Showing posts with label IDD AMIRI. Show all posts
Showing posts with label IDD AMIRI. Show all posts

14 Oct 2010


Profesa Nkunya na vyuo vya kutengeneza shahada.

Na Idd Amiri



Wiki iliyopita Profesa Mayunga Nkunya, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, aliongea na waandishi wa habari na baadaye akatoa tangazo juu ya kuwepo kwa vyuo vikuu visivyotambulika hapa nchini na huko nchi za nje vinavyotoa shahada za udaktari wa heshima wa falsafa kwa watu mbalimbali mashuhuri hapa nchini na kwingineko barani Afrika hususa ni kwa Wabunge, Mawaziri na hata Marais. Marais wetu wawili nao ni madaktari wa falsafa.

Katika tangazo lake kuhusu kuzuka kwa vyuo hivyo amebainisha kuwa kumekuwa na mbadilishano wa fedha kati ya wahusika na vyuo hivyo na hili ni kwa nia ya kujipa hadhi wasiyositahili waheshimiwa hao kwa wanajamii.

Profesa Nkunya amekuja na kauli hii baada ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi profesa Jumanne Maghembe, kutoa ufafanuzi juu ya kutolewa kwa shahada hizo kutoka katika vyuo hivyo ambavyo kwake yeye hakuviita visivyotambulika au vyuo vya kutengeneza shahada kama profesa Nkunya alivyoviita.

Profesa Maghembe alitoa ufafanuzi katika mkutano wa mwisho wa Bunge La Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Dodoma, Waheshimiwa aliowataja Profesa Maghembe ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Kwera, Mheshimiwa Chrisant Mzindakaya na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Abeid Karume.

Katika kikao hicho cha Bunge wakati wa kuchangia mijadala mbalimbali Mheshimiwa Juma Ngasongwa, ambaye kwa kiwango cha elimu au usomi ni daktari wa falsafa alilalamika kuwa pamoja na kuwa na shahada nzuri ya udaktari wa falsafa katika uchumi lakini haiitwi Member of the learned brothers!. Mara nyingi wanasheria huiitwa hivyo ingawa binafsi sijui inakuwaje msomi mwenye shahada ya kwanza awe katika kundi hilo na madaktari wa falsafa katika fani nyingine wasiwe katika kundi hilo, Kwa leo hilo siyo sehemu ya mjadala wangu.

Profesa Maghembe alisema kuwa Mheshimiwa Mzindakaya amepewa shahada ya heshima ya udakatari wa falsafa kwa kutambua mchango wake katika upenzi, ujenzi na maendeleo ya viwanda na Mheshimiwa Karume alitunukiwa shahada yake kwa kufanikiwa kutokomeza malaria katika visiwa vya Zanzibar.

Lakini hii si mara ya kwanza kuhojiwa kwa shahada za heshima za watu mbalimbali, katika vikao vya Bunge miaka ya nyuma huko Mheshimiwa Dr. Hansy Kitine aliwahi kuongelea suala hilo na aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia Dr. Pius Sabasi Ng’wandu alimjibu kuwa haoni kama kuna ubaya wowote kwani hakuna madhara kwa mtu kupewa hadhi hiyo. Lakini hoja ya Kitine ilikuwa zaidi kwa maprofesa wa mitishamba. 

Kwa wale waliowahi kutembelea makumbusho ya Bagamoyo watakuwa wanamfahamu Profesa Kejeli, huyu jamaa ni mahiri kwa kuelezea historia ya mji wa Bagamoyo tena kwa kasi ya ajabu, Kumbukumbu za watu, miaka na mahali alizonazo profesa Kejeli kwa kweli zinakuacha mdomo wazi anaposimulia. Nilibahatika kumwuliza ilikuwaje akaitwa profesa alinijibu kuwa alipewa hadhi hiyo na Marehemu Meshack Maganga aliyekuwa Mkuu wa Chuo Cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ).

Miaka mitatu iliyopita nilikuwa nikifuatilia mwendelezo wa kipindi cha kweli (Reality show) cha kila mwaka cha runinga ya shirika la utangazaji la uingereza (BBC) katika BBC Two, kinachoitwa You’re Fired ambacho huongozwa na Milionea wa Kiingereza Sir Alan Sugar. Lengo la kipindi hiki huwa ni kutafuta mtu mmoja ambaye bila kuangalia kiwango cha elimu yake anaweza kuwa na mbinu za kijasiliamali na kimenejimenti kwa kuwaongoza wenzie katika kutafuta faidi iwe katika hoteli, kiwanda na mahali popote ambapo uzalishaji kwa lengo la kutafuta faidi unafanyika. Mshindi wa mchakato huo huajiriwa katika moja ya makampuni ya milionea huyo na kwa mwaka analipwa paundi za kiingereza laki moja (100,000). 

Ili kufanikisha mkakati wake huo Sir Alan Sugar, aliwagawa washiriki wake wapatao 20 katika makundi mawili ya kila upande watu kumi, akawagawia mtaji wa kuendesha biashara ya kufua nguo ambapo makundi yote mawili yalitakiwa kupita kwa wateja majumbani na kujitangaza na hatimaye wateja walikubali kuwapa nguo zao zikafuliwe na kunyooshwa kwa gharama walizokubaliana.

Hatimaye ikafika wakati wa kuangalia nani kapata nini na kapoteza nini, makundi yote mawili yalipata faidi lakini moja lilipata faidi ndogo na hapo Sir Alan akawa mbogo akitaka kujua nani kasababisha kutopatikana kwa faidi kubwa na kwa bahati mbaya nguo za mmoja wa wateja zilikwenda kwa mteja ambaye siye mwenye nazo!

Katika kutafuta uzembe ulikuwa wapi alijitokeza mshiriki mmoja katika kundi hilo akapaza sauti kuwa tatizo katika kundi lao kuna washiriki ambao siyo wasomi, ndipo Sir Alan akamwuliza kuwa ana elimu ya kiwango gani? mshiriki yule akajibu kuwa ana shahada ya uzamili katika uchumi. Swali la mwisho na ambalo lilimwondoa katika ushiriki ule lilikuwa ametumiaje elimu yake katika kuleta faida, mshiriki akawa kimya na Sir Alan hakuwa na la ziada ila kumfukuza huku akisema wale wafanyakazi wake ambao hawana shahada lakini wanamwingizia faida wana tatizo gani.

Mshiriki aliyekuja kushinda na hatimaye kuajiriwa kwa mshahara wa paundi 100,000 alikuwa ni yule aliyekaa chuo kikuu kwa miezi mitatu na kuacha kwa sababu alionyesha kuwa ana mbinu za kijasiliamali na kimenejimenti za kuweza kuzalisha faida katika kampuni.

Sasa nirejee kwenye usomi na shahada za bandia na za kweli, hapa najiuliza maswali mengi lakini kwa uchache ni inawezekana vipi kwa msomi ambaye ni profesa kuteuliwa kuwa waziri wa mawasiliano na uchukuzi na baada ya muda Fulani anapoondoka wizara ile mashirika karibu yote katika ile wizara yanakuwa taabani? Msomi mwingine ambaye ni profesa anaanzisha taasisi isiyokuwa ya kiserikali huku fedha zote za kuendeshea taasisi hiyo zikitoka nje kwa wahisani wake, anajenga jumba lake kubwa la kifahari, ananunua gari la kifahari pia na anasomesha watoto wake ughaibuni na katika kufanikisha mradi anaendesha utafiti ambao mara zote ni kuangalia kama mwanasiasa fulani anapendwa na watanzania au la? Fikra zangu duni ni kuwa baada ya kuwa mtu yeyote amesoma na kuwa na hadhi ya profesa na chuo kumkubali nadhani anatakiwa kuonyesha kwa vitendo thamani ya elimu aliyopata.

Kwahiyo unaweza kujiuliza kutokana na yale niliyoeleza hapo juu kuwa hii ndiyo gharama ya kodi za watanzania walizotumia kumlipia yeye wakati akisoma inasaidia nini kujua kuwa fulani anapendwa au hapendwi? Unakuwa na msomi mwingine ambaye ni daktari wa falsafa na waziri vilevile lakini hajui hata kutoka Mwenge jijini Dar es Salaam hadi jimboni kwake ni kilomita ngapi na huyu ndiye anayetakiwa kusimamia ujenzi wa barabara? Jambo linalonipa taabu ni kama kwa utashi wangu niwape heshima ya usomi waheshimiwa hawa? Upo mfano mmoja hivi inakuwaje kwa msomi kung’ang’ania kufanya kazi katika chuo kimoja tu wakati anaweza kusaidia mahala pengine hata kama siyo kwa kufundisha, kwanini msomi kama huyu asifanye kazi nyingine yoyote zaidi ya kufundisha na kufanya utafiti ambao matumizi yake ni yamkini?

Kwa bahati mbaya nimekuwa nikijikuta nawasilikiza au kuwatazama wasomi mbalimbali wakiongea katika runinga na redio na wengi ni wakosoaji wazuri, kuna wakati Mzee Ali Hassani Mwinyi alipokuwa rais wa Tanzania alikuwa na mshauri wa uchumi ambaye ni profesa na ni huyo huyo leo hii anasema kuwa serikali inategemea sana misaada katika bajeti yake na ijaribu kuja na mbinu za kujitegemea, lakini wote tunajua jinsi nchi hii ilivyopoteza viwanda na raslimali chungu mbovu wakati msomi huyu alipokuwa msahuri wa mzee ruksa.

Wakati Rais Jakaya Kikwete akitoa hutoba ya kulivunja Bunge, Mjini Dodoma kulikuwa na wasomi wawili ambao walialikwa na Runinga ya Taifa(TBC) ili watoe tathmini yao kutokana na hutoba ile na kwa kuwa ilikuwa na takwimu nyingi hapo ulikuwa ni uwanja wao. Kilichonishangaza ni moja wa wasomi wale alipokuwa akiunga mkono takwimu zile kwa kusema kuwa zinatokana na utafiti uliofanyika wakati hali halisi haiendani kabisa na yaliyokuwa yakitoka kwenye takwimu zile, hii ilinipa simanzi sana.

Kwa mfano, katika hotuba ile kulitajwa kuwa umasikini umeshuka kwa kiwango cha kuridhisha na kwa bahati mbaya wiki ile ile katika kituo kingine cha televisheni ilionyesha mama moja akiwa katika kijiji kimoja wilayani Kyela akiomba msaada wa kujengewa nyumba na wazungu waliokuwa katika ziara ya kujifunza maisha ya watu wa nchi hii. Mama yule ana watoto saba ambao bado hawajawa na uwezo wa kujitegemea, yeye mwenyewe ni mgonjwa, nyumba anayoishi ipo mbioni kudondoka, katika hali ile takwimu za Mheshimiwa zilizopata baraka za wasomi zilikuwa sahihi kweli?

Nirudi kwa kuuliza swali usomi wake umeisaidiaje nchi hii? Kuwa daktari wa falsafa, profesa kama hakuna ulichosaidia kupambana na matatizo ya watanzania na kwa bahati mbaya ukafanya mambo kama siyo msomi bado ni hasara kwa taifa.

Kwa wale tunaofuatilia mienendo ya hawa wote wawili naamini hatuna shaka kwa sababu zilizotolewa na vyuo hivyo kuamua kuwaenzi kwa kwatunuku shahada za falsafa za udaktari wa heshima kwani michango yao tumeiona na hata profesa Maghembe alikubaliana na vyuo hivyo kutoa shahada hizo.

Hivi Karume kuitwa daktari kwa kuwaondolea wazanzibari gonjwa linalotafuna maisha ya watu chungu mbovu katika nchi za kitropiki kuna ubaya? Wasomi wanaotambulika kwa kupitia vyuo vinavyotambulika mbona wameshindwa kuwaangamiza wale mbu pale Hospitali ya taifa Muhimbili? Mzindakaya kuanzia kwenye uanzishaji wa SIDO hadi kuwa na kiwanda chake mwenyewe hilo ni tatizo? Wasomi wangapi hatujui wameifanyia nini nchi hii?

Ninao mfano moja wa kijana aliyemaliza masomo yake kutoka chuo cha maji pale ubungo, jijini Dar Esa salaam, miaka ya mwanzo ya themanini aliporudi kijijini kwake mkoani Iringa alijaribu kufanya matembezi katika moja ya milima inayozunguka kijiji chake, kwa bahati nzuri alifanikiwa kuona chemchem ya maji katika moja ya milima ile, wazo likamjia akawasilisha serikalini na wanakijiji wakafanya harambee ya kuchimba mtaro wa kupitishia mabomba ya maji na yeye akatumia utaalamu wake kukinga maji yale ili yatiririke kuelekea vijiji vya karibu.

Kwa bahati nzuri serikali ilimsikia na kwa juhudi na maarifa aliyokuwa nayo mradi ule unatoa maji kwa vijiji zaidi ya 10 leo hii na hakuna hata siku moja maji yamekatika na wanachi wanaulinda mlima ule kama almasi yao.  Baada ya mradi ule kufanikiwa aliendelea kufanya kazi katika miradi ya maji sehemu mbalimbali nchini na kila alipokwenda na kuondoka wananchi walimlilia, je huyu akipewa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa kuna tatizo?

Kuna wakati niliwahi kuuliza swali kwa raia moja wa nchi za magharibi kuwa kwanini Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo Gordon Brown, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, Condereza Rice hawapendi kuitwa kwa majina ya kisomi ya Daktari na profesa wakati wanasitahili hivyo kwa elimu zao, alinijibu kuwa siyo vizuri kuitwa msomi na kesho yake ukafanya mambo kama siyo mtu aliyekwenda shule.

Lakini hoja ya Profesa Nkunya ni kama hapendezwi na tunu wanazopata watu mbalimbali kutoka katika vyuo visivyotambulika na kwa hili yuko sahihi, angependa shahada hizi zitolewe zaidi kwa wale wanaosomea kwa kukaa vyuoni na kusimamiwa na wahadhiri na kwa vile huwezi kupata shahada ya udaktari wa falsafa bila kufanya utafiti kwa vigezo vilivyowekwa na chuo ni dhahiri ni lazima uhenyeke au utaabike kabla hujavaa joho hilo.

Kwangu mimi ambaye siyo msomi sioni tofauti yoyote kati ya viwanda vya kutengeneza shahada kama profesa Nkunya alivyoviita na vyuo vinavyotambulika. Lazima tukubali kuwa Vyuo vyetu ni mahali pa kwenda kuchukua vyeti ili kupata ajira kwa sababu hilo ndilo sharti kubwa kuwa na elimu ya shahada ya kwanza, ya pili, tatu hadi mwisho na hii yote inategemea mshahara atakaolipwa mtarajiwa kwa elimu yake na majukumu atakayopangiwa na ofisi inayomwajiri.

Hapa ni kama mashindano ya Bongo Star Search kwani aliyeshinda mwaka jana amefanya kazi yoyote ya muziki? Si ni fedha tu ndizo zinazotafutwa kipaji ni jambo la wengine, unaweza kuiga mwanamuzi unayempenda na kumudu vizuri ili watu wakupigie kura upate mahela! Na kwa upande wa shahada ni hivyo hivyo kinatafutwa cheti kwa gharama yoyote iwe kwa kuiba mitihani, kuhonga mwalimu kwa fedha na ngono, kukodi mtu akufanyie mtihani, kunakili utafiti wa mtu mwingine na hata kukodi mtu wa kufanya utafiti wenyewe suala ni maisha nani anabisha?

Siyo siri kuwa kupata shahada hakuendani na hadhi au muktadha na mantiki ya shahada hiyo, tujiulize wakati tuna wanasheria wenye shahada lukuki inakuwaje mikataba ya madini inakuwa kama ya akina Mangungo wa Msovelo? Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuwa chafu na wahasibu wasomi ndiyo hao? Waandishi wa habari wanaofanya uandishi wa habari kama maofisa uhusiano wa makampuni na shahada zao? Makocha wa mpira wasioleta kombe hata moja la kimataifa huku wakitaka waitwe super coach? Wahandisi wa barabara zinazoharibika siku ya kwanza ya ufunguzi na shahada zao? Wahandisi wa maji wanaotandaza mabomba ya maji wakati wakijua kuwa hakuna maji yatakayotoka na shahada zao? Fani zote zina matatizo na ni wasomi wa vyuo vyetu tunavyovipenda sana na kuviita vinatambulika. Kutambulika kwa chuo bila ufanisi ni sifuri tu. Kama wasomi wetu wangekuwa wanaonyesha mifano kwa wasiosoma ingekuwa ni halali kuwanyooshea kidole wanaofanya ujanja wa kielimu. Msomi hawezi kutuonyesha jinsi alivyoweza kutumia elimu yake kuwa na shamba lenye mazao na mifugo iliyonona kila siku anafanya utafiti ili kiwe nini?

Kwa hapa nirudi miaka ya nyuma kwa upande wa Mahakama, kulikuwa na Mawakili ambao watu wengi walipenda kwenda kuwaona wakitoa hoja zao mahakamani kwa mfano, akina Murtaza Lakha, Ismail Mukhadam, Francis Uzanda na baadaye wakaja akina Abasi Mselem, Dr. Masumbuko Lamwai na Michael Wambali.

Wakati huo mashahidi walikuwa na wakati mgumu sana kwa waheshimiwa hawa kwa hoja na maswali waliyokuwa wakiwatupia wakati wakitoa ushahidi wao mahakamani nilitegemea leo tungekuwa na wanasheria wakali zaidi ya hawa lakini hilo halipo na bado tuendelea kuzalisha kundi la werevu ambao ni members of the learned brothers kila mwaka katika vyuo mbalimbali hapa ndani na nje ya nchi kwani sivinatambulika kwenye mafaili yetu!

Kwa waandishi wa habari ambao kwa kweli kwa wakati huo kulikuwa hakuna hata chuo kimoja ambacho kilikuwa kikitoa shahada za uandishi wa habari watawakumbuka akina Stanley Katabalo na John Rutayisingwa, hawa wote ni marehemu kwa sasa kwa jinsi walivyoweza kuandika habari za uchunguzi wa kikachero na kuwafanya wasomaji wa magazeti kufuatilia habari zao kila magazeti yalipokuwa yakitoka, naye Mnenge Suluja alivyokuwa akiandika habari za mahakamani na kumfanya msomaji ahisi kama alikuwepo mahakamani siku ya shauri. Leo tunao wenye shahada si ndiyo! Habari gani ambayo wameandika ikionyesha kuwa inaendana na usomi wao?

Nimeanzisha mjadala huu ili wachangiaji wengine wanisaidie kupata picha halisi ya viwanda vya kutengeneza shahada na vyuo vinavyotambulika kwani mimi siyo msomi na sina nia mbaya ya kuleta utetezi wa shahada za heshima tatizo langu ni ujinga na uelewa mdogo nilio nao, bado sielewi tofauti iko wapi na nini mchango wa wale tunaowaita wasomi waliobobea katika maendeleo ya nchi hii?


Waweza kunisaidia kwa hili kwa kuniandikia barua pepe kwa anwani hii [email protected]

ASANTE SANA MDAU IDD KWA MAKALA HII MWANANA.WADAU WENGINE PIA MNAKARIBISHWA KUTUMA MAKALA ZENU AU CHOCHOTE KILE CHA MANUFAA KWA JAMII.




Tunahitaji taasisi ya kijasusi ya uchumi na biashara?

Na Idd Amiri

Julai mosi mwaka huu soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki lilianza rasmi, soko hili linajumuisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Ni soko ambalo moja ya mihimili yake ni kuruhusu bidhaa kuuzwa au kusafirishwa toka nchi moja mwanachama kwenda nyingine pasipo kutozwa kodi.

Wakati huo huo wiki iliyopita Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ilitimiza miaka 30 toka ianzishwe ambayo Tanzania ni Mwanachama. Malengo na Madhumuni ya Jumuiya zote mbili ni kama yanafanana ingawa kuna tofauti za hapa na pale. Wakati Tanzania inajitoa kutoka Umoja wa soko la pamoja la ushuru na forodha kwa nchi za kusini na mashariki mwa Afrika(COMESA) ilikuwa na nia ya kujiimarisha zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) kama alivyotamka wakati huo aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Idd Simba.

Lakini mwanachama mwingine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya bado ni mwanachama wa COMESA na hata Zambia ambayo ni mwanachama wa SADC bado ni mwanachama wa COMESA vile vile. Nchi zote mbili zimeendelea kuwepo katika Jumuiya hizo kwa maslahi ya kiuchumi zaidi. Kwa Tanzania bado hatujapata kuelezwa au kuona faida za moja kwa moja ambazo kama nchi imepata kwa kuwepo katika Jumuiya ya SADC kwa kipindi chote cha Miaka 30 iliyopita ingawa wanasiasa na baadhi ya wachumi wanaendelea kuhudhuria vikao vya Jumuiya hii. SADC ilitokana na nguvu ya kisiasa ya wakati huo ya nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi kusini mwa Afrika.

Lengo la kuleta mada hii katika safu hii ni kujaribu kuona kama wanaohusika na sera katika Serikali ya Tanzania wamekuwa wakifanya utafiti wa kutosha kwa nia ya kujua faida halisi za kuwa katika jumuiya yoyote kabla ya kujiingiza au imekuwa ni kufuata mkumbo. Faidi kubwa ambayo kama nchi inaingia katika jumuiya yoyote siyo siasa na maneno ya kuremba, kinachotizamwa zaidi ni kuendeleza ajira kwa watu wa nchi ile na hivyo kujenga usitawi wa kiuchumi na kijamii mengine huwa ni ziada tu, kwa mfano Afrika ya Kusini kwa kuwa Mwanachama wa SADC imefanikiwa kuuza bidhaa za viwanda kwa kiasi kikubwa sana kwa nchi hizi bila mizengwe na hivyo kujenga, kulinda, kupanua na kuimarisha mfumo wa ajira katika nchi ya Afrika ya Kusini, suala hapa ni uhakika wa kuwepo kwa soko la bidhaa zake ili kuneemesha watu wake na kupunguza vurugu za kijamii ambazo huchochewa na kutokuwepo kwa ajira.

Kumekuwa na mazoea ya kufikiri kuwa kuendelea kwetu kunategemea kujiingiza katika jumuiya hizi kwani wenzetu katika nchi zao wamekuwa na ujanja wa kutoa maelezo mengi kama vile kupitia SADC au EAC kutakuwepo na maendeleo ya Sekta ya nishati, barabara, Afya na mambo chungu mbovu lakini mwishoni mwa siku tunajikuta kama umeme, maji, barabara na vinginevyo tunajitafutia wenyewe kwa sababu kila nchi inataka kupata soko kwa mwenzie na hivyo haiko tayari kusaidia kuondoa matatizo ya umeme kwa mwenzie kwani kwa kufanya hivyo itakuwa inamwendeleza kiviwanda na hatimaye itakosa mahali pa kuuza bidhaa zake. Ni jambo liliowazi kuwa kama viwanda vya Tanzania havifanyi vizuri Afrika ya Kusini itafurahi vile vile Kenya itafanya inafurahi zaidi.

Hapa lipo angalizo dogo tu, Kenya inapanua Bandari yake ya Mombasa kwa sababu bidhaa nyingi ambazo zingepitia Dar Es Salaam kwa sasa zinapitia huko hivyo basi haitaki kumwamsha aliyelala ingawa ni Mwanafrika Msahariki mwenzie!

Nikirejea katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, yapo masuala mengine kama kuruhusu watu wa nchi hizi kusafiri, kuishi katika nchi nyingine na kupata ajira pasipo vikwazo kwa kazi za aina fulani, soko la ajira lililo huru na yapo mambo mengine mengi ambayo sina shaka wananchi katika nchi hizi wanayajua kwani tunaambiwa serikali zote tano zimefanya juhudi kubwa kuwafahamisha watu wake ingawa bado nina mashaka juu ya hili.

Nia yangu katika kuzungumzia suala hili la kuwemo katika Jumuiya hizi za ushirikiano ni kujaribu kuamusha hoja ya kuwa na Economic Intelligence au taasisi ya uchunguzi wa kijasusi wa uchumi na biashara ambayo kuna wakati ilipendekezwa na Mheshimiwa mmoja ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini haikuuungwa mkono na Waheshimiwa wengi na hatimaye ilikufa kifo cha mende.

Najua kuwa zipo taasisi zinazofanya tafiti (Think Tank) mbalimbali katika masuala ya uchumi na biashara hapa nchini lakini bado kunahitajika uamusho wa kujua nia ya wanaoshawishi kuwepo kwa jumuiya hizi, kwa sababu Kenya ambayo ndiyo ilikuwa kinara wa kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya Afrika Mashariki wakati huo ndiyo hiyo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Jumuiya ya sasa inafanikiwa tena kwa kasi ya ajabu na tumekwishaona kuwa yenyewe ndiyo inayofaidi sana na kuwepo kwake!

Taasisi hii ingekuwa inakusanya taarifa mbalimbali kutoka kwa nchi hizi ili kujua baadhi ya mambo ya msingi ambayo kwa kila nchi inayahitaji au ilikuwa inafikiri itapata faida ikiwa itaingia katika soko hili au lile na mengine ambayo labda kwa ujanja inayaweka kando ili kufunika kombe ili mwanaharamu apite na wakati mwafaka ukifika iyaibue. Kazi yake ingekuwa kujua nini msimamo wa kila nchi na kuwasilisha taarifa yake kwa wajumbe wetu ambao wanaingia katika vikao mbalimbali vya majadiliano kwa nia ya kulinda maslahi ya Taifa na siyo kwenda kukusanya posho za vikao na masurufu ya safari.

Wakati haya na mengine yakiendelea kuna habari kuwa kuna majadiliano yanaendelea ili watalii wanaotembelea nchi hizi washukie nchi yoyote na kwenda popote katika nchi hizi bila kufuata taratibu za kimipaka kwa Watalii.

Kenya kwa muda mrefu imekuwa ikitangaza kuwa Mlima Kilimanjaro upo nchini humo na kwa kutumia shirika lake la ndege na mawakala mbalimbali wa utalii imefanikisha hilo na wakazi wa nchi za magharibi wanaotembelea Afrika Mashariki kwa nia ya kufanya utalii wameamini hivyo na wameutumia uwanja wa ndege wa Nairobi kama njia ya kwenda kupanda na kuuona mlima Kilimanjaro. Nenda nchi yoyote barani Ulaya uone maajabu ya matangazo hayo ndipo utaposhindwa kuelewa kama kweli tuna watu katika taasisi zetu zinazoshughulika na utalii kwa nini hawabishi na wao kutoa matangazo yanasema siyo kweli kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya!

Hili likikubaliwa itakuwa faida kubwa kwa Kenya ambayo miaka nenda miaka rudi imedanganya watalii wa nchi zote duniani kuwa mlima Kilimanjaro upo kwake na siyo Tanzania na hivyo imefanikiwa sana kuteka makundi ya watalii kutoka sehemu mbalimbali duniania, kwa kukubaliana na hili Kenya haitakuwa na kazi nyingine ya kuutangaza mlima Kilimanjaro kwa hadaa tena, kazi imekwisha!

Wakati Kenya inaendelea na mikakati yake hiyo kwetu tumelala usingizi fofo na hakuna anayebisha si tunahudhuria vikao ili tulipwe posho kuna ubaya ugani? Wenzetu wa Kenya huwa wanatusoma mapema kuwa tunataka nini na wao wachukue vipi kile wanachokihitaji. Wengi tunaona jinsi Jumuiya hii inavyowanufaishi wao zaidi kuliko sisi.

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na kutoelewana kwa nchi mbili wanachama za Tanzania na Kenya katika suala la kuuza meno ya tembo yaliyopo katika maghala mbalimbali hapa nchini, wakati Tanzania inataka kuuza meno hayo imekuwa ikitafuta kibali kutoka katika shirika lisilo la kiserikali la Kimataifa la CITES ambalo huwa linajishulisha zaidi na kuzuia uvunaji wa wanyama au viumbe walio katika hatari ya kutoweka duniani.

Tanzania na Kenya wote ni wanachama wa Taasisi hii, Tanzania inataka kuuza meno hayo ili fedha zitakazopatikana ziweze kusaidia katika kupambana na vitendo vya ujangili vinavyoendelea katika mbuga na hifadhi zake za kitaifa. Kenya inapinga kwa kudai kuwa kwa kuuza meno hayo kutachochea vitendo vya ujangili katika mbuga zake na inaishauri Tanzania ichome kwani hata yenyewe ilifanya hivyo miaka ya nyuma na hivyo majangili watakosa upenyo wa kuendesha shughuli zao.

Hizi ni nchi mbili ndugu na marafiki ambazo zipo katika jumuiya moja, zinapingana kwa jambo moja ambalo zingekubaliana wala kusengekuwa na aibu ya ujumbe wa Tanzania kwenda kwenye mkutano wa CITES uliofanyika mwezi wa julai huko Doha, Quatar na kuangukia patupu baada ya Kenya kuendesha kampeni ya kuhakikisha kuwa Tanzania haipati kibali kutoka kwa wanachama wengine wa CITES ili iweze kuuza shehena ya meno ya tembo.

Ni kwa kuona mambo haya mawili ndipo nilipoamua kaundika makala haya ili kuwaamusha walio katika serikali wasiendelee kulala na kuamini kuwa wako na jirani na ndugu mwema wakati ukweli wa mambo hauko hivyo. Jirani yetu ni mjanja sana na anajua nyendo zetu.

Nikianza na lile la kwanza la meno ya tembo utaona kuwa Kenya ilishakuwa na msimamo wa kupinga mapema pale tu Tanzania ilipoanza kusambaza habari zake chini kwa chini kuwa inataka kuuza shehena ya meno yake ya tembo. Sababu kubwa ni kuwa Kenya inataka kulinda mbuga zake na kwa hilo hakuna ujomba wa Afrika Mashariki hapa. Swali la kujiuliza ni je, tunao watu ndani ya serikali ambao kazi yao kubwa ni kufanya ujasusi wa kiuchumi na kibiashara wa kujua nani analenga kuzuia maslahi yetu ya kiuchumi na kibishara kabla hatujayaweka wazi?

Jibu la swali hili ni kuwa hatuna watu wa aina hiyo na ndiyo sababu tumefika tulipo kwa sasa na aibu tuliyo nayo. Watu wa kazi hii wapo katika kila nchi duniani hasa ile inayolenga kulinda utaifa wake katika ajira, maliasili, teknolojia, viwanda, sayansi na katika yale mambo yote ambayo kwayo inaamini yana maslahi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Tumekabidhi utaifa wetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC wakati wenzetu wanaendelea kulinda maslahi yao ya kiuchumi na kibiashara kwa nia ya ustawi wa viwanda vyao na Mataifa yao.

Katika majadiliano ambayo yanaendelea kuhusu Soko la pamoja la Afrika Mashariki aliyewahi kuwa Waziri wa Utawala Bora katika Serikali ya Awamu ya tatu ya Benjamini Mkapa, Dk. Hassy Kitine alisema kuwa unapotafuta uhusiano na mtu masikini lazima ujiulize kuwa muda mwingi atataka kusaidiwa na wewe na ni hivyo hivyo Tanzania ilitakiwa kuunda jumuiya ya soko la pamoja na nchi tajiri za kiwango chake za Kongo DRC na Angola na siyo hizi za Afrika Mashariki ambazo kilaslimali zinaitegemea Tanzania.

Maneno ya Dk. Kitine yalinifanya nitafute baadhi ya watu ambao wamewahi kufika na wengine kuishi nchini Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo, maelezo waliyonipa yanakubaliana na DK. Kitine, ni nchi zenye utajiri wa maliasili na kama soko la bidhaa za vyakula huko ni mahali pake. Tatizo ni kuwa zote mbili hazikuwa kuiomba Tanzania kuunda umoja wa aina fulani na hivyo hivyo Watanzania tuliolala hatukuona utajiri wa wenzetu.

Majasusi wa shughuli za biashara na uchumi wanaliona hili ni halali kabisa kwani hata Biblia imeagiza hivyo pale Canaan alipokwenda kutafuta nchi ya asali na maziwa, Ipo mifano mingi lakini kwa uchache nitachukua kwa nchi za Marekani na Ufaransa ambapo Mwandishi wa Habari za Kijasusi na Ulinzi wa Gazeti la Daily Telegraph, nchini Uingereza Michael Smith katika kitabu chake The Spying Game, the secret history of British Espionage, anabainisha kuwa mnamo mwaka 1971 Ufaransa kwa kutumia taasisi yake ya kijasusi SDECE (Service de Documentation Exeterieure et de Contre-Espionage) aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Alexandre de Marenches aliongoza shughuli za kijasusi na kufanikiwa kuujua mapema mpango wa Marekani wa kushusha thamani ya sarafu yake ya dola na kwa kufanya hivyo Wizara ya fedha ya Ufaransa ilitengeneza faidi kubwa katika soko lake la fedha.

Utafutaji wa Habari za siri kuhusu masuala ya kifedha, kiuchumi, maendeleo ya Viwanda na Sayansi na teknolojia katika Ulinzi na usalama yaliendelea kwa Ufaransa dhidi ya Marekani hata pale mwaka 1981 SDECE ilipobadili jina na kuitwa DGSE (DirectionGenerale de la Securite Exterieure) ambapo Mkurugenzi wake Mkuu wakati huo Pierre Marion alifanikiwa kupata taarifa za ushindani wa kibiashara katika mauzo ya ndege kwa India na kuipiku Marekani na Urusi wakati ambapo zote zilikuwa zikiwania biashara hiyo na baadaye kwa maneno yake mwenyewe akasema “Siyo jambo la kawaida kuwa tunafanya shughuli za kijasusi dhidi ya nchi hizi kwani kisiasa na kijeshi ni marafiki lakini katika mashindano ya kiuchumi na kiteknolojia ni washindani wetu.”

Vile vile kwa Ufaransa nayo ilipata pigo pale mwaka 1994 wakati Waziri Mkuu wa wakati huo Edouard Balladur aliposafiri kwenda Jeddah, Saudi Arabia kusaini mkataba wa dola bilioni sita ambapo Ufaransa ingeiuzia Saudia meli za kivita na makombora na pia kubadilisha ndege za abiria za shirika la ndege la nchi hiyo kutoka zile zilizotengenezwa Marekani ili kuipa bishara hiyo Airbus ambayo ni kampuni ya Ulaya ambapo Ufaransa ina hisa.

Mkataba huo haukusaniwa kwani mashirika ya kijasusi ya Marekani yakiongozwa na CIA (Central Intelligence Agency) yalipata habari za kina kuhusu mpango huo na Serikali ya Marekani ikiongozwa na Bill Clinton iliitia shinikizo serikali ya Saudia na Clinton alipimpigia simu Mfalme Fahd na mabadiliko yakafanywa ili Makampuni ya Kimarekani ya Boeing na Mcdonnell Douglas yakafanikiwa kupata mkataba huo na hatimaye kuiuzia Saudia ndege za kiraia na kijeshi.

Si hivyo tu hata katika majadiliano juu ya makubaliano ya kibiashara katika shirika la maendeleo ya bishara la kimataifa la wakati huo yaani GATT Marekani na Ufaransa kila moja ilikuwa ikitafuta siri za mwenzake ili kujua msimamo wa mwenziwe kabla ya kuhudhuria vikao vya Shirika hilo. DGSE iliwahi kuitisha mkutano wa wandishi wa habari na kuwafahamisha kuwa ilikuwa imemkamata jasusi moja kutoka CIA ambaye alikuwa akitoa hongo ya fedha kwa ofisa moja wa Ufaransa aliyekuwa akijua siri na msimamo wa nchi hiyo kuhusu mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea wakati huo.

Kwa wale wanaofuatilia habari za mataifa mbalimbali watakuwa wanajua kuwa Japan ina taasisi yake ya ujasusi wa kiuchumi na kibiashara(JETRO) toka mwaka 1958 ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Bishara ni kwa kupitia taasisi hii Japan imefanikiwa sana kuhodhi masoko ya vifaa vya electoniki na magari hadi katika masoko yenye masharti magumu na vikwazo ya Ulaya na Marekani.

Hivyo basi hata Tanzania kwa kuangalia mifano hiyo ni dhahiri kuwa ujumbe wa Tanzania uliokuwa umeongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Shamsa Mwangunga na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dr. Ladislaus Komba, ulitakiwa kujua mapema ni nchi ngapi na zipi zilikuwa na msimamo tofauti na Tanzania na ingetumia mikakati gani kuzima misimamo kinzani wakati wa mkutano wenyewe kwa kuendesha kampeni ya nchi kwa nchi ili kuhakikisha kuwa inasonga mbele.

Waliporejea nchini wote wawili waliitisha mkutano na waandishi wa habari, kuelezea kile kilichowasibu na wakaahidi kuwa wataendelea na mapambano ya kuhakikisha kuwa wanauza shehena hiyo ya meno ya tembo, lakini kama hawatakuwa na mkakati mbadala ya ule walioutumia itakuwa ni vigumu sana kushinda vita hiyo. Bila kufanya hivyo itakuwa mchezo wa kuvaa suti na kusafiri Business Class katika ndege kwa gharama za watanzania bila kuleta tija.


Wapiganaji husema: “Huwezi kwenda kupigana na adui usiyemjua uwezo wake.” Ni kwa kutumia watu ambao wako tayari kulinda maslahi yetu ndipo tutakuwa taifa lenye heshima mbele ya wengine. Watu hawa watakuwa watoa habari tu na watawapa wale wanaohusika katika majjadiliano ili kusoma alama za nyakati kwa upande mwingine.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingene inapasa kutambua kuwa siyo kila utuchekeaye ana mapenzi na sisi kwani upo msemo wa kiswahili usemao hapendwi mtu ni pochi tu na pochi letu sisi ni raslimali zetu ambazo kwa wingi wake yapo mataifa mengi yanatolea macho. Watu wetu wengekaa katika ofisi za ubalozi hadi kwenye migodi ya dhahabu, almasi, tanzanite, rubi na kote kule ambako kizazi hiki na kijacho kinategemea kuvuna maliasili hizo. Kuwa na Economic Intelligence siyo kwa majirani tu hata katika mataifa yaliyoendelea ambapo watakuwepo wachambuzi wa mambo kujua nia ya dola fulani kwetu ni ipi?

Niandikie [email protected] 

ASANTE SANA MDAU IDD KWA DARASA HILI MARIDHAWA.WADAU WENGINE WENYE MADA KAMA HII AU NYINGINEZO MNAKARIBISHWA KWA MIKONO MIWILI


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.