Showing posts with label Ambilikile Mwasapile. Show all posts
Showing posts with label Ambilikile Mwasapile. Show all posts

28 Jun 2011

Na Luqman Maloto
Kikombe cha Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapile ‘Babu Ambi’ ni janga la kitaifa, hali halisi ni mbaya na madaktari wametahadharisha.

Kitendo cha idadi kubwa ya wagonjwa wa kisukari na ukimwi kuacha kutumia dawa za kurefusha maisha na baadhi yao kuanza kufariki dunia mmoja baada ya mwingine, imeelezwa kuwa hali itakuwa mbaya baadaye.

Kwa mujibu wa madaktari waliozungumza na gazeti hili, watu wengi wanaokunywa kikombe cha Babu Ambi, wanadharau dozi za dawa za kisukari na ukimwi kwa imani kuwa tiba ya Loliondo inaponya.
Mbali na madaktari, ipo ripoti kuwa kila kukicha watu wanapoteza maisha pande mbalimbali za nchi, ikielezwa kwamba sababu ya vifo ni wagonjwa kuacha kutumia dozi za kurefusha maisha walizopewa hospitalini baada ya kunywa kikombe cha Babu Ambi wa Samunge, Loliondo.

“Wanakosea sana, hivi sasa watu wanakufa lakini mbele ya safari watapukutika zaidi. Tunapokea watu wakiwa mahututi, wapo ambao wanakufa lakini wengine tunafanikiwa kuokoa maisha yao na kuwaanzishia dozi,”  alisema daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa, Muhimbili (jina tunalo) na kuongeza:

“Taifa litapata msiba mkubwa baadaye kwa sababu watu wengi watakufa. Mamilioni ya watu wameshatibiwa Loliondo. Hivi kati ya hao, watu milioni moja ikiwa wanaumwa kisukari na ukimwi, wakiacha tiba inakuaje?
“Ni ruhusa watu kwenda Loliondo kwa sababu ni ngumu kuingilia imani za watu, lakini ni vizuri watu wakapokea ushauri wa kitaalamu ambao tunawapa. Wasithubutu hata siku moja kupuuza wala kuacha tiba za hospitali.”

Daktari mwingine wa Muhimbili (jina linahifadhiwa) alionya kuwa taifa linakabiliwa na mtihani mkubwa kwa sababu hata baadhi ya viongozi hawataki kuamini wanapoambiwa ukweli kwamba kikombe cha Babu Ambi hakijathibitika kuwa kinaponya.

“Hapa tunamuomba Rais Jakaya Kikwete (pichani) aingilie kati. Tunatakiwa kujua ni watu wangapi wamekwenda Loliondo, waliopimwa baada ya kunywa kikombe tuambiwe hali zao. Hapo tutapata jawabu kama Babu anapaswa kuendelea kuruhusiwa kutoa tiba au afungiwe,” alisema daktari huyo.

Aliendelea kusema: “Leo nazungumza lakini inaweza kuonekana ni mzaha, ukweli ni kuwa tiba ya kikombe cha Babu ni janga zaidi ya ajali ya MV Bukoba. Vifo vingi vinatokea, watu wenye ukimwi watakufa zaidi kwa sababu wameacha dawa za kurefusha maisha.”
MV Bukoba ni meli iliyopata ajali Mei 21, 1996 karibu na Bandari ya Mwanza na kuua watu 900.

Kutokana na takwimu hiyo, daktari huyo alisema: “Mamilioni ya watu wamekwenda Loliondo, wengi wanaacha kutumia dawa, ni matokeo gani yanangojewa? Loliondo ni janga zaidi ya MV Bukoba, ukweli upo hivyo. Tusubiri matokeo, wagonjwa wengi wanakuja kupima, tunawabaini bado hawajapona lakini wanatuambia wametoka Loliondo.

“Mimi ni daktari, kuna kasoro Wizara ya Afya katika kulifanyia kazi suala la Loliondo. Wanalichukulia kawaida wakati linabeba watu wengi. Kuna watu wamejipa matumaini hewa, wanamwaga fedha kwenda kunywa kikombe lakini hakuna kupona. Rais Kikwete aingilie kati.”

Mbali na madaktari hao walioomba hifadhi ya majina yao gazetini, Daktari Leopold Mwinuka wa Munufu Clinic alishauri wagonjwa kutoacha dawa za hospitali, hasa wale wenye kisukari.

Saidi Mohamed ambaye ni daktari mstaafu aliliambia gazeti hili: “Kuna rafiki yangu alitaka kwenda Loliondo nikamshauri asifanye hivyo. Kwenda Loliondo ni kujitafutia matatizo zaidi, wengi wakitoka huko wanaacha kutumia dozi walizoelekezwa hospitali, hivyo wanazidiwa kabisa. Sijaona mtu aliyepona. Nina mifano ya watu watano waliopoteza maisha.”

Kwa upande wa Mchungaji wa Kanisa moja, Kibaha Pwani, Godfrey Mtani alisema kuwa suala la Loliondo wamelitazama kwa maono ya kiroho na kubaini kuwa wote waliokunywa kikombe inawezekana wakafariki dunia baada ya miaka miwili.
Wakati huo huo, Makongoro Oging’, aliyekuwa Kahama mkoani Shinyanga anaripoti kuwa watu tisa waliokunywa kikombe cha Babu Ambi wa Loliondo wameangua kilio baada ya kupima na kugundua kuwa bado wana virusi vya ukimwi.

Dk. Timoth Mhezzi wa Kituo cha Mhezzi kinachojihusisha na ushauri na kupima virusi vya ukimwi kwa hiari, Kijiji cha Kakola, Kahama alisema, wagonjwa hao tisa walifika kituoni hapo mwezi uliopita kupima afya zao lakini walimwaga machozi walipopewa majibu kuwa Loliondo haikuwasaidia kitu.

“Baadhi ya wagonjwa hao walianza kububujikwa machozi baada ya kugundua hawajapona, huku  wengine walidai kwamba walitumia fedha zao nyingi kwenda Loliondo bila mafanikio,” alisema Mhezzi.


CHANZO: Global Publishers

28 Apr 2011



Kujali "vipaji" vyetu,kutojua vipaumbele vyetu au ufisadi wa kiakili?

Tukiamini takwimu kutoka huko Loliondo kuwa wastani wa wagonjwa wanaofika sehemu hiyo matibabu ni 2000 kwa siku,kwa wiki ni watu 14,000,kwa mwezi ni (wastani) 42000-au tukuze makadirio na kufanya watu 50,000 kwa mwezi,na tunaambiwa "Babu" alianza matibabu kitambo kidogo kabla habari hazijashika moto kwenye mwezi Februari,basi kuna uwezekano takriban watu milioni moja wameshapatiwa tiba na mtumishi huyo wa Mungu. (habari zinasema alianza matibabu tangu mwaka 2009,lakini kwa minajili ya kuamsha tafakuri tufanye alianza mwezi Januari mwaka jana.


Swali moja gumu ambalo nashindwa kabisa kupata jibu lake ni USHUHUDA KUTOKA KWA WALIOPONA.Hivi kweli kati ya watu milioni moja,au kwa kumtendea haki tuseme watu nusu milioni,hakuna hata 100 kati yao wanaoweza kutangaza hadharani kuwa walikuwa na ukimwi kisha wakapona baada ya kupewa kikombe?Vyombo vyetu vya habari vimekuwa bize zaidi kuripoti matukio badala ya kuchunguza ufanisi wa tiba hiyo ya kikombe.


Anyway,hebu soma habari ifuatayo kuhusu namna "Babu" anavyotukuzwa kama VIP flani.Msafara kwenda kwenye msiba wa mwanae ukiongozwa na polisi na maafisa usalama,stahili zinazotolewa kwa viongozi wa juu wa kitaifa kama vile Rais,Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.




Babu aenda msibani chini ya ulinzi

MCHUNGAJI Ambilikile Mwasapila anayetoa tiba ya magonjwa sugu huko Samunge Loliondo, juzi jioni aliondoka hapa kwenda Babati, Manyara kuhudhuria mazishi ya mtoto wake huku safari yake hiyo ikiratibiwa na Serikali na akipewa ulinzi mkali wa maofisa usalama na polisi.

Aliondoka Samunge saa 12:20 jioni na gari la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro akiwa na maofisa hao wa usalama, polisi na wasaidizi wake.Kabla ya kuondoka Samunge, watu mbalimbali walikuwa wamejitolea kumpatia usafiri mchungaji huyo lakini walizuiwa kutokana na sababu za kiusalama.

"Tulikaa kama kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, tukaona ni busara tuchukue jukumu la kumsafirisha Mchungaji hasa kutokana na sababu za kiusalama," alisema ofisa mmoja mwandamizi wa serikali wilayani hapa.Alisema mchungaji huyo atalindwa akiwa msibani na atakaporejea Samunge.

CHANZO: Mwananchi

TAFAKARI

9 Apr 2011

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akikodolea macho ambulance ya bajaji.Labda macho yangu tu lakini naona kama Pinda hana hakika kama tupo karne ya 21 au tunarejea Zama za Mawe!
Na mwenye dhamana ya afya ya Watanzania kwa sasa ni Babu wa Loliondo.

HII NDIO TANZANIA ZAIDI YA UNAVYOIJUA


4 Apr 2011

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Teresya Huvisa akipata kikombe cha Babu Loliondo.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dk Yohana Balelel wakipata tiba ya mchungaji Ambilikile Mwasapile wa kijiji cha Samunge, Loliondo.

Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira (aka Tyson) na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, akipata kikombe cha tiba ya babu, katika Kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro

Waziri wa Mwasiliano na Ujenzi DOKTA John Pombe Magufuli.International insult to the Doctorate of Philosophy (PhD)?


At least ishu ya "Babu" imetusaidia wengine kufahamu kuwa wengi wa viongozi wetu wana afya zenye mgogoro.Na haihitaji rocket science kuhisi kilichowapeleka kwa "Babu" ni tiba ya maradhi gani...

KWA VIONGOZI WA NAMNA HII TUANDIKE TUMELIWA

1 Apr 2011



Moto ulioikumba Tanzania na nchi jirani baada ya kupatikana habari kwamba Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT),Ambilikile Mwasapile,anatoa matibabu ya magonjwa sugu ukiwemo Ukimwi,sasa unatarajiwa kuhamia Bara la Ulaya na Marekani.

Kwa mujibu wa Mchungaji Conrad Munro wa Jumuiya ya Makanisa la Kiluteri Duniani,Mchungaji Ambikile,almaarufu kama "Babu",atazuru nchi kadhaa za Ulaya kabla ya kuelekea Marekani kwa huduma za uponyaji.

Akieleza ratiba ya "Babu",Mchungaji Munro alibainisha kuwa ziara hizo za uponyaji zilizopewa jina Jesus Heals,yaani Yesu Huponya,zitaanzia jijini Edinburgh Scotland mnamo April 15,kabla ya kuendelea katika majiji ya London,Manchester na Birmingham.Baada ya hapo,Mchungaji Ambilikile ataelekea Sweden,Ujerumani,Poland na hatimaye Ufaransa,kabla ya kuhitimisha ziara hiyo yake ya kwanza nje ya Tanzania kwa kutembelea Marekani.Mchungaji Munro alitaja baadhi ya majimbo yatakayobahatika kupata huduma ya "Babu" ni pamoja na Texas (ambapo atazuru Houston na Dallas).

Tovuti hii ilipowasiliana na Mchungaji Munro kwa barua-pepe  ili kufahamu utaratibu wa jinsi ya kuhudhuria huduma hiyo ya maombezi,alieleza kuwa wanaohitaji kuhudhuria wanaweza kuwasiliana naye kupitia tovuti hii kuanzia leo April Mosi hadi hapo utapoandaliwa utaratibu maalum wa mawasiliano.Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa kila anayetaka kuhudhuria kujiandikisha mapema ili kuwezesha upatikanaji wa ukumbi utakaomudu idadi ya wahudhuriaji.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.