mdomo sio tu kwa vile wanahofia kuathiri posho na
marupurupu yao bali kwa vile nao ni mateka wa "madudu" waliyofanya
walipokuwa madarakani. Ukiwa mchafu unajinyima uhuru wa kukemea uchafu.
James Comey mkuu wa zamani wa FBI na John Brennan mkuu wa zamani wa CIA ni miongoni mwa sauti muhimu kuhusu mustakabali wa taifa la Marekani. Wako wapi "akina Comey na Brennan" wetu kuhusu mustakabali wa Tanzania yetu? pic.twitter.com/DSA0mWYZ8A— Evarist Chahali (@Chahali) February 17, 2018
Basi niishie
hapa kwa kurejea tena salamu zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na
marafiki wa marehemu Daudi na Acquiline. Ni vigumu kuwaambia maneno yanayotosha
kuwaliwaza lakini la muhimu ni kuendelea kuzikumbuka roho za marehemu hao, hasa
katika kipindi hiki cha Kwaresma ambapo sisi Wakristu tunaadhimisha mateso ya
Bwana Yesu Kristo. Pumziko la Milele awape Bwana, na Mwanga wa Milele
awaangazie, wapumzike kwa amani. Amen