15 Oct 2010


Mimi si mwanasheria japo nasaka uhitimu wa kiwango cha kati (katika Sheria) kwa njia ya masafa.Kwahiyo nina uelewa wa wastani kuhusu masuala ya jumla-jumla kuhusiana na taaluma ya Sheria.Na ni katika hilo ndipo nafahamu kuhusu CLASS ACTION.Kwa uelewa wangu wa wastani,Class Action ni aina ya kesi ya madai inayofunguliwa na kundi (mara nyingi kundi kubwa) dhidi ya taasisi au kundi flani.

Kwa mfano,kundi la wavuta sigara linaweza kufungua class action dhidi ya kiwanda cha tumbaku au cha sigara kulingana na madai yao dhidi ya wadaiwa.Aina hii ya kesi ni maarufu zaidi huko Marekani,na sina ufahamu kama imeshawahi kutokea huko nyumbani.

Naamini tuna Watanzania wazalendo katika kila fani.Naamini pia tuna Watanzania wazalendo wenye taaluma ya sheria hususan kesi za madai au kwenye sheria za mawasiliano.Lengo la makala hii ni kuuliza kama wazalendo hao hawawezi kutoa fundisho kwa makampuni mbalimbali ya simu huko nyumbani ambayo yayumkinika kuyatuhumu kuwa yanakiuka haki za usiri (privacy) wa wateja wao.

Kuna hayawani flani amekuwa akisambaza SMS za kumchafua mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,Dokta Wilbroad Slaa.Haihitaji uchambuzi wa aina yoyote kufahamu uhuni huo wa SMS usingekuwepo laiti Dokta Slaa asingekuwa tishio.

Na japo CCM wamekanusha kuhusika na uhuni huo lakini kama waliweza kuchafuana wenyewe kwenye mchakachuo wa kura za maoni watashindwaje katika mpambano huu wa kufa na kupona hapo Oktoba 31?Unajua tatizo la CCM ya Jakaya Kikwete ukilinganisha na ile ya Mwalimu,Mwinyi au hata Mkapa,ni ombwe kuuuuubwa la uongozi katika chama hicho.Kama ambavyo Kikwete amemudu kutengeneza ombwe la uongozi wa kitaifa akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano,ndivyo ambavyo ameshindwa kwa kiasi kikubwa kumudu nidhamu ndani ya CCM.Tatizo kubwa linalomkabiri Kikwete ni kujazana kwa viumbe kadhaa waliofadhili kampeni zake za kupata urais mwaka 2005.Hana jeuri ya kuwadhibiti (japo angeweza kufanya hivyo kama angemudu kuweka ushkaji pembeni).

Katika mazingira ya sasa ambapo CCM imekuwa kama povu linaloelea angani likisubiri japo pini litoboke,chizi yoyote yule anaweza kukurupuka na mkakati wa kihuni wa kusambaza SMS dhidi ya Dokta Slaa.Baadhi ya taarifa zinamhusisha mhuni huyo na familia ya fisadi mmoja mwenye wadhifa mkubwa ndani ya CCM (Like Father Like Son).Au inawezekana kabisa kuwa SMS zina baraka zote za CCM na Kikwete mwenyewe.Katika siasa za kichakachuaji lolote linawezekana.

Back to my point kuhusu uwezekano wa Class Action.Makampuni ya simu yanayoruhusu wateja wao kubughudhiwa na SMS hizo hayawezi kukwepa lawama kuhusu uhuni huu.CCM wanakiri kuwa wao wanatuma SMS njema tu.Je nani anawapa namba za kutuma SMS hizo njema?Jibu ni makampuni yetu ya simu.

Sasa,iwe ni SMS njema au za kihuni kama hizo za dhidi ya Dokta Slaa,lililo dhahiri ni kuwa makampuni hayo yanavunja haki za wateja wao kutobughudhiwa.Na hapo ndipo napojaribu kuwahamasisha wanasheria wazalendo kuangalia uwezekano wa Class Action dhidi ya makampuni hayo.

Nilishawahi kuandika kwenye makala zangu kwenye jarida la Raia Mwema kuhusu upole wa Watanzania hata pale wanaponyimwa haki zao za msingi.Kwa mfano,ni Watanzania wangapi ambao nyumba na mali zao zimeshawahi kuungua kutokana na uzembe wa Shirika la Umeme (TANESCO) lakini wahanga hao wameishia kunung'unika tu badala ya kuwashikisha adabu wana-umeme hao?Ni dhahiri kuwa laiti TANESCO wangefikishwa mahakamani kwa kusababisha shoti japo ya pasi ya umeme tu wangekuwa makini kabla ya kukurupuka kuzima umeme kila wanapojiskia.

Au ni Watanzania wangapi wamepoteza wapendwa wao (kama sio wao wenyewe kupoteza viungo vyao) kutokana na ajali zinazochangiwa na mchanyato wa ufisadi wa matrafiki na wamiliki wa vyombo vya usafiri,lakini wahanga hao wameishia kuomba msaada wa Mungu badala ya kudai fidia?Of course,hakuna fidia inayotosheleza kifo cha mtu lakini tunafundishwa kwenye sosholojia kuwa negative sanctions (kwa mfano adhabu kama faini,kifungo,nk) zinaweza kuzuia wakosaji kurejea tena makosa yao.

Pengine hakuna mwanasheria mzalendo anayepita kwenye blogu hii.Lakini pengine unamfahamu mwanasheria wa aina hiyo.Basi ombi langu ni kumfikishia ujumbe huu wa kuangalia uwezekano wa Class Action dhidi ya makampuni ya simu yanayopuuza haki za wateja wao kwa kuruhusu SMS za kihuni.

TUSIPOZIBA UFA TUNAWEZA KUJENGA UKUTA.LEO SMS NI DHIDI YA DOKTA SLAA KWA VILE MAFISADI HAWATAKI AINGIE IKULU.KESHO KUNAWEZA KUWA NA SMS ZA KUHAMASISHA YALEYALE YA WAHUTU DHIDI YA WATUTSI AU WAISLAMU DHIDI YA WAKRISTO.NA HAYO YANAWEZEKANA ZAIDI KATIKA MAZINGIRA HAYA YA OMBWE LISILOELEZEKA (INCONCEIVABLE) KATIKA MEDANI YA UONGOZI WA TAIFA LETU "CHANGA".2 comments:

  1. Usitudanganye Chahali, hizo SMS mnaziandika wenyewe na kuzituma ili kutafuta huruma ya watanzania. Sijaona SMS za kuchafuana kwenye kura za maoni ila naona sasa kwa Dr.Slaa na ukizingatia mwenyekiti wenu Mbowe ni mjanja kuliko ...anaweza kuwa na mbinu chafu kama hizo ili aisingizie CCM. Hatuna sababu ya kumchafua Dr.Slaa kwa kuwa hatuamini kama anaweza kutuongoza kwani uongozi huanzia nyumbani, na kama nyumba imemshinda jee taifa ataliweza?

    ReplyDelete
  2. Laiza wewe ni mlevi ama chizi, jiweke katika kundi mojawapo kati ya hayo mawili....naona unaropokaropoka tuu, kama mlevi tena wa pombe za kienyeji kama vile chimpumu au chizi aliyetoroka wodi ya vichaa hospitali

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube