15 Jun 2010

Wakati Waingereza wanasubiri Bajeti ya Dharura ya Serikali mpya iliyoingia madarakani hivi karibuni,watawala hapa wameweka bayana kuwa baadhi ya hatua zitakazochukuliwa kurekebisha uchumi zitapelekea machungu kwa wananchi wengi.Hakuna haja ya kudanganyana kwa vile hata wangeficha ukweli huo,muda wa makali hayo ukifika watawala wangeumbuka.Na ni vema pia kuwatayarisha wananchi ili pindi hali itapokwenda mrama wawe katika tahadhari na wamejiandaa vya kutosha.

Lakini kwa watawala wetu,kusema ukweli ni kama kujivunjia heshima.Na si kwa wao tu,bali hata wananchi wanapoamua kuweka bayana hisia zao kuwa nchi yetu inapelekwa pabaya,watawala wanaona kama wanakosewa heshima.Kilichopelekea niandike makala hii ni kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa ahadi ambazo hazijatekelezwa katika miaka minne iliyopita zitatekelezwa katika bajeti hii.Sijui ni ushauri mbovu wa washauri wake,sijui ndio kampeni,au sijui ni kuwafanya Watanzania mabwege sana,lakini kwa kila anayefahamu hali ya uchumi wetu na wingi wa ahadi zilizokwishatolewa ni dhahiri kuwa kauli hiyo sio ya kweli.

Kikwete anapaswa kurejea ahadi alizotoa wakati wa kampeni zake mwaka 2005,na alizoendelea kutoa katika miaka minne iliyopita,kisha angejaribu kuangalia nini kimekwaza ahadi hizo.Hebu kwa minajili ya makala hii tuangalie baadhi ya ahadi hizo na kutathmini kama kweli bajeti hii ya kutegemea hisani za wafadhili itaweza kutimiza ahadi hizo.JK alinukuliwa mwezi August 2008 akisema tatizo la umeme lingepatiwa ufumbuzi wa kudumu.Miezi michache baadaye ufumbuzi ukapatikana,si kwa wananchi bali kwa akaunti za matapeli wa Richmond.Je ni kweli kuwa bajeti hii itaweza kutimiza ahadi hiyo ya JK kuhusu tatizo la umeme?Na mbona hatuelezi utatuzi huo utakuwaje?

Twende kwenye suala la rushwa na ufisadi.JK alitamka bayana kuwa watu wasitafsiri vibaya tabasamu lake kwani hatakuwa na huruma kwa fisadi yoyote yule.Akaenda mbele zaidi kutanabaisha kuwa anawafahamu wala rushwa na anawapa muda wa kujirekebisha.Sote tunajua kinachoendelea katika Awamu hii ya Nne chini ya JK.Ufisadi umeota mizizi kupita kiasi huku mafisadi wakiendelea kulindwa,na wanaojiuzulu wanafarijiwa kuwa "kuna siku watarejea serikalini".Hivi ni kweli kuwa bajeti hii itawezesha utekelezaji wa ahadi hiyo ya JK kupambana na mafisadi?Kilichomshinda katika miaka minne iliyopita kitawezekanaje miezi hii michache kabla ya uchaguzi?Na je inahitaji bajeti moja kabla ya uchaguzi kumwezesha kuwadhibiti mafisadi?


Anyway,hebu soma kauli zake katika habari ifuatayo kisha ufanye tafakuri jadidi Ahadi za JK kukamilika Bajeti hii
Imeandikwa na Na Maulid Ahmed, Dodoma; Tarehe: 12th June 2010 @ 23:52

Ahadi ambazo hazijatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nne zitatekelezwa katika Bajeti hii ya mwaka 2010/11, imeelezwa.

Akizungumza jana mjini hapa katika kikao cha kazi na wakuu wa mikoa na wa wilaya pamoja na makatibu tawala wa mikoa yote Tanzania Bara, Rais Jakaya Kikwete aliwataka viongozi hao kusimamia shughuli za Serikali kikamilifu.

Aliwataka kutokwenda likizo katika kipidi hiki cha kuelekea uchaguzi na wasimamie kazi kama wanavyofanya wakati wote.
Rais Kikwete alisema katika kipindi cha miaka mitano tangu Serikali yake iingie madarakani mengi waliyoahidi yametekelezwa.

“Juzi kabla ya Bajeti hata kwenye Baraza la Mawaziri, tulizungumzia ahadi zetu na nyingi tumeshazitekeleza, lakini zilizobaki na majukumu tuliyojipangia kwa miaka yote hii tutatekeleza katika Bajeti hii … tulipoingia mwaka wa kwanza, tulitekeleza ya Awamu ya Mzee Mkapa (Rais mstaafu Benjamin) sasa tunaendelea na kutekeleza yetu,” alisema.

Akizungumzia uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, alisema “tunakwenda kwenye uchaguzi na michakato imeshaanza, lakini Serikali haiendi likizo, usione uchaguzi nawe ukaenda likizo, fanya shughuli za maendeleo kwa kuzisimamia kama mnavyofanya wakati wote”.

Alisema hataki kuona uchaguzi unaharibikia mikononi mwa viongozi hao na kuwataka kuhakikisha wagombea hawanyimwi haki ya kumwaga sera zao majukwaani, kura zinapigwa kwa amani na kunakuwa na utulivu wakati wote, kuanzia mchakato wa wagombea hadi uchaguzi.

Rais Kikwete aliyehutubia viongozi hao kwa dakika 10, alitaja baadhi ya mafanikio ya Serikali yake, kuwa ni kuendelea na ujenzi wa barabara za lami, watoto kusoma elimu ya msingi na sekondari, upanuzi wa elimu ya juu na huduma bora za afya kupatikana...

CHANZO: Habari Leo

3 comments:

  1. NASIKIA RAISI KAOA MKE MWINGINE JE KUNA UKWELI WOWOTE??

    ReplyDelete
  2. Hapo ni ubabaishaji tuu, hakuna viongozi makini hata kidogo...

    ReplyDelete
  3. Fainali ni 2015 kwa kuwa yanayotokea ni mpiango ya rais alopita. Hakuna la kikwete hata moja labda richmond :-(

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube