20 Feb 2011
Picha hizi za kutisha zinajieleza zenyewe.Hakuna maelezo yanayotosheleza kueleza kwa ufasaha kuhusu janga hili.Lakini kwa vile kamwe hatutoelezwa chanzo cha milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto,kama ambavyo hatukuelezwa chanzo cha milipuko iliyotokea mwaka juzi huko Mbagala,ni muhimu kwa kila Mtanzania kudai haki yake ya kikatiba ya usalama wa maisha yake.


Ni wazi kuwa wahusika wanapata jeuri ya kutangaza hadharani kuwa hawatajiuzulu kwa vile wanafahamu bayana kuwa aliyewateua kushika madaraka hayo ni mzembe,dhaifu na asiyejua kinachoendelea.Kwa lugha nyingine,YUPO YUPO TU.

Nilighadhibika sana niliposoma kauli ya Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa JWTZ Brigedia Jenerali Paul Meela kuwa hakuna atakayejiuzulu kwa sababu uongozi jeshini sio nafasi za kisiasa.Haya ni matusi kwa Watanzania.Kwani Amatus Liyumba alipohukumiwa kwenda jela kwa ubadhirifu wa fedha za umma hapo Benki Kuu alikuwa mwanasiasa?

Kwa akili finyu ya Brigedia Meela,ni wanasiasa pekee wanaopaswa kuwajibika wanapoboronga.Lakini kwa vile kamanda huyo alikuwa anamwakilisha Mkuu wa Mwajeshi Jenerali Davis Mwamunyange,yayumkinika kuamini kuwa kauli hiyo pia ni msimamo wa mkuu huyo wa majeshi.

Tuliowahi kupitia mambo ya kijeshi tunafahamu kasumba ya jeuri na u-mungu mtu ilivyokomaa vichwani mwa viongozi jeshini.Hii inaimarishwa zaidi na utaratibu wa kawaida jeshini kwamba amri ina mwelekeo mmoja tu: kutoka juu kwenda chini,na haihojiwi.

Kwahiyo,wakati Kamanda Meela anaongea na waandishi wa habari,akilini mwake alikuwa kama anaongea na makuruta ambao ni dhambi kuu kwao kuhoji lolote lile.Na kwa vile Meela alikuwa anawakilisha mabosi wake,mtu pekee ambaye angeweza kumwadabisha ni Amiri Jeshi Mkuu,Rais Jakaya Kikwete.

Lakini takriban miezi mitano tangu baadhi ya Watanzania wenzetu watusaliti kwa kumrejesha Kikwete madarakani (tukiweka kando uchakachuaji wa Tume ya Uchaguzi),naamini kila Mtanzania anafahamu fika kuwa ombwe la uongozi wa taifa lililojiokeza wakati wa awamu ya kwanza ya utawala wa Kikwete,sio tu limezidi kukua bali pia limeifanya Tanzania kuishi kwa kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu.Ni kama hatuna Rais wala serikali.

Na taasisi muhimu kwa ustawi wa taifa kama Idara ya Usalama wa Taifa ziko katika usingizi mzito unaosababishwa zaidi na marupurupu makubwa licha ya utendaji kazi duni na wa chini ya kiwango.Sijui kama watu hawa wanasumbuliwa na mwenendo wa nchi yetu,kwani ingekuwa hivyo tusingeshuhudia mazingaombwe ya kuruhusu mtu kama Edward Lowassa kuwa Mwenyekiti wa kamati nyeti ya bunge ya Ulinzi na Usalama,leave alone ishu kama za Dowans,EPA,nk.

Na kwa kuonyesha watu wa Usalama wamegubikwa na usingizi,wameshindwa hata kumshauri bosi wao Kikwete kuwa safari yake kwenda Mauritania kusaka ufumbuzi wa mgogoro huko Ivory Coast,sio mwafaka wakati huu wa majonzi makubwa kwa Watanzania.Kikwete na washauri wake wanajifanya hawajui kuwa janga la Gongo la Mboto linawagusa zaidi Watanzania kuliko matatizo ya wa-Ivory Coast.Ni rahisi kwa baadhi ya watu kuhisi kuwa Kikwete anakwepa majukumu na kuamua kwenda kuzurura huko ng'ambo.

Tukirejea kauli za wanajeshi wetu,Brigedia Jenerali Meela anasema taarifa za milipuko iliyopita ni kwa matumizi ya jeshi.Kwani JWTZ limegeuka jeshi la mtu binafsi?Sote tunafahamu kuwa hilo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania.Sasa iweje madudu wanayofanya na yanayopelekea kuwaathiri wananchi wasio na hatia yaishie kuchungiuzwa na wao wenyewe kisha findings nazo zibaki kuwa siri yao?

Jibu la maswali haya na mengineyo mengi ni rahisi:Rais tuliyenae ni dhaifu na asiye na uwezo wa kuwawajibisha hata wale aliowateua yeye mwenyewe.Sasa kwa wanaotegemea Kikwete anaweza kudili na maharamia kama wa Dowans (ambao hakuwateua,na sanasana wanamdai fadhila) watakuwa wana jibu la msingi kuhusu kusuasua kwake kuwashughulikia mafisadi.

Picha kwa hisani ya Rev Masanilo wa Jamii Forums

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.