Utawala wa Rais Jakaya Kikwete unaendelea na jithada zake za kutaka kuifanya Tanzania isitawalike baada ya jeshi lake la polisi kuendeleza ubabe dhidi ya viongozi wa Chadema.
Katika matukio yanayoweza kuingizwa kwenye vitabu vya historia (chafu),jeshi hilo maarufu zaidi kwa ubabe kuliko uwezo wake kukabiliana na uhalifu limewatia mbaroni Mwenyekiti wa taifa wa Chadema,Freeman Mbowe,na Mbunge maarufu wa chama hicho Zitto Kabwe.Wakati Mbowe,ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Upinzani Bungeni (wadhifa unaomfanya kuwa Waziri Mkuu Kivuli) alikamatwa kwa madai ya kukiuka taratibu za dhamana katika kesi inayomkabili huko Arusha,Zitto alikamatwa kwa madai ya kuzidisha muda wa kuhutubia mkutano wa hadhara.
Tangu Tanzania iridhie uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa,mahusiano kati ya vyombo vya dola na vyama hivyo yamekuwa mabaya na ya ounevu kupindukia.Tatizo la wazi ni vyombo hivyo vinavyoendeshwa kwa fedha za walipa kodi pasipo kujali itikadi zao za kisiasa kuendelea kutekeleza majukumu yake kana kwamba ni matawi ya chama tawala.Wakati jeshi la polisi ndilo linaloongoza kwa kuwanyanyasa wapinzani,taasisi nyingine za dola kama Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania pia kwa nyakati mbalimbali zimeonyesha kuweka mbele unazi wa kisiasa na kuipendelea CCM.
Lakini licha ya kushamiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani,kuibuka kwa Chadema kama ngome kuu ya upinzani kumekuwa mithili ya pilipili inayowawasha polisi kiasi cha kuwaandama viongozi wa chama hicho kila kukicha.
Ni dhahiri kuwa matendo haya yana baraka za Rais Kikwete kwani laiti angemwamuru rafiki yake Said Mwema,Inspekta Jenerali wa Polisi,kuhakikisha jeshi la polisi sio tu linawapa heshima viongozi wa upinzani bali pia lizingatie haki zao za kibinadamu,ni dhahiri tusingeshuhudia manyanyaso kama hayo waliyopewa Mbowe na Zitto.
Kikwete na jeshi lake la polisi wanapaswa kutambua kuwa kadri wanavyotumia nguvu nyingi kuwadhibiti Chadema ndivyo wanavyozidisha huruma ya Watanzania kwa chama hicho.Mtu yeyote mwenye akili timamu hatoshindwa kubaini kuwa unyanyasaji unaofanywa na jeshi la polisi dhidi ya chama hicho unalenga kukipunguzia nguvu katika jitihada zake za kupambana na ufisadi unaolelewa na serikali ya Kikwete na chama chake cha CCM.
Uzoefu unaonyesha kuwa tunaweza kulilaani jeshi la polisi hata kila sekunde lakini hiyo haitopelekea jeshi hilo lililosheheni mbumbumbu wa sheria za haki za binadamu kubadili utendaji kazi wao wa ovyo ovyo.Tunahitaji kwenda mbali zaidi ya kulaumu na kulaani pekee.
Ni muhimu basi kwa Chadema kuchukua hatua za kisheria dhidi ya jeshi la polisi.Kwa vile mahakama zetu nazo zinaendeshwa kisiasa,basi pengine ni muhimu kujaribu kufungua mashtaka ya aina hiyo katika mahakama za kimataifa.
Tetesi zinadai kuwa tawi la serikali ambalo kikatiba lina jukumu la kutafsiri ya sheria (Mahakama) chini ya uongozi wa Jaji Mkuu Othman Chande linaendesha shughuli zake "kishkaji" na tawi la serikali lenye jukumu la kusimamia sheria,yaani serikali kwa maana ya Executive branch.Tetesi hizo zinapigia mstari hoja kuu mbili.Kwanza,Jaji Mkuu Othman ni kaka wa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa Othman Rashid,ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Kikwete,kama alivyo IGP Mwema.Sasa ukiwa na kaka wawili kwenye nafasi nyeti kama hizo,na ambazo kikatiba zinapaswa kufanya kazi zake kwa kuzingatia mgawanyiko wa mamlaka (separation of powers),ni wazi kuwa nchi inaendeshwa kama kampuni ya mtu binafsi.
Kwa upande mwingine,Jaji Mkuu alikuwa miongoni mwa waalikwa kwenye semina elekezi iliyofanyika majuzi jijini Dodoma.Yayumkinika kuhisi kuwa ushiriki wa Jaji Mkuu kwenye semina hiyo kumepelekea Mahakama kumezwa na Serikali (Executive),na si aabu Mahakama ikawa inatekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya serikali.Changanya hali hiyo na hizo teuzi za kufahamiana...!!!
All in all,ni lazima ukatili wa jeshi la polisi sio tu ulaaniwe kwa nguvu zote bali pia ukomeshwe kwa hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.Na kwa vile mahakama za ndani ndio hivyo tena zishakuwa kama matawi ya CCM,kuna haja ya kutafuta haki kwenye mahakama za kimataifa.
Mwisho,Kikwete na watendaji wake,na jeshi lake onevu la polisi wanaweza kuwatupa ndani viongozi wa vyama vya upinzani kadri watakavyo...kwa muda flani, lakini kamwe hali hiyo haitaendelea milele.Kama ameshindwa dikteta Hosni Mubarak ataweza Kikwete?Tawala dhalimu zinaweza kudhani kuwa ubabe na uonevu ni silaha muhimu za ustawi wake lakini ukweli ni kwamba vitendo hivyo huharakisha uchimbaji kaburi la kuzika tawala za aina hiyo.
Ni muhimu kwa kila mpenda haki na usawa kukemea kwa nguvu zote uhuni huu wenye lengo moja tu: kudhoofisha mapambano yanayoongozwa na Chadema dhidi ya ufisadi unaolelewa na serikali ya Kikwete na CCM yake.Kadhalika,kashkash dhidi ya Chadema inamsaidia Kikwete na CCM yake kupooza mvurugano unaoendelea ndani ya chama hicho ambao umesababishwa na mgongano wa kimaslahi ya kifisadi.
Enough is enough!