26 Apr 2011
Makala hii ya Profesa Mbele imenigusa sana (kama ilivyo kwa maandiko yake mengi ambayo kwa hakika ni hazina kubwa kwa Taifa).Tanzania haina uhaba wa wazalendo,ndani na nje ya nchi hiyo,lakini tatizo ni kasumba ya kutowaenzi wazalendo hao.Na namna bora ya kuwaenzi ni kufanyika kazi ushauri wao wa kitaaluma na/au kitaalamu.

Makala husika ni hii:

Wa-Tanzania wanalalamika sana kuhusu mikataba bomu ambayo inalisababishia Taifa hasara kubwa. Tafsiri yao, kwa ujumla, ni kwamba tunaingizwa katika janga hili na mafisadi ambao wanasaini kwa makusudi mikataba hii, kwamba hao ni wa-Tanzania wenye ubinafsi na uroho, na hawana uchungu na nchi, bali wanatafuta namna ya kunufaika wao. Mafisadi wetu hao wanashirikiana na mafisadi wa nje kuitafuna nchi yetu.

Kwa ujumla, nami nina hisia hizo. Kwanza kuna ukweli usiopingika kuwa maadili katika nchi yetu yanazidi kuporomoka. Vile vile nazingatia usemi wa wahenga kuwa lisemwalo lipo, na kama halipo laja. Pia tunaona taarifa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuhusu uozo wa rushwa katika masuala ya mikataba, zabuni, na kadhalika.

Lakini msimamo wangu hauishii hapa. Naamini kuwa hata kama tukiondoa kabisa rushwa na ufisadi, tukawa na watu wanaojali maslahi ya nchi na hao ndio wakawa wanaosaini mikataba yetu, bado tutaendelea kulizwa na mikataba bomu.

Kitakachosababisha janga hili ni kuanguka kwa elimu katika Tanzania. Kama ninavyosema daima katika blogu hii na sehemu zingine, wa-Tanzania tumejichimbia kaburi kwa kutothamini elimu ipasavyo. Ushahidi ni ufahamu wa lugha ulivyo duni, na utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ulivyofifia au kutoweka miongoni mwetu.

Nikifafanua suala la lugha na kulihusisha na suala la mikataba, napenda kusema kuwa tupende tusipende, mikataba ya kimataifa itaendelea kuandikwa kwa ki-Ingereza, nasi tutajikuta tunasaini bila kuelewa vizuri kilichomo. Kuna matapeli wengi duniani, ikiwamo katika uwanja wa biashara na uwekezaji.

Wajanja, kwa kutambua umbumbumbu wetu, watachukulia mwanya huu kama mbinu ya kutukomoa. Laiti tungekumbuka msisitizo wa Mwalimu Nyerere pale tulipopata Uhuru, kuhusu maadui watatu tuliopaswa kupambana nao: umaskini, maradhi na ujinga.

Mwaka jana, serikali ya CCM ilitamka mara kwa mara kwamba imefanya marekebisho katika mikataba ya madini, ili kuziba mianya iliyokuwepo, iliyokuwa inatukosesha mapato tunayostahili. Sasa hapo nina suali. Ni nini kilichotufanya tusione hizo dosari tangu mwanzo? Kama si ufisadi, labda ni huu ujinga ninaoongelea. Binafsi, nakerwa kwamba serikali haijatuelezea undani wa suala hilo.
Kwa makala hiyo na nyingine za Profesa Mbele,mtembelee kwenye blogu zake, MBELE na HAPA KWETU. Pia katika blogu hizo kuna orodha ya vitabu mbalimbali vilivyoandikwa naye.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube