12 Dec 2010WAKATI biashara ya magogo ikiendelea kutikisa vichwa vya viongozi wa serikali, imebainika kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, kada wa CCM, wakuu wa polisi na maafisa wa Takukuru ndio wanaomiliki vibali vya kuvuna magogo katika msitu wa serikali wa Sao Hill ulio wilayani Mufindi.Biashara ya magogo ambayo ilishamiri mwaka 2005/06 ilipigwa marufu baada ya kuonekana kasoro kwa wasafirishaji magogo nje ya nchi ambao walionekana kukiuka masharti ya leseni zao na wiki iliyopita Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige alisema marufuku hiyo inaendelea kwa kuwa ni kinyume cha sheria za nchi.
Lakini msimamo huo wa Waziri Maige utakuwa mgumu kuutekeleza baada ya Mwananchi kubaini kuwa wanaomiliki vibali vya kuvuna magogo ni baadhi ya viongozi wa serikali ambao badala ya kuvitumia kwa malengo waliyoombea, wamekuwa wakivikodisha kwa wafanyabiashara.

Baadhi ya vigogo mbao majina ambayo yamo kwenye orodha watu wanaomiliki vibali hivyo ni pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Cyril Chami, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Uratibu na Bunge-, William Likuvi, mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evalista Kalalu, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita na wengine waliotumia majina ya jamaa zao.

Wengine ni Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene na kampuni ya Rombo Green View inayomilikiwa na mmoja wa mawaziri wa zamani katika serikali za awamu tofauti. Katika orodha hiyo pia yamo majina ambayo ubini wake unafanana na baadhi ya viongozi kama vile Selemani KIKWETE, Aneth P. Msekwa na Juma Abdallah Zombe.

Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama watu hao wana uhusiano wa moja kwa moja na watu ambao majina yao ya ubini yanafanana na ya viongozi wa serikali.Vyanzo vyetu vya habari vimebainisha kuwa vigogo walioficha majina yao wanafahamika na kwamba itakapohitajika watatajwa hadharani na raia wema walioapa kuwa tayari kufanya hivyo.
Habari za kiuchunguzi zimebaini kuwa kuwepo kwa watumishi hao wa serikali katika biashara ya magogo kumezua mgogoro mkubwa wa kimaslahi kati yao na wavunaji wadogo wanaolalamika kupunjwa kwenye mgao wa vitalu vya uvunaji.

Uchunguzi umebaini kuwa mgao wa kitaifa unaelekeza meneja mradi wa Sao Hill kugawa magogo yasiyozidi mita za ujazo (cubic metre) milioni moja kwa mwaka.Hata hivyo, katika hali inayoweka mashaka, mgao huo unaonekana kuwapendelea zaidi vigogo hao wanaotumia nyadhifa zao kupata vibali bila kuwa na sifa za kupata mgao huo, huku wengine wanaonufaika wakitajwa kuwa ni baadhi ya wawekezaji wakubwa.Imeelezwa kuwa masharti yaliyowekwa na serikali kwa kila kibali ni kwamba lazima muombaji awe na vifaa kama malori makubwa ya kukokota magogo (break down), mashine zenye uwezo mkubwa wa kuchana magogo na lazima muomba kibali awe ameajiri wataalamu toka chuo cha misitu kinachotambuliwa na serikali, masharti ambayo Mwananchi imedokezwa kuwa hayajatekelezwa na vigogo hao.

Katika kipindi ambacho Rais Jakaya Kikwete amewataka mawaziri na wasaidizi wao kuwa tayari kutoa habari kwa wananchi, katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Ladslaus Komba hakuweza kuzungumzia suala hilo kila mara Mwananchi ilipowasiliana naye kuanzia Jumatano iliyopita.Badala yake, katika simu zote sita alizopigiwa kati ya Jumatano na jana jioni, Dk Komba alipokea lakini baada ya mwandishi kujitambulisha na kueleza kile anachotaka kufahamu kutoka kwake, alijibu:
"Kwa sasa niko kwenye kikao nitakutafuta baadaye.Hata hivyo, hakutekeleza ahadi hiyo hata mara moja.

Katika moja ya simu hizo, Dk Komba alisema: “Kuna kitu hapa nakinukuu, naomba unipe muda nitakujulisha.”
Hata hivyo alipotafutwa baadaye simu yake ilikuwa haipatikani.
Hata alipofuatwa ofisini kwake, katibu muhtasi wake alieleza kuwa Dk Komba alikuwa ameenda kikazi nje ya ofisi na kumtaka mwandishi amsubiri.

Mmoja wa vigogo waliotajwa kwenye orodha ya mgao wa magogo, WaziriLukuvi alikiri kupokea mgao huo, lakini akasema aliomba kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari zilizo jimboni kwake Isimani na si kwa nia ya biashara.

Kwenye mgao huo, Lukuvi amepewa kibali cha kuvuna magogo yenye mita za ujazo 1,000, kulingana na orodha iliyobandikwa kwenye ubao wa matangazo wa Sao Hill Mufindi. Katika  orodha hiyo Lukuvi ni mtu wa 564.
“Ni kweli niliomba na nikapewa kibali cha kuvuna magogo. Lakini, si kwa nia ya biashara bali kwa ajili ya kupata mbao za ujenzi wa sekonda zilizopo jimboni kwangu, ikiwemo ile iliyoungua moto ya Idodi,” alisema.

Mbunge wa jimbo la Kibakwe, George Simbachawene alipoulizwa kuhusu suala hilo alikiri kuomba mgao wa uvunaji magogo katika msitu huo, lakini akasema lengo lake si kwa ajili ya kufanya biashara bali ni ujenzi wa madarasa.
"Ni kweli niliomba wala sibishi, lakini si kwa ajili ya kufanya biashara. Ilikuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule zetu zilizo katika halmasahauri yetu, kwa sababu kununua mbao zikiwa zimeshaandaliwa ni gharama kuliko kuomba kuvuna magogo na kuchana mwenyewe," alisema Simbachawene.

Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni jitihada za kumpata Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Cyril Chami na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita zilishindikana.

Taarifa zinasema kuwa licha ya kujipatia vibali vinavyotolewa bure na Wizara ya Maliasili na Utalii, wamekuwa hawavitumii kwa uvunaji bali huvikodisha kwa wavunaji wadogo kwa gharama ya Sh5 milioni hadi Sh7 milioni kwa kibali kimoja huku ikielezwa kuwa wapo wanaomiliki vibali zaidi ya 10 na wanavitumia kwa majina tofauti.
Hali hiyo imefanya wavunaji wadogo kupunjwa mgao wa uvunaji magogo tofauti na ilivyokuwa kabla ya watumishi hao wa umma na vigogo kuvamia sekta hiyo.

Hivi sasa wavunaji wadogo zaidi ya 400 wanaambulia mgao kiduchu na wengine kukosa kabisa, hivyo wengi wamelazimika kufunga viwanda vyao kutokana na kukosa malighafi.
“Kama watoa vibali ndio wahusika katika biashara hii je, haki itatendeka kwa wavunaji wadogo?,” kilihoji chanzo kimoja.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube