Hivi kuna uwezekano kwamba Mwenyekiti wa CCM,ambaye pia ni Rais wa Tanzania,Jakaya Kikwete,hamtakii mema Katibu Mkuu wa chama hicho,Yusuph Makamba,na ndio maana (Kikwete) hamshauri Makamba achunge kauli zake.Kwa vile wengi tunafahamu 'upole' (uzembe?) wa Kikwete katika kuwajibisha watendaji fyongo,labda anasubiri Makamba akutane na tukio la 'mchimba kisima kazama kisimani' ie kauli zake za ovyo ovyo zije kumlipukia mwenyewe.
Hebu soma kwanza stori ifuatayo,kisha tutaijadili kidogo.
Makamba amjibu Askofu Laizer
Thursday, 13 January 2011 21:07
Raymond Kaminyoge
KATIBU Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, amesema kuwa na uelewa finyu wa biblia si jambo la ajabu kwake kwa sababu yeye siyo askofu.
Makamba aliliambia Mwananchi jana kwa simu, kuwa licha ya uelewa finyu wa biblia, lakini amekuwa akitoa vifungu hivyo kwenye biblia.Makamba alisema hayo kufuatia, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Thomas Laizer kusema Makamba ana uelewa finyu wa biblia.
Laizer alisema hayo juzi mjini Arusha wakati wa kuwaaga watu wawili waliofariki kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano na Chadema yaliyofanyika Januari 5 mwaka huu.
“ Ni kweli ninauelewa finyu wa biblia kwa sababu mimi siyo askofu, hata Qurani naweza kuwa siifahamu vizuri kwa sababu mimi siyo Sheikh, ndiyo maana kila ninachozungumza kuhusu dini hizo nakariri vifungu kutoka katika vitabu hivyo,” alisema. Makamba alisema alimweleza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kutoandamana kwa sababu serikali ilipiga marufuku maandamano hayo, wao wakapuuza.
Alimtaka Laizer kutoa tafsiri ya kitabu cha Warumi 13 sehemu ya kwanza hadi ya saba, inayosema kuwa kila mtu hana budi kutii serikali inayotawala kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.Alisema kwa hiyo anayepinga mamlaka inayotawala anapinga chombo kilichowekwa na Mungu na watu wanaoasi hujiletea hukumu.
“ Kwa maana watawala hawatishi watu wanaotenda mema bali wale wanaotenda maovu, kama hupendi kuishi kwa kumwogopa mwenye mamlaka basi tenda mema naye atakusifu,” alisema.
“ Laizer anieleze ufinyu wangu katika uelewa wa biblia upo wapi ikilinganisha na tukio lililotokea mkoani Arusha,” alisema.
CHANZO: Mwananchi
Sasa Makamba anaelekea kubaya.Na kama kuna watu wanamtakia mema (angalau ndani ya familia yake) ni vema wakamdhibiti mapema.
Kutumia Maandiko Matakatifu kuhalalisha maovu ni mithili ya matusi kwa waumini wa dini husika.Makamba si Mkristo,na amekiri kuwa uelewa wake wa Biblia Takatifu ni mdogo.Sasa kama ni hivyo,iweje basi aanzishe malumbano na kiongozi wa madehehebu ya Kikristo,achilia mbali kiongozi huyo kuwa ni Askofu Mkuu wa KKKT?
Makamba anaelewa vyema kuwa Maandiko Matakatifu,hayawezi kunukuliwa kwa vipande vipande.Kadhalika,uwezo wa kunukuu haumaanishi uelewa wa nukuu husika.Pia naamini Makamba anafahamu fika kuwa aya aliyotumia kuhalalisha udikteta wa CCM na polisi wake (uliopelekea mauaji ya raia wasio na hatia)haimaanishi kuwa hata mamlaka inayokandamiza watu wasio na hatia iendelee kunyenyekewa.
Kama suala la kutii mamlaka iliyo madarakani,kwanini basi hapo 1979 tulimng'oa Nduli Idi Amini ambaye wakati huo alikuwa Rais halali wa Uganda?Au kwanini basi Hitler nae alivurumishwa ilhali alikuwa kiongozi halali wa Ujerumani?Au kwanini tulisapoti harakati za mapambano dhidi ya makaburu ilhali wabaguzi hao wa rangi walitengeneza "serikali halali"?
Kwa wanaompenda Makamba,ni vema wakamshauri kuwa madaraka aliyonayo,sambamba na kuwa chini ya bosi mwenye huruma kwa wanaoboronga (ie Kikwete),visimfanye apate jeuri ya kuanzisha bifu na Watumishi wa Mungu.Ni vema pia akatambua unyeti wa kutumia Biblia kuhalalisha maovu ilhali yeye ni Muislam.Kiongozi mwenye akili timamu anapaswa kutambua hatari na madhara ya KUDHARAU MAANDIKO MATAKATIFU (kama ambavyo Makamba anavyoichezea Biblia Takatifu mithili ya Manifesto ya Uchaguzi ya CCM-iliyosheheni kila ahadi ya uongo).
Na kama Makamba mwenyewe ameshawahi kusoma blogu hii (which I doubt) basi ushauri wangu mwepesi kwake ni AACHAE KUMCHEZEA MUNGU,hata kama haamini kuwa Mungu ambaye Askofu Mkuu Lazier ni mtumishi wake,ni Mungu wake yeye Makamba.
Na kwa Kikwete,hivi lini utajaribu angalau kuwaonyesha Watanzania kuwa una uwezo japo haba wa kukemea mambo hatari?Ah,yani umekuwa hapo Ikulu kama pambo huku watendaji wako wakizidi kuhangaika kusaka moto na petroli ya kuiunguza Tanzania?
0 comments:
Post a Comment