23 Aug 2010

Wakati wa kuelekea kampeni za uchaguzi mkuu wa hapa Uingereza kulijitokeza tetesi za wasiwasi kuhusu afya ya aliyekuwa Waziri Mkuu Gordon Brown.Katika kilichotafsiriwa kama kukata mzizi wa fitina,mtangazaji maarufu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),Andrew Marr,alimuuliza Brown katika mahojiano naye kuhusu tetesi hizo.Katika tetesi hizo ilidaiwa kuwa Brown alikuwa akitumia dawa za kutuliza mara kwa mara.

"Jambo ambalo kila mtu amekuwa akiongelea katika kijiji cha Westminster...Watu wengi katika nchi hii wamekuwa wakitumia dawa walizoelekezwa kununua na daktari (prescription drugs)...Je wewe ni mmoja wao?",aliuliza Marr."Hapana.Nadhani uulizaji swali wa aina hii umekuwa ukiingia sana kwenye ulingo wa siasa za Uingereza",alijibu Brown.Jitihada za mwanahabari huyo kutaka kudadisi zaidi zilizimwa na Brown aliyesema ameshajibu swali hilo.


Nimekumbuka tukio hilo kufuatia kuanguka kwa mara nyingine kwa Rais Jakaya Kikwete na namna vyombo vingi vya habari vilivyokwepa kuripoti tukio hilo kwa uwazi.Hata video iliyomwonyesha Kikwete akianguka iliondolewa mtandaoni kwa haraka,kwa sababu wanazojua waliyoiondoa.Na hata video yenyewe ya tukio hilo ilionyesha "kiduchu" tu kuanguka kwa JK kisha ikaelekezwa kwenye umati wa watu hapo Jangwani.Inaelezwa pia kuwa baadhi ya vituo vya runinga huko nyumbani havikuonyesha tukio hilo katika taarifa zao za habari.

Kichekesho ni kwamba kabla hajakumbwa na dhahma ya kuanguka,JK alijigamba kuwa serikali yake imeboresha uhuru wa habari.Sasa uhuru wa habari ambao tukio la kusikitisha na kuhudhunisha linalomkumba Rais wetu linabanwa ni uhuru kweli au hadithi tu?Na hapa simpingi JK kuwa amejitahidi kudumisha uhuru wa habari bali tatizo langu lipo kwa wanahabari wenyewe.

Je,kulikuwa na maagizo kwamba,kwa mfano,clip ya kuanguka kwa JK iodolewe mtandaoni?Kama jibu ni ndiyo,basi uhuru wa habari anaozungumzia JK una walakini.Lakini kama jibu ni hapana basi wanahabari walioamua kuminya habari hiyo wana maswali ya kuwajibu wasomaji wao na Watanzania kwa ujumla.

Natambua kuwa pamoja na majigambo ya JK uhuru wa habari unaodumishwa zaidi ni ule wa "habari za kawaida" na sio zinazogusa masuala ya watawala.Baadhi yetu ni wahanga wa matumizi hayohayo ya uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza.Ukizungumzia mafisadi walio ndani ya CCM,baadhi ya "wenye nchi" wanakurupuka kudai ni utovu wa nidhamu dhidi ya serikali.Yaani kukemea maovu inakuwa nongwa!?

Tukio la kuanguka kwa JK lilikuwa haki ya kila Mtanzania kufahamishwa na wanahabari.Ikumbukwe kuwa ni Watanzania haohao ndio waliompigia kura kiongozi huyo kuwa Rais wao,na mkutano wake wa Jumamosi ulikuwa na madhumuni ya kuwaomba ridhaa ya kuwaongoza tena.Jakaya Kikwete alikuwa hapo kama mgombea wa CCM,na japo hatuwezi kutenganisha urais wake na ugombea wake huko CCM,ukweli unabaki kuwa katika harakati hizi za kampeni anapaswa kuchukuliwa kama wagombea wengine wa vyama vilivyosimamisha wagombea wao.

Japo mkono mrefu wa dola uko makini zaidi katika udhibiti wa habari "zisizopendeza",yayumkinika kusema kwamba baadhi ya wanahabari na vyombo vya habari hawawezi kukwepa lawama.Nachoshindwa kuelewa kwanini  mara nyingi "habari zisizopendeza machoni mwa watawala" zinaminywa ni kama hali hiyo inasababishwa na uoga tu wa wanahabari au/na vyombo vya habari au ni lile tatizo sugu la kujikomba kwa watawala?

Kama sababu ni uoga,basi hayo ni mapungufu ya wazi kwa mwanahabari au chombo cha habari husika.Hata hivyo,inawezekana uoga huo kuwa ni matokeo ya mfumo wa siasa za chama kimoja ambapo ilikuwa mithili ya kosa la jinai "kumsema vibaya" kiongozi (yaani kusema au kuandika kitu kisichompendeza kiongozi).Tuliaminishwa kuwa viongozi wetu ni kama miungu-watu,hawawezi kukosea,kila wanalofanya ni jema na siku zote wako sahihi.Uoga huu unapaswa kuepukwa kwa vile tupo katika  mfumo mpya wa siasa za uwingi zisizo na nafasi ya "zidumu fikra sahihi za A au B".

Kujikomba ni tatizo sugu si kwa baadhi ya Watanzania tu bali hata baadhi ya Waafrika kwa ujumla.Kwa mbali,kujikomba ni matokeo ya mfumo wa ujima na hatimaye ujamaa ambapo mhusika hujibidiisha "kufanya jambo zuri" hata kama hajaombwa.Kwa bahati mbaya,"jambo hilo zuri" linaweza kuwa lisilo na manufaa kwa jamii.Kwahiyo,mwanahabari aliyebania tukio la kuanguka kwa JK anaweza kuwa alifanya hivyo akiamini kuwa "ni vibaya kumwonyesha Rais akianguka hadharani".Lakini imani hiyo potofu ilimaanisha baadhi ya Watanzania kukoseshwa haki ya kuona kilichomsibu mgombea wa CCM ambaye pia ni Rais wao.

Simnyooshei mtu kidole bali hii ni changamoto tu kwa wanahabari na vyombo vya habari.

1 comment:

  1. Watanzania bado wako utumwani tofauti nikwamba wanatawaliwa na mtu huyo huyo waliomchagua (mtanzania mwenzao). Ukweli ni kwamba viongozi wetu wanapaswa kuwa watumishi na wawakilishi wetu. Sisi ndio tunawapa kazi, bila kura yako na yangu hawana kazi hao. Vyombo vyetu vya habari vinamatatizo ya uoga na hasa ukizingatia wengi wanaoitwa waandishi wa habari wamevamia fani. Hawajui maadili ya uandishi wa habari wao wanafuata wanachoambiwa tu . Wale waliobobea kwenye fani hiyo hawatimizi wajibu wao kwasababu wanazojua wao wenyewe. Lakini hawana uzalendo kabisaa. Wanaoipenda Tanzania sidhani kama wanazidi asilimia 10 kwasasa. Wengi wetu ni ubinafsi tu. Kama kweli unaipenda nchi yako you will do anything kuitoa utumwani kwa wajanja hawa. Je ni wangapi wanaweza kulifanya hili? watanzania wenzangu mchango wako unahitajika kuuondoa huu utawala uliojilimbikizia mali. Unaweza kuchangia pesa, unaweza kumpigia kampeni Dr Slaa nyumba hadi nyumba kuhakikisha anashinda uchaguzi octoba, unaweza kumwambia mwenzio uozo wa serikali ya CCM na kwanini hatuwachagui.Unaweza kutengeneza t-shirt, vipeperushi,beji,scarf etc za Chadema. Fanya uwezalo kwa nafasi yako kuuondoa ufisadi.It is nothing personal it is about doing the right thing for the country. Tusimbebeshe Dr Slaa na wengine wachache mzigo wote wa watanzania itakuwa rahisi wao kukata tamaa. Mimi na wewe tunaweza kuwaunga mkono kwa namna moja au nyingine kuikomboa Tanzania. thanks very much!!!

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube