26 Aug 2010

Na Frederick Katulanda, Mwanza na Sadick Mtuly

LICHA ya sheria na kanuni za Uchaguzi kuzuia matumizi ya magari ya serikali, msafara wa mgombea urais wa CCM Jakaya Kikwete umetumia magari kadhaa ya serikali katika mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.

Mbali na magari hayo, wakuu wa wilaya waliokuwa wameshiriki msafara wa mwenyekiti huyo wa CCM, walitumia magari yao ya kazi yakiwa yamewekwa namba binafsi huku wakivalia sare za chama hicho.

Ukiondoa magari maalumu ya walinzi wa mgombea huyo ambaye pia ni rais, magari mengine ya wakuu wa wilaya na wakuu wa idara mbalimbali za serikali, yalitumika na kuwekwa namba binafsi.

Kwa mujibu wa habari tulizozipata kutoka vyanzo vyetu zinaeleza kuwa hivi sasa Ikulu ya Dar es Salaam ina upungufu kwa kuwa wafanyakazi wa Ikulu hasa madereva pamoja na wapishi na wagawa vinywaji (waandazi), wanatumika katika kampeni za Rais Kikwete.

Wapishi na waandazi hao wamepelekwa mikoani kulingana na ziara za kampeni.

“Cha ajabu ni kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Ikulu hasa madereva, wapishi na waandazi wanatumika katika kampeni za CCM kupitia Rais Kikwete.

“Wamegawanywa katika mikoa tofauti kulingana na ratiba za ziara za kampeni za rais,’’ kilisema chanzo chetu.

Juzi jijini Mwanza Mkuu wa wilaya Ilemela, Serenge Mrengo ambaye alifika majira ya saa 4:35 asubuhi uwanja wa ndege na gari lenye namba za STK 3551 huku wote wawili na dereva wake wakiwa wamevalia sare za CCM, lakini baada ya kusalimiana na viongozi wenzake, aliondoka.

Akiwa wilayani Geita, Mkuu wa wilaya hiyo Philemon Shelutete alitumia gari lake la serikali ambalo lilikuwa limebandikwa namba T 804 BCZ huku akiwa amevalia sare za CCM. Pia gari la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Benson Katala lilitolewa namba za serikali na kubandikwa namba T 180 BKW.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Abbas Kandoro alitetea hatua hiyo akisema sio kosa kwa kuwa Kikwete bado ni rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanania.

Kandoro, alikiri kutumika kwa magari hayo ya serikali na kusema kuwa viongozi hao waliyatumia kumpokea na baadhi yao waliambatana naye katika ziara hiyo kwa kuwa mbali na kuwa mgombea wa CCM pia anayo hadhi ya urais.

“Huyu ni Rais, amekuja kama kiongozi licha ya kwamba anagombea, bado hajavuliwa urais, sasa ma-DC walikuja kama viongozi wa serikali kumpokea rais. Kama kuna mkuu wa wilaya alivaa shati la CCM alivaa kwa sababu ya mapenzi yake kwa chama,” alifafanua Kandoro ambaye alitumia gari binafsi la kiongozi mmoja wa CCM Kanda ya Ziwa.

"Makosa ni kiongozi wa serikali kufanya kazi za chama na sioni kama kuna kiongozi wa serikali ambaye alifanya kazi za chama,"alisema

Msafara wa Kikwete kuambatana na magari ya serikali haukuishia Mwanza na Geita pekee bali pia hata mkoani Kagera ambako magari mengi yalikuwa na namba za STK.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando umetoa ufafanuzi kwamba uamuzi wake wa kutoa gari la kubebea wagonjwa katika msafara wa mgombea urais wa CCM kuhakikisha usalama wa mgombea huyo.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk Charles Majinge alisema kwa kawaida jukumu la kutoa magari huwa lipo mikononi mwa uongozi wa mkoa ambao uliomba gari kwao na wao waliamua kutoa gari hilo la wagonjwa namba T 848 AWN.

“Sisi hatutoi ambulance kwa wagombea, ila tulitoa kwa Kikwete kutokana na kuwa ni kiongozi wa nchi. Kutoa magari huwa ni kazi ya uongozi wa mkoa, lakini sisi kama watalaamu wa matibabu tulichukua tahadhari na kuweka gari hilo,” alieleza Dk Majinge.

Alisema kwa vile akiwa jijini Mwanza aliwahi kuanguka, basi waliamua kuchukua tahadhari kuepuka kukosa huduma haraka iwapo jambo hilo lingejirudia akiwa mbali na hospitali ya rufaa.

Akizungumzia gari hilo, Kandoro alisema uwapo wake ni utaratibu wa kawaida katika misafara ya viongozi wa serikali.

“Huu ni utaratibu wa kawaida katika misafara ya viongozi, tumetoa kama utaratibu wa kawaida….unajua huyu ni kiongozi wa nchi, sasa unataka wakija na wagombea wengine wa upinzani nao tuwapatie magari ya wagonjwa, wao ni akina nani?” alieleza na kuhoji Kandoro ambaye pia aligombea kura za maoni kuwania kuteuliwa na CCM kuwa mgombea ubunge Jimbo la Kalenga na kushindwa.

Akizungumza kwa sharti la kutotaja jina gazetini mmoja wa viongozi ambao walikuwa wakishughulika na kuratibu msafara huo alieleza kuwa gari hilo la wagonjwa ni lile ambalo lilitolewa na serikali ya Ujerumani chini ya ushirikiano wa Jiji la Mwanza na Wurzburg.

“Gari hili liliandaliwa kutokana na maofisa wa usalama kuliomba na hili agizo limetolewa katika mikoa yote ambako atafika, kwani katika kampeni anakuwa amekwenda hadi katika wilaya ambazo haina hospitali na ikitokea dharura akimbizwe haraka hospitali huku akiendelea kupatiwa matibabu” alieleza kiongozi huyo wa chama.

Hata hivyo, alisema gari hilo wao kama chama hawakuambiwa wala kuelekezwa kulilipia kwa vile ofisi ya mkoa ilisema watachukua wao katika hospitali ya Bugando, baada ya kuwasiliana na ofisi ya mganga mkuu wa mkoa.

CHANZO: Mwananchi

USHAURI: Imefika wakati sasa kukomesha uhuni huu wa CCM dhidi ya Watanzania hususan wale wasio wanachama wa chama hicho tawala.Matumizi yoyote ya mali za umma zinazogharamiwa na walipakodi pasipo kujali itikadi za vyama zao ni ubadhirifu wa wazi.Haitowezekana kuwa na uchaguzi huru na wa haki iwapo raslimali za taifa zinatumika kwa manufaa ya chama tawala,tena pasipo ridhaa ya walipakodi.Wito wa blogu hii kwa kila mpenda haki na usawa ni kuuweka wazi uhuni huu kwa dunia ili ifahamike mapema kuwa CCM inatengeneza mazingira ya kuhujumu uchaguzi mkuu ujao.

TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA


2 comments:

  1. Mi naona kutumia ambulance sidhani ni tatizo kwani ni ajili ya usalama tatizo litakuwepo kamakutakuwa na mgombea yeyote wa upinza iwapo ataomba kupatiwa hiyo ambulance kwa ajili ya usalama kama huoa kanyimwa after all JK is still a president mpaka pale mgombea mwingine atakapo tawaswa urais

    ReplyDelete
  2. Inahitaji uchanganuzi wa kina, haina ubishi kwamba kweli yeye bado president! sasa sijui una shughulikiaje suala hili, anahitaji ulinzi na huduma nyingine kama rais vinginevyo si linaweza kutokea lolote!then inakuwaje. Labda mi nadhani ku neutralize hili na wagombea wengine wapewe huduma kwa kiasi fulani i.e huduma ya ambulance na magari mawili matatu kwenye maeneo ya tukio.
    I STAND TO BE CORRECTED

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.