14 Jan 2011


Kuna msemo wa kiswahili kuwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.Naomba niende moja kwa moja kwa kuhusisha msemo huu na mahusiano ya kibaradhuli kati ya vyombo vya dola na Serikali ya CCM chini ya utawala wa Jakaya Kikwete.Katika msemo wetu,Serikali inaweza kulinganishwa na baba,huku vyombo vya dola vikilinganishwa na mtoto. Na hapa sina nia ya kuonyesha undugu uliopo kati ya vyombo hivyo vya dola na CCM iliyozaa serikali tuliyonayo (hata kama ni kwa uchakachuaji).

Serikali ya Kikwete haina tatizo kuona vyombo vya dola vikikiuka maadili ya kazi yao alimradi kwa kufanya hivyo,yeye kama Rais,chama chake na maswahiba wake mafisadi wanaendelea kufakamia keki ya taifa pasipo usumbufu.

Kwa mfano,Kikwete na serikali yake haisumbuliwi na ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu unaofanywa na jeshi la polisi.Na hapa sijagusia mauaji ya huko Arusha na haya ya hivi punde huko Mbarali,Mbeya.Hapa nazungumzia namna haki za msingi za Watanzania wa kawaida (wasio vigogo au mafisadi) zinavyofinyangwa na askari polisi kila kukicha.Madereva na makonda wa daladala ambao wanalazimika "kuziba pengo kati ya kipato halisi cha askari trafiki na mahitaji ya kawaida kwa siku/wiki/mwezi".

Sote tunajua ni rahisi zaidi kugema damu kwenye jiwe kuliko askari Trafiki kumpongeza "suka" (dereva).Sasa nini kinaendelea katika picha hiyo kati ya "maadui" hawa?
Rushwa kwa trafiki imekuwa ni sehemu ya sheria za usalama barabarani,na ndio maana kila kukicha ajali zinaendelea kugharimu maisha ya abiria wasio na hatia.Unategemea nini kama askari mla rushwa anaweza kuruhusu basi lenye injini ambayo hata kwenye trekta haifai?

Unapozungumzia amani na utulivu wa Tanzania,unaweza kuwa umeshahau nini kilichotokea mara ya mwisho ulipokutana na askari polisi wakiwa "kazini".Unless una undugu au ukaribu na kigogo au fisadi flani,ni dhahiri kuwa polisi wetu watatumia mbinu zote za medani kuhakikisha unawapa fedha.Ukibisha,utapigwa na kutumbukiziwa kete ya bangi kama sio cocaine feki.Askari hawa ambao wengi wao hawakujiunga na jeshi hilo kwa vile wanaipenda sana nchi yetu bali kwa sababu ya aidha ugumu wa ajira au wazazi kumwadhibu mtoto mtukutu kwa kumwingiza katika ajira ya polisi.

Hili kundi la pili ni la hatari zaidi kwa sababu linajumuisha watu wenye jeuri ya "baba ni flani" na wanajua hata "wakilikoroga" hakuna wa kuwaadhibu.Pia ni viumbe hatari zaidi kwa vile sababu ya wazazi wao kuwaunganishia ajira ndani ya jeshi hilo ni "kushindikana" kwao katika familia zao.Hawa ni binadamu ambao laiti uchunguzi wa kubaini ufanisi wa kiakili na uwezo wa mwajiriwa mtarajiwa ungefanyika (au ungefanyika bila kupindisha matokeo) wasingepatiwa ajira mahala popote pale.Unatarajia nini kutoka kwa binadamu ambaye kichwa chake kimegeuka ulingo wa vita kati ya ubongo na moshi wa bangi?


Lakini tukiweka kando matatizo binafsi ya askari polisi wetu,hebu fanya ziara kwenye makazi yao kisha jiulize mood watakayokuwa nayo kazini!Yayumkinika kusema kuwa miongoni mwa watumishi wa umma wanaoishi katika hali ya udhalilishaji mkubwa ni askari polisi.Sasa badala ya wao kuelekeza hasira zao kwa mwajiri wao,wanaelekea kuhamishia hasira hiyo kwa kila Mtanzania "wa kawaida".Njaa na dhiki zao zinakuwa kichocheo cha chuki yao dhidi ya walalahoi.Kwa upande mmoja,wamewageuza walalahoi hao kuwa shamba lao la kuchuma rushwa,na kwa upande mwingine wamewageuza sehemu za kutolea hasira zao za manyanyaso wanayovumilia kutoka serikalini.


Makazi ya polisi Msimbazi

Serikali ya Kikwete na CCM yake haina cha kupoteza (at least kwa sasa) kwani malalamiko ya askari polisi kuhusu maslahi duni yanapunguzwa na "ruhusa" waliyopewa kuchuma kipato kwa walalahoi,sambamba na kuhalalishiwa viumbe wa kumalizia hasira za askari hao.


 
Kilichonifanya niandike makala hii ni tamko la Jeshi la Polisi kuhusu mauaji waliyofanya huko Arusha.Ukiangalia juu juu,unaweza kudhani wanajitetea tu.Lakini ukiingia kwa undani zaidi utabaini kauli hiyo ni dalili za wazi za kiburi kinachoanza kujitokeza kutoka kwa "mtoto aliyekosa malezi bora".

Kwanini nasema hivyo?Kwanza Rais Kikwete alitoa kauli ya kizushi kwa mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania na kudai kuwa "MAUAJI YA ARUSHA NI BAHATI MBAYA".Nilishalizungumzia hilo kwa mapana zaidi HAPA .Jumatatu iliyopita,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe alijaribu kutuliza hasira za Watanzania kwa kukiri bayana kuwa Jeshi la Polisi lilikiuka maadili ya kazi yao, lilipokuwa likikabiliana na raia waliokuwa wakiandamana kupinga suala la uteuzi wa meya wa Arusha.

Lakini katika kile blogu hii inatafsiri kuwa JEURI,KICHWA NGUMU na UBABE,jana jeshi hilo lilitoa tamko ambalo haihitaji elimu yoyote kufahamu kuwa ni jibu lao kwa Membe.Katika tamko hilo la kihuni,jeshi hilo sio tu linahalalisha ukatili na uonevu uliopelekea vifo vya mashujaa wawili na majeruhi luluki,pia linafanya mzaha mbaya kwa kudai ni viongozi wa Chadema waliosababisha vurugu na mauaji (kana kwamba viongozi hao ndio waliofumua risasi zilizoua na kujeruhi).

Haihitaji kuumiza kichwa kujiuliza tamko hilo la jeshi la polisi limetolewa na nani.Forget about yule mbabaishaji aliyesimama mbele ya waandishi wa habari kusoma tamko hilo.Huyu alikuwa anatimiza agizo la bosi wake,yaani Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema.Ni Mwema ambaye haafikiani na kauli ya Membe kuwa jeshi hilo lilikiuka maadili.Na kwa vile Mwema ni "mungu wa polisi" basi msimamo wake automatically unakuwa msimamo wa jeshi hilo.Na Mwema ni "mungu-mtu" kweli hasa baada ya kujipachika jukumu la kutoa uhai wa binadamu (kama ilivyotokea huko Arusha na sasa huko Mbarali).

Lakini je Mwema anapata wapi jeuri hiyo ya kupingana na kauli ya Membe,ambaye katika uhusiano wa kimataifa,ni kama mwakilishi mkuu wa Rais katika mahusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani?Jibu jepesi lipo katika uhusiano wa karibu uliopo kati ya Mwema na aliyemteua,yaani Rais Kikwete.Mwema anaweza kusema lolote lile lakini Kikwete hawezi kumfukuza kazi.Na sio kwa sababu Kikwete ni dhaifu na mgumu wa kufukuza kazi watendaji wazembe,bali ni huo uhusiano wa karibu kati ya wawili hao.

Sijui kicheko hicho kinahusiana na usalama wa raia au mengineyo

Je inawezekana Kikwete anatuchezea shere kwa kumwelekeza Membe aseme hili kisha kumwambia swahiba wake Mwema aseme tofauti?Nahoji hivyo kwa vile sidhani kama kauli za Membe na Mwema hazina baraka za Kikwete.Ikumbukwe pia kuwa Kikwete na Membe ni "washkaji" mno,huku ikielezwa kuwa Membe alimsaidia sana Kikwete kukubalika ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa wakati wa kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Ushkaji

All in all,Kikwete na Serikali yake ya CCM wanapaswa kutambua kuwa wanacheza mchezo hatari sana ambao unaweza kupelekea balaa kubwa huko mbeleni.Of course,wengi wetu tunafahamu kuwa kuna ombwe kubwa la uongozi linalosababishwa na uwezo duni wa Kikwete katika medani ya uongozi,lakini pengine ni vema akajiweka kando badala ya kuitumbukiza nchi yetu kwenye mtaro wa kupotea kwa amani.

Kikwete anaendesha nchi katika namna ileile anavyoendesha CCM ambapo hana hata nguvu ya kuwakemea wasema-ovyo wa Chama hicho wanaoongozwa na Yusuph Makamba,Tambwe Hizza na mropokaji brand new Mary Chatanda.Sijui anahofia akiwakemea watamgeuka na kutoboa siri ambazo hataki umma ufahamu!Yaleyale ya akina Rostam na Lowassa.Hawa wanamjua Kikwete in and out,na Kikwete anatambua kuwa akiwatibua tu,amekwisha.Yaani kwa kifupi,uongozi wa Kikwete ni kama umewekwa rehani vile.



Sijui kesho au keshokutwa watakurupuka na lipi jipya kuhusu mauaji ya binadamu wasio na hatia.Midomo inawaruhusu kusema lolote lile,na vyombo vya habari vya KURIPOTI BILA KUCHAMBUA vitajibidiisha kurusha habari hizo.Lakini,wakati wanaendelea kubwatuka,ni muhimu wakaitafakari kwa makini kauli ya Paroko wa Parokia ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Padre Henry Mushi aliyetanabaisha kuwa damu ya vijana waliouawa kwa kupigwa risasi na Polisi Jijini Arusha, itawaandama polisi waliouhusika katika maisha yao yote.

Namnukuu
"...polisi waliohusika na mauaji hayo, hawawezi kujitetea kuwa walitumwa kwani wao sio mashine kiasi cha kuua raia bila kutafakari...Tendo la kumwaga damu lililotokea Arusha ni baya na yeyote aliyefanya kitendo hicho damu hiyo itamsumbua kama ilivyomsumbua Kaini…Huyo aliyefanya hivyo naye atafuata njia hiyo hiyo...wewe ni binadamu sio mashine kwa hiyo hata kama utasema ulitumwa kufyatua risasi lakini, wewe unayepiga risasi ndiye utakayeulizwa mbele za Mungu kwa kushindwa kutafakari...polisi aliyefanya kitendo hicho asifikiri atajificha mbele ya uso wa Mungu"


“Huyo aliyefanya kitendo hicho hatujui yuko wapi lakini afahamu yuko chini ya Mwanga wa Mungu na njia pekee ya kuepuka hasira ya Mungu ni kutubu dhambi hiyo vinginevyo damu aliyoimwaga itaendelea kumsumbua,”

Padre Mushi alitoa kauli hiyo kijijini Makiidi wilayani Rombo wakati wa ibada maalumu ya mazishi ya mmoja wa wafuasi wa Chadema aliyeuawa katika tukio hilo, Dennis Shirima.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.