9 Dec 2010JAMAA mmoja ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Joseph, leo asubuhi alikutwa na kamera yetu akiwa ameanguka katika Barabara ya Forest mjini Morogoro, pembezoni mwa uzio wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Morogoro, akidai kwamba alikuwa ametokea katika hospitali hiyo na kwamba hali yake ilikuwa imezidi kuwa mbaya.

Akizungumza na mtandao huu, Joseph alisema: "Nimetoka humu ndani (hospitali) kutibiwa na baada ya kupewa dawa niliruhusiwa kurudi nyumbani, nilipofika hapa nimezidiwa na njaa pamoja na ukali wa dawa hizo na kujikuta nikiishiwa nguvu na kuanguka.

Kama kuna mtu ana shilingi elfu moja anisaidie nikanunue walau uji," alisema Joseph huku akionekana akitetemeka kwa njaa pamoja na ukali wa dawa hizo.Alipoulizwa anasumbuliwa na ugonjwa gani alidai ni homa ya matumbo (typhoid) iliyoambatana na homa kali.

Mwandishi wetu alimpatia kiasi hicho cha fedha ambapo pia baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo walimuunga mkono mpiga picha wetu kwa kumuongezea kiasi cha fedha na baadaye kumwinua hadi kwenye mgahawa uliopo jirani na Shule ya Sekondari ya Morogoro.

Baada ya kupata hudumu hizo, Joseph alizinduka na kauli yake ya kwanza ilikuwa ni kuushukuru mtandao huu na wananchi wengine kwa kumpatia msaada huo.

Picha na Habari kwa Hisani ya Global PublishersWAKATI HALI IKIWA HIVYO KWA MLALAHOI HUYU,GAZETI LA Mwananchi LILIRIPOTI HABARI IFUATAYO.ISOME KISHA ULINGANISHE NA HABARI HIYO YA KUSIKITISHA HAPO JUU,KISHA TAFAKARI KUHUSU MIAKA 49 YA UHURU WETU

Mashangingi ya mawaziri yazua utata 
Sunday, 28 November 2010 21:05

Sadick Mtulya

WAKATI mawaziri na manaibu wawaziri wakikabidhiwa magari mapya, baada ya kuapishwa Jumamosi iliyopita, serikali imeibuka na kusema sio mapya ni ya zamani.Kauli hiyo inaibua utata kutokana na kuwa baada ya kuapishwa viwanja vya Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, kila waziri alikabidhiwa dereva mpya na gari jipya aina ya Toyota GX V8, badala ya gari aina ya Toyota VX V8 iliyokuwa ikitumiwa na mawaziri waliopita.

Ununuzi wa Toyota GX V8 mpya, unashiria serikali bado haijawa tayari kuunga mkono msimamo wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye amekuwa akisikika akitaka kusitishwa ununuzi wa magari ya kifahari ili kupunguza matumizi ndani ya serikali.

Toyota GX V8 moja huuzwa kati ya Sh210 milioni hadi Sh240 milioni, hukuToyota VX V8 moja inauzwa sio chini ya Sh180 milioni.Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Miundombinu, Omari Chambo, alisema magari hayo sio mapya na kwamba, yaliyotumiwa na mawaziri waliopita.Rais Jakaya Kikwete ameigawanya iliyokuwa Wizara ya Miundombinu na kuwa wizara mbili; Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi.

“Yale magari sio mapya, yalikuwepo. Kwanza uliyaona au unasema tu, hamjayachunguza vizuri jamani, fanyeni uchunguzi,’’ alisema Chambo na kukata simu.
Mawaziri wote na baadhi ya manaibu walikabidhiwa magari hayo (GX V8), huku manaibu wengine wakikabidhiwa VX V8.Sababu ya baadhi ya manaibu mawaziri kukabidhiwa VX V8 badala ya GX V8, ni kutokana na kutokamilishwa kwa taratibu za kutokamilika.

Mmoja wa manaibu mawaziri (jina tunalo), alikabidhiwa VX V8 iliyokuwa ikitumiwa na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifungo na Uvuvi, John Magufuli, ambaye sasa ni Waziri wa Ujenzi.Gazeti moja la kila siku (si Mwananchi) limeeleza kuwa ununuzi wa magari hayo, umegharimu serikali Sh9.3 bilioni na kwamba, takwimu za iliyokuwa Wizara ya Miundombinu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2005/06 magari makubwa ya kifahari yapatayo 6,000 yalikuwa yamenunuliwa na serikali kwa gharama inayokadiriwa kufikia Sh160 bilioni.

Miongoni mwa magari hayo ni Toyota Land Cruiser (VX/ GX V8, Prado) yapatayo 1,655, Nissan Patrol na Land Cruiser 885, Mitsubishi Pajero 400 na mengineyo.

Tangu kipindi cha serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kumekuwepo na mjadala kuhusu matumizi makubwa ya serikali hasa katika ununuzi wa magari ya kifahari kutokana na kuendeshwa kwa gharama kubwa.Wadau wengi wanataka viongozi watumie magari ya kawaida kama ilivyo kwa nchi ya Kenya na Rwanda


2 comments:

  1. Inatia huzuni sana, Watanzania kama wamelogwa na hiki Chama Cha Mafisadi!Uhuru upi wakusherehekea hata maji wala umeme hamna kweli karne ya 21 Tanzania!! shame upon government!! hivi hao wanaojiita wasomi serikalini wanafanya kazi gani? Hivi hizi aibu za waziwazi hawazioni?...I think inabidi waTZ wapate sindano za kuwachangamsha kudaihazi zao

    ReplyDelete
  2. SHAME KABISA, SHAME HATA KUJIITA MTANZANIA RIGHT NOW!! SISI SIO WAJINGA HIVI JAMANI! TUNALETA UBISHOO HAPA? NIMEINGIA KWENYE BLOG FLANI NIMEKUTA WATU MUHIMBILI HAWANA VIFAA VYA X-RAY HIVYO WANASUBIRI FUNDI!!! OOH MUNGU BABA! HIVI JAMANI TUNA WANAUME HAPO BONGO KWELI? AU MPAKA WANAWAKE TUINGIE FRONT LINE? MMESHIDWA WANAUME MMESHINDWA?? MNAWEZA MKAONA NI TUSI LAKINI UDINDAJI WENU NI WA UOGA! DINDENI WANAUME DINDA, YANYUWENI MISHIPA HIYO, WAKE ZENU, WATOTO WENU, WANAKUFA KILA LEO KWA HUDUMA MBAYA ZA NCHI, WAKATI NCHI INA PESA ZA KUPOTEZA HIVI?!

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube