1 Apr 2011



Moto ulioikumba Tanzania na nchi jirani baada ya kupatikana habari kwamba Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT),Ambilikile Mwasapile,anatoa matibabu ya magonjwa sugu ukiwemo Ukimwi,sasa unatarajiwa kuhamia Bara la Ulaya na Marekani.

Kwa mujibu wa Mchungaji Conrad Munro wa Jumuiya ya Makanisa la Kiluteri Duniani,Mchungaji Ambikile,almaarufu kama "Babu",atazuru nchi kadhaa za Ulaya kabla ya kuelekea Marekani kwa huduma za uponyaji.

Akieleza ratiba ya "Babu",Mchungaji Munro alibainisha kuwa ziara hizo za uponyaji zilizopewa jina Jesus Heals,yaani Yesu Huponya,zitaanzia jijini Edinburgh Scotland mnamo April 15,kabla ya kuendelea katika majiji ya London,Manchester na Birmingham.Baada ya hapo,Mchungaji Ambilikile ataelekea Sweden,Ujerumani,Poland na hatimaye Ufaransa,kabla ya kuhitimisha ziara hiyo yake ya kwanza nje ya Tanzania kwa kutembelea Marekani.Mchungaji Munro alitaja baadhi ya majimbo yatakayobahatika kupata huduma ya "Babu" ni pamoja na Texas (ambapo atazuru Houston na Dallas).

Tovuti hii ilipowasiliana na Mchungaji Munro kwa barua-pepe  ili kufahamu utaratibu wa jinsi ya kuhudhuria huduma hiyo ya maombezi,alieleza kuwa wanaohitaji kuhudhuria wanaweza kuwasiliana naye kupitia tovuti hii kuanzia leo April Mosi hadi hapo utapoandaliwa utaratibu maalum wa mawasiliano.Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa kila anayetaka kuhudhuria kujiandikisha mapema ili kuwezesha upatikanaji wa ukumbi utakaomudu idadi ya wahudhuriaji.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.