14 Oct 2010Tunahitaji taasisi ya kijasusi ya uchumi na biashara?

Na Idd Amiri

Julai mosi mwaka huu soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki lilianza rasmi, soko hili linajumuisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Ni soko ambalo moja ya mihimili yake ni kuruhusu bidhaa kuuzwa au kusafirishwa toka nchi moja mwanachama kwenda nyingine pasipo kutozwa kodi.

Wakati huo huo wiki iliyopita Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ilitimiza miaka 30 toka ianzishwe ambayo Tanzania ni Mwanachama. Malengo na Madhumuni ya Jumuiya zote mbili ni kama yanafanana ingawa kuna tofauti za hapa na pale. Wakati Tanzania inajitoa kutoka Umoja wa soko la pamoja la ushuru na forodha kwa nchi za kusini na mashariki mwa Afrika(COMESA) ilikuwa na nia ya kujiimarisha zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) kama alivyotamka wakati huo aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Idd Simba.

Lakini mwanachama mwingine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya bado ni mwanachama wa COMESA na hata Zambia ambayo ni mwanachama wa SADC bado ni mwanachama wa COMESA vile vile. Nchi zote mbili zimeendelea kuwepo katika Jumuiya hizo kwa maslahi ya kiuchumi zaidi. Kwa Tanzania bado hatujapata kuelezwa au kuona faida za moja kwa moja ambazo kama nchi imepata kwa kuwepo katika Jumuiya ya SADC kwa kipindi chote cha Miaka 30 iliyopita ingawa wanasiasa na baadhi ya wachumi wanaendelea kuhudhuria vikao vya Jumuiya hii. SADC ilitokana na nguvu ya kisiasa ya wakati huo ya nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi kusini mwa Afrika.

Lengo la kuleta mada hii katika safu hii ni kujaribu kuona kama wanaohusika na sera katika Serikali ya Tanzania wamekuwa wakifanya utafiti wa kutosha kwa nia ya kujua faida halisi za kuwa katika jumuiya yoyote kabla ya kujiingiza au imekuwa ni kufuata mkumbo. Faidi kubwa ambayo kama nchi inaingia katika jumuiya yoyote siyo siasa na maneno ya kuremba, kinachotizamwa zaidi ni kuendeleza ajira kwa watu wa nchi ile na hivyo kujenga usitawi wa kiuchumi na kijamii mengine huwa ni ziada tu, kwa mfano Afrika ya Kusini kwa kuwa Mwanachama wa SADC imefanikiwa kuuza bidhaa za viwanda kwa kiasi kikubwa sana kwa nchi hizi bila mizengwe na hivyo kujenga, kulinda, kupanua na kuimarisha mfumo wa ajira katika nchi ya Afrika ya Kusini, suala hapa ni uhakika wa kuwepo kwa soko la bidhaa zake ili kuneemesha watu wake na kupunguza vurugu za kijamii ambazo huchochewa na kutokuwepo kwa ajira.

Kumekuwa na mazoea ya kufikiri kuwa kuendelea kwetu kunategemea kujiingiza katika jumuiya hizi kwani wenzetu katika nchi zao wamekuwa na ujanja wa kutoa maelezo mengi kama vile kupitia SADC au EAC kutakuwepo na maendeleo ya Sekta ya nishati, barabara, Afya na mambo chungu mbovu lakini mwishoni mwa siku tunajikuta kama umeme, maji, barabara na vinginevyo tunajitafutia wenyewe kwa sababu kila nchi inataka kupata soko kwa mwenzie na hivyo haiko tayari kusaidia kuondoa matatizo ya umeme kwa mwenzie kwani kwa kufanya hivyo itakuwa inamwendeleza kiviwanda na hatimaye itakosa mahali pa kuuza bidhaa zake. Ni jambo liliowazi kuwa kama viwanda vya Tanzania havifanyi vizuri Afrika ya Kusini itafurahi vile vile Kenya itafanya inafurahi zaidi.

Hapa lipo angalizo dogo tu, Kenya inapanua Bandari yake ya Mombasa kwa sababu bidhaa nyingi ambazo zingepitia Dar Es Salaam kwa sasa zinapitia huko hivyo basi haitaki kumwamsha aliyelala ingawa ni Mwanafrika Msahariki mwenzie!

Nikirejea katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, yapo masuala mengine kama kuruhusu watu wa nchi hizi kusafiri, kuishi katika nchi nyingine na kupata ajira pasipo vikwazo kwa kazi za aina fulani, soko la ajira lililo huru na yapo mambo mengine mengi ambayo sina shaka wananchi katika nchi hizi wanayajua kwani tunaambiwa serikali zote tano zimefanya juhudi kubwa kuwafahamisha watu wake ingawa bado nina mashaka juu ya hili.

Nia yangu katika kuzungumzia suala hili la kuwemo katika Jumuiya hizi za ushirikiano ni kujaribu kuamusha hoja ya kuwa na Economic Intelligence au taasisi ya uchunguzi wa kijasusi wa uchumi na biashara ambayo kuna wakati ilipendekezwa na Mheshimiwa mmoja ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini haikuuungwa mkono na Waheshimiwa wengi na hatimaye ilikufa kifo cha mende.

Najua kuwa zipo taasisi zinazofanya tafiti (Think Tank) mbalimbali katika masuala ya uchumi na biashara hapa nchini lakini bado kunahitajika uamusho wa kujua nia ya wanaoshawishi kuwepo kwa jumuiya hizi, kwa sababu Kenya ambayo ndiyo ilikuwa kinara wa kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya Afrika Mashariki wakati huo ndiyo hiyo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Jumuiya ya sasa inafanikiwa tena kwa kasi ya ajabu na tumekwishaona kuwa yenyewe ndiyo inayofaidi sana na kuwepo kwake!

Taasisi hii ingekuwa inakusanya taarifa mbalimbali kutoka kwa nchi hizi ili kujua baadhi ya mambo ya msingi ambayo kwa kila nchi inayahitaji au ilikuwa inafikiri itapata faida ikiwa itaingia katika soko hili au lile na mengine ambayo labda kwa ujanja inayaweka kando ili kufunika kombe ili mwanaharamu apite na wakati mwafaka ukifika iyaibue. Kazi yake ingekuwa kujua nini msimamo wa kila nchi na kuwasilisha taarifa yake kwa wajumbe wetu ambao wanaingia katika vikao mbalimbali vya majadiliano kwa nia ya kulinda maslahi ya Taifa na siyo kwenda kukusanya posho za vikao na masurufu ya safari.

Wakati haya na mengine yakiendelea kuna habari kuwa kuna majadiliano yanaendelea ili watalii wanaotembelea nchi hizi washukie nchi yoyote na kwenda popote katika nchi hizi bila kufuata taratibu za kimipaka kwa Watalii.

Kenya kwa muda mrefu imekuwa ikitangaza kuwa Mlima Kilimanjaro upo nchini humo na kwa kutumia shirika lake la ndege na mawakala mbalimbali wa utalii imefanikisha hilo na wakazi wa nchi za magharibi wanaotembelea Afrika Mashariki kwa nia ya kufanya utalii wameamini hivyo na wameutumia uwanja wa ndege wa Nairobi kama njia ya kwenda kupanda na kuuona mlima Kilimanjaro. Nenda nchi yoyote barani Ulaya uone maajabu ya matangazo hayo ndipo utaposhindwa kuelewa kama kweli tuna watu katika taasisi zetu zinazoshughulika na utalii kwa nini hawabishi na wao kutoa matangazo yanasema siyo kweli kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya!

Hili likikubaliwa itakuwa faida kubwa kwa Kenya ambayo miaka nenda miaka rudi imedanganya watalii wa nchi zote duniani kuwa mlima Kilimanjaro upo kwake na siyo Tanzania na hivyo imefanikiwa sana kuteka makundi ya watalii kutoka sehemu mbalimbali duniania, kwa kukubaliana na hili Kenya haitakuwa na kazi nyingine ya kuutangaza mlima Kilimanjaro kwa hadaa tena, kazi imekwisha!

Wakati Kenya inaendelea na mikakati yake hiyo kwetu tumelala usingizi fofo na hakuna anayebisha si tunahudhuria vikao ili tulipwe posho kuna ubaya ugani? Wenzetu wa Kenya huwa wanatusoma mapema kuwa tunataka nini na wao wachukue vipi kile wanachokihitaji. Wengi tunaona jinsi Jumuiya hii inavyowanufaishi wao zaidi kuliko sisi.

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na kutoelewana kwa nchi mbili wanachama za Tanzania na Kenya katika suala la kuuza meno ya tembo yaliyopo katika maghala mbalimbali hapa nchini, wakati Tanzania inataka kuuza meno hayo imekuwa ikitafuta kibali kutoka katika shirika lisilo la kiserikali la Kimataifa la CITES ambalo huwa linajishulisha zaidi na kuzuia uvunaji wa wanyama au viumbe walio katika hatari ya kutoweka duniani.

Tanzania na Kenya wote ni wanachama wa Taasisi hii, Tanzania inataka kuuza meno hayo ili fedha zitakazopatikana ziweze kusaidia katika kupambana na vitendo vya ujangili vinavyoendelea katika mbuga na hifadhi zake za kitaifa. Kenya inapinga kwa kudai kuwa kwa kuuza meno hayo kutachochea vitendo vya ujangili katika mbuga zake na inaishauri Tanzania ichome kwani hata yenyewe ilifanya hivyo miaka ya nyuma na hivyo majangili watakosa upenyo wa kuendesha shughuli zao.

Hizi ni nchi mbili ndugu na marafiki ambazo zipo katika jumuiya moja, zinapingana kwa jambo moja ambalo zingekubaliana wala kusengekuwa na aibu ya ujumbe wa Tanzania kwenda kwenye mkutano wa CITES uliofanyika mwezi wa julai huko Doha, Quatar na kuangukia patupu baada ya Kenya kuendesha kampeni ya kuhakikisha kuwa Tanzania haipati kibali kutoka kwa wanachama wengine wa CITES ili iweze kuuza shehena ya meno ya tembo.

Ni kwa kuona mambo haya mawili ndipo nilipoamua kaundika makala haya ili kuwaamusha walio katika serikali wasiendelee kulala na kuamini kuwa wako na jirani na ndugu mwema wakati ukweli wa mambo hauko hivyo. Jirani yetu ni mjanja sana na anajua nyendo zetu.

Nikianza na lile la kwanza la meno ya tembo utaona kuwa Kenya ilishakuwa na msimamo wa kupinga mapema pale tu Tanzania ilipoanza kusambaza habari zake chini kwa chini kuwa inataka kuuza shehena ya meno yake ya tembo. Sababu kubwa ni kuwa Kenya inataka kulinda mbuga zake na kwa hilo hakuna ujomba wa Afrika Mashariki hapa. Swali la kujiuliza ni je, tunao watu ndani ya serikali ambao kazi yao kubwa ni kufanya ujasusi wa kiuchumi na kibiashara wa kujua nani analenga kuzuia maslahi yetu ya kiuchumi na kibishara kabla hatujayaweka wazi?

Jibu la swali hili ni kuwa hatuna watu wa aina hiyo na ndiyo sababu tumefika tulipo kwa sasa na aibu tuliyo nayo. Watu wa kazi hii wapo katika kila nchi duniani hasa ile inayolenga kulinda utaifa wake katika ajira, maliasili, teknolojia, viwanda, sayansi na katika yale mambo yote ambayo kwayo inaamini yana maslahi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Tumekabidhi utaifa wetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC wakati wenzetu wanaendelea kulinda maslahi yao ya kiuchumi na kibiashara kwa nia ya ustawi wa viwanda vyao na Mataifa yao.

Katika majadiliano ambayo yanaendelea kuhusu Soko la pamoja la Afrika Mashariki aliyewahi kuwa Waziri wa Utawala Bora katika Serikali ya Awamu ya tatu ya Benjamini Mkapa, Dk. Hassy Kitine alisema kuwa unapotafuta uhusiano na mtu masikini lazima ujiulize kuwa muda mwingi atataka kusaidiwa na wewe na ni hivyo hivyo Tanzania ilitakiwa kuunda jumuiya ya soko la pamoja na nchi tajiri za kiwango chake za Kongo DRC na Angola na siyo hizi za Afrika Mashariki ambazo kilaslimali zinaitegemea Tanzania.

Maneno ya Dk. Kitine yalinifanya nitafute baadhi ya watu ambao wamewahi kufika na wengine kuishi nchini Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo, maelezo waliyonipa yanakubaliana na DK. Kitine, ni nchi zenye utajiri wa maliasili na kama soko la bidhaa za vyakula huko ni mahali pake. Tatizo ni kuwa zote mbili hazikuwa kuiomba Tanzania kuunda umoja wa aina fulani na hivyo hivyo Watanzania tuliolala hatukuona utajiri wa wenzetu.

Majasusi wa shughuli za biashara na uchumi wanaliona hili ni halali kabisa kwani hata Biblia imeagiza hivyo pale Canaan alipokwenda kutafuta nchi ya asali na maziwa, Ipo mifano mingi lakini kwa uchache nitachukua kwa nchi za Marekani na Ufaransa ambapo Mwandishi wa Habari za Kijasusi na Ulinzi wa Gazeti la Daily Telegraph, nchini Uingereza Michael Smith katika kitabu chake The Spying Game, the secret history of British Espionage, anabainisha kuwa mnamo mwaka 1971 Ufaransa kwa kutumia taasisi yake ya kijasusi SDECE (Service de Documentation Exeterieure et de Contre-Espionage) aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Alexandre de Marenches aliongoza shughuli za kijasusi na kufanikiwa kuujua mapema mpango wa Marekani wa kushusha thamani ya sarafu yake ya dola na kwa kufanya hivyo Wizara ya fedha ya Ufaransa ilitengeneza faidi kubwa katika soko lake la fedha.

Utafutaji wa Habari za siri kuhusu masuala ya kifedha, kiuchumi, maendeleo ya Viwanda na Sayansi na teknolojia katika Ulinzi na usalama yaliendelea kwa Ufaransa dhidi ya Marekani hata pale mwaka 1981 SDECE ilipobadili jina na kuitwa DGSE (DirectionGenerale de la Securite Exterieure) ambapo Mkurugenzi wake Mkuu wakati huo Pierre Marion alifanikiwa kupata taarifa za ushindani wa kibiashara katika mauzo ya ndege kwa India na kuipiku Marekani na Urusi wakati ambapo zote zilikuwa zikiwania biashara hiyo na baadaye kwa maneno yake mwenyewe akasema “Siyo jambo la kawaida kuwa tunafanya shughuli za kijasusi dhidi ya nchi hizi kwani kisiasa na kijeshi ni marafiki lakini katika mashindano ya kiuchumi na kiteknolojia ni washindani wetu.”

Vile vile kwa Ufaransa nayo ilipata pigo pale mwaka 1994 wakati Waziri Mkuu wa wakati huo Edouard Balladur aliposafiri kwenda Jeddah, Saudi Arabia kusaini mkataba wa dola bilioni sita ambapo Ufaransa ingeiuzia Saudia meli za kivita na makombora na pia kubadilisha ndege za abiria za shirika la ndege la nchi hiyo kutoka zile zilizotengenezwa Marekani ili kuipa bishara hiyo Airbus ambayo ni kampuni ya Ulaya ambapo Ufaransa ina hisa.

Mkataba huo haukusaniwa kwani mashirika ya kijasusi ya Marekani yakiongozwa na CIA (Central Intelligence Agency) yalipata habari za kina kuhusu mpango huo na Serikali ya Marekani ikiongozwa na Bill Clinton iliitia shinikizo serikali ya Saudia na Clinton alipimpigia simu Mfalme Fahd na mabadiliko yakafanywa ili Makampuni ya Kimarekani ya Boeing na Mcdonnell Douglas yakafanikiwa kupata mkataba huo na hatimaye kuiuzia Saudia ndege za kiraia na kijeshi.

Si hivyo tu hata katika majadiliano juu ya makubaliano ya kibiashara katika shirika la maendeleo ya bishara la kimataifa la wakati huo yaani GATT Marekani na Ufaransa kila moja ilikuwa ikitafuta siri za mwenzake ili kujua msimamo wa mwenziwe kabla ya kuhudhuria vikao vya Shirika hilo. DGSE iliwahi kuitisha mkutano wa wandishi wa habari na kuwafahamisha kuwa ilikuwa imemkamata jasusi moja kutoka CIA ambaye alikuwa akitoa hongo ya fedha kwa ofisa moja wa Ufaransa aliyekuwa akijua siri na msimamo wa nchi hiyo kuhusu mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea wakati huo.

Kwa wale wanaofuatilia habari za mataifa mbalimbali watakuwa wanajua kuwa Japan ina taasisi yake ya ujasusi wa kiuchumi na kibiashara(JETRO) toka mwaka 1958 ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Bishara ni kwa kupitia taasisi hii Japan imefanikiwa sana kuhodhi masoko ya vifaa vya electoniki na magari hadi katika masoko yenye masharti magumu na vikwazo ya Ulaya na Marekani.

Hivyo basi hata Tanzania kwa kuangalia mifano hiyo ni dhahiri kuwa ujumbe wa Tanzania uliokuwa umeongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Shamsa Mwangunga na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dr. Ladislaus Komba, ulitakiwa kujua mapema ni nchi ngapi na zipi zilikuwa na msimamo tofauti na Tanzania na ingetumia mikakati gani kuzima misimamo kinzani wakati wa mkutano wenyewe kwa kuendesha kampeni ya nchi kwa nchi ili kuhakikisha kuwa inasonga mbele.

Waliporejea nchini wote wawili waliitisha mkutano na waandishi wa habari, kuelezea kile kilichowasibu na wakaahidi kuwa wataendelea na mapambano ya kuhakikisha kuwa wanauza shehena hiyo ya meno ya tembo, lakini kama hawatakuwa na mkakati mbadala ya ule walioutumia itakuwa ni vigumu sana kushinda vita hiyo. Bila kufanya hivyo itakuwa mchezo wa kuvaa suti na kusafiri Business Class katika ndege kwa gharama za watanzania bila kuleta tija.


Wapiganaji husema: “Huwezi kwenda kupigana na adui usiyemjua uwezo wake.” Ni kwa kutumia watu ambao wako tayari kulinda maslahi yetu ndipo tutakuwa taifa lenye heshima mbele ya wengine. Watu hawa watakuwa watoa habari tu na watawapa wale wanaohusika katika majjadiliano ili kusoma alama za nyakati kwa upande mwingine.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingene inapasa kutambua kuwa siyo kila utuchekeaye ana mapenzi na sisi kwani upo msemo wa kiswahili usemao hapendwi mtu ni pochi tu na pochi letu sisi ni raslimali zetu ambazo kwa wingi wake yapo mataifa mengi yanatolea macho. Watu wetu wengekaa katika ofisi za ubalozi hadi kwenye migodi ya dhahabu, almasi, tanzanite, rubi na kote kule ambako kizazi hiki na kijacho kinategemea kuvuna maliasili hizo. Kuwa na Economic Intelligence siyo kwa majirani tu hata katika mataifa yaliyoendelea ambapo watakuwepo wachambuzi wa mambo kujua nia ya dola fulani kwetu ni ipi?

Niandikie [email protected] 

ASANTE SANA MDAU IDD KWA DARASA HILI MARIDHAWA.WADAU WENGINE WENYE MADA KAMA HII AU NYINGINEZO MNAKARIBISHWA KWA MIKONO MIWILI


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.